JUMATATU WIKI YA 9 YA MWAKA-C
Somo: 2Pet 1:2-7
Zab: 91:1-2, 14-15b, 15c-16
Injili: Mk 12:1-12
Nukuu:
“kwa
wale waliopata imani moja na sisi, yenye thamani, katika hali ya Mungu wetu, na
Mwokozi Yesu Kristo,” 2Pet 1:1b
“Na katika
kutamani watajipatia faida kwenu kwa maneno yaliyotungwa; ambao hukumu yao
tangu zamani haikawii, wala uvunjifu wao hausinzii,” 2Pet 1:3
“Hata kwa wakati wake akatuma mtumwa kwa wale wakulima, ili
apokee kwa wakulima katika matunda ya mizabibu,” Mk 12:2
“Basi
alikuwa na mmoja bado, mwana mpendwa wake; huyu naye akamtuma kwao mwisho,
akisema, Watamstahi mwanangu,” Mk 12:6
“Lakini
wale wakulima wakasemezana, Huyu ni mrithi; haya, na tumwue, na urithi utakuwa
wetu,” Mk 12:7
“Wakamkamata,
wakamwua, wakamtupa nje ya shamba la mizabibu,” Mk 12:8
TAFAKARI: “Jiwe walilolikataa waashi, Hilo
limekuwa jiwe kuu la pembeni.”
Wapendwa wana wa Mungu, ufunuo wa wazi wa Mungu katika historia ya
wokovu wetu imekamilishwa kwa tendo lile la kumwilishwa, yaani, neno kufanyika
mwili na kukaa kwetu, Yoh 1:14. Tendo hili linakuwa mtikisiko mkubwa kwa watu
wengi, na hasa wale ambao hawakuwa katika njia ya kweli na haki. Ni wazi kabisa
tendo hili la kumwilishwa kwa neno linaubadilisha mtazamo mzima wa maisha, na
tumaini jipya la wale wote Mungu aliowaridhia. Kwa kupitia Musa, watu walipata
tumaini kwa kuishika torati. Ila kwa kupitia Kristo, neema na kweli likazaliwa
tumaini jipya na mwanzo mpya. “Kwa
kuwa torati ilitolewa kwa mkono wa Musa; neema na kweli zilikuja kwa mkono wa
Yesu Kristo,” Yoh 1:17. Hivyo mtikisiko wa wazi unaonekana kwa wale wote
waliojihesabia haki na kuhodhi mamlaka kama wao ndio miungu watu.
Injili ya leo inaeleza
historia nzima ya wokovu wetu hadi, kilele chake kikiwa ni ufunuo wa wazi wa
Mungu kwa watu wake, yaani Neno kufanyika mwili na kukaa kwetu. Mfano wa
wakulima katika shamba la mizabibu unatupa taswira halisi ya wale waliokuwa
wapinzani wa mpango huo wa wokovu wa Mungu. Wapinzani hawa amboa walijihesabia
haki na kujitwalia nafasi ya Mungu na
kuwa miungu watu, ndio waliowaangamiza wale wote waliolitangulia Neno,
yaani, Bwana wetu Yesu Kristo. Kundi hili kabla ya Neno ndilo lililowachukua
Mababa wa Imani, Manabii mbalimbali, na waamuzi. “Hata kwa wakati wake akatuma mtumwa kwa wale wakulima, ili
apokee kwa wakulima katika matunda ya mizabibu,” Mk 12:2. Hata hivyo hawa wote waliuwawa.
Mungu hakuchoka, kukata
tamaa, na wala kusitisha nia yake ya kumkomboa mwanadamu. “Basi
alikuwa na mmoja bado, mwana mpendwa wake; huyu naye akamtuma kwao mwisho,
akisema, Watamstahi mwanangu,” Mk 12:6. Jambo la kushangaza mambo hayakuwa
hivyo kutokana na ugumu wa mioyo ya watu, na hasa Wayahudi. Kwa kusukumwa na
ubinafsi wao (ikia ni pamoja na mila na desturi zao) na kutetea maslahi yao
kama miungu watu, Mwana huyu ya Mungu asiye na kosa wakamfanya kama
walivyowafanya watangulizi wake. “Lakini wale wakulima wakasemezana, Huyu ni
mrithi; haya, na tumwue, na urithi utakuwa wetu,” Mk 12:7. Lengo hapa ni
kulinda maslahi yao, na kuendelea kudumu katika dhambi. Yesu Kristo anawaambia
yote haya na sisi leo, kwa lengo la kubadili mwelekeo wa maisha na kuanza naye
upya kwani kwake lipo tumaini la kweli na lililojaa neema.
Hata
hivyo, kwa kuing’ang’ania dhambi na furaha zake, “Wakamkamata,
wakamwua, wakamtupa nje ya shamba la mizabibu,” Mk 12:8. Na haya ndiyo mauti
yaliyomfika mtu yule mwenye haki, ambaye ndiyo Kristo mwenyewe kwa kifo kile
cha Msalaba. Na hili ndilo jiwe la Msingi ambalo kwalo kila ajengaye nyumba juu yake (Imani juu ya Mwana
wa Mungu), nyumba hiyo itakuwa imara daima. Na hili ndilo itimisho ya andiko
lile kwamba, “Jiwe walilolikataa
waashi, Hilo limekuwa jiwe kuu la pembeni,” Mk 12:10. Maneno haya ya Yesu kwa wakuu wa makuhani, na waandishi, na wazee, Mk 11:27, yanazua tafrani kubwa kwani yaliwachoma vizuri ndani ya
mioyo yao. Kama ni ujumbe, ulifika na kupokelewa! Hivyo “wakatafuta
kumkamata, wakaogopa mkutano; maana walitambua ya kwamba ule mfano amewanenea
wao. Wakamwacha wakaenda zao,” Mk 12:12. Ndugu yangu, hii ni moja ya changamoto
ya Imani yetu, hasa pale tunapopambana na giza kwa kuileta nuru ya kweli.
Kwa
kuishi kweli ahadi zako za Ubatizo ni mwitikio wa wazi wa kupambana na lile
lililo giza na gizani. Ni kuwa tayari kuyapokea na kuyapata yote aliyompata
Kristo kwa sababu, “Kulikuwako Nuru
halisi, amtiaye nuru kila mtu, akija katika ulimwengu. Alikuwako ulimwenguni,
hata kwa yeye ulimwengu ulipata kuwako, wala ulimwengu haukumtambua. Alikuja
kwake, wala walio wake hawakumpokea,” Yoh 1:9:11. Je, katika hali hii mimi na
wewe tufanye nini?
Mpendwa katika Kristo,
simulizi alilolitoa Yesu latukumbusha ni kwa namna gani mpango wa Mungu
ulivyokuwa kuhusu wokovu wetu, na lina lengo la kuviendeleza vita hivi vya
imani bila kuogoba. Nuru yapasa kuwa nuru ili giza lisiwepo. Hivyo mimi na wewe
kwa kuwa nuru kuna mapaswa na sadaka yake. Basi pale tunapokuwa nuru kwa
mapaswa na sadaka yake, isiwe sababu ya kuhuzunika wala kujiona tumesahauliwa
na Mungu, bali tufurahi katika hali hiyo. Kwetu na iwe heri. Naye Yesu anasema
hivi pale tutakapopatwa na hali hiyo, kwamba, “Heri
ninyi watakapowashutumu na kuwaudhi na kuwanenea kila neno baya kwa uongo, kwa
ajili yangu. Furahini, na
kushangilia; kwa kuwa thawabu yenu ni kubwa mbinguni; kwa maana ndivyo
walivyowaudhi manabii waliokuwa kabla yenu,” Mt 5:11-12. Hapa tunahesabiwa haki
na kuwa na dhawabu kubwa mbinguni.
Mitume,
na hata wafuasi katika jumuiya ile ya kwanza ya Wakristo, hawakuacha kuwa nuru
pale walipokuwa licha ya ugumu wa mazingira ya wakati ule. Mtume Petro haachi
kujitambulisha katika Imani ya kweli ndani na katika Kristo kwa watu kama asemavyo,
“kwa
wale waliopata imani moja na sisi, yenye thamani, katika hali ya Mungu wetu, na
Mwokozi Yesu Kristo,” 2Pet 1:1b. Leo mimi kuwa Mkristo bila kielezo hai cha
Kristo ndani yangu, ni sawa na kutokuishi nuru ile halisi ya Kristo ndani
yangu. Kwa kutokufanya hivyo, Mtume Petro anasema, “wengi
watafuata ufisadi wao; na kwa hao njia ya kweli itatukanwa,” 2Pet 1:2. Kristo
hatoheshimika kabisa mbele za watu, na hasa kwa matendo ya kifisadi
yanapofanywa na wale ambaye hujishuhudia mbele za watu kama Wakristo. Moja ya
uwepo wa nuru halisi ndani ya maisha yetu ni kule kuwa watu wa haki, na
watetezi wa haki kama Kristo Yesu alivyofanya na hata kuifia haki hiyo ili mimi
na wewe leo tuwe huru. Huku ni kuishi tumaini la kweli ndani na katika Kristo
pale ulipo na kadiri ya wito wako. Kwa kutokufanya hivyo ukijua kwa faidi
binafsi ni kujiandalia hukumu. “Na katika kutamani watajipatia faida kwenu kwa
maneno yaliyotungwa; ambao hukumu yao tangu zamani haikawii, wala uvunjifu wao
hausinzii,” 2Pet 1:3. Je, Mungu hupendezwa haya yatokee kwako bila kusema
lolote?
Wapendwa wana wa Mungu,
dhamiri yako ndiyo mwalimu wako wa ndani. Dhamiri safi ni mwalimu wa kweli na
haki ndani yako. Bila shaka mwalimu huyu ndani yako ni uwepo wa nguvu za Mungu
ndani yako zenye lengo la kukufikisha pale Mungu alipo. Ni kwa maana hiyo
kwamba, “Mungu hakuwaachilia malaika
waliokosa, bali aliwatupa shimoni, akawatia katika vifungo vya giza, walindwe
hata ije hukumu; wala
hakuuachilia ulimwengu wa kale, bali alimhifadhi Nuhu, mjumbe wa haki, na watu
wengine saba, hapo alipoleta Gharika juu ya ulimwengu wa wasiomcha Mungu,” 2Pet
1:4-5. Ndugu yangu, hukumu utakayoipata kwa kutokuitii sauti ya Mungu ndani
yetu, yaani, ile dhamiri hai na njema ndani yetu, itakuwa nimeiandaa wenyewe
kwa kujua. Hapa ndipo kwenye kulia na kusaga meno (Mt 8:12, 13:42, 50, 22:13,
24:51, 25:30, Mk 9:18, na Lk 13:28), maana yake, hutakuwa na jambo lolote la
kujitetea. Na hivi ndivyo ilivyokuwa juu ya miji ile ya Sodoma na Gomora,
kwamba, “akaihukumu..,
akiipindua na kuifanya majivu, akaifanya iwe ishara kwa watu watakaokuwa
hawamchi Mungu baada ya haya,” 2Pet 1:6.
Wapendwa wana wa Mungu, heshimu na
kuitii dhamiri yako njema. Walizitii dhamiri zao na kusimama katika kweli na
haki, Mungu aliwaepusha na aina zote za ufisadi na mwisho akawahesabia haki. Ni
kwa namna hiyo, Mungu “akamwokoa
Lutu, yule mwenye haki aliyehuzunishwa sana na mwenendo wa ufisadi wa hao
wahalifu,” 2Pet 1:7. Basi tuenenda kama wana wa Nuru kwa kuwa na hofu ya Mungu
ndani yetu. Amina.
Tumsifu Yesu Kristo!
“Huyu ni mrithi;
haya, na tumwue, na urithi utakuwa wetu. Wakamkamata, wakamwua, wakamtupa nje
ya shamba la mizabibu,” Mk 12:7b-8
Tusali:-Ee Yesu, uliye neema
na kweli, tuwezesha mara zote kuishi katika neema hiyo na kweli hiyo kila siku
ya maisha yetu. Amina
No hay comentarios:
Publicar un comentario