IJUMAA
WIKI YA 6 YA PASAKA
Somo:
Mdo 18:9-18
Zab:
47:2-3, 4-5, 6-7
Injili:
Yoh 16:20-23a
Nukuu:
“Hata
Galio alipokuwa liwali wa Akaya, Wayahudi wakamwinukia Paulo kwa nia moja,
wakamleta mbele ya kiti cha hukumu, wakisema
Mtu huyu huwavuta watu ili wamwabudu Mungu kinyume cha sharia,” Mdo 18:12-13
“bali
ikiwa ni hoja juu ya maneno na majina na sheria yenu, liangalieni ninyi
wenyewe, maana mimi sitaki kuwa mwamuzi wa mambo hayo,” Mdo 18:15
“Amin,
amin, nawaambia, Ninyi mtalia na kuomboleza, bali ulimwengu utafurahi; ninyi
mtahuzunishwa, lakini huzuni yenu itageuka kuwa furaha,” Yoh 16:20
“Basi
ninyi hivi sasa mna huzuni; lakini mimi nitawaona tena; na mioyo yenu
itafurahi, na furaha yenu hakuna awaondoleaye,” Yoh 16:22
TAFAKARI:
“Furaha katika Mateso.”
Wapendwa wana wa Mungu,
leo tutafakari neno hili kadiri ya masomo yetu ya leo, “Furaha katika Mateso.”
Licha ya kuwepo kwa mitazamo tofauti kuhusu mateso kadiri ya Imani zetu,
uhalisia wa mateso ni mang’amuzi ambayo kila mmoja wetu anaweza kuuelezea. Wapo
ambao wameenda mbali zaidi na kusema kwamba kitendo cha mtoto mdogo kulia baada
ya kuzaliwa tu, ni ujumbe kwetu kwamba dunia hii tunayoishi hatuwezi
kuitenganisha na mahangaiko na mateso yetu.
Mateso ni hali na pia
ni sehemu ya maisha ya binadamu yeyote bila kujali imani yake. Ila
"mateso" huwa na maana tu katika sababu na tafsiri yake.
Swali
kwako na kwangu: Nini sababu ya mateso yangu? Nini sababu
ya uwepo wetu? Je, kuna maana yeyote
ya mimi kuwepo? Kama ipo; malengo
yake ni nini hasa kwa hali hii niliyonayo sasa? Wapendwa yapo majibu rahisi hasa pale tu tunapojua chanzo chake. Mfano;
1. kuna magonjwa ambayo
tunayapata tukijua chanzo chake ni nini, tiba yake, na matokeo yake hujulikana.
Hapa mwathirika ni kufuata ushauri wa daktari na yote huueleweka.
2. Yapo pia mateso
yatokanayo na magonjwa fulani twajua tu chanzo chake, ila tiba na kupona kwake
bado ni kitendawili kikubwa.
3. Yapo pia mateso
ambayo uelekea kuwa na magonjwa ambayo hatujui chanzo chake, tiba yake, na
mwisho hatujui kupona kwake. Hapa binadamu hupita katika uvuli mzito wa umauti.
Hapa pia yawezekana kukawa na Mateso tu ambayo si ugonjwa ila ni hali ya
"sintofahamu." Unakuta unateseka ila huna maelezo yanayojitosheleza.
Aina hii ya tatu ina
ugumu sana kwa binadamu kuipokea. Tunajisikia kutengwa hata kutokuona umaana wa
Mungu kwetu kama (upendo wake, uwezo wake na hata umuhimu wake). Bila tafsiri
yenye kujumuisha, "sababu, lengo, na uwepo wa Yesu katika historia nzima
ya wokovu wetu," ni vigumu kuona maana, lengo, na FURAHA katika mateso
yetu kwa ujumla na zaidi kwa kipengele cha tatu.
Ni ndani ya Yesu
Kristo, na katika Yesu Kristo twaweza elewa "fumbo" la TESO na siyo
"jibu" lake. Ufahamu huu ukiwepo basi ni mwanzo wa FURAHA katika TESO
lolote lile.
Jambo
la kufahamu:
Teso au mateso si jambo
au hali ya kudumu milele likiwa ndani ya Yesu Kristo na katika Yesu Kristo. Rejea; Mt 4:24, Mt 16:21, Mk 8:31; Lk 9:22, Lk 16:28,
Lk 17:25, Lk 24:26; Rum 8:18; 2 Kor 1:6, 2 Kor 1:7; Flp 3:10; Kol 1:24; 2 Tim
1:12, 2 Tim 3:11; 1 Pet 4:13, 1Pet 5:9; Ufu 1:9
Kwa kushiriki ubinadamu wetu na katika safari ya
wokovu wetu, Yesu Kristo kaondoa umilele wa Teso/mateso yetu na kulipa/kuyapa
maana. Akiwa ndiye Njia, ukweli, na uzima (Yoh 14:6), Yesu anachagua njia ya
mateso kutupatia wokovu wetu. Hapa ndipo mateso au teso huwa na maana ndani ya
Yesu Kristo na kwa ajili ya Yesu Kristo.Twashiriki pia mateso na wengine katika
Kristo tukitambua ukweli huu wa fumbo la teso kwa njia ya sala na majitoleo
yetu tukiwa katika muunganiko na Kristo.
Wapendwa wana wa Mungu, Mtume Paulo anaburuzwa na
Wayahudi mbele ya Mahakama ya Kirumi kushtakiwa kwa kosa la kuwavuta watu ili
wamwabudu Mungu. Je, kunakosa lolote kumwabudu Mungu? Kumwabudu Mungu kama
tendo la kujisalimisha kwake ndiyo njia pekee ya kujenga mahusiano yetu na
Mungu ya karibu. Ndio njia pekee ya kuzijua siri na
ufahamu wa Kimungu. Kwa Mtume Paulo mambo yalikuwa kama hivi: ““Hata Galio alipokuwa liwali wa Akaya, Wayahudi
wakamwinukia Paulo kwa nia moja, wakamleta mbele ya kiti cha hukumu, wakisema Mtu huyu huwavuta watu ili
wamwabudu Mungu kinyume cha sharia,” Mdo 18:12-13. Kwa vile Mtume Paulo
alisimama katika kweli na haki, Galio anawashangaa Wayahudi kwa madai yao juu
ya Paulo, naye anasema, “bali ikiwa ni hoja
juu ya maneno na majina na sheria yenu, liangalieni ninyi wenyewe, maana mimi
sitaki kuwa mwamuzi wa mambo hayo,” Mdo 18:15. Tukio hili ni mateso katika
furaha. Ni furaha kwa sababu tunajua tunateseka katika kweli, ila hatujui kwa
nini tunateswa, na watesi wetu wameingiwa upofu wa kujui kweli. Mtume Paulo
analitambua jambo hili kwa undani kabisa na hivyo anasema, “kwa maana
nayahesabu mateso ya wakati huu wa sasa kuwa si kitu kama utukufu ule
utakaofunuliwa kwetu,” Rum 8:18
Kuyaona mateso katika
mtazamo huu wa Mtume Paulo ni kukomaa katika Imani, na kujua kusudi la malengo
yako hapa duniani. Malengo yetu hapa duniani ni ya muda mfupi, ukilinganisha na
umilele baada ya maisha haya. Yesu Kristo anatufumbulia kitendawili hiki katika
Injili ya leo kwa kusema, “Amin, amin,
nawaambia, Ninyi mtalia na kuomboleza, bali ulimwengu utafurahi; ninyi
mtahuzunishwa, lakini huzuni yenu itageuka kuwa furaha,” Yoh 16:20. Wito wa
Bwana wetu Yesu Kristo kuhusu mateso ni kwamba yatupasa kutazama mbele zaidi,
yaani, kile kitakachokuwa baada ya mateso hayo. Kwa hiyo ni lazima kuona na
kutambua kiini cha mateso yako, na mahusiano yake ndani na katika Kristo.
Wapendwa wana wa Mungu,
furaha halisi na isiyo na kikomo ni furaha ya kuteseka pamoja na Kristo na
kufufuka pamoja naye. Kuteseka pamoja na Kristo ni kuyatazama mateso yote ndani
na katika Kristo, na kumshirikisha mateso hayo ambayo kwayo yeshapewa maana na
Kristo mwenyewe. Maana ya mateso katika Kristo ni USHINDI. Kristo kayashinda
mateso na kwake tu, mateso yana maana. Hivyo “basi
ninyi hivi sasa mna huzuni; lakini mimi nitawaona tena; na mioyo yenu
itafurahi, na furaha yenu hakuna awaondoleaye,” Yoh 16:22. Ndugu yangu
tuliyesafiri sote katika tafakari hii, baada ya ushindi huu wa mateso ndani na
katika Kristo, ni furaha ya kweli na isiyo na kikomo.
Hivyo wapendwa katika
Kristo, kamwe tusiyasahau maneno haya mazito ya Bwana wetu Yesu Kristo; “Kwani
atafaidiwa nini mtu akiupata ulimwengu wote, na kupata hasara ya nafsi yake? Au
mtu atatoa nini badala ya nafsi yake?” Mt 16:26. Kuyakimbia mateso ndani na
katika Kristo ni kuukimbia utukufu wa Mungu.
Tumsifu Yesu Kristo!
“Basi
ninyi hivi sasa mna huzuni; lakini mimi nitawaona tena; na mioyo yenu
itafurahi, na furaha yenu hakuna awaondoleaye,” Yoh 16:22
Tusali:-Ee
Bwana wetu Yesu Kristo, tupe uwezo wa kuyapokea yote katika Wewe na ndani ya
Wewe ili tupate maana ya furaha katika mateso yetu. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario