JUMANNE WIKI YA 2 YA MWAKA-C
19/1/2016
Somo: 1Sam 16:1-13
Zab: 98:20, 21-22, 27-28
Injili: Mk 2:23-28
Nukuu:
“Lakini Bwana
akamwambia Samweli, Usimtazame uso wake, wala urefu wa kimo chake; kwa maana
mimi nimemkataa. Bwana haangalii kama binadamu aangaliavyo; maana wanadamu
huitazama sura ya nje, bali Bwana huutazama moyo,” 1Sam 16:7
“Kisha Samweli akamwambia Yese, Watoto
wako wote wapo hapa? Naye akasema, Amesalia
mdogo wao, na tazama, anawachunga kondoo. Basi Samweli akamwambia Yese, Tuma
watu, wamlete; kwa sababu hatutaketi hata atakapokuja huku,” 1Sam 16:11
“Basi akatuma mtu,
naye akamleta kwao. Naye alikuwa mwekundu, mwenye macho mazuri, na umbo lake
lilikuwa la kupendeza. Bwana akasema, Ondoka, umtie mafuta; maana huyu ndiye,”
1Sam 16:12
“Ndipo Samweli
akaitwaa pembe yenye mafuta, akamtia mafuta kati ya ndugu zake; na roho ya
Bwana ikamjilia Daudi kwa nguvu tangu siku ile. Basi Samweli akaondoka, akaenda
zake Rama,” 1Sam 16:13
“Akawaambia, Sabato
ilifanyika kwa ajili ya mwanadamu, si mwanadamu kwa ajili ya sabato,” Mk 2:27
“Basi Mwana wa Adamu
ndiye Bwana wa sabato pia,” Mk 2:28
TAFAKARI:
“Bwana haangalii kama binadamu aangaliavyo; maana wanadamu
huitazama sura ya nje, bali Bwana huutazama moyo.”
Wapendwa wana wa Mungu, ni mang’amuzi yangu na bila shaka
yako pia kwamba Mungu hutenda mambo makuu kwa watu ambao kadiri ya mtazamo wetu
uliojijenga katika mila na desturi utushangaza kabisa. Huyu ndiye Mungu kama asemavyo Mama Bikira
Maria, “Amewaangusha
wakuu katika viti vyao vya enzi; Na wanyonge amewakweza,” Lk 1:52. Mungu wetu
aliye haki, upendo, huruma na wema kamwe hatendi na kutazama kama sisi
wanadamu. Tatizo kubwa la mwanadamu huwa haoni vitu kama vilivyo, bali huviona
vitu kama alivyo yeye. Ni kwa mantiki hii mtu husongwa na mila na desturi
zilizomkuza katika maamuzi yake.
Baada ya
Sauli kukosa sifa mbele za macho ya Mungu, Mungu anafanya zaidi kwa manufaa ya
watu wake. Hivyo Mungu anawachagulia tena Mfalme wana wa Israeli. Samweli
mtumishi wa Mungu anapewa maelekezo na Mungu na anafanya kadiri ya maelekezo
hayo. Yese alikuwa na wana wazuri na wenye uwezo. Pamoja na hayo yote, Mungu
anamchagua yule amtakaye kwa makusudi yake. Baada ya kukosekana yule amtakaye
Mungu, Samweli mtumishi mwaminifu anamuuliza Yese, “Watoto wako wote wapo hapa?
Naye akasema, Amesalia mdogo wao, na tazama, anawachunga kondoo. Basi Samweli
akamwambia Yese, Tuma watu, wamlete; kwa sababu hatutaketi hata atakapokuja
huku,” 1Sam 16:11
Mtazamo
wa leo na msukumo wa kijamii na kisiasa ni vigumu sana kusikia sauti ya Mungu
ndani ya mioyo yetu. Tunaishi sana katika ushabiki na wakati mwingine
tunaingiwa upofu na kutokuona vitu sawasawa. Leo si jambo la ajabu kuona mtu
asiyependwa na watu ndiye anayetangazwa kuwa mshindi na aliyechakuliwa na watu.
Demokrasia yetu leo kwa nchi zenye mfumo wa kimla ni kwamba wengi usema ila
baadhi ndio wanaoamua. Udhalimu huu hauna nafasi mbele ya Mungu. Kilicho cheupe na kiwe cheupe na kilicho giza
na kitambulike kuwa giza. Kwa nini tunatanguliza nafsi zetu mbele zaidi ya kile
atakacho Mungu kupitia watu wake?
Mungu wetu hatazami kama
sisi tutazamavyo katika hulka na ushabiki wetu. Mungu hufanya kadiri na
ukamilifu wake. Nasi kama wanadamu tunaalikwa kila siku kuwa wakamilifu kama
alivyo Mungu wetu. “Basi ninyi mtakuwa wakamilifu, kama Baba yenu wa mbinguni
alivyo mkamilifu,” Mk 5:48. Ni vyema ufahamu uwepo wako hapa duniani. Ndugu
yangu unanyesafiri nami katika tafakari hii elewa kwamba upo hapa nduniani
kupigana kufa na kupona juu ya cheo chako ambacho ni utakatifu wako. Mengine
yote na fahari zake ni mbwembe tu. Huwezi kumwona Mungu kama si mtakatifu. Je,
unajua hilo?
Hivyo, Daudi anapata sifa mbele za Mungu ingawa hakuwa
matarajio ya familia ya Yese. “Lakini Bwana
akamwambia Samweli, Usimtazame uso wake, wala urefu wa kimo chake; kwa maana
mimi nimemkataa. Bwana haangalii kama binadamu aangaliavyo; maana wanadamu
huitazama sura ya nje, bali Bwana huutazama moyo,” 1Sam 16:7. Mungu utazama
moyo ule unaomwelekea na kufanya mapenzi yake. Na katika jambo hili, kutenda
lililo jema hakuwezi kugubikwa na mila na desturi zetu.
Leo
katika Injili Yesu anatukumbusha lililo la muhimu. Ni kweli mila na desturi
zetu zina umuhimu wake, ila sauti ya Mungu ni muhimu zaidi kwa sababu ndiyo
hatma yetu. Wanafunzi wa Yesu wanakoselewa na kulaumiwa kwa kufanya lisilo sahihi
siku ya sabato kadiri ya mapokeo ya kiyahudi. Yesu anawajibu, “Sabato
ilifanyika kwa ajili ya mwanadamu, si mwanadamu kwa ajili ya sabato,” Mk 2:27.
Utu wa mtu ni kitu cha kwanza kabisa kutazama zaidi ya mitazamo. Ndani ya mtu
kuna chapa ya Mungu ndani yake. Mtu lazima aheshimiwe kama alivyo bila
kuangalia nafasi na cheo chake katika jamii. Hivyo Kristo ndiye sababu ya yake
yote kuyafanyayo. “Basi Mwana wa Adamu ndiye Bwana wa sabato pia,” Mk 2:28. Kristo
amekuja kuitakatifuza sheria na kuikamilisha. “Msidhani ya kuwa nalikuja kuitangua torati au manabii; la,
sikuja kutangua, bali kutimiliza,” Mt 5:17. Binadamu na utu wake kwanza,
mengine yafuate.
Tumsifu Yesu Kristo
“Toka mbinguni Bwana huchungulia, Huwatazama wanadamu wote
pia. Toka mahali pake aketipo
Huwaangalia wote wakaao duniani,” Zab 33:13-14
No hay comentarios:
Publicar un comentario