sábado, 28 de mayo de 2016

TAFAKARI: JUMAMOSI WIKI YA 8 YA MWAKA-C

JUMAMOSI WIKI YA 8 YA MWAKA-C
Somo: Yud 17, 20-25
Zab: 63:2, 3-4, 5-6
Injili: Mk 11:27-33
Nukuu:
Bali ninyi, wapenzi, mkijijenga juu ya imani yenu iliyo takatifu sana, na kuomba katika Roho Mtakatifu, jilindeni katika upendo wa Mungu, huku mkingojea rehema ya Bwana wetu Yesu Kristo, hata mpate uzima wa milele,” Yud 20-21

Wahurumieni wengine walio na shaka, na wengine waokoeni kwa kuwanyakua katika moto; na wengine wahurumieni kwa hofu, mkilichukia hata vazi lililotiwa uchafu na mwili,” Yud 22-23

Yeye aliye Mungu pekee, Mwokozi wetu kwa Yesu Kristo Bwana wetu; utukufu una yeye, na ukuu, na uwezo, na nguvu, tangu milele, na sasa, na hata milele. Amina,” Yud 25

Ubatizo wa Yohana ulitoka mbinguni, au kwa wanadamu? Nijibuni. Wakasemezana wao kwa wao, wakisema, Kama tukisema, Ulitoka mbinguni, atasema, Mbona, basi, hamkumwamini?” Mk 11:30-31 

Ila tukisema, Ulitoka kwa wanadamu, -- waliogopa watu; maana watu wote walimwona Yohana kuwa nabii halisi,” Mk 11:32

Wakamjibu Yesu, wakasema, Hatujui. Yesu akawaambia, Wala mimi siwaambii ninyi ni kwa mamlaka gani nayatenda haya,” Mk 11:33

TAFAKARI: “Kisukumacho maisha yako ndicho kisemacho kuhusu mwisho wako.”

Wapendwa wana wa Mungu, “kile kisukumacho maisha yako ndicho kisemacho kuhusu mwisho wako.” Kwa tafakari ya leo kadiri ya masomo yetu, nitawashirikisha misukumo mitatu; hatia, chuki, upendo. Ndugu yangu tunayesafiri sote katika tafakari hii,  wapo baadhi yetu kwa kujua au kutokujua maisha yao yanasukumwa na ‘hatia,’ na mara zote hata wakiwa kwenye mazungumzo ya kawaidi huisi kutuhumiwa, au kuwatuhumu wengine. Tokeo la hali hii ni jereha la dhambi. Na kama mtu akifanya dhambi, na kutenda mambo hayo mojawapo ambayo Bwana alizuilia yasifanywe, ajapokuwa hakuyajua, ni mwenye hatia vivyo, naye atachukua uovu wake,” Law 5:17. Kutoka kwenye hali hii ya ‘hatia’ yakupasa kujisalimisha au kuirejea huruama ya Mungu ambayo ipo wakati wowote kupitia Sakramenti ya Upatanisho. Ni vyema nikaipatanisha nafsi yangu katika mgawanyiko wake, nafsi yangu na yule niliyemtenda au kutendwa naye, nafsi yangu na Mungu, na pia nafsi yangu na mazingira sababishi au ninayoyaishi.

Kama hiyo haitoshi, wapo pia baadhi yetu maisha yao yanasukumwa na roho ya chuki na kutokupokea chochote kizuri kutoka kwa mwingine. Hupoteza muda mwingi kwa kutafuta sababu za kuhalalisha uovu wako. Hawa ni wale ambao wapo muda wote kutafuta ugomvi, kujirundikia sababu za kuumiza na hata kufanya kisasi hata pale pasipo sababu ya kufanya hivyo. Bali macho yako na moyo wako hauna utakalo ila kutamani, na kumwaga damu isiyo na hatia, na kudhulumu, na kutenda jeuri,” Yer 22:17. Mtu wa mtindo huu ni mjeruhiwa wa yote matatu: Mwili, Nafsi, na Roho. Kila aguswapo kwa kila moja ya hayo matatu, ni maumivu makubwa. Maumivu haya huyabeba wao wenyewe na wakati mwingine kuyatwika kwa wengine. Hakika mwisho wa mtu wa mtazamo na msukumo huu hauwezi kuwa mzuri.

Njia salama na sahihi ya kufuata ni kuyafanya maisha yako kusukumwa na pendo. Na kwa ajili ya hayo yote, nikatia moyo wangu katika kuyatafuta-tafuta haya; ya kuwa wenye haki, na wenye hekima, pamoja na matendo yao yote, wamo mkononi mwa Mungu; kwamba ni pendo au kwamba ni chuki, mwanadamu hajui; mambo yote yawapita,” Mhu 9:1. Huo ndio wito wa kila mwenye hofu ya Mungu. Ndugu yangu, kwa kuumbwa kwako ni tokeo la upendo wa Mungu kwako. Upo kwa sababu ya Upendo na Utukufu wa Mungu. Kupenda na kusukumwa na upendo ni amri na siyo hiari. Kusukumwa na pendo hutufanya rafiki wa amri za Mungu na amri hizo hujeuka na kutokuwa mzigo kwetu. Huku ndiko kuzishika amri za Mungu na kukaa katika pendo la Kristo. Mkizishika amri zangu, mtakaa katika pendo langu; kama vile mimi nilivyozishika amri za Baba yangu na kukaa katika pendo lake,” Yoh 15:10. Hapa kuna usalama na amani.

Kutokana na kusukumwa na hatia na chuki, Wayahudi hawakuwa tayari kupokea pendo la Mungu na hata kusikia mafundisho ya Kristo kwani walisutwa nafsi zao. Wayahudi hawakuwa tayari kuachilia hatia zao na chuki na kuukumbatia upendo wa Mungu Baba kupitia Mwanaye Mpenzi Yesu Kristo katika neno lile la uzima. Leo tuliompokea Kristo katika maisha yetu hatupaswi kusukumwa na hatia, wala chuki. Bali ninyi, wapenzi, mkijijenga juu ya imani yenu iliyo takatifu sana, na kuomba katika Roho Mtakatifu, jilindeni katika upendo wa Mungu, huku mkingojea rehema ya Bwana wetu Yesu Kristo, hata mpate uzima wa milele,” Yud 20-21. Ndugu yangu, hata kama ukifaulu kwa kiwango cha juu kabisa cha ‘hatia au ‘chuki,’ tokeo lake halina uzima wa milele.

Wayahudi wapo tayari kuukosa uzima wa milele kwa kuruhusu mwendelezo wa chuki na hatia. Wakuu wa makuhani, Waandishi, na Wazee wanamuundia zogo Yesu ili wamtie hatiani ‘kwa kutaka kujua mamlaka aliyokuwa nayo kwa yale yote aliyokuwa akiyafanya.’ Tuelewe kwamba yote aliyokuwa akiyafanya Kristo ulikuwa ni upendo wa Mungu. Kristo kamwe hakuyafanya hayo kwa lengo la kujiinua wala kujitanguliza kwa sababu Yeye-Yesu kama Mungu, hakuwa na sababu ya kufanya hivyo. Hapo mwanzo kulikuwako Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu. Vyote vilifanyika kwa huyo; wala pasipo yeye hakikufanyika cho chote kilichofanyika,” Yoh 1:1,3. Kuwafanya waelewa ukweli huu vizuri, na kabla ya kuwajibu, Yesu anawauliza, Ubatizo wa Yohana ulitoka mbinguni, au kwa wanadamu? Nijibuni. Wakasemezana wao kwa wao, wakisema, Kama tukisema, Ulitoka mbinguni, atasema, Mbona, basi, hamkumwamini?” Mk 11:30-31. Tunaweza kuona hapa ukubwa wa kiburi cha watu hawa.

Bado waliendelea kuzihoji nafsi zao. Ila tukisema, Ulitoka kwa wanadamu, -- waliogopa watu; maana watu wote walimwona Yohana kuwa nabii halisi,” Mk 11:32. Hata hivyo kwa kuujua ukweli juu ya Yesu Kristo wakaamua kufa na tai zao shingoni. Wakamjibu Yesu, wakasema, Hatujui. Yesu akawaambia, Wala mimi siwaambii ninyi ni kwa mamlaka gani nayatenda haya,” Mk 11:33. Yesu hakuwa na sababu ya kusema zaidi au kufafanua zaidi kwani ujumbe ulishawafikia. Wakuu wa makuhani, Waandishi, na Wazee hawapendi kabisa kuupokea ukweli huu. Wamejawa hofu na mashaka juu ya hatma yao na hasa wakiziangalia nafasi na ubinafsi wao. Kilele cha kweli hii ni kuinuliwa kwake Yesu pale msalabani. Hakika hapa wataijua kweli.  “Basi Yesu akawaambia, Mtakapokuwa mmekwisha kumwinua Mwana wa Adamu, ndipo mtakapofahamu ya kuwa mimi ndiye; na ya kuwa sifanyi neno kwa nafsi yangu, ila kama Baba alivyonifundisha ndivyo ninenavyo,” Yoh 8:28.

Wapendwa wana wa Mungu, pendo la kweli hutusogeza karibu na shida na mahangaiko ya watu. Pendo hili ndilo Kristo alilotuombea kabla ya kujongea kikombe kile cha mateso. Yesu anasali, Nami naliwajulisha jina lako, tena nitawajulisha hilo; ili pendo lile ulilonipenda mimi liwe ndani yao, nami niwe ndani yao,” Yoh 17:26. Upendo huu usukuma ndani yetu moyo wa huruma kwa wengine na kujitoa kwa ajili ya mahangaiko yao. Kwa pendo la udugu, mpendane ninyi kwa ninyi; kwa heshima mkiwatanguliza wenzenu,” Rum 12:10. Na kwa kujali huko ndugu zangu, Wahurumieni wengine walio na shaka, na wengine waokoeni kwa kuwanyakua katika moto; na wengine wahurumieni kwa hofu, mkilichukia hata vazi lililotiwa uchafu na mwili,” Yud 22-23.

Kwenye upendo wa kweli hakuna hofu na pendo halina hofu. Katika pendo hamna hofu; lakini pendo lililo kamili huitupa nje hofu, kwa maana hofu ina adhabu; na mwenye hofu hakukamilishwa katika pendo,” 1Yoh 4:18. Kristo ndiye ndiye kiu yetu na kamilisho letu katika pendo la kweli tukaapo ndani na katika Yeye. Kama vile Baba alivyonipenda mimi, nami nilivyowapenda ninyi, kaeni katika pendo langu,” Yoh 15:9. Kwa Kristo kuna usalama wa kweli na furaha isiyokipimo. Yeye aliye Mungu pekee, Mwokozi wetu kwa Yesu Kristo Bwana wetu; utukufu una yeye, na ukuu, na uwezo, na nguvu, tangu milele, na sasa, na hata milele. Amina,” Yud 25. Ndugu yangu kama kuna kitu cha thamani na unapaswa kuwa nacho, tafuta na jenga uhusiano mzuri na Kristo Yesu.

Tumsifu Yesu Kristo!

Yeye aliye Mungu pekee, Mwokozi wetu kwa Yesu Kristo Bwana wetu; utukufu una yeye, na ukuu, na uwezo, na nguvu, tangu milele, na sasa, na hata milele. Amina,” Yud 25


Tusali:-Ee Yesu na Mwokozi wangu, uliyekubali kufa kifo cho aibu pale msalabani kwa kunipenda upeo, yaumbe upya maisha yangu, na kwa uchache wa siku zangu hapa duniani, maisha yangu yasukumwe na upendo wako wa kweli.

No hay comentarios:

Publicar un comentario