domingo, 3 de enero de 2016

TAFAKARI: JUMATATU, KIPINDI CHA NOELI

JUMATATU, KIPINDI CHA NOELI
4/1/2016
Somo: 1Yoh 3:7-10
Zab: 97:1, 7-8, 9
Injili: Yoh 1:35-42
Nukuu:
Watoto wadogo, mtu na asiwadanganye; atendaye haki yuna haki, kama yeye alivyo na haki,” 1Yoh 3:7

atendaye dhambi ni wa Ibilisi; kwa kuwa Ibilisi hutenda dhambi tangu,” 1Yoh 3:8

Katika hili watoto wa Mungu ni dhahiri, na watoto wa Ibilisi nao. Mtu ye yote asiyetenda haki hatokani na Mungu, wala yeye asiyempenda ndugu yake,” 1Yoh 3:10 

Akamtazama Yesu akitembea, akasema, Tazama, Mwana-kondoo wa Mungu!” Yoh 1:36

Yesu aligeuka, akawaona wakimfuata, akawaambia, Mnatafuta nini? Wakamwambia, Rabi, (maana yake, Mwalimu), unakaa wapi?” Yoh 1:38

Akawaambia, Njoni, nanyi mtaona. Wakaenda, wakaona akaapo, wakakaa kwake siku ile. Nayo ilikuwa yapata saa kumi,” Yoh 1:39

Andrea, nduguye Simoni Petro, alikuwa mmoja wa wale wawili waliomsikia Yohana na kumfuata Yesu,” Yoh 1:40
Huyo akamwona kwanza Simoni, ndugu yake mwenyewe, akamwambia, Tumemwona Masihi (maana yake, Kristo),” Yoh 1:41

Akampeleka kwa Yesu. Naye Yesu akamtazama, akasema, Wewe u Simoni, mwana wa Yohana; nawe utaitwa Kefa (tafsiri yake Petro, au Jiwe),” Yoh 1:42

TAFAKARI: Yesu akawaambia, Mnatafuta nini? Wakamwambia, Rabi, (maana yake, Mwalimu), unakaa wapi?” Yoh 1:38

Wapendwa wana wa Mungu, kila mmoja wetu kwa kuishi kwake hapa duniani utafuta maana ya maisha yake. Kwa maana nyingine yote uyafanyayo mwisho wake nini? Yohane Mbatizaji akiwa na wanafunzi wake wawili anamwona Yesu kwa mbali na kusema, “Tazama, Mwana-kondoo wa Mungu!” Yoh 1:36. Kwa maneno haya, Yohane Mbatizaji anaona hitimisho lote kwa Yesu. Huyu ndiye tumtazamiaye na tumtafutaye kwani kwake upo ukamilisho wote. Pamoja na ukweli huu, Yesu anauliza swali la msingi kabisa, ‘Mnatafuta nini?’ Kwa maana nyingine Yesu anataka kujua haya kutoka kwako na kwangu; pamoja na mahangaiko uliyonayo nini msingi wa maisha yako? Nini kisukumacho maisha yako na kufanya ufanyavyo? Na mwisho, nini hatma ya hayo yote? Maisha ya mtu yaweza kuongozwa na hali zifuatazo ambazo kwa uhakika hali hizo hazitatupeleka kule Yesu aliko na anapotaka tuwe.

1. Watu wengi huongozwa na hatia.

Watu hawa hutumia muda wa maisha yao yote wakiepuka lawama na kuficha aibu. Watu wanaoongozwa na hatia wanaonewa sana na kumbukumbu. Wanaruhusu mambo yaliyopita kutawala mambo yao ya usoni. Wanajiadhibu bila kujua kwa kuharibu mafanikio yao. Kaini alipotenda dhambi, hatia yake ilimtenga na Mungu, na Mungu akasema, "utakapoilima ardhi haitakupa mazao yake; utakuwa mtoro na mtu asiye na kikao duniani," Mwa 4:12. Hii inawaeleza jinsi watu wengi walivyo siku hizi-wanatangatanga katika maisha bila lengo. Mfano mzuri angalia katika vyama vyetu vya kitume. Wapo walio wengi huama chama kimoja cha kitume kwenda kingine na mwisho huishia katika nyumba za sala. Nyumba za sala hapa ninamaanishisha vijikanisa vinavyojiibua na kujiinua kwa wachungaji wao kuwa manabii.

Ndugu yangu, sisi ni matokeo ya muda wetu uliopita lakini hatupaswi kuwa wafungwa wa muda huo. Kusudi la Mungu halifungwi na muda wako uliopita. Ona! Alimbadilisha muuaji Musa na kuwa kiongozi mzuri; akambadilisha Gidioni aliyekuwa mwoga akawa shujaa na hodari; anaweza kufanya mambo ya ajabu na maisha yako yaliyobaki. Tazama pia maisha ya Mt. Augustino wa Hippo kabla na baada ya kuongoka kwake.

Mungu ni mtaalam wa kutupa mawazo mapya. "Heri aliyesamehewa dhambi, na kusitiriwa makosa yake," Zab 32:1. Kwa maana nyingine twaweza kusema, "wana furaha kubwa wale waliosamehewa hatia zao. Na wana amani wale waliotubu dhambi zao na Mungu amefuta mashtaka yao." Ni kwa Kristo tu tupo huru tunapoziungama dhambi zetu. Watoto wadogo, mtu na asiwadanganye; atendaye haki yuna haki, kama yeye alivyo na haki; atendaye dhambi ni wa Ibilisi; kwa kuwa Ibilisi hutenda dhambi tangu,” 1Yoh 3:7-8.

2. Watu wengi wanaongozwa na chuki na hasira.

Wapendwa wana wa Mungu, kati yetu wapo wanaoshikilia maumivu (machungu) bila kuyaacha. Badala ya kutoka katika maumivu kwa kusamehe, wanaendelea kuyakumbuka katika mawazo yao tena na tena. Baadhi ya watu wanaongozwa na chuki kutunza ndani uchungu wao, na wengine huwalipukia watu wengine. Hali zote hizi si nzuri na hazisaidii maishani. Chuki mara nyingi huleta maumivu kwako kuliko yule unayemchukia. Mtu aliyekukosea anaweza kuwa amesahau lile kosa na anaendelea na maisha yake vizuri, wewe unaendelea kuumia na kuhangaika na yaliyopita.

Sikiliza ndugu yangu: Wale waliokuumiza wakati uliopita hawawezi kuendelea kufanya hivyo sasa "isipokuwa" kama utaendelea kutunza uchungu. Yakiyopita yamepita! Hakuna kitakachoyabadilisha. Unajiumiza tu na uchungu wako. Kwa ajili yako, jifunze kutokana na hilo na kisha achana nalo. Maandiko matakatifu yanatuakumbusha kuwa, "kwani hasira humwua mtu mpumbavu, nao wivu humwua mjinga." Ayu 5:2.  Kuwa na hofu kiasi cha kufa kwa sababu ya uchungu ni upumbavu, ni kitu kipumbavu kukifanya. Ndugu, kwa nini wajifungia katika tanuru hili? Katika hili watoto wa Mungu ni dhahiri, na watoto wa Ibilisi nao. Mtu ye yote asiyetenda haki hatokani na Mungu, wala yeye asiyempenda ndugu yake,” 1Yoh 3:10.

3. Watu wengi wanaongozwa na woga.

Ndugu, woga hapa unaweza kutokana na jambo baya sana lililokupata au lililowapata, matarajio yasiyotekelezeka, kukulia katika jamaa isiyo na uhuru, au hata maumbile ya asili. Bila kujua sababu, watu wanaongozwa na woga mara nyingi hupitwa na nafasi kubwa kwa sababu wanaogopa kuchukua hatua. Badala yake wanajitahidi kuwa salama, wakiepuka hasara na hivyo hujaribu kulinda hadhi yao. Woga ni kifungo ambacho mtu hujifunga mwenyewe na chaweza kukuzuia kuwa mtu yule ambaye Mungu anapenda uwe.
Unatakiwa kutoka humo kwa silaha ya IMANI na UPENDO. "Katika pendo hamna hofu; lakini pendo lililo kamili huitupa nje hofu, kwa maana hofu ina adhabu, na mwenye hofu hakukamilishwa katika pendo." 1Yoh 4:18. Kwa maneno mengine, upendo halisi huiondoa hofu kwa kuwa hofu hulemaza, maisha ya hofu-hofu ya kifo, hofu ya hukumu- ni maisha ambayo hayajakamilika katika upendo.

4. Watu wengi wanaongozwa na mali

Ndugu tupo pamoja? Tamaa yao ya kupata vitu linakuwa ndilo lengo la maisha yao yote. Jambo hili haijalishi upo utawani au kwenye maisha ya ndoa. Msukumo huu wa kutaka zaidi kila siku una misingi yake katika udanganyifu wa kuwa nikiwa na vingi nitakuwa na furaha zaidi, nitakuwa wa muhimu, na nitakuwa salama; lakini mawazo hayo yote matatu si ya kweli. Mali huleta furaha ya "muda mfupi tu." Na sababu kubwa ndugu yangu, vitu havibadiliki, hivyo vinatuchosha na tunataka vipya, vikubwa, na bora zaidi.

Kuna imani pia kwamba nitapata mali nyingi nitakuwa wa muhimu. Umuhimu wako na mali ni vitu viwili tofauti. Thamani yako haitegemei mali zako, Mungu anasema kitu cha muhimu maishani mwako si vitu! Imani ya watu wengi kuhusu fedha ni kwamba kuwa nazo nyingi kutanipa usalama. Huwezi! Tulio utawani hatuchoki kuwa na tumiradi binafsi twa siri twingiiii. Usicheke ndiyo ukweli kwa baadhi yetu. Mambo yanapokwenda vibaya kwenye huto tumiradi tupresha twa kupanda na kushuka hatukomi. Yesu anawaambia wale wafuasi wa Yohane Mbatizaji, “Mnatafuta nini?” Wanafunzi wale wakamjibu,  Rabi, (maana yake, Mwalimu), unakaa wapi?” Yoh 1:38. Anapokaa Yesu ndipo kwenye usalama kupita vitu vyote na hali zote tunazoweza kufikiria. Mt. Augustino anasema, “mioyo yetu haitulii mpaka itakapotulia kwako Ee Bwana.”

Ndugu yangu, utajiri unaweza kupotezwa mara moja kwa sababu zisizozuilika. Usalama halisi unaweza kupatikana katika kile ambacho huwezi kunyang'anywa yaani uhusiano wako na Mungu. Mt. Augustino anatuwasa kutoka kwenye kanuni yake, "kuna furaha kubwa kuwa na vichache kuliko kuwa na vingi." Hata hivyo tatizo hapa ni kipimo cha huo uchache na huo wingi.

5. Watu wengi wanaongozwa na kutaka sifa

Ndugu yangu, wakati mwingine watu hawa wanaruhusu matarajio ya wazazi, waume, au wake, watoto, waalimu au rafiki zao kutawala maisha yao. Watu wazima bado wanajaribu kupata sifa kwa wazazi wao ambao hawajafurahi kamwe. Wengine wanasukumwa na vikundi vya marafiki, wanahofu wenzao watawafikiriaje. Kwa bahati mbaya, wale wafuatao kundi au maoni ya mtu binafsi hupotea ndani yake. Ndugu yangu, kwa nini kujifungia katika gereza hili la fikra na maoni?

Ndugu yangu mpendwa katika Kristo, sijui funguo zote za mafanikio, lakini ufunguo mmoja wa kushindwa ni kujaribu kumpendeza kila mtu. Kutawaliwa na maoni ya watu wengine ni njia wazi ya kukosa makusudi ya Mungu katika maisha yako. Bwana wetu Yesu Kristo anatupa angalizo kwa jambo hili, "hakuna mtu awezaye kutumikia mabwana wawili; kwa maana atamchukia huyu, na kumpenda huyu, ama atashindana na huyu na kumdharau huyu: hamwezi kumtumikia Mungu na mali." Mt 6:24.

Kuna nguvu nyingi zinazoweza kuongoza maisha yako lakini zote mwisho wake ni mfu: kutotumia vipawa ulivyo navyo, mahangaiko ya moyo, na maisha yasiyo ya utoshelevu.
Ndugu yangu, kuishi maisha yanayoongozwa na malengo, ni kutawaliwa, na kuelekezwa na makusudi ya Mungu. Hakuna kitu cha muhimu zaidi kama kujua malengo ya Mungu kwa maisha yako, na hakuna mbadala kwa hilo-siyo mafanikio, utajiri, kujulikana, au anasa. Bila malengo, maisha ni mwendo usio na maana, shughuli bila mwelekeo, na matukio bila sababu. Bila malengo, maisha ni kitu duni, kidogo sana, kisicho na umuhimu wowote.

Wapendwa wana wa Mungu, usalama wetu upo ndani na katika Kristo. Yesu leo anatuambia, Njoni, nanyi mtaona,” Wanafunzi wale wa Yohane Mbatizaji waliunjo amani ya kweli kwa muda ule waliofuatana na Yesu na kukaa naye jioni ile. “Wakaenda, wakaona akaapo, wakakaa kwake siku ile. Nayo ilikuwa yapata saa kumi,” Yoh 1:39. Unapogundua siri hii usiacha mshirikisha na mwenzako furaha hii iliyopo ndani na katika Kristo kama alivyofanya Andrea kwa ndugu yake Simoni. Huyo akamwona kwanza Simoni, ndugu yake mwenyewe, akamwambia, Tumemwona Masihi (maana yake, Kristo),” Yoh 1:4. Huu ni wajibu wa kila mbatizwa kuwapeleka wale wote wenye hofu ya Mungu kwa Kristo. Wewe uliyesafiri nami katika tafakari hii una deni hili kubwa kwa Kristo.

Tumsifu Yesu Kristo!


Ikinibidi kujisifu, nitajisifia mambo ya udhaifu wangu,” 2Kor 11:30

No hay comentarios:

Publicar un comentario