miércoles, 6 de enero de 2016

TAFAKARI: ALHAMISI BAADA YA EPIFANIA, KIPINDI CHA NOELI

ALHAMISI BAADA YA EPIFANIA, KIPINDI CHA NOELI
7/1/2016
Somo: 1Yoh 4:19-5:4
Zab: 72:1-2, 14, 15abc, 17
Injili: Lk 4:14-22
Nukuu:
Sisi twapenda kwa maana yeye alitupenda sisi kwanza,” 1Yoh 4:19

Mtu akisema, Nampenda Mungu, naye anamchukia ndugu yake, ni mwongo; kwa maana asiyempenda ndugu yake ambaye amemwona, hawezi kumpenda Mungu ambaye hakumwona,” 1Yoh 4:20

Katika hili twajua kwamba twawapenda watoto wa Mungu, tumpendapo Mungu, na kuzishika amri zake.” 1Yoh 5:1 

Kwa maana kila kitu kilichozaliwa na Mungu huushinda ulimwengu; na huku ndiko kushinda kuushindako ulimwengu, hiyo imani yetu,” 1 Yoh 5:4 

Roho wa Bwana yu juu yangu, Kwa maana amenitia mafuta kuwahubiri maskini habari njema. Amenituma kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao, Na vipofu kupata kuona tena, Kuwaacha huru waliosetwa, Na kutangaza mwaka wa Bwana uliokubaliwa,” Lk 4:18-19 

Akaanza kuwaambia, Leo maandiko haya yametimia masikioni mwenu,” Lk 4:21 

Wakamshuhudia wote, wakiyastaajabia maneno ya neema yaliyotoka kinywani mwake, wakasema, Huyu siye mwana wa Yusufu?” Lk 4:22

TAFAKARI:Mtu akisema, Nampenda Mungu, naye anamchukia ndugu yake, ni mwongo.”
Wapendwa wana wa Mungu, si jambo la ajabu kati yetu kuona mtu kila siku hakosi katika ibada mbalimbali ikiwa ni pamoja na kushiriki Misa Takatifu za kila siku. Kwa Mkristo mwenye hofu ya Mungu ni jambo jema kwani amechagua fungu lililo jema kama Yesu alivyomwambia Martha ndugu yake Mariamu ambaye alionekana anajishughulisha sana na kazi kama kazi. Bwana akajibu akamwambia, Martha, Martha, unasumbuka na kufadhaika kwa ajili ya vitu vingi; lakini kinatakiwa kitu kimoja tu; na Mariamu amelichagua fungu lililo jema, ambalo hataondolewa,” Lk 10:41-42. Lakini pamoja na uchaji huu ambao unaonekana kwa watu kama tendo jema, hauendani na namna baadhi yetu tunavyoishi na ndugu zetu na majirani zetu. Leo kuwa kwako mwanachama wa shirika fulani la kitume, au chama cha kitume na kushiriki kila siku sala katika chama hicho cha kitume ilhali hauna uelewano na ndugu yako, wazazi wako au jirani kuna maana gani??? Mtu akisema, Nampenda Mungu, naye anamchukia ndugu yake, ni mwongo; kwa maana asiyempenda ndugu yake ambaye amemwona, hawezi kumpenda Mungu ambaye hakumwona,” 1Yoh 4:20. Ni Mungu gani huyo unayempenda na kumwabudu? Ukweli ni kwamba, Sisi twapenda kwa maana yeye alitupenda sisi kwanza,” 1Yoh 4:19. Hivyo kama shukrani na kutambua upendo huu wa Mungu, yanipasa kuwapenda wote wanaonizunguka bila kujali historia zao, uhusiano uliopo kati yangu na wao,  familia zao, koo zao, kabila zao, jiografia zao, na utaifa wao. Yanipasa nimpende huyo kwa sababu ana sura na mfano wa Mungu na anaufunua Utukufu wa Mungu kama mimi nilivyosehemu ya Utukufu huo wa Mungu.

Si jambo la ajabu pia kati yetu kila siku tunasali sala ya Baba Yetu, Sala ya kutubu, kuzitaja amri za Mungu kama kasuku, na kushiriki Ekaristi Takatifu ili hali naishi kama kisiwa. Je, naonja moyoni ninayotamka mdomoni? Kipimo cha upendo kama asemavyo Mt. Augustino ni kupenda bila kipimo. Hivyo hivyo mizania ya kusamehe ni kusamehe bila kipimo. Na ndivyo ilivyo katika sala ya Baba yetu, “utusamehe makaso yetu kama vile tunavyowasamehe wale waliotukosea, Lk 11:4.” Kumbe msamaha wa makosa yetu ni mizania ya kuwasamehe wale tuliowakosea. Je, ninalitambua jambo hili? Ni Katika hili twajua kwamba twawapenda watoto wa Mungu, tumpendapo Mungu, na kuzishika amri zake.” 1Yoh 5:1. Bila shaka mimi na wewe tumekuwa kama yule ndege KASUKU aliye maarufu kurudia maneno asiyoyajua.

Wapendwa wana wa Mungu, katika vita hii ya kuushinda ubinadamu wetu kwa kutenda yale yampendezayo Mungu yatupasa kuzama zaidi ndani na kuzaliwa upya katika Roho Mtakatifu kama asemavyo Mtume Paulo. Kuzaliwa huku si kwa matendo ya mwili, bali kwa rehema ya Mungu. Hii ni nguvu ya ziada kutoka kwa Mungu mwenyewe. Hivyo, si kwa sababu ya matendo ya haki tuliyoyatenda sisi; bali kwa rehema yake, kwa kuoshwa kwa kuzaliwa kwa pili na kufanywa upya na Roho Mtakatifu; ambaye alitumwagia kwa wingi, kwa njia ya Yesu Kristo Mwokozi wetu; ili tukihesabiwa haki kwa neema yake, tupate kufanywa warithi wa uzima wa milele, kama lilivyo tumaini letu,” Tit 3:5-7. Huu ndio uthibitisho wa sisi kuzaliwa na Mungu, kwa ajili ya Mungu, na kwa sababu ya Mungu ili kuushinda ulimwengu kwa imani hiyo. Kwa maana kila kitu kilichozaliwa na Mungu huushinda ulimwengu; na huku ndiko kushinda kuushindako ulimwengu, hiyo imani yetu,” 1 Yoh 5:4. Je, bila kusamehe wathubutu kusema kweli unampenda Mungu?

Yesu Kristo ndiye mfano hai na hali kwetu wa kuiga na kufuata hata kama kwa hali yetu na ubinadamu wetu si rahisi. Leo Yesu katika Sinagogi huko Nazareti, wanapomjua vizuri anawaacha midomo wazi. Ni kweli walimfahamu Yesu katika maana ya historia yake. Mara zote tunajisikia vizuri na nyumbani pale tunapofikiri sawa, na hata kuishi maisha yaliyowiyana. Kwa hali hii tunahitaji nguvu ya pekee kuwa tofauti. Yesu anatufundisha kuwa tofauti na kutokufanya mambo kimazoea. Ukweli na hali ibaki kama ilivyo. Yesu kama ilivyokuwa kawaida ya siku ya sabato, anaingia kwenye sinagogi na kulisoma neno la Mungu, Roho wa Bwana yu juu yangu, Kwa maana amenitia mafuta kuwahubiri maskini habari njema. Amenituma kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao, Na vipofu kupata kuona tena, Kuwaacha huru waliosetwa, Na kutangaza mwaka wa Bwana uliokubaliwa,” Lk 4:18-19. Hii ndiyo tofauti ya Yesu na kauli mbiu yake. Hiki ndicho kinachomtofauti Yesu na wengine ingawa neno hili lilishasomwa na wengi waliomtangulia. Kwa kukazia Yesu anasema, “Leo maandiko haya yametimia masikioni mwenu,” Lk 4:21. Maneno haya ndiyo msukumo wa mabadiliko yote na mtazamo mpya juu ya Yesu.

Mwana sayansi Isaac Newton wa Uingereza (1643-1727) alipolichukua jiwa na kulirusha juu na likarudi ardhini na kugundua nadharia “theory” ya mvutano “gravitation,”  hakuwa mwanadamu wa kwanza kurusha jiwe juu na likarudi ardhini. Ila kwa kwenda zaidi ya mazoea ya urushwaji wa jiwe na kurudi ardhini ndiko kunakomfanya leo tofauti na wengine waliomtangulia. Yesu anatualika kutokuishi kwa mazoea, bali tuende zaidi ya kile kilichozoeleka. Ukweli huu ni kwa hali zote za maisha na kwa namna ya pekee mahusiano yetu na wenzetu ambayo msingi wake ni Upendo, kweli na haki. Kwenda tofauti na yaliyozoeleka ni mshangao kwa wale wasiopenda kuwa tofauti katika kile kilichojificha. Hivyo, wakamshuhudia (Yesu) wote, wakiyastaajabia maneno ya neema yaliyotoka kinywani mwake, wakasema, Huyu siye mwana wa Yusufu?” Lk 4:22. Historia ya Mtu siyo kikwanzo cha yeye kuwa vizuri, mzuri, au kufanya vizuri zaidi hata kama historia ya kule alikotoka kuonekana kuwa mbaya.

Tumsifu Yesu Kristo!


Njia ya mtu mbaya ni chukizo kwa Bwana; Bali humpenda mtu afuatiaye wema,” Mit 15:9

No hay comentarios:

Publicar un comentario