IJUMAA WIKI YA 2 YA MWAKA-C
22/1/2016
Somo: 1Sam 24:3-21
Zab: 57:2, 3-4, 6, 11
Injili: Mk 3:13-19
Nukuu:
“Tena, baba yangu,
tazama, tafadhali, tazama upindo wa vazi lako mkononi mwangu; maana ikiwa
nimeukata upindo wa vazi lako, nisikuue, ujue, na kuona ya kuwa hakuna uovu
wala kosa mkononi mwangu, wala sikukukosa neno; ingawa wewe unaniwinda roho
yangu ili kuikamata,” 1 Sam 24:11
“Bwana atuamue, mimi
na wewe, na Bwana anilipizie kisasi changu kwako; lakini mkono wangu hautakuwa
juu yako,” I Sam 24:12
“Akamwambia Daudi,
Wewe u mwenye haki kuliko mimi; maana wewe umenitendea mema, nami nimekutenda
mabaya. Nawe umeonyesha leo jinsi
ulivyonitendea mema, kwani Bwana aliponitia mikononi mwako, hukuniua,” 1Sam
24:17-18
“Na sasa, angalia,
najua ya kuwa hakika utakuwa mfalme, na ufalme wa Israeli utafanyika imara
mkononi mwako,” 1 Sam 24:20
“Akaweka watu kumi na
wawili, wapate kuwa pamoja naye, na kwamba awatume kuhubiri, tena wawe na amri ya
kutoa pepo,” Mk 3:14-15
TAFAKARI: “Ushinde uovu kwa kutenda wema.”
Wapendwa wana wa Mungu, ni hali ya ubinadamu wetu kurudisha
kwa kiwango kile kile cha uovu tulichotendewa na watesi wetu. Ila kwa kufanya
hivyo hata kama kutatupatia furaha na amani, amani na furaha hiyo ni ya muda
mfupi tu. Uovu si asili ya ukamilifu ambao ni Mungu mwenyewe. Kumbe amani ya
kweli tunaipata pale tunapoushinda uovu kwa wema. Tusipoteze muda kushindana na
uovu, bali tuenende kwa kutenda mema. “Lakini mimi nawaambia, Msishindane na mtu mwovu; lakini mtu
akupigaye shavu la kuume, mgeuzie na la pili,” Mt 5:39. Kumgeuzia mtesi wako
shavu la pili kuna maana ya kutokulipiza kisasi zaidi ya kuenenda katika
kutenda mema. Wengi kati yetu twaonekana waovu na watenda maovu kwa sababu
katika maisha yetu hatujawahi kuonyeshwa upendo wa kweli.
Ugomvi kati ya Mfalme Sauli na Daudi ni matokeo ya wivu.
Jambo la ajabu na kujifunza kutoka kwa Daudi ni uelewa wake juu ya Ufalme kama
dhamana na kile kilichompasa kufanya, yaani kuushinda uovu kwa wema. Mungu
aliujaribu moyo wa Daudi kwa kumweka
Sauli katika mikono yake na kumwamuru kumfanya atakacho. Ila Daudi
hakuruhusu kisasi kiwe silaha katika maisha yake. Kwa kuonyesha nia njema
aliyokuwa nayo Daudi, anamwambia Mfalme wake na kuonyesha uovu wake, “Tena, baba yangu, tazama, tafadhali, tazama upindo wa vazi lako
mkononi mwangu; maana ikiwa nimeukata upindo wa vazi lako, nisikuue, ujue, na
kuona ya kuwa hakuna uovu wala kosa mkononi mwangu, wala sikukukosa neno;
ingawa wewe unaniwinda roho yangu ili kuikamata,” 1 Sam 24:11. Daudi ni mfano
mzuri kwetu wa kuwa na hofu ya Mungu. Daudi anayaweka yote mikononi mwa Mungu
kama mwamuzi wa kweli na wa haki. “Bwana atuamue, mimi
na wewe, na Bwana anilipizie kisasi changu kwako; lakini mkono wangu hautakuwa
juu yako,” I Sam 24:12. Uovu unamwisho wake kwa sababu siyo makusudi ya Mungu.
Wema una umilele kwa sababu ndiyo makusudi ya Mungu katika maisha yetu.
Wapendwa
wana wa Mungu, kuna ushindi mkubwa sana kwa kutenda wema pale tunapotendewa
uovu. Tendo hili ni shule nzuri sana kwa watesi wetu. Mfalme Sauli alipaza sauti
yake akalia, “Akamwambia Daudi, Wewe u mwenye haki kuliko mimi; maana wewe
umenitendea mema, nami nimekutenda mabaya. Nawe
umeonyesha leo jinsi ulivyonitendea mema, kwani Bwana aliponitia mikononi
mwako, hukuniua,” 1Sam 24:17-18. Kurudisha mema pale tunapotendewa mabaya ndiyo
njia pekee ya kumfundisha mtu mwovu. Hiki ndicho kitanzi kikubwa kuliko vyote
kama kweli unataka kumniga mtesi wako kuliko kujibizana na kupigana naye. Sauli
anakiri uovu wake na kuelewa mpango wa Mungu kwake na kwa yule aliyekuwa anamtendea
uovu, yaani, Daudi. Mfalme Sauli anamwambia Daudi kwa kinywa chake, “na sasa, angalia, najua ya kuwa hakika utakuwa mfalme, na ufalme
wa Israeli utafanyika imara mkononi mwako,” 1 Sam 24:20. Ndugu yangu kwa wivu
wako huwezi kuibadili nyote ya rafiki au jirani yako.
Mpendwa
katika Kristo, jitahidi kila siku kutambua vipawa vyako na vitendee haki kwani
kwa kuvijua ndivyo utakavyoweza kumtumikia Mungu vizuri katika maisha yako.
Usipoteze muda wako kuvikodolea macho vipawa vya wengine na kutokufanya chochote
kuhusu vile alivyokupa Mungu ambavyo bado hujavigundua. Moja ya kuwa mikono
salama ya Mungu ni kufanya mapenzi yake, na hasa kuwa mwaminifu kwa kile
unachokifanya sasa. Kwa kuliwezesha hili, Yesu anawafunda wanafunzi wake
waenende katika idadi ya watu kumi na mbili kama moja ya njia ya kufanya vizuri
na kuwa na mshikamano. Hivyo Yesu, “akaweka watu kumi na
wawili, wapate kuwa pamoja naye, na kwamba awatume kuhubiri, tena wawe na amri ya
kutoa pepo,” Mk 3:14-15. Umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu.
Tumsifu
Yesu Kristo!
“Wabaya huinama mbele ya wema, Na wasio haki malangoni mwao
wenye haki,” Mit 14:19
No hay comentarios:
Publicar un comentario