JUMAPILI
YA SABA YA PASAKA-C
SHEREHE
YA KUPAA BWANA
Somo
I: Mdo 1:1-11
Zab:
47:1-2, 5-6, 7-8,
Somo
II: Efe 1:17-23
Injili:
Mt 28:16-20
Injili:
Mk 16:15-20
Injili: Lk 24:46-53
Nukuu:
“hata
siku ile alipochukuliwa juu, alipokuwa amekwisha kuwaagiza kwa Roho Mtakatifu
wale mitume aliowachagua; wale aliowadhihirishia nafsi yake, kwa
dalili nyingi, baada ya kuteswa kwake, ya kwamba yu hai, akiwatokea muda wa
siku arobaini, na kuyanena mambo yaliyouhusu ufalme wa Mungu,” Mdo 1:2-3
“Akawaambia,
Si kazi yenu kujua nyakati wala majira, Baba aliyoyaweka katika mamlaka yake
mwenyewe,” Mdo 1:7
“Lakini
mtapokea nguvu, akiisha kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu; nanyi mtakuwa
mashahidi wangu katika Yerusalemu, na katika Uyahudi wote, na Samaria, na hata
mwisho wa nchi,” Mdo 1:8
“Enyi
watu wa Galilaya, mbona mmesimama mkitazama mbinguni? Huyu Yesu aliyechukuliwa
kutoka kwenu kwenda juu mbinguni, atakuja jinsi iyo hiyo mlivyomwona akienda
zake mbinguni,” Mdo 1:11
“Mungu
wa Bwana wetu Yesu Kristo, Baba wa utukufu, awape ninyi roho ya hekima na ya
ufunuo katika kumjua yeye,” Efe 1:17
“akavitia
vitu vyote chini ya miguu yake, akamweka awe kichwa juu ya vitu vyote kwa ajili
ya kanisa; ambalo ndilo mwili wake, ukamilifu wake anayekamilika kwa vyote
katika vyote,” Mdo 1:22-23
“Yesu
akaja kwao, akasema nao, akawaambia, Nimepewa mamlaka yote mbinguni na
duniani,” Mt 28:18
“Basi,
enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba,
na Mwana, na Roho Mtakatifu; na
kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi; na tazama, mimi nipo pamoja
nanyi siku zote, hata ukamilifu wa dahari,” Mt 28:19-20
Akawaambia,
Enendeni ulimwenguni mwote, mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe. Aaminiye na kubatizwa ataokoka;
asiyeamini, atahukumiwa,” Mk 16:15-16
“Na
ishara hizi zitafuatana na hao waaminio; kwa jina langu watatoa pepo; watasema
kwa lugha mpya; watashika nyoka;
hata wakinywa kitu cha kufisha, hakitawadhuru kabisa; wataweka mikono yao juu
ya wagonjwa, nao watapata afya,” Mk 16:17-18
“Na
tazama, nawaletea juu yenu ahadi ya Baba yangu; lakini kaeni humu mjini, hata
mvikwe uwezo utokao juu,” Lk 24:49
“Akawaongoza
mpaka Bethania, akainua mikono yake akawabariki,” Lk 24:50
TAFAKARI:
“Bwana Kapaa kwenda kwa Baba Mbinguni; katuachia agizo: Enendeni ulimwenguni mwote, mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe. Aaminiye na kubatizwa ataokoka;
asiyeamini, atahukumiwa”
Wapendwa wana wa Mungu,
Leo Mama Kanisa anafanya Sherehe ya Kupaa Bwana wetu Yesu Kristo Mbinguni. Somo
la kwanza na la pili husomwa mwa miaka yote mitatu ya Kanisa kadiri ya
liturjia. Hivyo ikiwa leo tupo mwaka “C” wa Kanisa, tutasoma Habari Njema ya
Bwana wetu Yesu Kristo kama ilivyoandikwa na Mwinjili Luka. Mwaka “B” wa Kanisa
tulisoma kama ilivyoandikwa na Mwinjili Marko, na Mwaka “A” wa Kanisa tutasoma
Habari Njema hiyo ya Yesu Kristo kama ilivyoandikwa na Mwinjili Mathayo. Hivyo
ndugu yangu tunayesafiri sote katika tafakari hii, kupaa huku mbinguni ni moja
ya sharti ya kuletewa Roho Mtakatifu kama mshauri wetu. Kupaa kwa Yesu Mbinguni
kunatuwajibisha kila mmoja wetu, yaani kila mbatizwa, na Kanisa kwa ujumla wake
kama Sakramenti ya wokovu wetu. Ni Kanisa katika maana hii, “akavitia
vitu vyote chini ya miguu yake, akamweka awe kichwa juu ya vitu vyote kwa ajili
ya kanisa; ambalo ndilo mwili wake, ukamilifu wake anayekamilika kwa vyote
katika vyote,” Mdo 1:22-23
Hivyo leo tutafakari
kwa undani wajubu huu tulioachiwa na Kristo na tuufanye kweli tukitambua jambo
hili si la kupita tu, bali li hai kila siku ya maisha yetu kama sehemu muhimu
ya ufuasi wetu kwa Kristo. Hivyo basi wazo kuu na tafakari yetu leo ni kwamba,
“Bwana Kapaa kwenda kwa Baba Mbinguni; katuachia agizo: Enendeni ulimwenguni mwote, mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe. Aaminiye na kubatizwa ataokoka;
asiyeamini, atahukumiwa.”
Ndugu yangu, katika
maisha ya Bwana wetu Yesu Kristo kuna mambo makuu matatu yanajionyesha: La
kwanza kabisa, yeye akiwa ndiyo Habari njema ya mwokovu wetu, jambo hili
linakuwa ndicho kipaumbele chake cha kwanza na kielelezo cha maisha yake.
Kuhubiri habari njema za Ufalme wa mbinguni. "Wakati umetimia, na ufalme
wa Mungu umekaribia; tubuni, na kuiamini Injili," Mk 1:15. Hii ndiyo
ajenda mzito na mahususi Yesu aliyowaachia wanafunzi na Kanisa kwa upana wake
kabla ya kupaa mbinguni akisema, “Enendeni
ulimwenguni mwote, mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe. Aaminiye na kubatizwa ataokoka;
asiyeamini, atahukumiwa,” Mk 16:15-16. Ujumbe huu mahususi wa ufalme wa Mungu,
unaambatana na hukumu kwa Yule asiyeamini. Wajibu wetu, yaani kwa kila
mbatizwa, na Kanisa kwa ujumla wake ni kulihubiri neno la Mungu bila kukoma.
Mwijili Mathayo kalihusisha tendo hili la kuhubiri neno na ufalme wa Mungu na
Sakramenti ya Ubatizo. Maana yake, siyo tu kulihubiri neno la Mungu, bali na
kuwavuta watu kwa Mungu na kuuonja upendo na furaha hiyo. "Basi,
enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba,
na Mwana, na Roho Mtakatifu; na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru
ninyi" Mt 28:19-20.
Jambo la pili lilikuwa
kuwachagua wanafunzi wake ikiwa ndiyo mwendelezo wa "Habari njema"
kizazi na hata kizazi hadi mwisho wa nyakati. Yesu katika hili anatoa ahadi kwa
wanafunzi wake, "Sitawaacha ninyi yatima; naja kwenu," Yoh 14:18.
Na jambo la tatu
lilikuwa ni kulitakasa hekalu. Hekali libakie kuwa ni nyumba ya sala. Tunaona
mtafaruku wa Yesu hekaluni na wale wavunja fedha. Na hasa pale alipojibu na
kusema," livunjeni hekalu hili, nami katika siku tatu
nitalisimamisha," Yoh 2:19. Kwa naama ya ndani zaidi, "Hekalu"
ilimaanisha mwili wake mwenyewe na pia ni mwili wa kila mbatizwa. "Lakini
yeye alinena habari za hekalu la mwili wake," Yoh 2:21. Mtume Paulo anatuambia miili yetu
ni hekalu la Roho Mtakatifu. "Hamjui ya kuwa ninyi mmekuwa hekalu la
Mungu, na ya kuwa Roho wa Mungu anakaa ndani yenu?" 1Kor 3:16.
Ni kwa mtazamo huu,
Mtume Paulo anasema 'ole wake asipoihubiri njili,' 1Kor 9:16, na ni pale pia
Yesu anawakumbusha umati waliomjia kuwa yampasa kwenda sehemu nyingine pia kwa
ajili ya Habari njema za ufalme wa Mungu. "Akawaambia, "twendeni
mahali pengine, mpaka vijiji vilivyo karibu, nipate kuhubiri huko nako; maana
kwa HIYO NALITOKEA," Mk 1:38. Ndugu yangu ni kwa maana hiyo na sababu hiyo
"YESU KUTOKEA" kwetu-kuhubiri Habari njema za ufalme wa Mungu na
wokovu wetu. Tusipolifanya jambo hili kuwa ajenda muhimu kwa kila mmoja kama
mbatizwa, na kwa Kanisa kama chombo cha kutuwezesha kuelekea na kuufikia uzima
na utakatifu wetu, basi maisha yetu yatakuwa kama upepo tu hapa duniani. Ndugu
yangu, jambo la kujiuliza; nini umuhimu wa utume wako? Pili, nini hasa gharama
za kutimiza utume wako? Tuanze na hilo la kwanza. Kuna mambo sita muhimu kuhusu
umuhimu wa utume wako.
1.
Utume wako ni mwendelezo wa utume wa Yesu hapa duniani.
Wapendwa, kama wafuasi
wake, tunapaswa kuendeleza kile alichoanzisha Yesu. Yesu hatuiti tu kuja kwake,
lakini kwenda kwa ajili yake. Utume wako ni wa muhimu sana kiasi kwamba Yesu anauzungumzia
mara tano, katika njia tofauti tano;
-"Basi, enendeni,
mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana,
na Roho Mtakatifu; na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi; na
tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote, hata ukamilifu wa dahari," Mt
28:19-20.
Hili ndilo Agizo la
Yesu;
-"Akawaambia,
Enendeni ulimwenguni mwote, mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe," Mk 16:15
-"na kwamba
mataifa yote watahubiriwa kwa jina lake habari ya toba na ondoleo la dhambi,
kuanza tangu Yerusalemu," Lk 24:47
-"Basi Yesu
akawaambia tena, Amani iwe kwenu; kama Baba alivyonituma mimi, mimi nami
nawapeleka ninyi," Yoh 20:21
-"Lakini mtapokea
nguvu, akiisha kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu; nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu,
na katika Uyahudi wote, na Samaria, na hata mwisho wa nchi," Mate 1:8
Ndugu yangu, maagizo
hayo matano, ni kama Yesu anatuambia hivi, "hakika nataka ninyi mwelewe
jambo hili!" Agizo kuu la Yesu (Mt 28:19-20), amepewa kila mfuasi wa Yesu,
siyo la wachungaji "makleri" na wamishenari peke yao. Hili ni agizo
kutoka kwa Yesu, na si la hiari. Haya maneno ya Yesu siyo "pendekezo
kuu." Ndugu, kama wewe ni sehemu ya jamii ya Mungu, utume wako ni wa
lazima. Kuupuza itakuwa kutotii.
Ndugu, yawezekana
ulikuwa hujui kwamba Mungu anakuwajibisha kwa watu wasiomwamini wanaokuzunguka.
"Nimwambiapo mtu mbaya, Hakika utakufa; wewe usimpe maonyo, wala husemi na
huyo mtu mbaya ili kumwonya, kusudi aache njia yake mbaya na kujiokoa roho
yake; mtu yule mbaya atakufa katika uovu wake; lakini damu yake nitaitaka
mikononi mwako," Eze 3:18. Ndugu yangu, sina lengo la kukuogofya, ila
ndiyo ukweli wa Mungu. Wewe ni Mkristo pekee ambaye baadhi ya watu
watakufahamu, na utume wako ni kuwaambia Habari za Yesu.
2.
Utume wako ni upendeleo wa ajabu.
Ndugu yangu, ingawa ni
wajibu mkubwa, pia ni heshima kubwa kutumiwa na Mungu. Mtume Paulo anasema,
"Lakini vyote pia vyatokana na Mungu, aliyetupatanisha sisi na nafsi yake
kwa Kristo, naye alitupa huduma ya upatanisho," 2Kor 5:18. Kwa maana hiyo,
utume wako unahusisha upendeleo wa aina mbili: kumtumikia Mungu na
kumwakilisha. Tunakuwa na ubia na Mungu katika kujenga ufalme wake. Eneo hili
tunahitaji sana hekima ya Mungu na mwongozo wa Roho wake Mtakatifu. Yote
yanawezekana tunapojisalimisha kwake, ndani na katika Yeye. Hivyo, Yesu
anatuahidia jambo hili anaposema, “Mungu wa Bwana wetu Yesu Kristo,
Baba wa utukufu, awape ninyi roho ya hekima na ya ufunuo katika kumjua yeye,”
Efe 1:17. Hakuna woga wala hofu tuyafanyapo Mapenzi ya Mungu kwani yote hayo si
kwa nguvu zetu wenyewe, bali kwa mkono wa Mungu kwa sababu yote ni kwa ajili ya
ufalme wake aliyotuandalia.
3.
Kuwaambia wengine wanavyoweza kupata uzima wa milele ndiyo jambo kubwa
unaloweza kuwatendea
Ndugu yangu, kama
jirani yako angeugua KANSA au UKIMWI na ukawa unafahamu tiba, lingekuwa kosa
kubwa kutomfahamisha habari hizo za kuokoa maisha. Ni kosa pia kuficha njia ya
msamaha, lengo, amani, na uzima wa milele. Tuna habari kuu kuliko zote duniani,
na kushirikisha wengine ndiyo wema mkubwa kuliko wote unaoweza kumfanyia mtu.
Ndugu yangu, tatizo
moja tulilonalo Wakristo wa muda mfupi ni kwamba tunasahau jinsi tulivyokuwa
hatuna matumaini tulipoishi bila Yesu. Lazima tukumbuke kwamba haijalishi watu
wanaonekana kutosheka na kufanikiwa kiasi gani, bila Yesu hawana matumaini na
wamepotea na pia wanaelekea katika kutengwa na Mungu milele. "Wala hakuna
wokovu katika mwingine awaye yote, kwa maana hapana jina jingine chini ya
mbingu walilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo," Mate 4:12.
Ndugu yangu, kila mtu anamhitaji Yesu.
4.
Utume wako una umuhimu wa milele.
Ndugu yangu, ufanyacho
sasa kitakuwa na matokeo makubwa kwa hatima ya milele ya watu wengine, hivyo
utume wako ni wa muhimu kuliko kazi nyingine yoyote, mafanikio yoyote, au lengo
lolote utakalolifikia katika maisha yako hapa duniani. Matokeo ya utume wako
yatadumu milele; matokea ya kazi yako hayawezi.
Ndugu yangu, hakuna
tena narudia, hakuna Chochote unachofanya kitalingana na kuwasaidia watu
wafanye uhusiano wa milele na Mungu. Ndiyo maana lazima tuwe na juhudi kubwa
katika utume wetu. Yesu anasema, "imetupasa kuzifanya kazi zake yeye
aliyenipeleka maadamu ni mchana, usiku waja asipoweza mtu kufanya kazi,"
Ndugu, ukweli ni kwamba saa inakwenda na maisha yako ya utume yanapita. Anza
utume wako wa kuwafikia wengine sasa! Tutakuwa na muda wa milele wa kufurahi na
wale wote tuliowaleta kwa Yesu, lakini tuna muda mfupi tu wa maisha yetu ili
kuwafikia. Yesu anatuambia leo kwamba katika jambo hili la kujitoa muhanga kwa
ajili yake, litaambatana na ishara nyingi, na kuufichua umungu wake. “Na ishara hizi zitafuatana na hao waaminio; kwa jina
langu watatoa pepo; watasema kwa lugha mpya; watashika
nyoka; hata wakinywa kitu cha kufisha, hakitawadhuru kabisa; wataweka mikono
yao juu ya wagonjwa, nao watapata afya,” Mk 16:17-18
Ndugu, jambo hili
halimaanishi uache kazi yako ili uwe mwinjilisti wa kudumu. Mungu anakutaka
uwashirikishe watu wengine karibu yako Habari njema. Kama mwanafunzi, mama,
mwalimu wa shule, mfanya biashara, au meneja, au chochote unachofanya,
unatakiwa daima kutafuta watu Mungu anaowaweka mbele yako upate kuwashirikisha
Injili. Si lazima kutumia vipaza sauti, bali kwa maisha yako ya kumpendeza
Mungu huongea zaidi. Ni
kutoa ushuhuda wa ukimya "silence witness" na kuwa barua za kusomwa
na wengine. "Ninyi ndinyi barua yetu, iliyoandikwa mioyoni mwetu,
inajulikana na kusomwa na watu wote; mnadhihirishwa kwamba mmekuwa barua ya
Kristo tuliyoikatibu, iliyoandikwa si kwa wino, bali kwa Roho wa Mungu aliye
hai; si katika vibao vya mawe, ila katika vibao ambavyo ni mioyo ya
nyama," 2Kor 3:2-3
5. Utume wako hukupatia umuhimu wa maisha yako.
William James alisema, "Matumizi bora ya maisha
ni kuyatumia kwa kufanya kitu kitakachodumu kuliko maisha yako." Ndugu
yangu, ukweli ni kwamba, ni ufalme wa Mungu tu ndio utadumu milele. Achana na
"viprojekti" vya zima moto! Wakoleze watu Imani. Unacheka!
Kwa sababu hiyo,
tunatakiwa kuishi maisha yanayoongozwa na malengo-maisha ya kuabudu, kuwa na
ushirika, kukua kiroho, huduma, na utume wetu duniani. Matokeo ya shughuli hizi
yatadumu milele. Mipango yetu ya kichungaji ilenge kwenye malengo hayo.
"Viprojekti" vyovyote visivyo lenga mambo hayo ni sawa na kupiga
mashutu kwa bidii kubwa na ustadi mkubwa pasipokuwa na goli.
Ndugu yangu, kama
utashindwa kutimiza utume uliopewa na Mungu hapa duniani, utakuwa umepoteza
maisha Mungu aliyokupa. Mtume Paulo anasema, "Lakini siyahesabu maisha
yangu kuwa kitu cha thamani kwangu kama kuumaliza mwendo wangu na huduma ile
niliyopokea kwa Bwana Yesu, kuishuhudia Habari njema ya neema ya Mungu,"
Mate 20:24
Ndugu yangu, kuna watu
katika sayari hii ambao ni wewe tu unayeweza kuwafikia kwa sababu ya mahali
unapoishi na jinsi Mungu anavyokufinyanga. "Mikono yako ilinifanya
ikanitengeneza, Unifahamishe nikajifunze maagizo yako," Zab 119:73
Ndugu yangu, iwapo mtu
mwingine atakuwa mbinguni kwa sababu yako, maisha yako yatakuwa yamefanya
tofauti ya milele. Anza kuangaza katika maeneo ya utume wako binafsi na usali,
"Mungu, nani umemweka katika maisha yangu ili nimweleze Yesu?
6.
Ratiba ya Mungu ya kuhitimisha historia inashikamana na ukamilishaji wa agizo
tulilopewa.
Siku hizi kuna hamu
kubwa ya kujua kuhusu kurudi kwa Yesu mara ya pili na mwisho wa ulimwengu.
Swali: Je, itakuwa lini?
Ndugu yangu, kabla Yesu
hajapaa mbinguni wanafunzi walimuuliza swali hili hili na jibu lake lilikuwa
wazi. Yesu anasema, "si kazi yenu kujua nyakati wala majira, Baba
aliyoweka katika mamlaka yake mwenyewe. Lakini mtapokea nguvu, akiisha
kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu; nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika
Yerusalemu, na katika Uyahudi wote, na Samaria, na hata mwisho wa nchi,"
Mate 1:7-8. Wanafunzi wanapotaka kuongea juu ya unabii, Yesu kwa haraka
aligeukia uinjilishaji akiwataka wakazanie utume wao ulimwenguni. Anasema jambo
hilo akimaanisha, “mambo ya kina kuhusu kurudi kwangu hayawahusu. Jambo la
muhimu kwenu ni utume niliowapa. Kazanieni hilo!”
Ndugu yangu, kusikia
juu ya muda halisi wa kurudi kwa Yesu Kristo ni upuuzi, kwa sababu anasema,
"walakini wa Habari ya siku ile na saa ile hakuna aijuaye, hata malaika
walio mbinguni, wala mwana, ila Baba peke yake," Mt 24:36. Kwa nini wewe
unajaribu kuibashiri? Tunachokijua kwa hakika ni kwamba: Yesu hatarudi mpaka
kila mmoja Mungu anayemtaka asikie habari njema awe amesikia. Unashangaa! Yesu
anasema, "tena habari njema ya ufalme itahubiriwa katika ulimwengu wote,
kuwa ushuhuda kwa mataifa yote; hapo ndipo ule mwisho utakapokuja," Mt
24:14. Umeipata hiyo?
Ndugu yangu, kama
unataka Yesu arudi haraka tia bidii kutimiza utume wako, siyo kubashiri unabii.
Ni rahisi kutiwa wasiwasi, kwa sababu shetani angependa wewe ufanye kitu
chochote kuliko kushirikisha watu wengine imani yako. Atakuruhusu ufanye aina
zote za mambo mema ili mradi hakuna mtu yeyote utakayempeleka mbinguni. Lakini
mara utakapokuwa na bidii katika utume wako, tegemea Ibilisi kukutupia kila
aina ya mambo yatakayokuachisha kazi hiyo. Ndugu yangu, inapotokea hivyo,
kumbuka maneno ya Yesu, "mtu aliyetia mkono wake kulima, kisha akaangalia
nyuma, hafai kwa ufalme wa Mungu," Lk 9:62
Je,
zipi gharama za kutimiza utume wako?
Ndugu yangu, kutimiza
utume wako vyema itakulazimu uache ajenda zako na ukubali mjadala wa Mungu kwa
ajili ya maisha yako. Huwezi tu kung'ang'ania mambo mengine yote ambayo
ungependa kufanya katika maisha yako. Lazima tuseme kama Yesu, "Ee, Baba,
ikiwa ni mapenzi yako, uniondolee kikombe hiki; walakini si mapenzi yangu, bali
yako yatendeke, "Lk 22:42.
Hapa unampatia Mungu
haki zako, matazamio yako, ndoto zako, mipango yako, na matakwa yako. Acha
kuomba sala za kibinafsi kama vile, "Mungu bariki ninachotaka
kukifanya." Badala yake sali hivi, "Mungu nisaidie nifanye kile
unachokibariki." Unamkabidhi Mungu karatasi tupu yenye jina lako chini na
unamwambia ajaze kwa kina sehemu iliyobaki. "bali jitoeni wenyewe kwa
Mungu kama walio hai baada ya kufa, na viungo vyenu kwa Mungu kuwa silaha za
haki." Rum 6:13b
Kama utajitoa kutimiza
utume wako katika maisha bila kujali gharama, utapata baraka za Mungu kwa njia
ambazo watu wachache huzipata. Hakuna kitu ambacho Mungu hawezi kufanya kwa
ajili ya mtu ambaye amejitoa kutumikia ufalme wa Mungu. Yesu anasema,
"Bali utafuteni kwanza ufalme wake, na haki yake; na hayo yote
mtazidishiwa," Mt 6:33. Tutimize wajibu huu muhimu. Hapa ndipo kwenye
KANISA HAI NA LINALOSAFIRI KATIKA NJIA ILIYO SALAMA. Kwa wale tuliobado na
ndoto ya kujua Yesu Kristo atarudi lini, tumeambiwa leo; “Enyi watu
wa Galilaya, mbona mmesimama mkitazama mbinguni? Huyu Yesu aliyechukuliwa
kutoka kwenu kwenda juu mbinguni, atakuja jinsi iyo hiyo mlivyomwona akienda
zake mbinguni,” Mdo 1:11. Mara baada ya ufufuko wa Bwana wetu Yesu Kristo, wale
wanawake walijidamka kwenda Kaburini malaika aliwaambia ujumbe huu, “enendeni
zenu, mkawaambie wanafunzi wake, na Petro, ya kwamba awatangulia kwenda
Galilaya; huko mtamwona, kama alivyowaambia,” Mk 16:7. Ujumbe mahususi kuhusu
Galilaya ni kwamba tutakutana naye katika maisha yetu ya kawaida kila mmoja
kadiri ya wito na maagano yake na Mungu. Kwa maana nyingine tunakutana na
Kristo mfufuka kwenye utume wetu. Hapo ndipo Galilaya yako. Leo Yesu anavyopaa
kwenda Mbinguni anawakumbusha Wagalilaya na sisi pia. Hivyo atakaporudi siku ya
mwisho ni vyema akukute vyema kwenye utume wako.
Mzee Masumbuko
alijaliwa kuwa na familia kubwa yenye watoto nane, na hivyo kufanya wote kwa
ujumla kuwa kumi. Kazi ya Mzee Masumbuko ili ulinzi wa kampuni moja ya wanyama
pori. Mara zote alipewa zamu ya usiku, hivyo kumfanya kuanza safari kuelekea
lindoni mida ya saa tisa alasiri.
Maisha kwa ujumla
kifamilia hayakuwa rahisi. Kipato
chake na ukubwa wa familia yake havikuendana kabisa. Jambo hili lilikuwa sababu
kubwa ya manung’uniko yake na hata kumlaumu Mungu kwa kutokuwa na usawa. Ila
kilichompa faraja mara zote ni tabia njema za watoto wake, na upendo wa watoto
wake na mke wake, na juhudi walizokuwa nazo katika masomo. Msingi mkubwa katika
familia hii ulikuwa sala. Walimtegemea Mungu kwa kila kitu, na hawakufanya
chochote kabla ya kukikabidhi mikononi mwa Mungu.
Siku mmoja akiwa anaelekea kazini akiwa anamenya limao
ili ale kwani mchana ulipita mkavu bila kitu, alitazama majumba barabarani huku
akivuta harufu nzuri ya vyakula kutoka kwenye majumba hayo, alijawa huzuni na
kuanza kumlalamikia Mungu. “Ee Mungu, tazama leo mimi na watoto wangu hatujala,
nami naenda huko lindoni sijui kitakachotokea usiku wa leo. Ee
Mungu ona, majumba haya na harufu hizi za vyakula, leo familia yangu ni kilio
tu,” alijisemea barabarani kama mwendawazimu hivi.
Akiwa anakula lile
limao, alitazama nyuma na kuona kuna mtu anaokota yale maganda na kuyala. Tendo
hilo lilimfanya asisikie tena harufu za vile vyakula kutoka majumba yale
yaliyokuwepo kando ya barabara. Akajiuliza, “Je, kama huyu anakula haya maganda
niliyoyatupa, si inanipasa kumshukuru Mungu katika jambo hili? Mimi nakula
limao hili na ninakibarua, je, huyu sidhani hata kama kibarua anacho. Ee Mungu
unirehemu na nifanye niwe na moyo wa shukrani hata kwa hiki kidogo
ninachokipata.”
Ni mara ngapi mimi na
wewe tunakuwa kama Mzee huyu Masumbuko?
Tumsifu Yesu Kristo!
“Na
tazama, nawaletea juu yenu ahadi ya Baba yangu; lakini kaeni humu mjini, hata
mvikwe uwezo utokao juu,” Lk 24:49
Tusali:-
Ee Mungu, tutumie vyema kama vyombo vyako kueneza Injili yako na hasa kwa
maisha yetu. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario