JUMAPILI WIKI YA 4 YA MWAKA-C
Somo I: Yer 1:4-5, 17-19
Zab: 71:1-6, 15-17
Somo II: 1Kor 12:31-13:13
Injili: Lk 4:21-30
Nukuu:
“Nijaposema kwa lugha za wanadamu na za malaika, kama
sina upendo, nimekuwa shaba iliayo na upatu uvumao,” 1Kor 13:1
“Tena nijapokuwa na unabii, na kujua siri zote na
maarifa yote, nijapokuwa na imani timilifu kiasi cha kuweza kuhamisha milima,
kama sina upendo, si kitu mimi,” 1Kor 13:2
“Tena nikitoa mali zangu zote kuwalisha maskini, tena
nikijitoa mwili wangu niungue moto, kama sina upendo, hainifaidii kitu,” 1Kor
13:3
“Upendo huvumilia, hufadhili; upendo hauhusudu; upendo
hautakabari; haujivuni,” 1Kor 13:4
“haukosi kuwa na adabu; hautafuti mambo yake; hauoni
uchungu; hauhesabu mabaya,” 1Kor 13:5
“haufurahii udhalimu, bali hufurahi pamoja na kweli,”
1Kor 13:6
“huvumilia yote; huamini yote; hutumaini yote;
hustahimili yote,” 1Kor 13:7
“Upendo haupungui neno wakati wo wote; bali ukiwapo
unabii utabatilika; zikiwapo lugha, zitakoma; yakiwapo maarifa, yatabatilika,”
1Kor 13:8
“Basi, sasa inadumu imani, tumaini, upendo, haya
matatu; na katika hayo lililo kuu ni upendo,” 1Kor 13:13
“Akaanza kuwaambia,
Leo maandiko haya yametimia masikioni mwenu,” Lk 4:21
“Akawaambia, Hapana
shaka mtaniambia mithali hii, Tabibu, jiponye nafsi yako; mambo yote
tuliyosikia kwamba yametendeka Kapernaumu, yatende na hapa pia katika nchi yako
mwenyewe,” Lk 4:23
“Akasema, Amin,
nawaambia ya kwamba, Hakuna nabii mwenye kukubaliwa katika nchi yake mwenyewe,”
Lk 4:24
“Wakajaa ghadhabu wote
waliokuwa katika sinagogi walipoyasikia hayo,” Lk 4:28
“Wakaondoka wakamtoa
nje ya mji, wakampeleka mpaka ukingo wa kilima ambacho mji wao umejengwa juu
yake, wapate kumtupa chini,” Lk 4:29
“lakini yeye alipita
katikati yao, akaenda zake,” Lk 4:30
“Kabla sijakuumba
katika tumbo nalikujua, na kabla hujatoka tumboni, nalikutakasa; nimekuweka
kuwa nabii wa mataifa,” Yer 1:5
“Maana,
tazama, nimekufanya leo kuwa mji wenye boma, na nguzo ya chuma, na kuta za
shaba, juu ya nchi yote; juu ya wafalme wa Yuda, na juu ya wakuu wake, na juu
ya makuhani wake, na juu ya watu wa nchi hii,” Yer 1:18
“Nao
watapigana nawe; lakini hawatakushinda; maana mimi nipo pamoja nawe, asema
Bwana, ili nikuokoe,” Yer 1:19
TAFAKARI: “Basi, sasa inadumu
imani, tumaini, upendo, haya matatu; na katika hayo lililo kuu ni upendo,”
Wapendwa wana wa Mungu, leo Mama Kanisa anaadhimisha
Dominika ya 4 ya mwaka ‘C’ wa Kanisa. Leo kwa namna ya pekee Mama Kanisa
anatutaka tuzame ndani zaidi katika fumbo hili la UPENDO. Uwepo wetu na yote
yaliyopo katika ulimwengu huu ni tokeo la Upendo wa Mungu Baba. Mungu alivijua
vitu vyote hata kabla ya kuumbwa kwayo, na ndivyo ilivyokuwa kwa mwanadamu. “Kabla sijakuumba katika tumbo nalikujua, na kabla hujatoka
tumboni, nalikutakasa; nimekuweka kuwa nabii wa mataifa,” Yer 1:5. Wito huu wa Nabii Yeremia unatukumbusha
kwamba hakuna aliyeko duniani hapa kwa bahati mbaya. Kila mmoja wetu ni kusudi
la Mungu, kwa sababu ya Mungu, na kwa ajili ya Mungu. Mungu aliviumba vitu
vyote kwa sababu alipenda kuviumba na kuvifanya kama vilivyo kwa sifa na
utukufu wake. Pamoja na uzuri huu, binadamu amependelewa zaidi kwa sababu ndiye
aliyechukua chapa halisi ya Mungu. Mungu alichagua kumuumba mtu kwa sura na
mfano wake, Mwa 1:27.
Hivyo asili ya Upendo ni Mungu, uwepo wa upendo ni Mungu,
na Upendo ni Mungu. Upendo wa Mungu Baba kwetu ni Upendo wa Mwana pia kwetu.
Kwa sababu, “Hapo mwanzo kulikuwako Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye
Neno alikuwa Mungu. Huyo mwanzo alikuwako kwa Mungu. Vyote vilifanyika kwa huyo;
wala pasipo yeye hakikufanyika cho chote kilichofanyika,” Yoh 1:1-3. Huu wote
ni upendo wa kweli wa Mungu Baba kwetu, na kupitia Mwana ambaye alifanyika
mwili akakaa kwetu, Yoh 1:14. Hivyo upendo huu asili yake ni Mungu mwenyewe
kama asemavyo Yesu, “Si ninyi mlionichagua mimi, bali ni mimi niliyewachagua ninyi;
nami nikawaweka mwende mkazae matunda; na matunda yenu yapate kukaa; ili kwamba
lo lote mmwombalo Baba kwa jina langu awapeni,” Yoh 15:16. Mungu ndiye
aliyetupenda kwanza. “Katika hili pendo la Mungu lilionekana kwetu, kwamba Mungu
amemtuma Mwanawe pekee ulimwenguni, ili tupate uzima kwa yeye. Hili ndilo pendo, si kwamba sisi
tulimpenda Mungu, bali kwamba yeye alitupenda sisi, akamtuma Mwanawe kuwa
kipatanisho kwa dhambi zetu. Sisi
twapenda kwa maana yeye alitupenda sisi kwanza,” 1Yoh 4:9-10, 19. Ni kwa namna
hiyo tunajifunza haya kama sababu ya kuumbwa kwetu.
Tumeumbwa
ili tumjue Mungu, tumpende Mungu, tumtumikie Mungu, na mwisho turudi kwake
mbinguni. Hivyo ishi ya binadamu hapa duniani na ustawi wake wampasa
kuustawisha upendo huo wa Mungu kwake mwenyewe, jirani, mazingira
yanayomzunguka, na Mungu. Upendo na ambatio lake, yaani, ‘jukumu’ hili la
msingi lisipoonekana kwa mwanadamu basi mwanadamu huyo kesha potea njia, na
ishi yake haina makusudi ya kuumbwa kwake.
Yesu anaanza safari
yake ya kukamilisha kile alichokijia kwa maneno haya, “Roho
wa Bwana yu juu yangu, Kwa maana amenitia mafuta kuwahubiri maskini habari
njema. Amenituma kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao, Na vipofu kupata kuona
tena, Kuwaacha huru waliosetwa, Na
kutangaza mwaka wa Bwana uliokubaliwa,” Lk 4:18-19. Huu ndiyo mpango kazi wa
Yesu ambao unasukumwa na UPENDO. Mpango kazi huenda pia na kauli mbiu ya kazi.
Kauli mbiu ya Yesu juu ya wokovu wetu ndiyo hii, “Wakati
umetimia, na ufalme wa Mungu umekaribia; tubuni, na kuiamini Injili,” Mk 1:15.
Upendo na huruma ya Mungu huenda pamoja.
Upendo
huu wa Mungu kupitia mwanaye Mpenzi Yesu Kristo unafungua mlango mpya wa huruma
ya Mungu, yaani, ‘mwaka wa Bwana uliokubaliwa.’ Hivyo tuutumie vyema mwaka huu
wa Kanisa wa huruma ya Mungu kwa kuchota baraka na neema za Mungu. Leo Yesu
anatuambia, “maandiko haya yametimia masikioni mwenu,” Lk 4:21. Maandiko haya
yametimia kwetu kwa sababu nguvu na uwezo vina yeye (Kristo) hata milele yote,
Yud 1:25. “Mwana hawezi kutenda neno mwenyewe ila lile ambalo amwona
Baba analitenda; kwa maana yote ayatendayo yeye, ndiyo ayatendayo Mwana vile
vile,” Yoh 5:19.
Ni wazi katika kutenda lililo la Mungu, yaani lenye
kuongozwa na upendo wa kweli, tujiandae kupata upinzani. Yule mwovu shetani
hafurahii yaliyo mazuri na mema yenye kuufunua Utukufu wa Mungu. Yesu Kristo
mwenyewe alipata upinzani nyumbani mwake mwenyewe. Katika hili Yesu anasema, “Amin, nawaambia ya kwamba, Hakuna nabii mwenye kukubaliwa katika
nchi yake mwenyewe,” Lk 4:24. Je, kama
hatukubaliki nyumbani kwetu na watu wanaotufahamu iwe sababu ya kutokutenda
mema? Jibu ni HAPANA! Tuendelee kutenda wema na upendo kwa wote, kwa sababu
asili ya upendo ni Mungu, uwepo wa upendo ni Mungu, na Upendo ni Mungu.
Mtume Paulo anaeleza kwa undani upendo na mapaswa yake na yenye
kutupeleka katika kusudi la uumbaji wetu. “Nijaposema kwa lugha za wanadamu na za malaika, kama sina upendo, nimekuwa
shaba iliayo na upatu uvumao,” 1Kor 13:1. Vipaji vyetu na karama zetu za pekee
tulizopewa na Mungu, kama hazitakuwa kwa ajili ya wengine na furaha ya Mungu na
jirani zetu, ni hasara kwetu. “Tena nijapokuwa na unabii, na kujua siri zote na maarifa yote, nijapokuwa
na imani timilifu kiasi cha kuweza kuhamisha milima, kama sina upendo, si kitu
mimi,” 1Kor 13:2. Wengine wamepewa unabii si kwa ajili yao binafsi au
kujineemesha, bali umepewa unabii ili upeleke ujumbe huo wa Mungu kwa faida ya
watu na wokovu wao na wewe mwenyewe.
Ndugu yangu, hata huo utajiri Mungu aliokupa si kwa ajili yako mwenyewe na
kujiburudisha nafsi yako, bali kwa ajili ya kufaidiana na hasa kuwajali kwa
njia ya pekee wale wahitaji wasio na chochote. Ni jambo la kusikitisha kuona
jirani yako kila siku anaomba Mungu amkirimie angalau apate mlo mmoja kwa siku,
wewe unayejua shida na dhiki ya jirani yako huyo ukiwa unasali na kuomba kila
siku Mungu akupe maisha marefu ili uendelea kuvitumbua vinono katika utajiri
wako. Ndugu yangu, swala hapa si tu kuona hitaji la jirani yako muhitaji, bali
kutambua upendo wa Mungu na paswa lake kama Paulo Mtume anavyosema, “Tena nikitoa mali zangu zote kuwalisha maskini, tena
nikijitoa mwili wangu niungue moto, kama sina upendo, hainifaidii kitu,” 1Kor
13:3. Ukweli ni kwamba unaweza kutoa bila kupenda, ila huwezi kupenda bila
kutoa.
Maisha ya upendo wa kweli yana tabia zifuatazo kama anavyotufundisha Mtume
Paulo. Sehemu ya kwanza ya tabia ya upendo ni hii, kwamba, “Upendo huvumilia, hufadhili; upendo hauhusudu; upendo
hautakabari; haujivuni,” 1Kor 13:4. Kwa maneno mengine ‘upendo haujifaidishi
wenyewe. Upendo wa kweli hutoka na kutafuta zaidi ya pale ulipo.’ Upendo huwa
kwa ajili ya kingine zaidi ya kile kilicho katika ukamilifu wake. Sehemu
ya pili ya tabia ya upendo ni kwamba, upendo “haukosi kuwa na adabu; hautafuti mambo yake; hauoni
uchungu; hauhesabu mabaya,” 1Kor 13:5. Kwa maneno mengine upendo ulenga katika
ukamilifu bila kupoteza hata kile kilicho katika hali ya udhaifu. Sehemu ya
tatu ya tabia ya upendo ni kwamba, upendo “haufurahii udhalimu, bali hufurahi pamoja na kweli,” 1Kor 13:6. Upendo huu
ulenga faida ya wote katika wote. Sote tu wana wa Mungu, wenye mahitaji yaliyo
sawa licha ya tofauti zetu.
Sehemu ya nne ya tabia ya upendo ni kwamba, upendo “huvumilia yote; huamini yote; hutumaini yote;
hustahimili yote,” 1Kor 13:7. Mwenye upendo wa kweli hana sababu ya kuishi
na mashaka pasipo sababu. Upendo huu utusaidia kukua mwili na roho. Upendo huu
upo kwa ajili ya kurekebishana katika kukua na kuongezeka pasipo kuangamizana.
Upendo huu unatoa fursa ya kuvumiliana katika kujengana na kujuana tabia. Upendo huu hutoa fursa bila
kipimo katika kusamehana. Sehemu ya tano ya tabia ya upendo ni kwamba, “Upendo haupungui neno wakati wo wote; bali ukiwapo
unabii utabatilika; zikiwapo lugha, zitakoma; yakiwapo maarifa, yatabatilika,”
1Kor 13:8. Upendo huu unatoa fursa ya mazungumzano hata pale ambapo hakuna
uwezekano kinadharia wa mazungumzano hayo ambayo hayazungumziki. Kwenye tabia
hii ya upendo hakuna lisilowezekana.
Tabia hizo tano za upendo hutuandaa kujibu maswali mawili la mwisho na ya
pekee mbele ya Mungu katika kitu chake cha hukumu na haki. Pasipo shaka yoyote
ile, ninashawishika kuona kwamba kila mmoja wetu kadiri ya wito na nafasi yake
ataulizwa maswali haya na Mungu;
Swali la kwanza: Je, ulifanya nini
na Upendo wa Mwanangu Yesu Kristo aliyekupenda hadi akayatoa maisha yake kwa
ajili yako?
Swali la pili: Je, umefanya nini na vipaji nilivyokupa?
Leo tuwapo hapa duniani tunaongozwa na mambo yote matatu, yaani, Imani kwa
kile tusichokijua sawasawa ila kina uzima ndani yake, pili, Matumaini tukijua
yote yatapita na uzuri wake na mwisho tutapata kile tunachokichuchumili yaani
maisha ya umilele. Na tatu, twaishi ulimwenguni hapa kwa mapendo na hasa
tukielekeza nguvu zetu katika tabia za upendo. Haya mawili, yaani Imani na
Matumaini ukomo wake ni pale tutakapo ifikia Mbingu. Upendo na tabia zake
zitadumu katika umilele wote kwa sababu UPENDO NI MUNGU. Hivyo, “Basi, sasa inadumu imani, tumaini, upendo, haya
matatu; na katika hayo lililo kuu ni upendo,” 1Kor 13:13.
Mzee Mapinduzi alikuwa mlinzi nyumbani kwa tajiri Mwana Mboka. Mzee
Mapinduzi kila siku ufikapo muda wa kwenda lindoni kwa tajiri yake huchukua
kindoo kidogo kwa ajili ya kubebea mabaki ya chakula na hasa mifupa ya nyama
ambayo kwa kiasi kikubwa hubaki.
Mzee Mapinduzi alifanya hivi kwa zaidi ya miaka mitano. Siku moja Tajiri
yake alimuuliza Mzee Mapinduzi, “hivi kwa sasa una mbwa wangani?” “Bosi idadi
ya mbwa wangu ni ileile,” Mzee Mapinduzi alimjibu tajiri yake kwa hali ya
uzuni. Muonekano ule wa Mzee Mapinduzi ulimfanya tajiri yake afikiri zaidi.
Kesho yake asubuhi na mapema Bwana Mboka kama ilivyo kawaida yake alidamka
kwa ajili ya kufanya mazoezi ya kukimbia. Ila siku ile alidhamiria kuondoka
mguu kwa mguu na Mzee Mapinduzi kuwatazama mbwa wake. Walipo karibia nyumbani,
mjukuu wa Mzee Mpinduzi alyejulikana kwa jina kama Tatu, alikuja mbio na
kumpokea Babu yake kile kindoo cha mifupa na mabaki ya chakula.
Mtoto huyu alienda na kindoo kile moja kwa moja jikoni. Bwana Mboka
alipotazama huku na kule hakuona dalili yoyote ya Mbwa. Hivyo alimuuliza Mzee
Mapinduzi, “wale mbwa unaowaletea mifupa wapo
wapi?” Mzee Mapinduzi alimwita mke wake na wajukuu wake watano nje.
“Hawa ndiyo mbwa wangu. Huyu ni mke wangu mpendwa Bibi Zaituna, na wajukuu
wangu watano ambao tunawalea tangu wazazi wao wafariki kwa ugonjwa wa ukimwi.”
Mzee Mapinduzi alimjibu tajiri yake huku machozi yakimtoka.
Bwana Mboka aliondoka
taratibu kurudi nyumbani bila kusema neno. Siku ile ilikuwa nzito sana kwa
Bwana Mboka. Jioni ilipofika, Mzee Mapinduzi alifika lindoni kama kawaida yake
na kindoo chake. Bwana Mboka alimwita Mzee Mapinduzi na kumwambia, “hali
niliyoiona leo asubuhi imenisikitisha sana. Mimi na familia yangu tumeamua haya
yafuatayo: kukujengea nyumba nzuri ya kuishi, kuwasomesha wajuu zako, na
kukutunza kama mzazi wetu wewe na familia yako.” Wote walikumbatiana kwa furaha
na uchungu huku machozi yakiwatoka.
Tumsifu Yesu Kristo!
“Heri amkumbukaye mnyonge; Bwana atamwokoa siku ya taabu. Bwana atamlinda na kumhifadhi hai,
Naye atafanikiwa katika nchi; Wala usimtie katika hali wamtakiayo adui zake,”
Zab 41:1-2
No hay comentarios:
Publicar un comentario