miércoles, 1 de junio de 2016

TAFAKARI: IJUMAA-SHEREHE YA MOYO MTAKATIFU WA YESU-C

sherehe ya moyo mtakatifu wa yesu-C
somo I: Eze 34:11-16
Zab: 23, (K) 1
Somo II: Rum 5:5 -11
Injili: Lk 15:3-7
Nukuu:
Maana, Bwana MUNGU asema hivi; Tazama, mimi mwenyewe, naam, mimi, nitawatafuta kondoo zangu, na kuwaulizia,” Eze 34:11 

Mimi mwenyewe nitawalisha kondoo zangu, nami nitawalaza, asema Bwana MUNGU,” Eze 34:15 

Nami nitawatafuta waliopotea, nitawarudisha waliofukuzwa, nitawafunga waliovunjika, nitawatia nguvu wagonjwa; nao wanono na wenye nguvu nitawaharibu; nitawalisha hukumu,” Eze 34:16

Kwa maana hapo tulipokuwa hatuna nguvu, wakati ulipotimia, Kristo alikufa kwa ajili ya waovu,” Rum 5:6 

Bali Mungu aonyesha pendo lake yeye mwenyewe kwetu sisi, kwa kuwa Kristo alikufa kwa ajili yetu, tulipokuwa tungali wenye dhambi,” Rum 5:8 

Basi zaidi sana tukiisha kuhesabiwa haki katika damu yake, tutaokolewa na ghadhabu kwa yeye,” Rum 5:9 

Wala si hivyo tu, ila pia twajifurahisha katika Mungu kwa Bwana wetu Yesu Kristo, ambaye kwa yeye sasa tumeupokea huo upatanisho,” Rum 5:11

Ni nani kwenu, mwenye kondoo mia, akipotewa na mmojawapo, asiyewaacha wale tisini na kenda nyikani, aende akamtafute yule aliyepotea hata amwone?” Lk 15:4

Nawaambia, Vivyo hivyo kutakuwa na furaha mbinguni kwa ajili ya mwenye dhambi mmoja atubuye, kuliko kwa ajili ya wenye haki tisini na kenda ambao hawana haja ya kutubu,” Lk 15:7 

TAFAKARI: “Moyo Mtakatifu wa Yesu ni thibitisho wazi la huruma ya Mungu.”

Wapendwa wana wa Mungu, leo Mama Kanisa anaadhmisha sherehe ya Moyo Mtakatifu wa Yesu. Kimantiki sherehe hii ilipaswa kuadhimishwa siku ile ya Ijumaa Kuu, kwa sababu siku ile ulimwengu mzima ulijionea jambo hili, yaani, “Mwana wa Mungu kuinuliwa msalabani, na kujitoa mwenyewe kwa ajili ya kutupenda sisi. Kwa tendo hilo la kutukuka lenye kubeba neema na huruma ya Mungu, alichomwa ubavu akamwaga damu na maji, zipate kutoka humo Sakramenti za Kanisa. Na kwa namna hivyo, sote tuvutwe na huo Moyo wazi wa Mwokozi, na kuchota kwa furaha neema katika chemchemi ya wokovu.” Hiki ndicho kwa hakika tukisherehekeacho leo. Hata hivo kwa mazingira yale ya Ijumaa Kuu yalighubikwa na majonzi makubwa na kutokupata nafasi ya kuutafakari kwa undani Moyo huu Mtakatifu wa Yesu. Leo ndiyo siku yake.

Maisha ya Bwana wetu Yesu Kristo hapa duniani, na hasa ile miaka yake mitatu aliyoitumia kupandikiza neno la uzima kwetu, mambo makuu matatu yalijidhihirisha pasipo shaka katika Moyo wake huu Mtakatifu. Moja, kutafuta kile kilichopotea. Katika kutafuta kile kilichopotea, Yesu anasema wazi mbele za watu sababu ya mahangaiko yake, na kusema,  Wenye afya hawahitaji tabibu, bali walio hawawezi; sikuja kuwaita wenye haki, bali wenye dhambi,” Mk 2:17. Ni upendo wa hali ya juu sana, Mungu aliyemwilishwa pamoja na ukamilifu wake, yupo tayari kuwa karibu na mkosefu (mwenye dhambi) na kufanya naye urafiki ili ampate katika kweli na haki. Mungu yupo tayari muda na wakati wowote kuwa karibu na mkosefu ili ampate. Hapa ndipo tunapoweza kuona kwa undani huruma ya Mungu tunapoyatafakari maneno haya: “Mtu mbaya na aache njia yake Na mtu asiye haki aache mawazo yake; Na amrudie Bwana, Naye atamrehemu; Na arejee kwa Mungu wetu, Naye atamsamehe kabisa.” Isa 55:7.

Mungu aliye hai na mwenye kusafiri nasi katika historia nzima ya wokovu wetu, huyaona mateso na mahangaiko yetu. Yupo nasi katika kila jambo, na yote tuyapatayo au kutokea, yanakusudi la Mungu hata pale tunaposhindwa kujua sababu yake kwa kadiri ya ufahamu wetu, kama asemavyo Mungu, “mawazo yangu si mawazo yenu, wala njia zanu si njia zangu.” Isa 55:8. Njia za Mungu ni tofauti na njia za mwanadamu. Njia zetu zimethibitiwa na nafasi na wakati, ilhali njia za Mungu zipo katika umilele wake. Na ndiyo maana, Bwana MUNGU asema hivi; Tazama, mimi mwenyewe, naam, mimi, nitawatafuta kondoo zangu, na kuwaulizia,” Eze 34:11. Mungu hachoki kukutafuta licha ya uovu wako. Ukiona umeufia uovu wako ujue ni chaguo la uhuru wako bila shinikizo lolote. Ni uhuru na utashi wako, na umefikia hapa ulipo kwa kuheshimu na kuutendea haki uhuru na utashi wako licha ya kwamba tokeo lake ni chukizo kwa Muumba wako.

Mungu wetu tunayemwamini utulisha yaliyo mema, ila baada ya kushiba umtendea yaliyo maovu. Naye asema hivi,  Mimi mwenyewe nitawalisha kondoo zangu, nami nitawalaza,” Eze 34:15. Kutokuukubali utawala wa Mungu na kulazwa naye katika nuru ya kweli na haki ni kukengeuka ukijua kuwa Yeye ndiye aliyetuumba kwa sura na mfano wake, Mwan 1:27. Hata hivyo Mungu huyu aliye Upendo na Huruma hachoki kututafuta hata pale unapomkana. Naye anasema, Nami nitawatafuta waliopotea, nitawarudisha waliofukuzwa, nitawafunga waliovunjika, nitawatia nguvu wagonjwa; nao wanono na wenye nguvu nitawaharibu; nitawalisha hukumu,” Eze 34:16. Ndugu yangu, hata  hukumu hii  ya Mungu aitoayo ni tokeo la Upendo mtupu. Ona jinsi Mungu anavyoangaika nawe. Huu ndiyo Moyo Mtakatifu Yesu. Moyo usiochoka kukutafuta hata kuwambwa juu ya Msalaba kwa sababu yako na yangu. Ujumbe Mkuu wa Moyo huu ni huu: “hakuna aliye na upendo mwingi kuliko huu, wa mtu kuutoa uhai wake kwa ajili ya rafiki zake,” Yoh 15:13. Hakika Moyo Mtakatifu wa Yesu ni bubujiko lisilo kifani la huruma ya Mungu.

Pili, miaka ile mitatu ya mwisho ya Yesu hapa duniani inathibitisha jambo hili; “utayari wake wa kujitoa kwa ajili ya kile kilichopotea. Hapa ndipo tunapouona utii wa Mungu kwa mwenye dhambi. Hii ni neema na huruma ya hali ya juu kwetu wenye dhambi. Katika hili Mtume Paulo anatuambia hivi juu ya Yesu; “tena, alipoonekana ana umbo kama la mwanadamu, alijinyenyekeza akawa mtii hata mauti, naam, mauti ya msalaba,” Flp 2:8. Je, wathamini hilo alilokutendea Yesu kwa sababu tu anakupenda kama ulivyo? Ndugu yangu, lazima uelewe jambo hili, kwamba, Kwa maana hapo tulipokuwa hatuna nguvu, wakati ulipotimia, Kristo alikufa kwa ajili ya waovu,” Rum 5:6. Je, mimi nimekamilika? Kama nimekamilika, je, mazingira yangu na tenda kwa watu wangu ina akisi upendo huu alionifia Kristo? Ukweli ni kwamba,  Mungu aonyesha pendo lake yeye mwenyewe kwetu sisi, kwa kuwa Kristo alikufa kwa ajili yetu, tulipokuwa tungali wenye dhambi,” Rum 5:8. Sadaka yangu kila siku ni kuwa mwaminifu pale nilipo, na kuvuja damu kila siku kwa kujitoa vilivyo kwa kile nikifanyacho kama moja ya huduma na kuwajibika kwangu. Kutafuta huruma mbele za watu ili kuonekana mwema ni kupoteza muda na neema ya Mungu ndani yako. Huu ndio mchezo haramu na usiopendeza mbele ya Mungu unaofanywa na viongozi wetu, hasa wa kisiasa kucheza na hisia zetu.

Wapendwa wana wa Mungu, mwanadamu hata kwa hali yake ya utakatifu hawezi kukuhesabia haki mbele za Mungu, kwani naye katika hali hiyo bado anahitaji huruma na neema ya Mungu. Kwa nini basi watafuta huruma mbele za watu na kumwacha Bwana Mungu wako anayekuhesabia haki? Kama Wakristo na wafuasi wake waaminifu wa Kristo, kwa matendo yetu mema yenye kuubeba wokovu, yaweza kutunahesabiwa haki kwa damu yake iliyomwagika pale Msalabani na si vinginevyo. Katika hili Mtume Paulo anasema, Basi zaidi sana tukiisha kuhesabiwa haki katika damu yake, tutaokolewa na ghadhabu kwa yeye,” Rum 5:9. Kuokolewa katika ghadhabu hii ni pamoja na kupatanishwa naye. Ndugu yangu, Moyo Mtakatifu wa Yesu ni uthibitisho wa upatanishi wetu na Mungu. Moyo huu ndiyo uliowezesha patanisho hilo kwa sadaka yake pale Msalabani. Ni kwa namna hiyo mimi na wewe leo, twajifurahisha katika Mungu kwa Bwana wetu Yesu Kristo, ambaye kwa yeye sasa tumeupokea huo upatanisho,” Rum 5:11. Hakika Kristo Yesu ni daraji imara la upatanisho wetu na Mungu.

Tatu, miaka ile mitatu ya mwisho ya Yesu hapa duniani inathibitisha furaha ya Mungu, na hasa kwa mwenye kutubu na kuacha njia yao mbaya. Furaha ya Mungu ni kuanza naye upya, na Yeye utuchukulia katika upya wetu bila kuyahesabu yaliyopita. Mungu usamehe yote bila kuhoji historia yake tufanyapo toba ya kweli na majuto. Mfano mzuri ni wa yule Mwana Mpotevu, Lk 15:11-32. Katika hili Yesu anazihoji dhamiri zetu katika kweli na haki, na kusema, Ni nani kwenu, mwenye kondoo mia, akipotewa na mmojawapo, asiyewaacha wale tisini na kenda nyikani, aende akamtafute yule aliyepotea hata amwone?” Lk 15:4. Ujumbe hapa ni kwamba, wewe na mimi kama Viiongozi tuwe tayari kukitetea kile kilicho dhaifu kwa sababu furaha ya kweli ni sote tuwe salama. Kama kiongozi ni wajibu wako wote wafike salama asipotee hata mmoja. Kiongozi anayekimbilia ukamilifu wa wachache, na kuwapoteza wengu na wakati mwingine bila kujua “kulikoni,” kiongozi huyo ni dhaifu sana. Kamwe Mungu hawezi kufurahia tendo hilo kwa sababu hata huyo unayemuona si mkamilifu kwa vigezo vya kibinadamu, ilhali mtu huyu yupo tayari kuiacha njia yake mbaya na kumrudia Mungu, ila wewe kwa kuishikilia sheria, tena mbovu haupo tayari kufikiri nje ya sheria ile. Ndugu yangu, tambua kwamba mtu huyo ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Na kwa sababu hiyo Mungu hachoki kutafuta kile kionekacho dhaifu na kilichopotea. Katika hili Yesu anasema, Vivyo hivyo kutakuwa na furaha mbinguni kwa ajili ya mwenye dhambi mmoja atubuye, kuliko kwa ajili ya wenye haki tisini na kenda ambao hawana haja ya kutubu,” Lk 15:7 

Wapendwa wana wa Mungu, bila shaka waweza kuona ni kwa namna gani Moyo huu wa Yesu Mtakatifu tunao usherehekea leo ulivyobeba uzito wa ubinadamu wetu, ile wewe na mimi tuhesabiwe haki. Tunahesabiwa haki si kwa matendo yetu mema tu na ukaribu wetu mbele ya Mungu, bali kwa utayari wetu wa kuona udhaifu ndani yetu na kufanya toba ya kweli na majuto ambayo kwa kutenda dhambi ndiyo sababu kubwa ya teso la Moyo huu Mtakatifu.

Tumsifu Yesu Kristo!

Bali Mungu aonyesha pendo lake yeye mwenyewe kwetu sisi, kwa kuwa Kristo alikufa kwa ajili yetu, tulipokuwa tungali wenye dhambi,” Rum 5:8


Tusali:-Ee Yesu Mwema, uniumbie Moyo safi, uifanye upya Roho iliyotulia ndani yangu, usinitenge na uso wako, Wala roho wako mtakatifu usiniondolee.  Amina

No hay comentarios:

Publicar un comentario