miércoles, 27 de enero de 2016

TAFAKARI: ALHAMISI WIKI YA 3 YA MWAKA-C

ALHAMISI WIKI YA 3 YA MWAKA-C

Somo: 2Sam 7:18-19, 24-29
Zab: 132:1-5, 11-14
Injili: Mk 4:21-25
Nukuu:
Kwa kuwa wewe, Bwana wa majeshi, Mungu wa Israeli umenifunulia mimi, mtumwa wako, ukisema, Nitakujengea nyumba; kwa hiyo mimi, mtumwa wako, nimeona vema moyoni mwangu nikuombe dua hii,” 2Sam 7:27

Na sasa, Ee Bwana MUNGU, wewe ndiwe Mungu, na maneno yako ndiyo kweli, nawe umemwahidia mtumwa wako jambo hili jema,” 2Sam 7:28 

basi, sasa, uwe radhi, ukaibarikie nyumba ya mtumwa wako, ipate kudumu milele mbele zako; kwa maana wewe, Ee Bwana MUNGU, umelinena na kwa baraka yako nyumba ya mtumwa wako na ibarikiwe milele,” 2Sam 7:29

Kwa maana hakuna neno lililositirika, ila makusudi lije likadhihirika; wala hakuna lililofichwa, ila makusudi lije likatokea wazi,” Mk 4:22 

Akawaambia, Angalieni msikialo; kipimo kile mpimacho ndicho mtakachopimiwa, na tena mtazidishiwa,” Mk 4:24

Kwa maana mwenye kitu atapewa, naye asiye na kitu, hata kile alicho nacho atanyang'anywa,” Mk 4:25

TAFAKARI:Kipimo kile mpimacho ndicho mtakachopimiwa, na tena mtazidishiwa.”

Wapendwa wana wa Mungu, hakuna binadamu asiyetaka kupendwa na hakuna asiyeyajua maumivu ya kutokupendwa. Upendo ni sehemu muhimu sana kwa mtu yeyote yule ikiwa ni pamoja na makuzi yake. Upendo wa kweli utuweka pia karibu na viumbe vile visivyo na utashi, mathalani; paka na mmbwa. Tunapowaonyesha upendo wa dhati viumbe hivi visivyo na utashi hutambua upendo huo na kwa namna moja au nyingine hurudisha upendo huo kwetu. Je, kama viumbe hivi visivyo na utashi urudisha upendo kwetu kwa yale tunayowafanyia itakuwaje vizuri na vyema tukipendana sisi kwa sisi?

Tumeumbwa ili tuwe na ushirika wa kweli sisi kwa sisi. Hivyo hakuna aishiye kama kisiwa bali tunategemeana katika kukamilishana. Ukamilisho huu huja pale tunapotambua uwezo na mapungufu yetu. Hivyo kujitoa kwa ajili ya mwingine ni sehemu ya maisha yetu ya kila siku. Hii ndiyo changamoto ya upendo kwamba ujitoavyo ndivyo navyo utakavyokirimiwa siku ile ya mwisho. ‘Kipimo cha upendo ni kupenda bila kipimo,’ Mt. Augustino. Naye Yesu Akawaambia, Angalieni msikialo; kipimo kile mpimacho ndicho mtakachopimiwa, na tena mtazidishiwa,” Mk 4:24. Je, usipofanya chochote juu ya jirani yako ili hali unajua wajibu huu itakuaje? Katika jambo hili Yesu anasema, Kwa maana mwenye kitu atapewa, naye asiye na kitu, hata kile alicho nacho atanyang'anywa,” Mk 4:25. Mwenye kitu ni yule anayetambua anao wajibu wa kufanya zaidi kwa ajili ya wengine. Na asiye na kitu ni yule anayefikiri hana wajibu wa kufanya chochote kwa ajili ya wengine na hasa wenye uhitaji. Kwa hawa kundi la pili Yesu anasema, “hata kile alicho nacho atanyang’anywa.”

Ndugu yangu, lazima tuelewa kwamba siyo sisi tuliyeanza kumpenda Mungu, bali ni Mungu mwenyewe alianza kutupenda, na kwa pendo hilo alichagua kutuumba kwa sura na mfano wake, Mwa 1:27. Hivyo kupenda ni amri ya Mungu mwenyewe aliyoiweka ndani mwetu. Hivyo upendo huo lazima uzae matunda kwa kujitoa kwa wengine bila kujibakiza. Na Yesu analisema jambo hili kwa ufasaha, Si ninyi mlionichagua mimi, bali ni mimi niliyewachagua ninyi; nami nikawaweka mwende mkazae matunda; na matunda yenu yapate kukaa; ili kwamba lo lote mmwombalo Baba kwa jina langu awapeni,” Yoh 15:16. Ndugu yangu lazima ufanya kitu kwa ajili ya baraka na neema Mungu anazokujalia kila siku.

Mfalme Daudi baaba ya kuupokea ujumbe ule wa Mungu kutoka kwa Nabii Nathani juu ya ujenzi wa nyumba ya Mungu, Daudi anauchukua wajibu huo kama sehemu muhumu katika Ufalme wake. Naye anasema, Kwa kuwa wewe, Bwana wa majeshi, Mungu wa Israeli umenifunulia mimi, mtumwa wako, ukisema, Nitakujengea nyumba; kwa hiyo mimi, mtumwa wako, nimeona vema moyoni mwangu nikuombe dua hii,” 2Sam 7:27. Maneno ya Mungu kwetu ni kweli na tena ni uhai. Kulifanya akuagizalo Mungu ni kutimiza kweli hiyo ya Mungu ndani yako na kuupata uhai huo ambao ni mali ya Mungu na zawadi kwako. Na sasa, Ee Bwana MUNGU, wewe ndiwe Mungu, na maneno yako ndiyo kweli, nawe umemwahidia mtumwa wako jambo hili jema,” 2Sam 7:28. Ni furaha iliyoje kuyafanya yale yampendezayo Mungu?

Hakuna shaka ya baraka na neema za Mungu pale tuyafanyapo mapenzi ya Mungu bila kujibakiza. Tulivyo navyo vyote ni mali yake mwenyewe na tunapovitumia kwa mapenzi yake ndivyo tunavyozidishiwa na kubarikiwa zaidi. Nchi na vyote viijazavyo ni mali ya Bwana, Dunia na wote wakaao ndani yake,” Zab 24:1. Je una kilicho chako zaidi ya dhambi zako? Hivyo kwa kulitambua hili, Mfalme Daudi anasema, basi, sasa, uwe radhi, ukaibarikie nyumba ya mtumwa wako, ipate kudumu milele mbele zako; kwa maana wewe, Ee Bwana MUNGU, umelinena na kwa baraka yako nyumba ya mtumwa wako na ibarikiwe milele,” 2Sam 7:29. Ndugu yangu, hakuna aliyekuwa masikini kwa kutoa, na ndivyo ilivyo kwa baraka huvuta baraka.

Tumsifu Yesu Kristo!


Azitegemeaye mali zake ataanguka; Mwenye haki atasitawi kama jani,” Mit 11:28

No hay comentarios:

Publicar un comentario