JUMATATU WIKI YA 4 YA MWAKA-C
Somo: 2Sam 15:13-14, 30, 16:5-13
Zab: 3:2-7
Injili: Mk 5:1-20
Nukuu:
“Daudi
akamwambia Abishai, na watumishi wake wote, Angalieni, huyu mwanangu, aliyetoka
viunoni mwangu, anautafuta uhai wangu; si zaidi Mbenyamini huyu sasa? Mwacheni
alaani, kwa sababu Bwana ndiye aliyemwagiza,” 2Sam 16:11
“Labda
Bwana atayaangalia mabaya yaliyonipata, naye Bwana atanilipa mema kwa sababu ya
kunilaani kwake leo,” 2Sam 16:12
“akapiga
kelele kwa sauti kuu, akasema, Nina nini nawe, Yesu, Mwana wa Mungu aliye juu?
Nakuapisha kwa Mungu usinitese,” Mk 5:7
“Akawapa
ruhusa. Wale pepo wachafu wakatoka, wakaingia katika wale nguruwe; nalo kundi
lote likatelemka kwa kasi gengeni, wakaingia baharini, wapata elfu mbili;
wakafa baharini,” Mk 5:13
“Wakaanza
kumsihi aondoke mipakani mwao,” Mk 5:17
“lakini
hakumruhusu, bali alimwambia, Enenda zako nyumbani kwako, kwa watu wa kwenu,
kawahubiri ni mambo gani makuu aliyokutendea Bwana, na jinsi alivyokurehemu,”
Mk 5:19
“Akaenda
zake, akaanza kuhubiri katika Dekapoli, ni mambo gani makuu Yesu aliyomtendea;
watu wote wakastaajabu,” Mk 5:20
TAFAKARI: “Kawahubiri
ni mambo gani makuu aliyokutendea Bwana, na jinsi alivyokurehemu.”
Wapendwa
wana wa Mungu, hakuna kati yetu asiye na jambo lolote la kumshukuru Mungu hata
kama tumesongwa na dhiki ya kupindukia. Kushukuru kwa jambo lolote lile ni
kuomba pia. Ni mara ngapi sala zetu zimekuwa na muono wa kushukuru? Mfalme
Daudi anasongwa na upinzani mkubwa kutoka nje na ndani ya ufalme wake. Pamoja
na hali hiyo, Mfalme Daudi hatoi nafasi ya kumlaumu Mungu. Kusamehewa kifo kwa kosa la kuzina na mke wa Uria,
hakukumwondolea upanga dhidi ya Ufalme wake. Bwana Mungu akasema, “Basi, sasa upanga hautaondoka nyumbani mwako,
kwa sababu umenidharau, ukamtwaa mkewe Uria, Mhiti, kuwa mke wako,” 2Sam 12:10.
Mtoto wake wa kumzaa, Absalomu anakuwa mwiba mkali katika
ufalme wake. Mfalme Daudi anakosa ujasiri na kuingiwa hofu na amani kutoweka.
Huyu ndiye aliyemua Goliathi kwa jiwe. “Daudi
akamwambia Abishai, na watumishi wake wote, Angalieni, huyu mwanangu, aliyetoka
viunoni mwangu, anautafuta uhai wangu; si zaidi Mbenyamini huyu sasa?” 2Sam
16:11a. Mfalme Daudi anatambua wazi matendo
aliyomtendea Mungu na kujikwaa kwake. Hivyo kila kinachomtokea kina sababu na
mkono wa Mungu ndani yake. Alipodhihakiwa njia na mtu asiyemjua alikotoka,
Mfalme Daudi alijibu, “Mwacheni
alaani, kwa sababu Bwana ndiye aliyemwagiza. Labda Bwana atayaangalia mabaya
yaliyonipata, naye Bwana atanilipa mema kwa sababu ya kunilaani kwake leo,”
2Sam 16:11b-12. Mfalme Daudi pamoja na kuujua ukweli huu, hakukata tamaa na
wala hakumwasi Mungu.
Injili
ya leo inaubeba ujumbe kama wa Mfalme Daudi ila kwa mtazamo mwingine. Hapa
tunakutana na uponyaji wa mtu aliyeteswa na kundi kubwa la pepo. Hata
walipoulizwa mpo wangapi haikuwa rahisi tutoa jibu la haraka. Badala yake
walijibu, ‘Legioni, kwa kuwa walikuwa wengi.’ Uwepo wa Yesu ni vita dhidi ya uovu. Ni vita vya
mwanga dhidi ya giza. Jina la Yesu linatisha. Jina hili ni tishio dhidi ya
Shetani na mamlaka yake. Ni kwa sababu hiyo, mtu yule alipomwona Yesu, “akapiga kelele kwa sauti kuu, akasema, Nina nini
nawe, Yesu, Mwana wa Mungu aliye juu? Nakuapisha kwa Mungu usinitese,” Mk 5:7. Pepo wachafu wanatambua nguvu na mamlaka
aliyokuwa nayo Yesu, na wanajua vita dhiki yake hawatashinda. Je, unaliamini
jina hili Tukufu na Kuu kuliko Majina Yote?
Na hali ilivyozidi kuwa mbaya, pepo wale
waliomba na kujisalimisha chini ya Mamlaka ya jina hili kuu, kwa kuwaingia
nguruwe. “Akawapa
ruhusa. Wale pepo wachafu wakatoka, wakaingia katika wale nguruwe; nalo kundi
lote likatelemka kwa kasi gengeni, wakaingia baharini, wapata elfu mbili;
wakafa baharini,” Mk 5:13. Ukiangalia tendo hili alilofanya Yesu kiuchumi la
kuwaruhusu wale pepo kuwaingia wale
nguruwe waweza kutafsiri kwamba Yesu hakutenda haki kwa mfugaji wa wale nguruwe.
Ndugu yangu, viumbe vyote ni mali ya Mungu, na Yeye Mungu anamamlaka yote juu
ya viumbe vyake vyote. Na maandiko Matakatifu yanatuambia, Neno huyu alifanyika
mwili na kukaa kwetu, Yoh 1:14, “Vyote vilifanyika kwa huyo; wala pasipo yeye hakikufanyika cho chote
kilichofanyika,” Yoh 1:2. Hivyo Yesu alikuwa na mamlaka yote na uamuzi wake
ulikowa sahihi.
Kwa upande mwingine, tendo hili la Yesu linathibitisha
upekee na thamani ya mwanadamu kati ya viumbe vyote. Na sababu kubwa ni kwamba
Mungu alipenda na kuchakua kumuumba mtu kwa sura na mfano wake, Mwa 1:27.
Kiumbe huyu, yaani mwanadamu imebeba chapa ya Mungu ndani yake. Binadamu
anastahili heshima kubwa licha ya tofauti za kibinadamu tunazojiwekea, na
zinazotokana na utofauti wa kimaisha, na kwa makusudi kabisa tunaruhusu
zitugawe kimatabaka. Pamoja na upekee huu aliokuwa nao Mwanadamu, kamwe
Mwanadamu huyu hawezi kumshurutisha Mungu atende kadiri atakavyo yeye. Kwani “Bwana huua, naye hufanya kuwa hai; Hushusha hata kuzimu, tena
huleta juu. Bwana hufukarisha
mtu, naye hutajirisha; Hushusha chini, tena huinua juu. Humwinua mnyonge kutoka mavumbini,
Humpandisha mhitaji kutoka jaani, Ili awaketishe pamoja na wakuu, Wakakirithi
kiti cha enzi cha utukufu; Kwa maana nguzo za dunia zina Bwana, Naye ameuweka
ulimwengu juu yake,” 1Sam 2:6-8. Kumbe kila alitendalo Bwana lina sababu yake
katika umilele wake.
Kama tendo la shukrani,
mtu yule aliyewekwa huru na Yesu kutoka mamlaka ya shetani, anaomba kuandamana
ya Yesu. “Lakini Yesu hakumruhusu, bali
alimwambia, Enenda zako nyumbani kwako, kwa watu wa kwenu, kawahubiri ni mambo
gani makuu aliyokutendea Bwana, na jinsi alivyokurehemu,” Mk 5:19. Ndugu yangu, unapotambua mkono wa Mungu katika
maisha yako, anza hapo hapo kutoa ushuhuda huo na kulisifu jina la Bwana.
Mtakatifu Fransisko wa Assis wakati fulani alisema, ‘hakuna sababu ya kwenda
sehemu fulani na kuhubiri, ila tuhubiri kadiri tutembeavyo.’ Kwa upande
mwingine, katazo hili ya Yesu kwa mtu huyu asiandamane naye linalenga kukoleza
Imani ya kweli sehemu ile Mungu aliyokutendea makuu yake. Hivyo mtu yule “akaenda zake, akaanza kuhubiri katika Dekapoli,
ni mambo gani makuu Yesu aliyomtendea; watu wote wakastaajabu,” Mk 5:20. Ndugu
yangu, wewe na mimi tunayo mengi ya kutoa shukrani kwa Mungu. Basi anza hapo
ulipo.
Tumsifu Yesu Kristo!
“Ee Bwana, Mungu wangu, uangalie, uniitikie; Uyatie nuru macho
yangu, Nisije nikalala usingizi wa mauti,” Zab 13:3
No hay comentarios:
Publicar un comentario