JUMATANO
WIKI YA 6 YA PASAKA
Somo:
Mdo 17:15, 22-18:1
Zab:
148:1-2, 11-12, 13, 14
Injili:
Yoh 16:12-15
Nukuu:
“Kwa
sababu nilipokuwa nikipita huko na huko na kuyaona mambo ya ibada yenu, naliona
madhabahu iliyoandikwa maneno haya, KWA MUNGU ASIYEJULIKANA. Basi mimi
nawahubirini habari zake yeye ambaye ninyi mnamwabudu bila kumjua. ” Mdo 17:23
“Mungu
aliyeufanya ulimwengu na vitu vyote vilivyomo, yeye, kwa kuwa ni Bwana wa
mbingu na nchi, hakai katika hekalu zilizojengwa kwa mikono; wala hatumikiwi kwa mikono ya wanadamu
kana kwamba anahitaji kitu cho chote; kwa maana ndiye anayewapa wote uzima na
pumzi na vitu vyote,” Mdo 17:24-25
“Basi,
kwa kuwa sisi tu wazao wa Mungu, haitupasi kudhani ya kuwa Uungu ni mfano wa
dhahabu au fedha au jiwe, vitu vilivyochongwa kwa ustadi na akili za wanadamu,”
Mdo 17:29
“Kwa
maana ameweka siku atakayowahukumu walimwengu kwa haki, kwa mtu yule
aliyemchagua; naye amewapa watu wote uthabiti wa mambo haya kwa kumfufua katika
wafu,” Mdo 17:31
“Basi
waliposikia habari za ufufuo wa wafu wengine walifanya dhihaka; wengine
wakasema, Tutakusikiliza tena katika habari hiyo,” Mdo 17:32
“Lakini
yeye atakapokuja, huyo Roho wa kweli, atawaongoza awatie kwenye kweli yote; kwa
maana hatanena kwa shauri lake mwenyewe, lakini yote atakayoyasikia atayanena,
na mambo yajayo atawapasha habari yake,” Yoh 16:13
“Yeye
atanitukuza mimi, kwa kuwa atatwaa katika yaliyo yangu na kuwapasha habari,”
Yoh 16:14
TAFAKARI:
“Basi mimi nawahubirini habari zake yeye ambaye ninyi mnamwabudu bila kumjua,”
Mdo 17:23b
Wapendwa wana wa Mungu,
leo tuone kwa undani kuhusu kuabudu. Inawezekana kabisa kuabudu kwetu
hakuendani kabisa na maana halisi ya tendo hilo. Mtume Paulo katika harakati
zake za uinjilishaji anafika Athene. Mji huu ulijulikana sana kwa ukuaji wa falsafa,
na watu walitumia muda wao kutafuta ukweli kwa fikra nyakinifu. Hivyo kiufahau
walikuwa katika hali ya pekee kabisa. Mtume Paulo alipofika mahali hapa,
aliwakuta watu hawa wana hofu ya Mungu asiyejulikana. Kwa kuliona jambo hilo,
Paulo anawashukuru, na kutoa sababu ya kuwashukuru. “Kwa
sababu nilipokuwa nikipita huko na huko na kuyaona mambo ya ibada yenu, naliona
madhabahu iliyoandikwa maneno haya, KWA MUNGU ASIYEJULIKANA. Basi mimi
nawahubirini habari zake yeye ambaye ninyi mnamwabudu bila kumjua. ” Mdo 17:23
Mungu huyu anayemwamini
Mtume Paulo na kumhubiri ni “Mungu
aliyeufanya ulimwengu na vitu vyote vilivyomo, yeye, kwa kuwa ni Bwana wa
mbingu na nchi, hakai katika hekalu zilizojengwa kwa mikono; wala hatumikiwi kwa mikono ya wanadamu
kana kwamba anahitaji kitu cho chote; kwa maana ndiye anayewapa wote uzima na
pumzi na vitu vyote,” Mdo 17:24-25. Kwa ufupi Mungu huyu anayemwamini na
kumhuribi Paulo, ahitaji kuumbwa nasi wanadamu. Hatuhitaji kumfinyanga kwa
mikono yetu. Mungu huyu haitaji kufananishwa na jambo lolote, kwani yote
tuyajuayo na kuyafikiri ndiye aliyeyafanya. Kumfananisha Mungu na kile
alichokifanya, ni kumshushia heshima yake na kumweka katika mizania ya
ubinadamu wetu. Hivyo, “kwa kuwa sisi tu
wazao wa Mungu, haitupasi kudhani ya kuwa Uungu ni mfano wa dhahabu au fedha au
jiwe, vitu vilivyochongwa kwa ustadi na akili za wanadamu,” Mdo 17:29. Kumfinyanga
Mungu kwa namna yeyote ile ni kutokujua tufanyacho na kupoteza Muda. Huu ndio
ujumbe anaoutoa Mtume Paulo kwa hawa watu wa Athene.
Wapendwa wana wa Mungu,
ibada ya kweli yenye kuleta furaha kwa Mungu hutokea unapojitoa kikamilifu kwa
Mungu. Kiini cha kuabudu ni kujisalimisha. Kujitoa kwa Mungu ndiyo kuabudu
hasa. Tendo hili la kujisalimisha binafsi linaitwa kwa majina mengi: Kujiweka
wakfu, Kumfanya Yesu Bwana wako, Kuchukuwa msalaba wako, Kuifisha nafsi, Kujitoa
kwa Roho Mtakatifu. Jambo muhimu hapa ni kwamba ulitende, siyo linaitwaje.
Mungu anapenda maisha yako-yote. Asilimia tisini na tano haitoshi. Kuna vizuizi
vitatu ambavyo huzuia kujisalimisha kwetu kikamilifu kwa Mungu: Hatuelewi kiasi
gani Mungu anatupenda, Tunataka kutawala maisha yetu wenyewe, na Tunashindwa
kuelewa maana ya kujisalimisha.
Kujisalimisha kwa Mungu si kujiuzulu na kukaa tu
kusubiri, au kuamini kuwa yote yameandikwa binadamu hana hiari, au kuwa na
udhuru na wivu. Siyo kukubali hali hiyo hiyo uliyo nayo. Inaweza kumaanisha
kinyume cha haya; kujitoa sadaka maisha yako au kuteseka ili kubadilisha yanayohitajika
kubadilishwa. Mara nyingi Mungu huwaita watu waliojisalimisha kwake kupiga vita
kwa jina lake. Kujisalimisha sio kwa uoga au mazulia. Mungu asingependa
kupoteza akili alizokupa! Mungu hapendi watu wawe kama mitambo (robots) ili
kumtumikia. Kujisalimisha siyo kukomesha utu wako. Badala ya kukomesha utu
wako, kujisalimisha huutia nguvu. C. S Lewis alisema, “kadiri tunavyomruhusu
Mungu atutawale ndivyo tunavyozidi kuwa sisi wenyewe-kwa sababu yeye ndiye
aliyetuumba. Alibuni namna mbalimbali za watu wote tofauti ambao mimi na wewe
tulikusudiwa kuwa…. Ni pale ninapomgeukia Kristo, ninapojikabidhi nafsi yangu
kwake, ndipo ninapokuwa na ule utu wangu halisi.”
Kujisalimisha kunadhihirika vyema katika kutii. Unasema
‘ndivyo, Bwana’ kwa chochote anachokueleza. Kusema “hapana, Bwana” ni kutamka
vinyume. Hatuwezi kumwita Yesu Bwana na wakati huo huo hatutaki kumtii. Baada
ya usiku kucha bila kupata samaki, Simioni alionyesha kujisalimisha pale Yesu
alipomwambia kujaribu tena” “Bwana tumefanya kazi kwa bidii usiku wote na
hatujakamata samaki yeyote. Lakini kwa sababu umesema, nitatia nyavu majini.”
Lk.5:5. Watu waliojisalimisha hutii neno la Mungu hata kama linaonekana
kutokuwa na maana.
Kila mtu hatimaye hujisalimisha kwa mtu au kitu fulani. Kama
sio kwa Mungu, utajisalimisha kwa matarajio au maoni ya watu wengine, au pesa,
chuki, hofu, au kwa kiburi chako au tama mbaya, au ubinafsi. Ulibuniwa
kumwabudu Mungu-na kama utashindwa kumwabudu, utatengeneza vitu vingine
(sanamu) ili uvipe maisha yako. Unao uhuru wa kuchagua usalimishe maisha yako,
lakini huko huru na matokeo ya uchaguzi huo. E. Stanly Jones alisema, “kama
hutajisalimisha kwa Kristo, utajisalimisha kwa machafuko.” Kujisalimisha si
njia bora ya kuishi; ni njia pekee ya kuishi. Hakuna kitu kingine cha
kukufanikisha. Njia nyingine zote hukuongoza kwenye kukukatisha tamaa, na
kuziangamiza nafsi. Tafsiri ya King James huita kujisalimisha “huduma yenu
yenye maana,” Rum. 12:1. Tafsiri nyingine inasema, njia yenye maana zaidi ya
kumtumikia,” Rum 12:1. Kusalimisha maisha yako si hisia za kipumbavu lakini ni
tendo la akili na busara ambalo unaweza kulifanya kwa ajili ya maisha yako.
Ndiyo maana Paulo alisema, “Ni lengo letu kwamba tumpendeze yeye”.2Kor 5:9
Nyakati zako za busara zitakuwa zile ambazo unasema ndiyo kwa Mungu.
Wakati mwingine huchukua miaka, lakini hatimaye unagundua
kwamba kizuizi kikubwa kwa Baraka za Mungu maishani mwako sio watu wengine, ni
wewe mwenyewe-matakwa yako binafsi, kiburi cha hali ya juu, na matarajio yako.
Huwezi kutimiza lengo la Mungu kwa maisha
yako huku ukikazania malengo yako binafsi.
Kama Mungu ataenda kufanya kazi ya kina ndani yako,
itaanza hivyo. Kwa hiyo mpe yote Mungu: kushindwa kwako hapo nyuma, matatizo
yako ya sasa, matarajio yako ya mbele, hofu zako, ndoto, udhaifu, tabia,
maumivu, na madhara yoyote uliyo nayo. Mweke Yesu katika kiti cha dereva wa
maisha yako na uondoe mikono yako toka kwenye usukani. Usiogope; hakuna
chochote katika uongozi wake kinaweza kupoteza dira. Chini ya uongozi wa Kristo
unaweza kudumu chochote. Utakuwa kama Paulo, “Niko tayari kwa lolote na kuwa
sawa na chochote kwa njia ya yeye anayetia nguvu ndani yangu, yaani,
ninajitosheleza katika utoshelvu wa Kristo,” Flp 4:13
Kwa kutotambua ukweli
huu hakutuondolea hukumu ya mwisho. Ufahamu tuliopewa wa kujua mema na mabaya,
ndipo kulipokuwa na hukumu yako. Pamoja na ukweli huu, Mungu amekwisha tupatia
hakimu wetu, yaani Mwanaye Yesu Kristo ambaye katuambia yote yanayohusu ufalme
wake. Yesu Kristo ni sawa na Sheria iliyokwishwa tungwa na kupitishwa kwa
kupigiwa sahihi na Rais. Mungu ndiye aliyethibitisha jambo hili pale mlimani
alipojeuka sura kwa kusema, “Huyu ni Mwanangu, mteule wangu, msikieni yeye,” Lk
9:35. Hivyo, Yesu Kristo ndiye hakimu wetu wa haki. “Kwa
maana ameweka siku atakayowahukumu walimwengu kwa haki, kwa mtu yule
aliyemchagua; naye amewapa watu wote uthabiti wa mambo haya kwa kumfufua katika
wafu,” Mdo 17:31. Jambo hili la ufufuko linakuwa tatizo kwa watu hawa wa Athene
na hivyo hawapo tayari kumsikiliza Paulo. “Basi
waliposikia habari za ufufuo wa wafu wengine walifanya dhihaka; wengine
wakasema, Tutakusikiliza tena katika habari hiyo,” Mdo 17:32.
Hata pamoja na
kutoeleweka huku wa Mtume Paulo, haikuwa sababu ya yeye kukata tamaa. Katika
utume wetu mara nyingi tunakutana na hali kama hii. Kristo anatukumbusha jambo
la muhimu sana. Hatupaswi kujisikia wapweke, ila tunaye Roho Mtakatifu ambaye
anatufunulia hayo yote yaliyojificha na kutuongoza katika kweli yote. “Lakini yeye atakapokuja, huyo Roho wa kweli,
atawaongoza awatie kwenye kweli yote; kwa maana hatanena kwa shauri lake
mwenyewe, lakini yote atakayoyasikia atayanena, na mambo yajayo atawapasha
habari yake,” Yoh 16:13. Uwepo wa Roho
Mtakatifu humtukuza Mwana na kuyanena yote ambaye mwana anataka kuyanena na
kuyafanya. “Yeye atanitukuza mimi,
kwa kuwa atatwaa katika yaliyo yangu na kuwapasha habari,” Yoh 16:14. Tunaye
msaidizi wa kweli atakayetufunulia yaliyo ya kweli. Hakuna sababu ya kuwa na
hofu tunapokutana na sintofahamu katika utume wetu, na hata katika maisha kama
kweli tunamwamini Mwana wa Mungu.
Tumsifu Yesu Kristo!
“Yeye
atanitukuza mimi, kwa kuwa atatwaa katika yaliyo yangu na kuwapasha habari,”
Yoh 16:14
Tusali:-Naam
najisalimisha kwako Ee Yesu Mwema. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario