lunes, 30 de mayo de 2016

TAFAKARI: SHEREHE YA BIKIRA MARIA KWENDA KUMWAMKIA ELIZABETI

SHEREHE YA BIKIRA MARIA KWENDA KUMWAMKIA ELIZABETI
Somo: Sef 3:14-18a.
Zab: Isa 12:2-3, 4abc, 5-6
Injili: Lk 1:39-56
Nukuu:
Bwana ameziondoa hukumu zako, Amemtupa nje adui yako; Mfalme wa Israeli, naam, yeye Bwana, yu katikati yako; Hutaogopa uovu tena,” Sef 3:15 

Bwana, Mungu wako, yu katikati yako shujaa awezaye kuokoa; Atakushangilia kwa furaha kuu, Atakutuliza katika upendo wake, Atakufurahia kwa kuimba,” Sef 3:17

“Elisabeti akajazwa Roho Mtakatifu; akapaza sauti kwa nguvu akasema, Umebarikiwa wewe katika wanawake, naye mzao wa tumbo lako amebarikiwa,” Lk 1:41b-42

Mariamu akasema, Moyo wangu wamwadhimisha Bwana, Na roho yangu imemfurahia Mungu, Mwokozi wangu; Kwa kuwa ameutazama Unyonge wa mjakazi wake. Kwa maana, tazama, tokea sasa Vizazi vyote wataniita mbarikiwa; Kwa kuwa Mwenye nguvu amenitendea makuu, Na jina lake ni takatifu,” Lk 1:46-49

TAFAKARI:Moyo wangu wamwadhimisha Bwana, Na roho yangu imemfurahia Mungu, Mwokozi wangu.” 

Wapendwa wana wa Mungu, leo Mama Kanisa anatambua ushiriki wa Mama Bikira Maria katika safari nzima ya wokovu wetu, na hivyo anaadhimisha siku hii, tendo lile ya Bikira Maria kwenda kumwamkia mpwa wake Elizabeti. Mama Bikira Maria naheshimiwa sana na kutukuzwa katika Kanisa letu Katoliki siyo kwa sababu ya uzuri wake, au upekee wake wa ajabu kama mwanamke, bali kwa unyenyekevu wake, hasa kwa kuwa tayari kuyapokea yote licha ya kutokujua nini hasa kitakachofuata au tokea katika maisha yake. Bikira Maria anaishinda hofu ile ya sintofahamu. Ukweli huu unajidhihirisha kwa maneno haya mazito ya Bikira Maria, “mimi ni mjakazi wa Bwana; na iwe kwangu kama ulivyosema,” Lk 1:38a. Maneno haya ya Mama yetu Bikira Maria, ni fundisho tosha ya kujiachia pasipo kujibakiza, hasa katika mazingira ya yale tusiyoelewa sawa sawa.

Leo tunaposherehekea siku ile Bikira Maria alipokwenda kumpasha habari Mpwa wake Elizabeti, itukumbushe kudumisha ujirani mwema. Ujirani mwema hudumishwa kwa kuwa na moyo safi, Lk 1:46-47. Moyo usio jilimbikizia maovu. Moyo uliyotayari kuona mazuri mara zote kwa watu wote. Moyo usipungukiwa kiti kwa nyakati zote na shida zote. Moyo uliyo tayari kutaambika kwa ajili ya wengine. Usafi wa moyo huu, ni tiketi ya kuuona uso wa Mungu. Moyo usio na hatia una nafasi kubwa sana kumwaona Mungu. Moyo huu una heri kama asemavyo Bwana wetu Yesu Kristo,  Heri wenye moyo safi; Maana hao watamwona Mungu,” Mt 5:8. Mama yetu Bikira Maria pamoja na kuhesabiwa haki hiyo ya kuwa Mama wa Mungu, nafasi hiyo haikuwa sababu ya kujivunia, bali kujinyenyekesha katika udogo wa hali ya chini kabisa. Kujinyenyekesha kwake huku kuna kuwa chanzo cha mawasiliano ya kimungu kati ya fumbo lile lilikokuwa limejificha kati ya kile kilichokuwa tumboni mwake, yaani, Neno kufanyika Mwili na kukaa kwetu, na kile kilichokuwa kimeandaliwa kwa ajili ya kuitaarisha njia ya Neno hili, yaani, Yohani Mbatizaji. Na mambo yalikuwa hivi, Ikawa Elisabeti aliposikia kule kuamkia kwake Mariamu, kitoto kichanga kikaruka ndani ya tumbo lake,” Lk 1:41. Huu ni uthibitisha wa ubebaji wa Habari Njema aliyokuwa nayo Mama Bikira Maria. Je, wewe ni habari njema hapo ulipo? Hatuwezi kuwa habari njema kama tu wafuasi wa majungu. Wengi wetu tumebeba mimba za majungu na kwa namna hiyo hatuwezi kuwa habari njema hata kama tutajifungua.

Ndugu yangu, palipo habari njema, Roho Mtakatifu aliye umoja na tunda la upendo wa Mungu Baba na Mwana, hutuunganisha katika umoja wa kweli, na usio na unafiki. Na hivi ndivyo ilivyotokea kwa mpwa wake Bikira Maria, Elizabeti.  “Elisabeti akajazwa Roho Mtakatifu; akapaza sauti kwa nguvu akasema, Umebarikiwa wewe katika wanawake, naye mzao wa tumbo lako amebarikiwa,” Lk 1:41b-42. Roho Mtakatifu ndiye anayezungumzu ndani ya Elizabeti. Ndugu yangu, hata pale ambapo hatuna cha kusema ila tumejiachia bila kujibakiza kwa Kristo Yesu, Roho Mtakatifu utusemea na kutushuhudia. Katika hili Yesu anasema, nanyi mtachukuliwa mbele ya maliwali na wafalme kwa ajili yangu, kuwa ushuhuda kwao na kwa mataifa. Lakini hapo watakapowapeleka, msifikiri-fikiri jinsi mtakavyosema; maana mtapewa saa ile mtakayosema. Kwa kuwa si ninyi msemao, bali ni Roho wa Baba yenu asemaye ndani yenu,” Mt 10:18-20. Mawasiliano haya kati ya Mama Bikira na Mpwa wake Elizabeti ni mawasiliano yenye Umungu ndani yake.

Naye bila kujibakiza, Bikira Maria anayasema yaliyo moyoni mwake,  Moyo wangu wamwadhimisha Bwana, Na roho yangu imemfurahia Mungu, Mwokozi wangu; Kwa kuwa ameutazama Unyonge wa mjakazi wake. Kwa maana, tazama, tokea sasa Vizazi vyote wataniita mbarikiwa; Kwa kuwa Mwenye nguvu amenitendea makuu, Na jina lake ni takatifu,” Lk 1:46-49. Mama Bikira Maria kwa tendo hili anaona mpango mzima wa Mungu ndani yake. Pamoja na Mpango huo, Mama Bikira Maria hakuwa na sababu ya kujivuna na kujiinua zaidi ya kujinyenyekesha mbele za Mungu. Tendo hili linamtafakarisha Mama Bikira Maria kuyaona makuu ya Mungu kupitia kwake. Naye anasema, Amewaangusha wakuu katika viti vyao vya enzi; Na wanyonge amewakweza,” Lk 1:52. Akiwa mnyonge na mwenye kutostahili chochote zaidi ya kuwa mtumishi wa Bwana, Mama Bikira Maria anapata fursa ya kumshukuru Mungu na kulitukuza jina lake daima kwa kuutazama upya unyonge wa watu wake na taifa lake. Amemsaidia Israeli, mtumishi wake; Ili kukumbuka rehema zake; Kama alivyowaambia baba zetu, Ibrahimu na uzao wake hata milele,” Lk 1:54-55. Hakika Mama Bikira Maria ni kielelezo cha fadhila ya unyenyekevu. Hivyo kama kuna sababu ya kujisifu tujisifu kwa mambo ya udhaifu wetu kama asemavyo Mtume Paulo, 2Kor 11:30. Na penye udhaifu ndipo penye nguvu, 2Kor 12:10. Ni kwa unyenyekevu tu tunaweza kuona udhaifu wetu.

Wapendwa wana wa   Mungu, unyenyekevu huu kama ulivyo wa Mama yetu Bikira Marian dio unaoweza kutuondolea hukumu ya Mungu pale tunapomkosea Mungu na kuwa tayari kuanza upya Naye kwa njia ya toba ya kweli na majuto. Unyenyekevu wetu huujenga upya ukaribu wetu na Mungu na kwa namna hivyo Mungu yupo tayari kughairi hukumu yake kwetu. Bwana ameziondoa hukumu zako, Amemtupa nje adui yako; Mfalme wa Israeli, naam, yeye Bwana, yu katikati yako; Hutaogopa uovu tena,” Sef 3:15. Mungu kamwe hafurahii kuangamia kwetu kama asemavyo Nabii Isaya, Mtu mbaya na aache njia yake, Na mtu asiye haki aache mawazo yake; Na amrudie Bwana, Naye atamrehemu; Na arejee kwa Mungu wetu, Naye atamsamehe kabisa,” Isa 55:7. Ndugu yangu, Bwana, Mungu wako, yu katikati yako shujaa awezaye kuokoa; Atakushangilia kwa furaha kuu, Atakutuliza katika upendo wake, Atakufurahia kwa kuimba,” Sef 3:17. Sifa na Utukufu kwa Mungu wetu ajuaye mwisho wa maisha yetu. Amini.

Tumsifu Yesu Kristo!

Bwana ameziondoa hukumu zako, Amemtupa nje adui yako; Mfalme wa Israeli, naam, yeye Bwana, yu katikati yako; Hutaogopa uovu tena,” Sef 3:15


Tusali:- Ee Mama Bikira Maria, tujalie unyenyekevu wako ili nasi tufumbuliwe siri na mpango wa Mungu katika maisha yetu. Amina

No hay comentarios:

Publicar un comentario