martes, 19 de enero de 2016

TAFAKARI: JUMATANO WIKI YA 2 YA MWAKA-C

JUMATANO WIKI YA 2 YA MWAKA-C
20/1/2016
Somo: 1Sam 17:32-33, 37, 40-51
Zab: 144:1b, 2, 9-10
Injili: Mk 3:1-6
Nukuu:
Daudi akamwambia Sauli, Asizimie moyo mtu ye yote kwa ajili ya huyu; mimi mtumishi wako nitakwenda kupigana na Mfilisti huyu,” 1Sam 17:32 

Sauli akamwambia Daudi, Huwezi wewe kumwendea Mfilisti huyu upigane naye; maana wewe u kijana tu; na huyu ni mtu wa vita tangu ujana wake,” 1Sam 17:33

Daudi akasema, Bwana aliyeniokoa na makucha ya simba, na makucha ya dubu, ataniokoa na mkono wa Mfilisti huyu. Sauli akamwambia Daudi, Enenda, na Bwana atakuwa pamoja nawe,” 1Sam 17:40 

Akaichukua fimbo yake mkononi, akajichagulia mawe laini matano katika kijito cha maji, akayatia katika mfuko wa kichungaji aliokuwa nao, maana ni mkoba wake, na kombeo lake alikuwa nalo mkononi mwake, akamkaribia yule Mfilisti,” 1Sam 17:40 

Mfilisti akamwambia Daudi, Je! Mimi ni mbwa hata umenijia kwa fimbo? Mfilisti akamlaani Daudi kwa miungu yake,” 1Sam 17:43 

Mfilisti akamwambia Daudi, Njoo huku kwangu; nyama yako nitawapa ndege wa angani na wanyama wa mwituni,” 1Sam 17:44 


Ndipo Daudi akamwambia yule Mfilisti, Wewe unanijia mimi na upanga, na fumo, na mkuki, bali mimi ninakujia wewe kwa jina la Bwana wa majeshi, Mungu wa majeshi ya Israeli uliowatukana,” 1Sam 17:45 

Siku hii ya leo Bwana atakuua mkononi mwangu, nami nitakupiga, na kukuondolea kichwa chako, nami leo nitawapa ndege wa angani na wanyama wa nchi mizoga ya majeshi ya Wafilisti, ili kwamba dunia nzima wajue ya kuwa yuko Mungu katika Israeli,” 1Sam 17:46 

Nao jamii ya watu wote pia wajue ya kwamba Bwana haokoi kwa upanga wala kwa mkuki; maana vita ni vya Bwana, naye atawatia ninyi mikononi mwetu,” 1Sam 17:47 

Daudi akatia mkono wake mfukoni, akatwaa humo jiwe moja, akalitupa kwa kombeo lake, akampiga Mfilisti katika kipaji cha uso; jiwe hilo likamwingilia kipajini, akaanguka chini kifudifudi,” 1Sam 17.49 

Hivyo Daudi akamshinda yule Mfilisti kwa kombeo na jiwe, akampiga Mfilisti, akamwua; walakini Daudi hakuwa na upanga mkononi mwake,” 1Sam 17:50

Ndipo Daudi akapiga mbio, akasimama juu ya Mfilisti, akautwaa upanga wake, akaufuta alani mwake, akamwua, akamkata kichwa kwa upanga huo. Nao Wafilisti walipoona ya kuwa shujaa wao amekufa, wakakimbia,” 1Sam 17:51 

Akaingia tena katika sinagogi; na palikuwako huko mtu mwenye mkono uliopooza; wakamvizia ili kuona kama atamponya siku ya sabato; wapate kumshitaki,” Mk 3:1-2

Akamwambia yule mtu mwenye mkono uliopooza, Simama katikati,” Mk 3:3 

Akawauliza, Ni halali siku ya sabato kutenda mema, au kutenda mabaya? Kuponya roho au kuiua? Wakanyamaza,” Mk 3:4 

Akawakazia macho pande zote kwa hasira, akiona huzuni kwa ajili ya ugumu wa mioyo yao, akamwambia yule mtu, Nyosha mkono wako. Naye akaunyosha; mkono wake ukawa mzima tena,” Mk 3:5 

Mara wakatoka wale Mafarisayo, wakawa wakifanya shauri juu yake pamoja na Maherodi, jinsi ya kumwangamiza,” Mk 3:6 

TAFAKARI: “Mimi ninakujia wewe kwa jina la Bwana wa majeshi. Nao jamii ya watu wote pia wajue ya kwamba Bwana haokoi kwa upanga wala kwa mkuki; maana vita ni vya Bwana.”

Wapendwa wana wa Mungu, Mungu wetu hakufanya makosa kutuumba kwa sura na mfano wake, Mwa 1:27. Ni kwa namna hiyo ilimpendeza kutuumba na kuweka chapa yake ndani yetu nasi leo ni wanadamu. Ni kwa ubinadamu wetu huu hadi siku ya mwisho wa uhai wetu hapa duniani ndivyo Mungu anapenda tuwe. Ni tatizo kubwa sana pale tunapokataa ubinadamu wetu na kutaka kuwa kitu kingine. Binadamu anapoukataa ubinadamu wake anakuwa mbaya kuliko shetani. Hata wale Malaika waliomwasi Mungu walitaka kuwa zaidi ya kile walichoumbwa kuwa na hivyo wakageuka kuwa Mashetani.

Binadamu anapokataa kuwa kile alicho kadiri ya uwezo na mipaka ya Mungu aliyependezwa awe, na kibinadamu huyo kuchukua nafasi ya Mungu hugeuka kuwa Shetani. Huku ndiko kuasi kulikofanywa na Msalaika. Ushetani wa mtu ni mtu mwenyewe! Shetani ni roho, kwayo yenyewe haiwezi kufanya chochote nje ya mtu bila kuikubali roho hiyo. Shetani kama roho hufanya kazi ndani ya mtu kama mwezeshaji wa ile roho. Hivyo, “shetani wa mtu ni mtu mwenyewe.”

Mara nyingi kinachotuponza kutokuukubali ubinadamu wetu na mapungufu yake ni yale tunayoyapokea kutoka kwa watu na namna wansemavyo juu yetu. Hapa ndipo sifa ujijengea mizizi, umaarufu unapokuzwa, uwezo unapoabudiwa kwa wale wanaokupaka mafuta kwa mgongo wa chupa, na nafasi ya pesa na utajiri unaposhika hatama. Yeyote yule anayeyakubali haya na kuyafanya kuwa sehemu ya maisha yake, hatochelea kuwa Shetani. Kama wabisha jaribu!

Waisraeli wanapatwa hofu juu ya Goliathi ambaye alikuwa tishio kubwa kwao. Historia ya Goliathi ilikuzwa sana na watu waliamini juu ya uwezo wake bila kuona nguvu na uwezo wa Mungu. Hivyo Sauli Mfalme anamwambia Daudi kuhusu Mfilisti huyu aliyekuwa tishio kwao, “huwezi wewe kumwendea Mfilisti huyu upigane naye; maana wewe u kijana tu; na huyu ni mtu wa vita tangu ujana wake,” 1Sam 17:33. Daudi kijana shupavu aliyeyaweka yote mikononi mwa Mungu, na mwenye hofu ya Mungu, anaona lililo kuu na zaidi ya mwanadamu na fahari yake. Naye anamwambia Mfalme Sauli, “Bwana aliyeniokoa na makucha ya simba, na makucha ya dubu, ataniokoa na mkono wa Mfilisti huyu. Sauli akamwambia Daudi, Enenda, na Bwana atakuwa pamoja nawe,” 1Sam 17:40. Huku ndiko kumtumaini Mungu kuliko kweli na haki. Maji uliyoyavulia nguo lazima kuyakoga!

Tunapojikabidhi kwa Mungu bila kujibakiza hasa katika nyakati hizi zilizojuu ya uwezo wetu, Mungu hutumia yale yaliyokawaida ndani ya uwezo wetu na kutimiza hazma yake iliyo kweli ndani yetu. Anayepigana vita hii kwa asilimia zote 100 ni Mungu mwenyewe. Wewe na mimi kwa upande wetu ni vyombo vya amani yake Mungu kama aombavyo Mtakatifu Fransisko, “Bwana unifanya chombo cha amani yako.” Hivyo Daudi Akaichukua fimbo yake mkononi, akajichagulia mawe laini matano katika kijito cha maji, akayatia katika mfuko wa kichungaji aliokuwa nao, maana ni mkoba wake, na kombeo lake alikuwa nalo mkononi mwake, akamkaribia yule Mfilisti,” 1Sam 17:40. Mpinzani wake Goliathi kutokana na uzoefu wake wa vita na sifa alizojichotea na kumvimbisha kichwa aliona ziaka kubwa kufanywa na Daudi. Anayepigana vita hivi vya kweli na haki si Daudi bali Mungu mwenyewe. Kwa dharau kubwa Goliathi anaukataa ubinadamu wake na kusema maneno mazito juu ya Mungu anayemtumia Daudi mtumishi wake, “Je! Mimi ni mbwa hata umenijia kwa fimbo? Mfilisti akamlaani Daudi kwa miungu yake. Mfilisti akamwambia Daudi, Njoo huku kwangu; nyama yako nitawapa ndege wa angani na wanyama wa mwituni,” 1Sam 17:43-44.

Daudi anayejua ni Mungu gani anayemtumikia hakuwa na hofu juu ya Mungu wake. Daudi hana shaka kabisa na kile akifanyacho kwa sababu anajua uwezo wa Mungu anayemwamini na kumtumikia. Ndipo Daudi akamwambia yule Mfilisti, Wewe unanijia mimi na upanga, na fumo, na mkuki, bali mimi ninakujia wewe kwa jina la Bwana wa majeshi, Mungu wa majeshi ya Israeli uliowatukana,” 1Sam 17:45. Silaha kubwa ya mtu ni unyenyekevu wake juu ya kile kilicho nje ya uwezo wake. Binadamu licha ya uwezo na akili zake bado kuna sintofahamu ndani ya ufahamu wake. Ni Mungu tu mwenye kukamilisha hiki ambacho bado hakijafunuliwa kwa binadamu. Ndiyo maana kwa ufahamu wetu na mahesabu zetu twaweza kupanga yote na mwisho wa siku yakaenda kinyume na ufahamu wetu na mahesabu zetu. Ndugu yangu bado huamini kuna kitu zaidi ya ufahamu wako?

Pamoja na vitisho vyote vya Goliathi, Daudi habadilishwi na kile anachokiamini juu ya Mungu anayemtumikia. Daudi kijana mdogo sana na asiyeshikika katika mikono ya Goliathi anamwambia Goliathi, Siku hii ya leo Bwana atakuua mkononi mwangu, nami nitakupiga, na kukuondolea kichwa chako, nami leo nitawapa ndege wa angani na wanyama wa nchi mizoga ya majeshi ya Wafilisti, ili kwamba dunia nzima wajue ya kuwa yuko Mungu katika Israeli,” 1Sam 17:46. Ndugu yangu unayesafiri nami katika tafakari hii, kamwe usitangulize mbele chochote kile wasemacho watu juu yako zaidi ya Mungu anayewezesha hayo wasemayo watu juu yako. Daudi anayafanya hayo yote si kwa kulitukuza jina lake, bali Mungu ainuliwe juu zaidi na ulimwengu wote ufahamu nafasi ya Mungu. Tumwache Mungu aitwe Mungu ndugu zangu. Watu wanapokusifia ni vyema kulichukulia jambo hilo kama jaribu kubwa kati ya uhusiano wako na Mungu. Ni vyema kujibu hivi, “Tumshukuru Mungu, na sote tubarikiwe!”

Wapendwa wana wa Mungu, yule aliyejulikana kama kikaka wa vita na kupata medali nyingi za ushindi wa kivita anasitishwa kwa jiwe moja tu la Daudi. Daudi akatia mkono wake mfukoni, akatwaa humo jiwe moja, akalitupa kwa kombeo lake, akampiga Mfilisti katika kipaji cha uso; jiwe hilo likamwingilia kipajini, akaanguka chini kifudifudi,” 1Sam 17.49. Ndugu zangu wapendwa, mara nyingi binadamu anapochagua kuwa shetani na kuukataa ubinadamu wake hutegemea vitu ambavyo vipo chini ya uwezo wake. Na kwa ajabu Mungu uthibitisha kwetu kwamba hivyo tunavyovitegemea haviwezi kamwe kutuokoa. Mungu huyu aliliangamiza jeshi kubwa la wamisri kwa maji tu.  Yale maji yakarudi yakafunikiza magari na wapanda farasi, hata jeshi lote la Farao lililoingia katika bahari nyuma yao; hakusalia hata mtu mmoja. Kwa maana farasi za Farao na magari yake na wapanda farasi wake waliingia ndani ya bahari, Bwana akayarudisha maji ya bahari juu yao; bali wana wa Israeli walikwenda katika nchi kavu katikati ya baharí,” Kut 14:28, 15:19 

Ndugu yangu unaweza kuchezea haki za watu kwa kujificha nyuma ya kivuli cha mitutu, vifaru vya kijeshi, na magari ya maji washa washa ili kuzima sauti zao, ila ipo siku Mungu atasimama na kusema inatosha juu ya watu wangu unaowanyanyasa. Hapo ndipo kwenye kulia na kusaga meno. Jambo la kufahamu ni hili, “mara zote elewa kwamba wewe siyo kipimo cha ukweli kwa hayo unayoyalazimisha yawe kwa manufaa yako na kile ukiwakilishacho kisicho kweli na haki, iwe jamii au chama chako cha siasa.” Mungu mara zote huzungumza na watu. “Kwa kuwa walipo wawili watatu wamekusanyika kwa jina langu, nami nipo papo hapo katikati yao,” Mt 18:20.

Kifo cha Goliathi ni jibu la Mungu kwamba sasa inatosha juu wa watu wangu wanaoteseka bila sababu. Goliathi awe mfano wetu wa kujifunza mipaka yetu na namna yetu ya kuenenda juu wa wale Mungu aliowaumba kwa sura na mfano wake. Kwa “maana wote waushikao upanga, wataangamia kwa upanga,” Mt 26:52b. Kwa kadiri tutumiavyo njia mbovu kukandamiza haki za watu ni kwa njia hiyo hiyo tutakavyofikwa na umauti. Ndipo Daudi akapiga mbio, akasimama juu ya Mfilisti, akautwaa upanga wake, akaufuta alani mwake, akamwua, akamkata kichwa kwa upanga huo. Nao Wafilisti walipoona ya kuwa shujaa wao amekufa, wakakimbia,” 1Sam 17:51. Kile alichokuwa anakitegemea Goliathi kuwaangamiza watu wa Mungu ndicho Daudi alichokitumia kuhitimisha udhalimu wake. Hakika wote waushikao upanga, wataangamia kwa upanga!

Wapendwa wana wa Mungu, Mungu wetu hututakia mema muda wote. Tatizo letu ni pale tunapotaka Mungu kufanya kadiri tuonavyo sisi. Tatizo kubwa ndani ya utashi wetu ni kwamba mara nyingi hatuoni vitu kama vilivyo bali huviona kama tulivyo. Injili ya leo Yesu anaturudisha katika makusu ya Mungu mwenyewe naye akiwa Mungu, yaani, Neno aliyefanyika mwili na kukaa kwetu. Ni kweli isiyo shaka kwamba mara nyingine ufahamu wetu unagota kwenye mila na desturi zetu na kutufanya kuendana na mitazamo hiyo ambayo haina uhai ndani yake zaidi ya ufu. Yesu hafanyi lolote kwa kujificha. Akamwambia yule mtu mwenye mkono uliopooza, Simama katikati,” Mk 3:3. Kila mtu lazima aone yale ayafanyao Yesu. Yote ayafanyayo Yesu katika maisha yetu siyo mazingaumwe. Ni kweli kabisa wapo baadhi yetu kwa kuyakuza majina yao uishia katika nguvu za giza na kuvaa miwani ya Kristo. Mwisho ya hayo yote wanayoyaigiza huwa aibu yao.

Yesu hachoki kutuelekeza kwa kile kilicho haki na kweli mbele ya Mungu na uzima wetu wa milele. Yesu anauliza swali la msingi sana juu ya mila na desturi zetu juu ya uhai ambao ni mali ya Mungu na zawadi ya Mungu kwetu. Akawauliza, Ni halali siku ya sabato kutenda mema, au kutenda mabaya? Kuponya roho au kuiua? Wakanyamaza,” Mk 3:4. Kwa namna nyingine Yesu anakuuliza wewe na mimi hivi: “je kile unachokiamini kinakuzuia kutenda lililo jema ambalo kwa uhalali ni zaidi ya kile unachokiamini?” Mila na desturi zetu zinaitaji kutakatifuzwa kwa sababu zimejawa hofu nyingi bila maelezo ya kina kwani lengo lake huwa utiii bila kuhoji. Utii upofu. Na ukitaka kuchunguza kwa undani mila hizi zilikuwa kwa manufaa ya wale walioziweka au kuzifanya. Pamoja na ukweli kwamba Yesu hakupata jibu ya swali lake, Yesu hakuacha kufanya lililo jema mbele ya Mungu Baba na watu wake kwa hofu ya macho ya watu na misimamo yao. Akawakazia macho pande zote kwa hasira, akiona huzuni kwa ajili ya ugumu wa mioyo yao, akamwambia yule mtu, Nyosha mkono wako. Naye akaunyosha; mkono wake ukawa mzima tena,” Mk 3:5. Ndugu yangu uliyesafari nami katika tafakari hii, ukweli utatuweka huru na si vinginevyo. “Ninyi mkikaa katika neno langu, mmekuwa wanafunzi wangu kweli kweli; tena mtaifahamu kweli, nayo hiyo kweli itawaweka huru,” Yoh 8:31-32

Tumsifu Yesu Kristo!


Bwana ni nuru yangu na wokovu wangu, Nimwogope nani? Bwana ni ngome ya uzima wangu, Nimhofu nani?” Zab 27:1

No hay comentarios:

Publicar un comentario