domingo, 24 de enero de 2016

TAFAKARI: SIKUKUU YA KUONGOKA KWA MTUME PAULO

Sikukuu ya kuongoka kwa mtume paulo
25/1
Somo: Mdo 22:3-16
Zab: 117:1bc, 2
Injili: Mk 16:15-18
Nukuu:
Mimi ni mtu wa Kiyahudi, nalizaliwa Tarso, mji wa Kilikia, ila nililelewa katika mji huu, miguuni pa Gamalieli, nikafundishwa sheria ya baba zetu kwa usahihi, nikawa mtu wa jitihadi kwa Mungu kama ninyi nyote mlivyo leo hivi; nikawaudhi watu wa Njia hii hata kuwaua, nikawafunga, nikiwatia gerezani, wanaume na wanawake,” Mdo 22:3-4 

Kama Kuhani Mkuu naye anishuhudiavyo, na wazee wa baraza wote pia, ambao nalipokea barua kwao kuwapelekea ndugu wale, nikaenda Dameski, ili niwalete wale waliokuwa huko hata Yerusalemu, hali wamefungwa, ili waadhibiwe,” Mdo 22:5

Ikawa nilipokuwa nikisafiri, nikikaribia Dameski, wakati wa adhuhuri, ghafula nuru kuu ilitoka mbinguni, ikanimulikia pande zote,” Mdo 22:6

Nikaanguka nchi, nikasikia sauti ikiniambia, Sauli, Sauli, mbona unaniudhi? Nikajibu, Wewe u nani, Bwana? Akaniambia, Mimi ni Yesu Mnazareti, ambaye wewe unaniudhi,” Mdo 22:7-8

Akasema, Mungu wa baba zetu amekuchagua wewe upate kujua mapenzi yake, na kumwona yule Mwenye haki, na kuisikia sauti itokayo katika kinywa chake,” Mdo 22:14 

Kwa maana utakuwa shahidi wake kwa watu wote, wa mambo hayo uliyoyaona na kuyasikia,” Mdo 22:15 

Basi sasa, unakawilia nini? Simama, ubatizwe, ukaoshe dhambi zako, ukiliitia jina lake,” Mdo 22:16 

Akawaambia, Enendeni ulimwenguni mwote, mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe,” Mk 16:15

Aaminiye na kubatizwa ataokoka; asiyeamini, atahukumiwa,” Mk 16:16 

Na ishara hizi zitafuatana na hao waaminio; kwa jina langu watatoa pepo; watasema kwa lugha mpya; watashika nyoka; hata wakinywa kitu cha kufisha, hakitawadhuru kabisa; wataweka mikono yao juu ya wagonjwa, nao watapata afya,” Mk 16:17-18 

TAFAKARI: “Kwa maana utakuwa shahidi wake kwa watu wote, wa mambo hayo uliyoyaona na kuyasikia.”

Wapendwa wana wa Mungu, simulizi la kweli la kuongoka kwa Mtume Paulo limesimiliwa mara tatu kutoka Kitabu cha Matendo ya Mitume (Mdo 9:1-19, 22:3-16, na 26:9-18. Kristofania-“Tokeo la Yesu,” njiani kuelekea Damasko ni tukio la msingi na lililojenga upya maisha na mtazamo wa Mtume Paulo. Mtume Paulo anasema, alipoona vema kumdhihirisha Mwanawe ndani yangu, ili niwahubiri Mataifa habari zake; mara sikufanya shauri na watu wenye mwili na damu,” Gal 1:16. Ni kweli isiyo shaka kwamba unapokutana na Yesu katika maisha yako hawezi kukuachi hivi hivi. Mtume Paulo ambaye kabla ya kuongoka kwake alitambulika kwa jina la Sauli, aliitetea vilivyo dini yake ya kiyahudi katika dhamiri ambayo kwake aliona safi na inafaa. Sauli alithibitisha jambo hili kuhusu imani, “na heri kuwa joto au baridi katika imani, kuliko kuwa vuguvugu.” Msimamo huu wake katika imani anaukiri mwenyewe kwa maneno yake: Mimi ni mtu wa Kiyahudi, nalizaliwa Tarso, mji wa Kilikia, ila nililelewa katika mji huu, miguuni pa Gamalieli, nikafundishwa sheria ya baba zetu kwa usahihi, nikawa mtu wa jitihadi kwa Mungu kama ninyi nyote mlivyo leo hivi; nikawaudhi watu wa Njia hii hata kuwaua, nikawafunga, nikiwatia gerezani, wanaume na wanawake,” Mdo 22:3-4. Hakika Sauli hakuwa na mchezo wala lelema juu ya imani na dini yake.

Kuongoka kwa Paulo kunaambatana na viashirio viwili vya wito wa kimasiha, yaani, kuona na kusikia ambavyo vinajirudia katika somo hili kwa msisitizo. Ikawa nilipokuwa nikisafiri, nikikaribia Dameski, wakati wa adhuhuri, ghafula nuru kuu ilitoka mbinguni, ikanimulikia pande zote. Akasema, Mungu wa baba zetu amekuchagua wewe upate kujua mapenzi yake, na kumwona yule Mwenye haki, na kuisikia sauti itokayo katika kinywa chake. Kwa maana utakuwa shahidi wake kwa watu wote, wa mambo hayo uliyoyaona na kuyasikia. Nikamwona, naye akiniambia, Hima, utoke Yerusalemu upesi, kwa sababu hawatakubali ushuhuda wako katika habari zangu,” Mdo 22: 6, 14, 15, 18. Msingi wa ushuhuda wa kuongoka kwake Paulo unajengwa na haya: “Kwa maana utakuwa shahidi wake kwa watu wote, wa mambo hayo uliyoyaona na kuyasikia. Nikamwona, naye akiniambia, Hima, utoke Yerusalemu upesi, kwa sababu hawatakubali ushuhuda wako katika habari zangu. Lakini inuka, usimame kwa miguu yako, maana nimekutokea kwa sababu hii, nikuweke wewe uwe mtumishi na shahidi wa mambo haya uliyoyaona, na wa mambo ambayo katika hayo nitajidhihirisha kwako,” Mdo 22:15, 18; 26:16

Utume wake wakimisioni wa Paulo unapata nguvu na mamlaka katika msingi huu: Naye akaniambia, Enenda zako; kwa kuwa mimi nitakutuma uende mbali kwa watu wa Mataifa. Lakini Bwana akamwambia, Nenda tu; kwa maana huyu ni chombo kiteule kwangu, alichukue Jina langu mbele ya Mataifa, na wafalme, na wana wa Israeli. Nikikuokoa na watu wako, na watu wa Mataifa, ambao nakutuma kwao; uwafumbue macho yao, na kuwageuza waiache giza na kuielekea nuru, waziache na nguvu za Shetani na kumwelekea Mungu; kisha wapate msamaha wa dhambi zao, na urithi miongoni mwao waliotakaswa kwa imani iliyo kwangu mimi,” Mdo 22:21; 9:15, 26:17-18

Kwa mantiki hiyo, Paulo ‘aliona’ nuru ya mwanga.  Ee Mfalme, ndipo wakati wa adhuhuri njiani naliona nuru inatoka mbinguni ipitayo mwangaza wa jua, ikinimulikia mimi, na wale waliofuatana nami pande zote,” Mdo 26:13. Na alipoona nuru hii alitiwa upofu na Yesu Mfufuka kama ishara ya kuuzika utu wake wa zamani na kufufuka naye kuelekea uzima. Na nilipokuwa sioni kwa sababu ya fahari ya nuru ile, nikaongozwa na mikono yao waliokuwa pamoja nami, nikaingia Dameski,” Mdo 22:11. Ni kabla ya kutiwa upofu huu alisikia ‘sauti’ ya Bwana na kumweleza kile kilichomsikitisha. Nikaanguka nchi, nikasikia sauti ikiniambia, Sauli, Sauli, mbona unaniudhi? Nikajibu, Wewe u nani, Bwana? Akaniambia, Mimi ni Yesu Mnazareti, ambaye wewe unaniudhi,” Mdo 22:7-8. Sauti hii ndiyo inayompa uhakika wa kile alichokifanya kuwa si halali wala haki, na hivyo kumtaka kubadili misioni yake ya zamani na kuanza upya na Kristo kwa kutoa ushuhuda huo mbele ya watu wote, na hasa mataifa alichokisika na kukiona. Kwa maana utakuwa shahidi wake kwa watu wote, wa mambo hayo uliyoyaona na kuyasikia,” Mdo 22:15

Wito wa Paulo ni ‘wongofu’ wa kweli. Maneno ya Ananias yenye hofu na mashaka juu ya Sauli aliyekuwa anamfahamu kwa ukatili wake, yanapata ufafanuzi wa kile kilichomtoke Sauli njiani kwa maneno ya Yesu. Huyu si Sauli tena bali Paulo alibadilishwa na Kristo. Ni Paulo mwongofu na mtu mpya sasa. Lakini Anania akajibu, Bwana, nimesikia habari za mtu huyu kwa watu wengi, mabaya mengi aliyowatenda watakatifu wako Yerusalemu; hata hapa ana amri itokayo kwa wakuu wa makuhani awafunge wote wakuitiao Jina lako. Lakini Bwana akamwambia, Nenda tu; kwa maana huyu ni chombo kiteule kwangu, alichukue Jina langu mbele ya Mataifa, na wafalme, na wana wa Israeli. Maana nitamwonyesha yalivyo mengi yatakayompasa kuteswa kwa ajili ya Jina langu. Anania akaenda zake, akaingia mle nyumbani; akamwekea mikono akisema, Ndugu Sauli, Bwana amenituma, Yesu, yeye aliyekutokea katika njia uliyoijia, upate kuona tena, ukajazwe Roho Mtakatifu,” Mdo 9:13-17. Yule aliyekuwa mtesi wa Watakatifu wa Mungu sasa ndiye chombo kiteule kitakachochukua jina la Yesu mbele ya Mataifa na kuteseka kwa ajili ya jina hilo. Ni kwa kupitia Jina hili lenye nguvu kupita majina yote, Yesu anatuhaidi haya; Na ishara hizi zitafuatana na hao waaminio; kwa jina langu watatoa pepo; watasema kwa lugha mpya; watashika nyoka; hata wakinywa kitu cha kufisha, hakitawadhuru kabisa; wataweka mikono yao juu ya wagonjwa, nao watapata afya,” Mk 16:17-18 

Misioni aliyopewa Mtume Paulo siku ya kuongoka kwake ndiyo maneno ya mwisho ya Yesu kabla ya kupaa kwake, kwa walio wake juu ya utume wa kimisioni kwa watu wote, na kuihubiri Injili kwa kila kiumbe. Akawaambia, Enendeni ulimwenguni mwote, mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe,” Mk 16:15. Tunasoma pia ujumbe huu mahusi kutoka, (Mk 13:10; 14:9; Mt 28:18-20; Lk 24:47). Hata hivyo huu utume wa kimisioni na wa dharura ulitimia kwa ufanisi  mkubwa wa wafuasi wake Yesu. Maana, ijapokuwa naihubiri Injili, sina la kujisifia; maana nimewekewa sharti; tena ole wangu nisipoihubiri Injili!” 1Kor 9:16. Hapa tunaweza kuona mkazo na utofauti kwa namna Mtakatifu Paulo alivyouchukulia kwa upekee utume wake wa kimisionari. Hakika ni Mtume wa mataifa na jitu la sifa!

Hata hivyo, sharti linalowekwa kwa wale ambao wanataka kufaidika na ‘Habari Njema,’ni KUAMINI na KUBATIZWA (Yoh 3:18; Mdo 2:38; 16:31-3). Haya mambo mawili ni muhimu sana kwa imani hai na ya wazi inayohitimishwa kwa fumbo la Sakramenti ya ubatizo. Kwa kuwa ninyi nyote mmekuwa wana wa Mungu kwa njia ya imani katika Kristo Yesu. Maana ninyi nyote mliobatizwa katika Kristo mmemvaa Kristo. Hapana Myahudi wala Myunani. Hapana mtumwa wala huru. Hapana mtu mume wala mtu mke. Maana ninyi nyote mmekuwa mmoja katika Kristo Yesu. Na kama ninyi ni wa Kristo, basi, mmekuwa uzao wa Ibrahimu, na warithi sawasawa na ahadi,” Gal 3:26-29. Kristo ndiye kielelezo chetu na ndiye njia, kweli, na uzima, na mtu hawezi kwenda ya Baba bila kupitia kwa Yesu, Yoh 14:6. Hivyo hivyo hakuna awezeye kwenda kwa Yesu kama hajavutwa na Baba. Hakuna mtu awezaye kuja kwangu, asipovutwa na Baba aliyenipeleka; nami nitamfufua siku ya mwisho,” Yoh 6:44. Ndugu yangu tuliyesafiri sote katika tafakari hii, watambua umuhimu wa Yesu katika maisha yako na hatma ya umilele wako? Kama bado, ni wakati wa kutafakari na kuchukua hatua.

Tumsifu Yesu Kristo!
Mtakatifu Paulo Mtume, Utuombee.


Na uzima wa milele ndio huu, Wakujue wewe, Mungu wa pekee wa kweli, na Yesu Kristo uliyemtuma,” Yoh 17:3

No hay comentarios:

Publicar un comentario