ALHAMISI WIKI YA 9 YA MWAKA-C
Somo: 2Tim 2:8-15
Zab: 25:4-5ab, 8-9, 10, 14
Injili: Mk 12:28-34
Nukuu:
“Nami
katika hiyo nimeteswa hata kufungwa kama mtenda mabaya; lakini neno la Mungu
halifungwi,” 2Tim 2:9
“Kwa
ajili ya hilo nastahimili mambo yote, kwa ajili ya wateule, ili wao nao waupate
wokovu ule ulio katika Kristo Yesu, pamoja na utukufu wa milele. Ni neno la kuaminiwa. Kwa maana, Kama
tukifa pamoja naye, tutaishi pamoja naye pia; Kama
tukistahimili, tutamiliki pamoja naye; Kama tukimkana yeye, yeye naye atatukana
sisi; Kama sisi hatuamini, yeye
hudumu wa kuaminiwa. Kwa maana hawezi kujikana mwenyewe,” 2Tim 2:10-13
“Katika amri zote ni ipi iliyo ya kwanza?” Mk 12:28b
“Yesu akamjibu, Ya kwanza ndiyo hii, Sikia, Israeli, Bwana
Mungu wetu ni Bwana mmoja; nawe
mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa akili
zako zote, na kwa nguvu zako zote,” Mk 12:29-30
“Na ya
pili ndiyo hii, Mpende jirani yako kama nafsi yako. Hakuna amri nyingine iliyo
kuu kuliko hizi,” Mk 12:31
“Naye
Yesu, alipoona kwamba amejibu kwa busara, alimwambia, Wewe hu mbali na ufalme
wa Mungu. Wala hakuthubutu mtu kumsaili neno tena tokea hapo,” Mk 12:34
TAFAKARI: “Kwa
ajili ya hilo nastahimili mambo yote, kwa ajili ya wateule, ili wao nao waupate
wokovu ule ulio katika Kristo Yesu, pamoja na utukufu wa milele.”
Wapendwa wana wa Mungu, mwanadamu kwa kuumbwa kwake, Mwa 1:27, na
uwepo wake hapa duniani, mara zote hutafuta maana ya maisha yake. Hufanya hivyo
si kwa bahati mbaya, au udadisi fulani, bali kama alivyo, mwanadamu ni tokeo la
historia yake na kijamii na jamii
anayoishi leo na sasa. Hivyo, mwanadamu huyu hapo alipo kadiri ya imani na
maadili yake, hakosi kuifikiria kesho ambayo bado kuiishi akiwa na matumaini
kuwa ipo. Na kama ni Mkristo achoki kuyafikiria maisha yale ya umilele na
hukumu yake ya mwisho, kwa sababu anatambua wazi maisha ya hapa nduniani ni
jukumu la muda mfupi tu. “Kwa
maana imetupasa sisi sote kudhihirishwa mbele ya kiti cha hukumu cha Kristo,
ili kila mtu apokee ijara ya mambo aliyotenda kwa mwili, kadiri alivyotenda,
kwamba ni mema au mabaya,” 2Kor 5:10
Kwa hali na mtazamo
huo, mwanadamu hakosi kutafuta maana ya maisha yake. Utafutaji wa maana juu ya
maisha yake humpa pia maana ya mahangaiko na mateso yake. Katika hali hii Mtume
Paulo anasema, “Nami katika hiyo nimeteswa
hata kufungwa kama mtenda mabaya; lakini neno la Mungu halifungwi,” 2Tim 2:9.
Neno la Mungu ni hai, na pia ni uhai. Tulisadiki neno kama alivyofanya Diwani
yule wa Kana ya Galilaya, Yoh 4:46, mwanaye aliyekuwa hajiwezi, naye akapata
uponyaji. “Yesu akamwambia,
Enenda; mwanao yu hai. Mtu yule akalisadiki lile neno aliloambiwa na Yesu, naye
akashika njia,” Yoh 4:50
Maisha yakikosa maana, binadamu hujikabidhi katika ‘ovu’ lolote lile
bila kujali chochote kwa sababu maisha yake kesha yahesabu kuwa si chochote.
Huku ni kutaka tamaa pale tunapokosa tumaini la kweli. Ila kwa upande wa Mtume
Paulo ni tofauti. Yesu Kristo ndiye nahodha wa maisha yake, na kwake, yaani kwa
Kristo, maisha yake (Paulo Mtume) yamepata maana halisi. “Kwa ajili ya hilo
nastahimili mambo yote, kwa ajili ya wateule, ili wao nao waupate wokovu ule
ulio katika Kristo Yesu, pamoja na utukufu wa milele. Ni neno la kuaminiwa. Kwa maana, Kama
tukifa pamoja naye, tutaishi pamoja naye pia; Kama
tukistahimili, tutamiliki pamoja naye; Kama tukimkana yeye, yeye naye atatukana
sisi; Kama sisi hatuamini, yeye
hudumu wa kuaminiwa. Kwa maana hawezi kujikana mwenyewe,” 2Tim 2:10-13. Huyu ndiye
Kristo ambaye kwake kama wafuasi wake, kuna tumaini la kweli.
Hata pamoja na ukweli
huo, “Jitahidi kujionyesha kuwa umekubaliwa
na Mungu, mtenda kazi asiye na sababu ya kutahayari, ukitumia kwa halali neno
la kweli,” 2Tim 2:15. Ndani na katika Yesu Kristo hakuna sababu ya kuishi kwa
hofu. Mmoja wa waandishi ili kupata uhakika na kuiondoa hofu yake, anamuuliza
Yesu, “Katika amri zote ni ipi iliyo ya kwanza?” Mk 12:28b.
Swali hili ni la msingi kabisa, ingawa yawezekena muuliza swali alifanya hivyo
ili kujiridhisha na pengine kujua ameegemea upande upi. Ni vizuri pia
kujihakiki kama kweli unatembea njia iliyo salama. “Yesu
akamjibu, Ya kwanza ndiyo hii, Sikia, Israeli, Bwana Mungu wetu ni Bwana mmoja; nawe mpende Bwana Mungu wako kwa moyo
wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa akili zako zote, na kwa nguvu zako
zote,” Mk 12:29-30. Jibu la Yesu linamkumbusha muuliza swali kuwa yeye ni tokeo
la historia yake, na hivyo historia hiyo ina nguvu katika maisha yake.
Yesu
hakuishia hapo tu, bali anaenda mbele zaidi ile muuliza swali afahamu vizuri
ubinadamu wake. Maisha huwa na maana unapoishi tumaini la kweli, yaani,
kuelekea ule umilele ambalo ndilo lengo kwa yeyote yule aishie duniani hapa.
Naye Yesu anamwambia, “Na ya pili ndiyo hii, Mpende jirani yako kama nafsi
yako. Hakuna amri nyingine iliyo kuu kuliko hizi,” Mk 12:31. Kumbe mimi na wewe
siyo tu tokeo la historia yetu, bali pia masisha ya kijamii tunayoishi kila
siku. Hapa duniani hatuishi kama visiwa. Mahusiano yetu (ya haki, kweli, usawa,
upendo) na wenzetu utujenga kimaadili na imani, na hivyo kutufanya kukua
kiroho. Huu pia ni mtihani muhimu sana wa kujipatia taji lile la gharama kupita
mataji yote, yaani, utakatifu wako. Bila hili kuiona Mbingu na Mungu ni ndoto!
Kuhusu historia yake, na mahusiano yake na wenzake, mwaandishi yule alijibu
vyema, Mk 12:32-33. “Naye Yesu, alipoona kwamba amejibu kwa busara, alimwambia,
Wewe hu mbali na ufalme wa Mungu. Wala hakuthubutu mtu kumsaili neno tena tokea
hapo,” Mk 12:34. Ndugu yangu, wewe na mimi
tuutafakari umbali wetu na ufalme ule wa Mungu.
Tumsifu Yesu Kristo!
“Naye
Yesu, alipoona kwamba amejibu kwa busara, alimwambia, Wewe hu mbali na ufalme
wa Mungu. Wala hakuthubutu mtu kumsaili neno tena tokea hapo,” Mk 12:34
Tusali:-Ee Yesu Mwema,
nijalie ufahamu wa kuona maana ya maisha yangu kila siku licha ya changamoto
nazokumbana nazo kila kukicha. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario