JUMAMOSI, KIPINDI CHA NOELI
2/1/2016
Somo: 1Yoh 2:22-28
Zab: 97:1, 2-3ab, 3cd-4
Injili: Yoh 1:19-28
Nukuu:
“Ni nani aliye mwongo
ila yeye akanaye ya kuwa Yesu ni Kristo? Huyo ndiye mpinga Kristo, yeye
amkanaye Baba na Mwana. Kila
amkanaye Mwana, hanaye Baba; amkiriye Mwana anaye Baba pia,” 1Yoh 2:22-23
“Ninyi basi, hilo
mlilolisikia tangu mwanzo na likae ndani yenu. Ikiwa hilo mlilolisikia tangu
mwanzo linakaa ndani yenu, ninyi nanyi mtakaa ndani ya Mwana, na ndani ya
Baba,” 1Yoh 2:24
“Na hii ndiyo ahadi
aliyotuahidia, yaani, uzima wa milele,” 1Yoh 2.25
“Nanyi, mafuta yale
mliyoyapata kwake yanakaa ndani yenu, wala hamna haja ya mtu kuwafundisha;
lakini kama mafuta yake yanavyowafundisha habari za mambo yote, tena ni kweli
wala si uongo, na kama yalivyowafundisha, kaeni ndani yake,” 1Yoh 2:27
“Na sasa, watoto
wadogo, kaeni ndani yake, ili kusudi, atakapofunuliwa, mwe na ujasiri, wala
msiaibike mbele zake katika kuja kwake,” 1Yoh 2:28
“Na huu ndio ushuhuda wake Yohana, Wayahudi walipotuma kwake
makuhani na Walawi kutoka Yerusalemu ili wamwulize, Wewe u nani?” Yoh 1:19
“Naye alikiri, wala hakukana; alikiri kwamba, Mimi siye Kristo,”
Yoh 1:20
“Akasema, Mimi ni sauti ya mtu aliaye nyikani, Inyosheni njia ya
Bwana! Kama vile alivyonena nabii Isaya,” Yoh 1:23
“Wakamwuliza, wakamwambia, Mbona basi wabatiza, ikiwa wewe si
Kristo, wala Eliya, wala nabii yule?” Yoh 1:25
“Yohana akawajibu akisema, Mimi nabatiza kwa maji. Katikati yenu
amesimama yeye msiyemjua ninyi,” Yoh 1:26
“Ndiye yule ajaye nyuma yangu, ambaye mimi sistahili kuilegeza
gidamu ya kiatu chake,” Yoh 1:27
TAFAKARI: “Na hii ndiyo ahadi
aliyotuahidia, yaani, uzima wa milele.”
Wapendwa wana wa Mungu, tumeumbwa ili tuishi milele. Hili
ndilo kusudi kubwa la Mungu kutuumba. Je, mbona tunakufa? Kifo siyo mwisho wa
umilele wetu, bali ni mwisho wa mwanzo mpya wa maisha ya umilele
tutakapohesabiwa haki na Mungu mwenyewe. Mauti haina nguvu tena kwani
ishabatilishwa na Kristo kwa kifo chake pale msalabani. “Maana kwa kuwa mauti ililetwa na mtu, kadhalika na kiyama ya
wafu ililetwa na mtu. Kwa kuwa
kama katika Adamu wote wanakufa, kadhalika na katika Kristo wote watahuishwa,”
1Kor 15:21-22. Ni kweli tutakufa ila hatuna sababu ya kuogopa kifo hiki cha
mwili. Yatupasa kuishinda hofu ya kufa tukijua kwamba, “Adui wa mwisho atakayebatilishwa ni mauti,” 1Kor 15:26. Ni kwa maana hii kwenye misa ya wafu tunasoma
utangulizi “Prefacio” ya wafu na hasa ile ya kwanza kwa maneno haya yenye
matumaini kwamba, “Sisi tumepata kwake tumaini la ufufuko. Tunasikitika kwa
sababu tunajua kwamba lazima tutakufa, lakini tunatulizwa kwa kuwa alituahidia
uzima wa milele. Ee Bwana, uzima wa waamini wako hauondolewi ila unageuzwa tu.
Nayo makao ya hapa duniani yakisha bomolewa, tunapata makao ya milele
mbinguni,” Misale ya Waumini, toleo la nane, 1996, uk. 403. Uzima huu mpya
baada ya anguko la wazazi wetu wa kwanza umeletwa na Kristo mwenyewe na hasa
sadaka yake pale msalabani. Hivyo yatupasa kumkiri Kristo na kuishi kadiri ya
mapenzi yake. Yesu anasema, “Mimi ndimi
njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi,” Yoh 14:6
Kama alivyo kiri Yohane
Mpatizaji juu ya Kristo, lazima nasi tukiri kwamba Yesu ni Kristo. “Ni nani aliye mwongo ila yeye akanaye ya kuwa Yesu ni Kristo?
Huyo ndiye mpinga Kristo, yeye amkanaye Baba na Mwana. Kila amkanaye Mwana, hanaye Baba;
amkiriye Mwana anaye Baba pia,” 1Yoh 2:22-23 .Uzushi ni kumchanganya Kristo na mawazo yetu na
kile tunachotaka awe. Kufanya hivyo ni kumfanya Kristo awe kutokeo la taswira
zetu na mfano wetu. Wakati mwingine namna hii ya kufikiri imekuwa ikifanyika
katika Kanisa. Tunamfanya Mungu mdoli au sanamu bila kufungua masikio yetu kwa
neno lile linalotupeleka katika fumbo lenyewe na uzima wenyewe. Yatupasa
kuyasika mafundisho ya kweli toka kwa manabii waliomtangulia Kristo, Yesu Kristo
mwenyewe, na mafundisho ya mitume wake walioishi ushuhuda huu wa kweli. “Ninyi basi, hilo mlilolisikia tangu mwanzo na likae ndani yenu.
Ikiwa hilo mlilolisikia tangu mwanzo linakaa ndani yenu, ninyi nanyi mtakaa
ndani ya Mwana, na ndani ya Baba,” 1Yoh 2:24
Hivyo namna ya pekee ya
kuwa na umoja na Mungu Baba na Mwana ni
kukubali hili fumbo na kujifungua kwalo. Na kwa namna tulivyo {kuumbwa kwetu},
sisi ni wasikilizaji wa Neno na kwa kulisikiliza ndivyo tunavyobadilishwa na
neno hilo. Mwisho wa siku hatutahitajika kutoa hesabu ya ufahamu wetu juu ya
neno, bali uaminifu wetu juu ya neno hilo la Mungu. Roho aliye ndani yetu ndiye
mwalimu wetu. Ili tuseme NDIYO kwa Kristo yatupasa kusema HAPANA kwa sisi
wenyewe ikiwa ni pamoja na madai yetu binafsi ya kimasiya kama alivyosema
HAPANA Yohane Mbatizaji.
Katika Injili tunaona
mkanganyiko na kuibuka kwa hisia mbalimbali juu ya nani hasa Kristo-Masiha,
Yohane Mbatizaji, na Eliya. Ni wazi matendo aliyokuwa anayafanya Yohane
Mbatizaji yalivuta hisia labda aweza kuwa Masiha au Eliya mwingine. Hata hivyo
Yohana Mbatizaji anakiri na anakanusha jambo hilo kwa kusema, “Mimi siye Kristo,” Yoh
1:20. Je, Yohane ni nani basi kama siye Kristo? “Akasema, Mimi ni sauti ya
mtu aliaye nyikani, Inyosheni njia ya Bwana! Kama vile alivyonena nabii Isaya,”
Yoh 1:23. Yohane ni mtangulizi na mwaandaji wa yule ajaye na ategemewaye kwa
kazi nzima ya ukombozi. Na hata ubatizo alioufanya Yohane Mbatizaji ulikuwa
ubatizo wa toba. Ni maandalizi ya ubatizo wenyewe wa Roho Mtakatifu. Hivyo Yohane
kwa unyenyekevu wake anasema, Mimi nabatiza kwa maji. Katikati yenu amesimama
yeye msiyemjua ninyi,” Yoh 1:26. Huyo ndiye Kristo wasiyemjua Wayahudi.
Yohane
Mbatizaji anajinasua katika hali yote ile ya kujikweza. Yeye siye Eliya na wala
siye Masiya. Kuhusu Masiya, ambaye ndiye Kristo, anasema, “Katikati yenu
amesimama yeye msiyemjua ninyi. Ndiye yule ajaye nyuma yangu, ambaye mimi
sistahili kuilegeza gidamu ya kiatu chake,” Yoh 1:26b-27. Hivyo ndugu yangu
tuliyesafiri wote katika tafakari hii, lini utajinasua katika hali yako ya
kujikweza ili Kristo aongezeke ndani yako? “Basi hii furaha yangu
imetimia. Yeye hana budi kuzidi, bali mimi kupungua,” Yoh 3:30
Tumsifu
Yesu Kristo!
“Na sasa, watoto
wadogo, kaeni ndani yake, ili kusudi, atakapofunuliwa, mwe na ujasiri, wala
msiaibike mbele zake katika kuja kwake,” 1Yoh 2:28
No hay comentarios:
Publicar un comentario