ALHAMISI WIKI YA 8 YA MWAKA-C
Somo: 1Pet 2:2-5, 9-12
Zab: 100:2, 3, 4, 5
Injili: Mk 10:46-52
Nukuu:
“Mmwendee yeye, jiwe
lililo hai, lililokataliwa na wanadamu, bali kwa Mungu ni teule, lenye
heshima,” 1Pet 2:4
“Bali ninyi ni
mzao mteule, ukuhani wa kifalme, taifa takatifu, watu wa milki ya Mungu, mpate
kuzitangaza fadhili zake yeye aliyewaita mtoke gizani mkaingie katika nuru yake
ya ajabu,” 1Pet 2:9
“Wapenzi,
nawasihi kama wapitaji na wasafiri, ziepukeni tamaa za mwili zipiganazo na
roho,” 1Pet 2:11
“Naye
aliposikia ya kwamba ni Yesu Mnazareti, alianza kupaza sauti yake, na kusema,
Mwana wa Daudi, Yesu, unirehemu,” Mk 10:47
“Yesu
akamjibu, akamwambia, Wataka nikufanyie nini? Yule kipofu akamwambia, Mwalimu
wangu, nataka nipate kuona,” Mk 10:51
TAFAKARI: “Wakata nikufanyie nini?”
Wapendwa wana wa Mungu, tupo wengi akina Bartimayo, mwana wa Timayo,
Yule mwombaji kipofu wa Yeriko, Mk 10:46. Hakika kilio chake Bartimayo “Mwana
wa Daudi, Yesu, unirehemu” Mk 10:47, alipousikia ule msafara wa Yesu ukipita,
kinaonyesha ni kwa namna gani alivyokuwa amechoshwa na hali yake ile. Licha ya
watu kumzuia, Yesu anasikia kilio kile na kutaka kumwona. Ndugu yangu
tunayesafiri sote katika tafakari hii, ni wazi kuna nyakati nyingine unakumbwa
na matatizo na unapoomba wajisikia kama vile sala yako haisikiki kabisa. Ukweli
ni kwamba Yesu Mwana wa Mungu aliye hai anasikia kilio chako, hivyo usiache
kumwita. Hata Bartimayo licha ya kusongwa na kundi na msafara ule hakukoma
kumwita Yesu. Je, unajua utakacho akufanyie Yesu atakapokuuliza?
Yesu kabla ya kumpa uponyaji Bartimayo, anamuuliza, “Wataka
nikufanyie nini? Yule kipofu akamwambia, Mwalimu wangu, nataka nipate kuona,”
Mk 10:51. Yesu bila kukawia kwa kuiona imani yake Bartimayo pasipo shaka yoyote
anajibu ombi lake hapo hapo nakumwambia, Enenda
zako, imani yako imekuponya. Mara akapata kuona; akamfuata njiani,” Mk 10:52.
Kwa uponyaji huu wa moja kwa moja, Bartimayo siyo tu anapata kuona kutoka upofu
wake, bali anaona njia sahihi ya kuifuata na yenye usalama, “mara akapata
kuona, akamfuata njiani.” Bartimayo anatufundisha na kutukumbusha fundisho la
Yesu, kwamba, ‘Yeye ndiye njia, na ukweli, na uzima,’ Yoh 14:6.
Unapopata kuona njia
kwa macho ya kiroho ni sawa na kuzaliwa upya. Ni kushibishwa nuru ile iangazayo
katika kweli halisi. Ni msukumo wa neema ndani yako unaoangaza na kuyaona yale
yaliyo juu ya uwezo wako kiakili kama wanadamu. Neema ya Mungu ndani na kwa
njia yake Yesu Kristo Mwana wa Mungu aliye hai, utuwezesha na kutuongoza kuyafikia
yale Mungu anayotamani sote siku moja kuyafikia. Hivyo ndugu yangu, “Mmwendee
yeye, jiwe lililo hai, lililokataliwa na wanadamu, bali kwa Mungu ni teule,
lenye heshima,” 1Pet 2:4. Jiwe hili ndilo Kristo Yesu Mwana wa Mungu aliye hai.
Kwa Sakramenti ya Ubatizo
miili yetu inakuwa Hekalu la Roho Mtakatifu, na viungo wa Kristo kama Kanisa.
Kwa Sakramenti ya Ubatizo tunashirikishwa ukuhani wa kawaida wa Yesu Kristo. “Ninyi
nanyi, kama mawe yaliyo hai, mmejengwa mwe nyumba ya Roho, ukuhani mtakatifu,
mtoe dhabihu za roho, zinazokubaliwa na Mungu, kwa njia ya Yesu Kristo,” 1Pet
2:5. Licha ya kuwa makuhani wa kawaida wa Kristo, kwa Sakramenti ya Ubatizo, tu
wa milki ya Mungu katika nuru ya ajabu-wana wa Mungu aliye Mtakatifu. “Bali
ninyi ni mzao mteule, ukuhani wa kifalme, taifa takatifu, watu wa milki ya
Mungu, mpate kuzitangaza fadhili zake yeye aliyewaita mtoke gizani mkaingie
katika nuru yake ya ajabu,” 1Pet 2:9. Tu wana wa nuru na kwa sababu hiyo ndicho
alichokijia Yesu. “Mimi nimekuja ili niwe nuru ya ulimwengu, ili kila
mtu aniaminiye mimi asikae gizani,” Yoh 12:46.
Kuishi
katika nuru hii aliyotuletea Yesu Kristo ni kutenda na kupenda tunda la Roho. “Tunda
la Roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, upole, kiasi; juu ya mambo kama hayo
hakuna sheria,” Gal 5:22-23. Kuishi tunda la Roho kunatuhesabia haki na Mungu
mwenyewe kuwa taifa lake na kupata rehema zake. “Ninyi
mliokuwa kwanza si taifa, bali sasa ni taifa la Mungu; mliokuwa hamkupata
rehema, bali sasa mmepata rehema,” 1Pet 2:10. Hivyo tukielewa hapa duniani tu
wapitaji na wasafiri, kuendelea kuneemeka na rehema hizi za Mungu kama sehemu
ya maandalizi ya maisha yale ya umilele, yakupasa wewe na mimi kuziepuka tamaa
za mwili zinazopingana na tunda la Roho. “Wapenzi, nawasihi kama wapitaji na wasafiri,
ziepukeni tamaa za mwili zipiganazo na roho,” 1Pet 2:11. Matendo ya mwili na
tamaa zake utuweka kando na nuru ya Mungu, na kwayo hakuna Mbingu. “Basi matendo ya mwili ni dhahiri, ndiyo haya,
uasherati, uchafu, ufisadi, ibada
ya sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, faraka, uzushi, husuda, ulevi, ulafi, na mambo
yanayofanana na hayo, katika hayo nawaambia mapema, kama nilivyokwisha
kuwaambia, ya kwamba watu watendao mambo ya jinsi hiyo hawataurithi ufalme wa
Mungu,” Gal 5:19-21. Ndugu yangu, tafakari na chukua hatua!
Mwaliko wa Kristo
kwangu na kwako leo ni kwamba tuwe na mwenendo mzuri, na tusomwe kwa matendo
yetu mazuri ili watenda mabaya wabadilike na kumtukuza Mungu. Wapendwa katika Kristo, “Mwe na mwenendo mzuri kati ya Mataifa, ili,
iwapo huwasingizia kuwa watenda mabaya, wayatazamapo matendo yenu mazuri,
wamtukuze Mungu siku ya kujiliwa,” 1Pet 2:12. Huku ndiko kuusulibisha mwili
ndani na katika Kristo Yesu kama asemavyo Mtume Paulo, “Na
hao walio wa Kristo Yesu wameusulibisha mwili pamoja na mawazo yake mabaya na
tamaa zake,” Gal 5:24. Tu katika yote ndani na katika Kristo Yesu. Je, wauonea
huruma Mwili wako na mwisho kuiangamiza Nafsi na Roho?
Tumsifu Yesu Kristo!
“Wapenzi,
nawasihi kama wapitaji na wasafiri, ziepukeni tamaa za mwili zipiganazo na
roho,” 1Pet 2:11
Tusali:-Ee Yesu, Mwana wa Mungu aliye hai,
niwezeshe niweze kuona nuru yako yenye kuangaza umilele wa maisha yetu. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario