ALHAMISI WIKI YA 2 YA MWAKA-C
21/1/2016
Somo: 1Sam 18:6-9; 19:1-7
Zab: 56:2-3, 9-10a, 10a-11, 12-13
Injili: Mk 3:7-12
Nukuu:
“Basi Sauli akaghadhibika sana, na maneno haya yakamchukiza;
akasema, Wamempa Daudi makumi elfu, na mimi wamenipa elfu tu; kuna nini tena
awezayo kupata, isipokuwa ni ufalme?” 1Sam
18:8
“Sauli akamwonea Daudi wivu tangu siku ile,” 1Sam 18:9
“Kisha Sauli akasema
na mwanawe Yonathani, tena na watumishi wake wote, kwamba wamwue Daudi,” 1Sam
19:1
“Lakini huyo
Yonathani, mwana wake Sauli, alikuwa akipendezwa sana na Daudi. Basi Yonathani
akamwambia Daudi, akasema, Sauli, baba yangu, anatafuta kukuua; basi, nakusihi,
ujiangalie sana asubuhi, ukae mahali pa siri na kujificha,” 1Sam 19:2
“Na pepo wachafu, kila
walipomwona, walianguka mbele yake, wakalia wakisema, Wewe ndiwe Mwana wa
Mungu,” Mk 3:11
“Akawakataza sana,
wasimdhihirishe,” Mk 3:12
TAFAKARI: “Sauli akamwonea Daudi wivu tangu siku ile.”
Wapendwa wana wa Mungu, wivu ni mbaya sana unapomtia mtu
upofu wa kutokuyaona mazuri ya mwenzake na kuyatafsiri kama kikwazo katika
maisha yako. Wapo wengi kati yetu wametendwa vibaya sana kwa sababu tu
wametenda yaliyo mema na yakawa na mwitikio chanya kwa watu. Chanzo kikubwa cha
wivu kadiri ya mang’amuzi yangu ni kutokutambua karama zako. Kila mmoja wetu
angetambua karama zake kusingekuwa na nafasi ya kuoneana wivu. Tatizo kubwa ni
kwamba tunapoteza muda mwingi kutaka kufanana na wengine na wakati mwingine
kuiga kusiko kujifunza.
Uungwana ni pale unapoona mazuri ya mwenzako na kusadifu
kama yalivyo. Sauli Mfalme anaingiwa na hofu kwa wasifu aliopewa Daudi baada ya
kumuua Goliathi. Goliathi Mfilisti alikuwa tishio kubwa kwa taifa zima la wana
wa Israeli. Ushindi wa Daudi ulipaswa kuwa furaha kwa wote na hasa Mfalme
ambaye kwa sasa ufalme wake amani imerejeshwa. Sauli anatafsi wasifu aliopewa
Daudi kama tishio kwa nafasi yake kama mfalme. “Basi Sauli akaghadhibika sana, na maneno haya yakamchukiza;
akasema, Wamempa Daudi makumi elfu, na mimi wamenipa elfu tu; kuna nini tena
awezayo kupata, isipokuwa ni ufalme?” 1Sam
18:8. Hivi kwa nini unakosa usingizi kwa vile tu mwenzako kafanya vizuri tena
kwa manufaa ya wote?
Wivu
unaegemeao upande hasi matokea yake ni umauti. Wivu kama ulivyo ni amsho la
ndani la moyo wa mtu juu ya kitu fulani. Wivu kama wivu si tatizo. Tatizo
linakuja kwenye egemeo la wivu huo, yaani egemeo hasi au chanya. Egemeo chanya
la wivu linamsukuma mtu kufanya vizuri zaidi ya kile kilichofanywa na
mtangulizi wake. Aliyoyafanya mtangulizi wake yanakuwa msingi na dira ya yeye
kuboresha na kufanya vizuri zaidi. Hapa ndipo tunapoongelea wivu wa maendeleo.
Mfano: kama mwenzako kajenge nyumba nzuri na kuweka bati za rangi nzuri na
imara, wewe ukijenga nyumba yako weka vigae vizuri na imara. Huu ni wivu wa
maendeleo. Egemeo hasi la wivu ni pale ambapo mtu anatumia akili zake, moyo
wake, nguvu zake na mbinu zake zote
kuyadhoofisha mazuri ya mwenzake. Hiki ndicho anachojaribu kukifanya
Mfalme Sauli. “Kisha Sauli akasema na mwanawe Yonathani, tena na watumishi wake
wote, kwamba wamwue Daudi,” 1Sam 19:1. Maamuzi haya ni sawa na wale wasemao
“wote tukose!”
Mtoto wa
Sauli, Yonathani, hakubaliani na wazo la Baba yake, hivyo anakuwa mtetezi wa
siri ya Daudi. Ndugu zangu tuelewe ukweli huu; chochote kile ufanyacho kiwe
kizuri au kibaya, watu huona palipo kweli na pasipo kweli. Hivyo kweli hubaki
kuwa kweli na uongo hujitenga. Ni kwa mantiki hii tunaona “Yonathani, mwana wake Sauli, alikuwa akipendezwa sana na Daudi.
Basi Yonathani akamwambia Daudi, akasema, Sauli, baba yangu, anatafuta kukuua;
basi, nakusihi, ujiangalie sana asubuhi, ukae mahali pa siri na kujificha,”
1Sam 19:2. Tofauti katika utendaji zipo na hatuwezi kuzizuia kwa sababu kila
mmoja wetu ni tofauti na wapekee. Tunachotakiwa kufanya ni kuruhusu ndani ya
mioyo yetu na katika utendaji wetu, umoja katika utofauti. Mfumo huu unatija
sana katika maendeleo ya mwanadamu na watu wanaomzunguka. Vipaji hukuzwa, na
jamii hufaidika navyo.
Wasifu
aliopewa Daudi na wanawake wale walioyaona makuu ya Mungu kupitia kifo kile cha
Goliathi, “Sauli amewaua elfu zake, Na Daudi
makumi elfu yake,” mapepo pia wanaona utofauti uliopo kwa Yesu kwa kile alicho
na huduma ile aitoayo. “Na pepo wachafu, kila walipomwona, walianguka mbele yake,
wakalia wakisema, Wewe ndiwe Mwana wa Mungu,” Mk 3:1. Jambo la ajabu Yesu
hayasadifu wala kuyashabikia haya yasemayo na mapepo. Kumbe tunakumbushwa kuwa
makini hasa na vyanzo vya wasifu tupewao. Yesu
“Akawakataza sana (mapepo), wasimdhihirishe,” Mk 3:12. Ndugu yangu, kila kishindo kina
maana yake. Mara uyapatapo hayo katika utume wako chukua nafasi ya pekee
kuyatafakari kwa kina.
Tumsifu Yesu Kristo
“Kwani hasira humwua mtu mpumbavu, Nao wivu humwua mjinga,”
Ayu 5:2
No hay comentarios:
Publicar un comentario