JUMAMOSI WIKI YA 3 YA MWAKA-C
30/1/2016
Somo: 2Sam 12:1-7a, 10-17
Zab: 59:12-17
Injili: Mk 4:35-41
Nukuu:
“Ndipo hasira ya Daudi ikawaka sana juu ya mtu yule;
akamwambia Nathani, Aishivyo Bwana, mtu huyo aliyetenda jambo hili, hakika yake
astahili kufa; naye atamrudishia
yule mwana-kondoo mara nne, kwa sababu ametenda neno hili, na kwa sababu hakuwa
na huruma,” 2Sam 12:5-6
“Basi Nathani akamwambia Daudi, Wewe ndiwe mtu huyo,” 2Sam
12:7
“Basi, sasa upanga hautaondoka nyumbani mwako, kwa sababu umenidharau,
ukamtwaa mkewe Uria, Mhiti, kuwa mke wako,” 2Sam 12:10
“Daudi akamwambia Nathani, Nimemfanyia Bwana dhambi. Nathani
akamwambia Daudi, Bwana naye ameiondoa dhambi yako; hutakufa,” 2Sam 12:12
“Naye mwenyewe
alikuwapo katika shetri, amelala juu ya mto; wakamwamsha, wakamwambia, Mwalimu,
si kitu kwako kuwa tunaangamia?” Mk 4:38
“Akaamka, akaukemea
upepo, akaiambia bahari, Nyamaza, utulie. Upepo ukakoma, kukawa shwari kuu,” Mk
4:29
“Akawaambia, Mbona
mmekuwa waoga? Hamna imani bado?” Mk 4:40
“Wakaingiwa na hofu
kuu, wakaambiana, Ni nani huyu, basi, hata upepo na bahari humtii?”
Mk 4:41
TAFAKARI: “Wewe ndiye Mtu
huyo.”
Wapendwa
wana wa Taifa la Mungu, kunatofauti kubwa kuusema ukweli na kuuishi ukweli.
Kuna tofauti kubwa pia ya kuhubiri haki na kutenda haki. Vile vile kunatofauti
kubwa sana ya kusema kuhusu upendo na kuishi upendo. Kuyasema mambo kwa ufasaha
ni taaluma ambayo mtu anaweza kuipa kwa kupitia njia na miongozo inayohusu
jambo hilo. Kuishi jambo fulani ni kugeuzwa na jambo hili na kuwa sehemu ya
jambo hilo. Kumbe kwa namna nyingine kama wasemavyo waswahili, ‘kuna kusoma na
kuelimika.’ Hivi ni vitu viwili tofauti.
Nabii
Nathani anatumwa na Mungu kwenda kwa Mfalme Daudi na kumwambia chukizo
alilomfanyia. Nathani anamweleza Daudi uzito wa tatizo na dhambi aliyoifanya
kwa jamii, kwa yeye mwenyewe na kwa Mungu. Kwa nafasi aliyokuwa nayo Daudi kama
Mfalme ilimpasa awe mtetezi wa kweli, haki, Amani na Upendo. Ufalme wake kama
ulivyo uliwakilishwa na taswira na fadhila hizo. Badala yake, Daudi anakuwa
muhujumu wa hiyo kweli, haki, Amani, na Upendo. Huu ndio ule mfano wa mtu yule
aliyekuwa na kondoo wake mmoja na aliyempenda kupita vitu vyote. Nathani hapa
anamaanisha, mtu yule ni Uria, na kondoo wake ni mkewe Bath-sheba Daudi aliyezini naye, na matokeo yake kupelekea umauti wa
Uria. Kama Kondoo, yaani wanawake, Daudi alikuwa nao wengi na ofisi yake kama
Mfalme iliruhusu kuwa na wake hao wengi.
Mazungumzo ya Nabii Nathani na Mfalme Daudi kwa kupitia mfano
wa Mtu na Kondoo wake aliyekuwa anampenda na hivyo kudhulumiwa, yanaamasisha
sifa kuu na uwepo wa falme yoyote ile iliyo kwa ajili ya watu, yaani: ufalme wa
haki, amani, kweli, na upendo. Hivyo Mfalme Daudi anaguswa na mfano ule na
kumwambia Nabii Nathani, “Aishivyo Bwana, mtu huyo aliyetenda jambo hili,
hakika yake astahili kufa; naye
atamrudishia yule mwana-kondoo mara nne, kwa sababu ametenda neno hili, na kwa
sababu hakuwa na huruma,” 2Sam 12:5-6. Mfalme Daudi anajiweka kitanzi mwenyewe
kwa makosa yake. Ndugu yangu, kumbuka maneno ya Yesu, “Wapeni watu vitu,
nanyi mtapewa; kipimo cha kujaa na kushindiliwa, na kusukwa-sukwa hata
kumwagika, ndicho watu watakachowapa vifuani mwenu. Kwa kuwa kipimo kile kile
mpimacho ndicho mtakachopimiwa,” Lk 6:38. Ni kwa mizania hii, Nabii Nathani
anamwambia Daudi bila kupepesa macho, “Wewe ndiwe mtu huyo,” 2Sam 12:7. Hivyo kosa na adhabu inamstahili yeye mwenyewe.
Mungu
anatoa adhabu kwa Mfalme Daudi kwa kosa lile ambayo ni chukizo kwake mwenyewe
kama Mfalme na mtetezi wa haki za watu, chukizo na makwazo kwa jamii, na
chukizo kwa Mungu aliye haki, kweli, amani, na pendo. “Basi, sasa upanga hautaondoka nyumbani mwako,
kwa sababu umenidharau, ukamtwaa mkewe Uria, Mhiti, kuwa mke wako,” 2Sam 12:10.
Kwa kutambua kosa lake na kulikiri, Mungu anathibitisha kuwa Yeye ni Upendo na
Huruma na kumwondolea adhabu ya kifo Mfalme Daudi. “Daudi akamwambia Nathani, Nimemfanyia Bwana dhambi. Nathani
akamwambia Daudi, Bwana naye ameiondoa dhambi yako; hutakufa,” 2Sam 12:12.
Pamoja na hayo, kiumbe kile kama tokeo la uzinifu wa Daudi hakikuishi.
Wapendwa katika Kristo, wewe na mimi kwa njia moja au
nyingine tumefanya kama Daudi na wakati mwingine zaidi hata ya Daudi. Hakuna
njia nyingine ya kujikwamua katika hali hii zaidi ya kufanya toba ya kweli na
majuto. Mungu aliye mwingi wa rehema na upendo yu tayari kutusamehe. Kwa maana “Wewe, Bwana, U Mungu wa rehema na neema,
Mvumilivu, mwingi wa fadhili na kweli,” Zab 86:15. Amina
Injili ya leo
inatufundisha kwamba tukiamini nguvu na uwepo wa Mungu yote huwa salama. Maisha
ni kama chombo cha kusafiri baharini, kuna nyakati husongwa na dhoruba kali. Chombo chetu cha kusafiri
“Mtumbwi”-pale tulipo, iwe maisha ya ndoa, au kitawa huanza kuzama kutokana na
dhoruba kali-changamoto nyingi katika maisha. Hata hivyo, katika hali hii Bwana
wetu Yesu Kristo si kwamba yupo mbali na dhoruba hizi. Katika sintofahau
habarini, wanafunzi wake Yesu walianza kupiga mayowe kwa hofu ya kuzama maji.
Yesu alikuwa nao, ila kalala. Wanafunzi wanamlalamikia Yesu wakiwa na tafsiri
ya Yesu kutokujali kuagamia kwao. Yesu hana muda wa kujibizana nao zaidi ya
kuokoa maisha kwanza. “Akaamka, akaukemea upepo, akaiambia bahari, Nyamaza,
utulie. Upepo ukakoma, kukawa shwari kuu,” Mk 4:29. Ndipo Yesu akawaambia, “Mbona mmekuwa waoga? Hamna imani bado?” Mk 4:40.
Mara nyingi tunapopatwa na
matatizo na mahangaiko katika maisha tunakosa utulivu na kuhangaika hapa na
pale, kuagua kwa mganga moja na mwingine, na kufanya matambiko kwa kila mzimu
katika ukoo. Kitu cha kwanza ndugu yangu yakupasa kuutafuta utulivu wa ndani.
Utulivu wa ndani tunaupata kwa Kristo mwenyewe kwa kuwa na Imani naye. Yesu
anatuambia, “Njoni
kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha. Jitieni nira yangu,
mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata
raha nafsini mwenu; kwa maana nira yangu ni laini, na
mzigo wangu ni mwepesi,” Mt 11:28-30. Je, yupo zaidi ya Yesu? Kwa akili yako tu
bila Yesu hutoweza, kwa umashuhuri wako tu bila Yesu hutoweza, kwa utajiri wako
tu bila Yesu hutoweza, na kwa nguvu ya madaraka yako tu bila Yesu hutoweza pia.
Basi na tuwe na hofu ya Mungu ndani yetu hata kama hatujamjua Yesu. Tuongozwe
na dhamiri njema katika utu wema.
Tumsifu Yesu Kristo!
“Kwa maana Wewe, Bwana, U mwema, Umekuwa tayari kusamehe, Na
mwingi wa fadhili, Kwa watu wote wakuitao,” Zab 86:5
No hay comentarios:
Publicar un comentario