JUMAMOSI WIKI YA 2 YA MWAKA-C
23/1/2016
Somo: 2Sam 1:1-4, 11-12, 19, 23-27
Zab: 80:2-3, 5-7
Injili: Mk 3:20-21
Nukuu:
“Daudi akamwambia, Yalikwendaje? Tafadhali uniambie. Akajibu,
Watu wamekimbia vitani, tena watu wengi wameanguka wamekufa; hata Sauli naye na
Yonathani, mwanawe, wamekufa,” 2Sam 1:4
“wakaomboleza, wakalia, wakafunga hata jioni, kwa ajili ya Sauli,
na kwa ajili ya Yonathani mwanawe, na kwa ajili ya watu wa Bwana na kwa ajili
ya nyumba ya Israeli; kwa sababu wameanguka kwa upanga,” 2Sam 1:12
“Nimesikitika kwa ajili yako, Yonathani, ndugu yangu, Ulikuwa
ukinipendeza sana; Upendo wako kwangu ulikuwa wa ajabu, Kupita upendo wa
wanawake,” 2Sam 1:26
“Mkutano wakakusanyika
tena, hata wao wenyewe wasiweze hata kula mkate,” Mk 3:20
“Jamaa zake walipopata
habari wakatoka kwenda kumkamata; maana walisema, Amerukwa na akili,” Mk 3:21
TAFAKARI: “Usifurahie anguko la mtesi wako, bali mwombee huruma,
msamaha, na upendo wa Mungu aliye hai
Wapendwa wana wa Mungu, ulimwengu wa ushindani tunaoishi
leo, ni ulimwengu uliopunguza kwa kiasi kukubwa thamani ya mtu na utu wake. Leo
tunafurahia sana kukua kwa sayansi na teknologia na hivyo kurahisiha mambo
mengi na wakati huo huo kuhathiri utu wa mtu. Katika hali hii ya ushindani ni
wazi ‘mwenye nguvu upishwa apite.’ Ni ukweli pia katika hali hii ambapo tunaona
utu wa mtu kutokuheshimiwa na wakati mwingine kulinganishwa na kitu, ni wazi
kuna anguko kubwa sana la kukua kiroho.
Kukua kiroho ni kufanana na Kristo katika kuona, kufikiri,
kuamua na kutenda. Ipo mifano mingi ya namna aonavyo Yesu. “Yesu akawaita wanafunzi wake, akasema, Nawahurumia mkutano, kwa
kuwa yapata siku tatu wamekaa pamoja nami, wala hawana kitu cha kula, tena
kuwaaga wakifunga sipendi, wasije wakazimia njiani,” Mt 15:32. Yesu anaona
zaidi ya kile kionekanacho kwa macho ya kawaida. Ni kuona katika kuzama ndani
ya fumbo zima ya kile ukionacho kwa macho. Namna hii ya kuona ni hatua ya
kufanana na Kristo.
Yesu
hufikiri tofauti akilenga lililo zuri na la umilele. Naye anatutaka tufikiri
kwa mwelekeo huu, anasema, “Au kuna mtu yupi kwenu, ambaye, mwanawe akimwomba
mkate, atampa jiwe? Au
akiomba samaki, atampa nyoka? Basi
ikiwa ninyi, mlio waovu, mnajua kuwapa watoto wenu vipawa vyema, je! Si zaidi
sana Baba yenu aliye mbinguni atawapa mema wao wamwombao? Basi yo yote myatakayo mtendewe na
watu, nanyi watendeeni vivyo hivyo; maana hiyo ndiyo torati na manabii,” Mt
7:9-12. Kumbe kukua kiroho ni kuwafikiria pia
wengine na kuwapenda kama unavyojipenda. Ni kutambua unaishi katika jamii, na
unawajibu wa kufikiri na jamii husika.
Maamuzi ya Yesu
yaliwashangaza wengi na hasa wale ambao walisukumwa na hisia, hasiri, visasi,
na hata utekelezaji wa sheria mbovu katika jamii. Yesu mara zote anakutaka
utoapo hukumu uende mbali ya kile kinachokuruhusu kufanya au kutekeleza hukumu
hiyo. Tazama jinsi Yesu anavyotoa hukumu juu ya mwanamke yule aliyeletwa kwake
kwa kosa la uzizi. “Nao walipozidi kumhoji, alijiinua, akawaambia, Yeye asiye na
dhambi miongoni mwenu na awe wa kwanza wa kumtupia jiwe. Akainama tena, akaandika
kwa kidole chake katika nchi. Nao
waliposikia, wakashitakiwa na dhamiri zao, wakatoka mmoja mmoja, wakianzia
tangu wazee hata wa mwisho wao; akabaki Yesu peke yake, na yule mwanamke
amesimama katikati,” Yoh 8:7-9. Kumbe kukua kiroho ni kujiweka katika hali ya
mtuhumiwa kabla ya kutoa hukumu husika. Lengo ni kumpata mwovu kuliko
kumpoteza.
Kutenda
kwa Yesu kulishangaza wengi na hasa wanafunzi wake. Kutenda kwa Yesu ni kwa
kutumika kuliko kutumikiwa. “aliondoka
chakulani; akaweka kando mavazi yake, akatwaa kitambaa, akajifunga kiunoni. Kisha akatia maji katika
bakuli, akaanza kuwatawadha wanafunzi miguu, na kuifuta kwa kile kitambaa
alichojifunga. Basi alipokwisha
kuwatawadha miguu, na kuyatwaa mavazi yake, na kuketi tena, akawaambia, Je!
Mmeelewa na hayo niliyowatendea? Ninyi
mwaniita, Mwalimu, na, Bwana; nanyi mwanena vema, maana ndivyo nilivyo. Basi ikiwa mimi, niliye Bwana na
Mwalimu, nimewatawadha miguu, imewapasa vivyo kutawadhana miguu ninyi kwa
ninyi,” Yoh 13:4-5, 12-14. Kumbe kufanana na Kristo ni kutenda kama
alivyotenda.
Wapendwa katika Kristo, namna hii ya kukua kiroho, yaani,
kufanana na Kristo Yesu katika kuona, kufikiri, kuamua, na kutenda ndicho
tunachotakiwa tuwe kama kweli sisi ni wafuasi wake Kristo. Maisha yako
yakiongozwa na mfanano huu wa Kristo wa kuishi ndani na katika Kristo, kamwe
hutofurahia anguko la mtesi wako, bali utamwombea huruma, msamaha, na upendo wa
Mungu aliye hai. Ni Mungu tu aliye muumba mtesi wako kwa sura na mfano wake
ndiye mwenye uwezi wa kumbadili na kuwa mwema.
Daudi mwenye hofu ya Mungu, hakufurahia kuanguka kwa Sauli
licha ya kwamba Sauli aliiwinda sana roho yake mchana na usiku. Badala yake,
Daudi alipopata habari za kifo cha Sauli, “wakaomboleza, wakalia, wakafunga hata jioni, kwa ajili ya Sauli,
na kwa ajili ya Yonathani mwanawe, na kwa ajili ya watu wa Bwana na kwa ajili
ya nyumba ya Israeli; kwa sababu wameanguka kwa upanga,” 2Sam 1:12. Ndugu yangu
tuliyesafiri pamoja katika tafakari hii, tujifunze kutoka kwa Daudi, na hasa
kufanana na Kristo Yesu katika ili tukue kiroho. Amina
Tumsifu
Yesu Kristu
“Maana hukumu haina
huruma kwake yeye asiyeona huruma. Huruma hujitukuza juu ya hukumu,” Yak 2:13
No hay comentarios:
Publicar un comentario