lunes, 1 de febrero de 2016

TAFAKARI: SIKU YA KUTOLEWA BWANA HEKALUNI-SIKU YA MAISHA YA WAKFU-MAISHA YA KITAWA

SIKUKUU YA KUTOLEWA BWANA HEKALUNI
Siku ya Maisha ya Wakfu-Maisha ya Kitawa
2/2/
Somo I: Mal 3:1-4
Zab: 24:7-9
Somo II: Ebr 2:14-18
Injili: Lk 2:22-40
Nukuu:
Angalieni, namtuma mjumbe wangu, naye ataitengeneza njia mbele yangu; naye Bwana mnayemtafuta atalijilia hekalu lake ghafula; naam, yule mjumbe wa agano mnayemfurahia, angalieni, anakuja, asema Bwana wa majeshi,” Mal 3:1 

Wakati ule ndipo dhabihu za Yuda na Yerusalemu zitakapopendeza mbele za Bwana, kama katika siku za kale, na kama katika miaka ya zamani,” Mal 3:4

 “awaache huru wale ambao kwamba maisha yao yote kwa hofu ya mauti walikuwa katika hali ya utumwa,” Ebr 2:15 

Hivyo ilimpasa kufananishwa na ndugu zake katika mambo yote, apate kuwa kuhani mkuu mwenye rehema, mwaminifu katika mambo ya Mungu, ili afanye suluhu kwa dhambi za watu wake,” Ebr 2:17 

Kisha, zilipotimia siku za kutakasika kwao, kama ilivyo torati ya Musa walikwenda naye hata Yerusalemu, wamweke kwa Bwana, (kama ilivyoandikwa katika sheria ya Bwana, Kila mtoto mwanamume aliye kifungua mimba ya mamaye na aitwe mtakatifu kwa Bwana),” Lk 2:22-23

wakatoe na sadaka, kama ilivyonenwa katika sheria ya Bwana, Hua wawili au makinda ya njiwa wawili,” Lk 2:24 

Sasa, Bwana, wamruhusu mtumishi wako, Kwa amani, kama ulivyosema; Kwa kuwa macho yangu yameuona wokovu wako,” Lk 2:29-30 

Simeoni akawabariki, akamwambia Mariamu mama yake, Tazama, huyu amewekwa kwa kuanguka na kuinuka wengi walio katika Israeli, na kuwa ishara itakayonenewa,” Lk 2:34 

Yule mtoto akakua, akaongezeka nguvu, amejaa hekima, na neema ya Mungu ilikuwa juu yake,” Lk 2:40 

TAFAKARI: “Kila mtoto mwanamume aliye kifungua mimba ya mamaye na aitwe mtakatifu kwa Bwana.”

Wapendwa wana wa Mungu, leo Mama Kanisa anaadhimisha Sikukuu ya Kutolewa Bwana Hekaluni. Yesu anapotolewa hekaluni kama ilivyo desturi ya Wayahudi kwa kila mzaliwa wa kwanza wa kiume. Kisha, zilipotimia siku za kutakasika kwao, kama ilivyo torati ya Musa walikwenda naye hata Yerusalemu, wamweke kwa Bwana, (kama ilivyoandikwa katika sheria ya Bwana, Kila mtoto mwanamume aliye kifungua mimba ya mamaye na aitwe mtakatifu kwa Bwana),” Lk 2:22-23. Hata hivyo, kumkomboa huyu mzaliwa wa kwanza kutoka hekaluni iliwapasa wazazi wake kumtolea Bwana sadaka kama shukrani. Wakatoe na sadaka, kama ilivyonenwa katika sheria ya Bwana, Hua wawili au makinda ya njiwa wawili,” Lk 2:24. Sadaka hii inaonyesha umasikini wa Familia hii Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu.

Ni katika tendo hili pale Hekaluni, Simeoni mtu wa kweli na haki ahadi yake inatimizwa na Mungu. Na tazama, pale Yerusalemu palikuwa na mtu, jina lake Simeoni, naye ni mtu mwenye haki, mcha Mungu, akiitarajia faraja ya Israeli; na Roho Mtakatifu alikuwa juu yake,” Lk 2:25. Yesu Kristo hapa ndiye nuru halisi na uhuru wa kweli wa wana wa Taifa la Mungu. Kristo ndiye  ile nuru aliyokuwa ikisubiriwa, Nuru ya kuwa mwangaza wa Mataifa, Na kuwa utukufu wa watu wako Israeli,” Lk 2:32. Mungu anaifunua nuru ya Yesu ndani ya moyo wa Simeoni naye anayaona makuu ndani ya Yesu: Simeoni akawabariki, akamwambia Mariamu mama yake, Tazama, huyu amewekwa kwa kuanguka na kuinuka wengi walio katika Israeli, na kuwa ishara itakayonenewa,” Lk 2:34. Kristo ndiye sababu ya kuanguka na kuinuka wengi, kwa sababu ulimwenguni hapa ni vita dhidi ya mwanga ambaye ndiye Kristo, na giza ambayo ndiye yule mwovu shetani. Watainuliwa wale watakaoambatana na mwanga na wataangushwa wale waambatanao na giza, yaani yule mwovu.

Katika vita hii Mama Bikira Maria hatakuwa salama katika maana ya kufurahia tu uwepo wa mwanaye. Ni katika uchungu na kushiriki mateso ya mwanaye nuru ya kweli na haki itafunuliwa ndani yake. Hivyo ni katika msalaba ambao mwanaye anauendea ndipo utakapokuwepo utukufu wake. Nawe mwenyewe, upanga utaingia moyoni mwako, ili yafunuliwe mawazo ya mioyo mingi,” Lk 2:35. Kwenye Msalaba Mtakatifu na wenye ushindi wa Bwana Yetu Yesu Kristo ndipo penye utukufu, kufunguliwa kwa mioyo yetu kutoka utumwa wa dhambi, na kuuelekea uzima wa milele. Hivyo kwa Mkristo na Mfuasi wa Kristo, hakuna UTUKUFU pasipo MSALABA.

 Kuyafanya mapenzi ya Mungu wakati mwingine hakuhakisi kabisa miono na mitazamo ya kibinadamu. Mitazamo yetu ni kwamba tuwapo karibu sana na Mungu na kufanya mapenzi yake, ndiyo miminiko ya baraka na neema. Ndugu yangu uliyesafiri nami katika tafakari hii, hatutendi mema wala kuwa waaminifu mbele ya Mungu ili tununue baraka na neema zake, bali tunayafanya hayo yote kwa sababu ndiyo hali na uwepo wa Mungu, na ndivyo impendezavyo sisi kufanya. Uwepo wetu hapa duniani ni moja ya uzuri na utukufu wa Mungu. Mfano wa wale waliyafanya yote vyema ila hayakuendana na miono na mitazamo ya kibinadamu ni Ana binti Fanueli. Tunaambiwa Palikuwa na nabii mke, jina lake Ana, binti Fanueli, wa kabila ya Asheri, na umri wake ulikuwa miaka mingi, alikuwa amekaa na mume miaka saba baada ya uanawali wake,” Lk 2:36. Bila shaka Ana kama Mwanamke na Mama, kuwa na familia kamili katika maana ya Yeye, Mumewe na mtoto au watoto ilikuwa moja ya  furaha yake kubwa hapa duniani. Pamoja na kukosa hilo, hakuwa na nafasi ya kumlaumu Mungu wala kuasi Imani yake. Aliishi kwa matumaini makubwa ingawa umri wake ulisogea. Naye ni mjane wa miaka themanini na minne; haondoki katika hekalu, ila huabudu usiku na mchana kwa kufunga na kuomba,” Lk 2:37. Wangapi kati yetu tunaujasiri huu tunapoona mbele yetu ni giza tupu?

Furaha ya Ana binti Fanueli inakamilika anapokutana na Yesu. Ni kama asemavyo Mt. Agustino kwamba ‘mioyo yetu haitulii mpaka itakapotulia kwako Ee Bwana.’ Ndivyo ilivyokuwa kwa Ana binti Fanueli alipokutana na Yesu. “Huyu (Ana binti Fanueli) alitokea saa ile ile akamshukuru Mungu, na wote waliokuwa wakiutarajia ukombozi katika Yerusalemu akawatolea habari zake,” Lk 2:38. Alichokua akikitazamia amekiona kwa macho yake.

Na Yule mtoto (Yesu) akakua, akaongezeka nguvu, amejaa hekima, na neema ya Mungu ilikuwa juu yake,” Lk 2:40. Maana yake aliyaishi maisha yetu, furaha zetu, mahangaiko yetu, na kuyashiriki yote bila kutenda dhambi hadi kikomo chake pale Msalabani kwa kutuweka huru. Hivyo Nanyi mfahamu kwamba mlikombolewa si kwa vitu viharibikavyo, kwa fedha au dhahabu; mpate kutoka katika mwenendo wenu usiofaa mlioupokea kwa baba zenu; bali kwa damu ya thamani, kama ya mwana-kondoo asiye na ila, asiye na waa, yaani, ya Kristo,” 1Pet 1:18-19. Je, una chochote chenye thamani  katika ulimwengu huu ambacho waweza kulinganisha na wokovu aliyokupatia Kristo Yesu? Je, tendo hili la Bwana kutolewa hekaluni na yale yote yaliyojiri kule hekaluni yanasema nini katika siku yetu hii ya Watawa duniani?

Wapendwa katika Kristo, Maisha ya Kitawa hayana tofauti na tendo hili la Bwana kutolewa hekalu na kile wafanyacho watawa wanapojiweka wakfu kwa Mungu. Kujiweka Wakfu ni kujitenga kwa kazi MAALUMU kwa ajili ya Kristo, kwa sababu ya Kristo, na Kwa Kristo. Huku ndiko KUJISALIMISHA kwa MTAWA na KUABUDU kuliko na AMANI, FURAHA, na NGUVU. Ndugu yangu, kujitoa kwa Mungu ndiyo kuabudu hasa. Tendo hili la kujisalimisha binafsi huitwa kwa majina mengine; Kujiweka wakfu, Kumfanye Yesu Bwana wako, Kuchukuwa msalaba wako, Kuifisha nafsi, na Kujitoa kwa Roho Mtakatifu. Cha muhimu hapa ni kwamba ulitende, siyo linaitwaje. Mungu anapenda maisha yako yote. Asilimia tisini na tano haitoshi. Ndugu, kuna vizuizi vitatu ambavyo huzuia kujisalimisha kwetu kikamilifu kwa Mungu; Hatuelewi kiasi gani Mungu anatupenda, Tunataka kutawala maisha yetu wenyewe, na Tunashindwa kuelewa maana ya kujisalimisha.

Je, naweza kumwamini Mungu?
Ndugu yangu, Imani ni jambo muhimu sana katika kujisalimisha. Huwezi kujisalimisha kwa Mungu kama Mtawa au yeyote yule mwenye hofu ya Mungu, mpaka uwe unamwamini, lakini huwezi kumwamini Mungu mpaka umfahamu vyema. Hofu hutuzuia kujisalimisha, lakini upendo huondoa hofu yote. Kadiri unavyotambua jinsi Mungu anavyokupenda, ndivyo kujisalimisha kunavyokuwa rahisi. Jambo hili halitegemei umri wetu wa ukristo wetu, wala kwa maisha ya utawani.

Je, unajuaje Mungu anakupenda?
Ndugu yangu, Mtawa mwenzangu, nawe mwenye hofu ya Mungu, Mungu anakupa ushindi mwingi: Mungu anasema anakupenda, "Bwana ni mwema kwa watu wote, Na rehema zake zi juu ya kazi zake zote." Zab 145:9. Hautoki kwenye uangalizi wake kamwe, "Umepepeta kwenda kwangu na kulala kwangu, umeelewa na njia zangu zote," Zab 139:3. Yeye anaangalia mambo yote ya maisha yako, "Lakini ninyi, hata nywele za vichwa vyenu zimehesabiwa zote," Mt 10:30. Alikupa uwezo wa kufurahia aina zote za viburudisho, "bali wamtumaini Mungu atupaye vitu vyote kwa wingi ili tuvitumie kwa furaha," 1Tim 6:17b. Ana mpango mzuri kwa ajili ya imani yako, "Maana nayajua mawazo ninayowawazia ninyi; asema Bwana, ni mawazo ya amani wala si ya mabaya, kuwapa ninyi tumaini siku zote za mwisho," Yer 29:11. Yeye hukusamehe, "Kwa maana Wewe, Bwana, Umekuwa tayari kusamehe, Na mwingi wa fadhili, kwa watu wote wakuitao," Zab 86:5. Na kwa upendo anakuvumilia, "Bwana ana fadhili, ni mwingi wa huruma, Si mwepesi wa hasira, ni mwingi wa rehema," Zab 145:8. Ndugu na Mtawa mwenzangu nawe mwenye hofu ya Mungu, Mungu anakupenda kiasi kisichopimika kuliko unavyoweza kufikiri.

Uthibitisho wa ukweli huu ni dhabihu ya Mwana wa Mungu kwa ajili yako. "Bali Mungu aonyesha pendo lake yeye mwenyewe kwetu sisi, kwa kuwa Kristo alikufa kwa ajili yetu, tulipokuwa tungali wenye dhambi, " Rum 5:8. Kama unataka kufahamu uthamani wako mbele za Mungu, mwangalie Yesu Kristo na mikono yake ilivyowambwa, akisema, "nakupenda sana! Bora nife kuliko kukukosa."

Ndugu yangu mwenye hofu ya Mungu, na Mtawa mwenzangu, Mungu siyo kiongozi katili wa msafara wa watumwa au mchokozi anayetumia mabavu kutulazimisha kumtii. Hajaribu kuvunja utashi wetu, lakini hutusihi ili tujitoe wenyewe kwake kwa kupenda. Mungu ni mpendwa na mkombozi, na kujisalimisha kwake huleta uhuru, siyo utumwa. Tunapojisalimisha kwa Yesu kikamilifu, tunagundua kwamba yeye si mtawala wa IMLA, lakini RAFIKI ANAYE KUKUBALI MIPAKA YETU. Kikwazo kingine cha kujisalimisha kikamilifu ni majivuno yetu. Hatukubali kwamba sisi ni viumbe tu na kwamba hatuna utawala juu ya kila kitu. Hili ni jaribu kila zamani "mtakuwa kama Mungu, " Mwa 3:8, tamaa hiyo ya kuwa na utawala juu ya kila kitu ni chanzo cha matatizo mengi katika maisha yetu. Maisha ni mapambano, lakini jambo ambalo watu wengi hawaelewi ni kwamba mapambano yetu kama yale ya Yakobo hakika ni mapambano na Mungu! Tunataka kuwa sawa na Mungu, na haitawezekana sisi kushinda pambano hilo.

A. W. Tower alisema, "sababu kwa nini watu wengi bado wanasumbuka, bado wanatafuta, bado wanafanya maendeleo kidogo ni kwa vile bado hawajafikia mwisho wao wenyewe. Bado tunajaribu kuamuru na kuingilia kazi ya Mungu ndani yetu."

Ndugu yangu, sisi siyo Mungu na hatuta kuwa kamwe. Sisi ni wanadamu. Ni pale tunapojaribu kuwa Mungu ndipo tunaishia kuwa kama Shetani kabisa, ambaye alitamani jambo hilo hilo.

Tunakubali ubinadamu wetu kiakili lakini siyo kihisia. Tunapokabiliwa na mapungufu yetu, ndipo tunaonyesha uchungu, hasira na chuki. Tunataka kuwa warefu (au wafupi), wenye akili, wenye nguvu, wenye vipawa, warembo, na matajiri. Tunataka kuwa na kila kitu na kufanya kila kitu na tunakata tamaa inaposhindikana. Kisha tunatambua kwamba Mungu aliwapa watu wengine vipawa ambavyo sisi hatuna, na hivyo tunapatwa husuda, wivu, na kujisikitikia.

Nini maana ya kujisalimisha?
Kujisalimisha kwa Mungu si kujiuzulu na kukaa tu kusubiri, au kuamini kuwa yote yameandikwa binadamu hana hiari, au kuwa na udhuru na wivu. Siyo kukubali hali hiyo hiyo uliyo nayo. Inaweza kumaanisha kinyume cha haya; kujitoa sadaka maisha yako au kuteseka ili kubadilisha yanayohitaji kubadilishwa. Mara nyingi Mungu huwaita watu waliojisalimisha kwake kupiga vita kwa jina lake.

Ndugu, kujisalimisha sio kwa uoga au mazulia. Mungu asingependa kupoteza akili alizokupa! Mungu hapendi watu wawe kama mitambo (robots) ili kumtumikia. Kujisalimisha siyo kukomesha utu wako. Badala ya kukomesha utu wako, kujisalimisha huutia nguvu. C. S. Lewis alisema, "kadiri tunavyomruhusu Mungu atutawale ndivyo tunavyozidi kuwa sisi wenyewe-kwa sababu yeye ndiye aliyetuumba. Alibuni namna mbalimbali za watu wote tofauti ambao mimi na wewe tulikusudiwa kuwa...Ni pale ninapomgeukia Kristo, ninapojikabidhi nafsi yangu kwake, ndipo ninapokuwa na ule utu wangu halisi."

Kujisalimisha kunadhihirika vyema katika kutii. Ukisema 'ndiyo, Bwana' kwa chochote anachokueleza. Kusema "Hapana, Bwana" ni kutamka vinyume. Hatuweza kumwita Yesu Bwana na wakati huo huo hatutaki kumtii. Baada ya usiku kucha bila kupata samaki, Simoni Petro alionyesha kujisalimisha pale Yesu alipomwambia kujaribu tena. "Simoni akajibu akamwambia, Bwana Mkubwa, tumefanya kazi ya kuchosha usiku kucha, tusipate kitu; lakini kwa neno lako nitazishusha nyavu," Lk 5:5. Watu waliojisalimisha hutii neno la Mungu hata kama linaonekana kutokuwa na maana.

Ndugu yangu na Mtawa mwenzangu, nawe mwenye hofu ya Mungu, jambo lingine katika kujisalimisha ni IMANI. Ibrahimu (Mwa 12: 1-4) alifuata maelezo ya Mungu bila kujua alikokuwa akienda. Hana (1Sam 1:1-20) alisubiri wakati wa Mungu bila kujua ni lini. Mama Bikira Maria (Lk 1:26-35) alitarajia muujiza bila kufahamu utatendekaje. Yusufu mume wa Bikira Maria (Mt 2: 19-25) aliamini lengo la mungu bila kujua kwa nini mazingira yalikuwa hivyo. Kila mmoja wa watu hawa alikuwa amejisalimisha kwa Mungu alipomtegemea bila kujibakiza.

Utafahamu umejisalimisha kwa Mungu unapomtegemea Mungu akutengenezee mambo yako badala ya kujaribu kuwafanyia hila wengine, ukapitisha jambo lako, na mwisho ukatawala mazingira hayo. "Ukae kimya mbele za Bwana, Nawe umngojee kwa saburi," Zab 37:7a. Baada ya kujaribu sana, umwamini zaidi. Pia ufahamu kwamba unajisalimisha unapokuwa huchukizwi na lawama na kukimbilia kujitetea. Mioyo iliyojisalimisha huonyesha mahusiano mazuri na wengine. Huwatupilia mbali wengine, hudai haki zako, na hutumikii nafsi yako kama umejisalimisha.

Eneo gumu kwa watu wengi kujisalimisha ni mali na pesa zao. Wengi wamefikiri, "Nataka kuishi kwa ajili ya Mungu lakini pia nataka kupata pesa nyingi ili niishi kwa raha baadaye nipumzike." Kupumzika siyo lengo la maisha ya kujisalimisha, kwa sababu huku ni kushindana na Mungu kwa sababu ya kuweka mkazo kwanza kwa maisha yetu. Yesu anasema, "hakuna mtu awezaye kutumikia mabwana wawili; kwa maana atamchukia huyu, na kumpenda huyu; ama atashikamana na huyu, na kumdharau huyu," Mt 6:24 na kwamba "kwa kuwa hazina yako ilipo, ndipo utakapokuwapo na moyo wako," Mt 6:21.

Ndugu yangu, kielelezo kikubwa cha kujisalimisha ni Yesu. Usiku ule kabla ya mateso Yesu alijisalimisha kwa mpango wa Mungu. Alisali, "Aba, Baba, yote yawezekana kwako; uniondolee kikombe hiki; walakini, si kama nitakavyo mimi, bali utakavyo wewe," Mk 14:36. Yesu hakuomba, "Baba, kama unaweza kuniondolea maumivu haya, tafadhali fanya hivyo." Alikuwa tayari amethibitisha kuwa Mungu ana uwezo wa kufanya lolote! Badala yake anaomba, "Mungu kama inapendeza kwako kuniondolea mateso haya, tafadhali fanya hivyo. Lakini kama yanatimiza kusudi lako, ndivyo ninavyotaka pia.

Kujisalimisha halisi husema, "Baba, kama tatizo hili, maumivu haya, ugonjwa huu, au hali yoyote inahitajika kutimiza lengo lako na utukufu kwako katika maisha yangu au ya mwingine, tafadhali usiliondoe." Kiwango hiki cha ukomavu hakiji kwa urahisi. Kwa upande wa Yesu, aliugua sana kuhusu mpango wa Mungu kiasi cha kutoa jasho la damu. Kwa upande wetu, ni vita kali dhidi ya asili yetu ya ubinafsi.

Je, baraka za kujisalimisha ni zipi?
Maandiko Matakatifu yapo wazi kabisa kuhusu unavyoweza kufaidika unapojisalimisha kikamilifu kwa Mungu. Kwanza unapata amani: "mjue sasa Mungu, ili uwe na amani; Ndivyo mema yatakavyokujia," Ayu 22:21. Pili, unapata uhuru: "lakini Mungu na ashukuriwe, kwa maana mlikuwa watumwa wa dhambi, lakini mliitii kwa mioyo yenu ile namna ya elimu ambayo mliwekwa chini yake," Rum 6:17.

Tatu, unapata nguvu za Mungu katika maisha yako. Majaribu makali na matatizo mazito yanaweza kushindwa na Kristo kama atakabidhiwa. Joshua alipoviendea vita vile vikubwa maishani mwake, (Yosh 5:13-15) alikutana na Mungu, akamsujudia, na akasalimisha mipango yake. Kujisalimisha huko kulileta ushindi mkubwa pale Yeriko.

Hiki ni kitendawili: Ushindi huja kwa kujisalimisha, kujisalimisha hakukudhoofishi wewe; kunakutia nguvu. Jisalimishe kwa Mungu, hauhitaji kuogopa au kujisalimisha kwa chochote kile. William Booth, mwanzilishi wa Jeshi la wokovu, alisema, "ukuu wa nguvu za ubinadamu unapimwa kwa kiwango chake cha kujisalimisha."Watu waliojisalimisha ndio Mungu anawatumia. Mungu alimchagua Bikira Maria Mama wa Yesu, siyo kwa sababu alikuwa na kipawa, au utajiri wa uzuri wa umbile, lakini kwa sababu alikuwa amejitoa kikamilifu kwake. Malaika wa Bwana alipomwelezea mpango mgumu wa Mungu, alijibu kwa upole, "Tazama, mimi ni mjakazi wa Bwana; na iwe kwangu kama ulivyosema," Lk 1:38a. Hakuna kitu kikubwa kama maisha ya kujisalimisha katika mikono ya Mungu. "Basi mtiini Mungu. Mpingeni Shetani, naye  atawakimbia," Yak 4:7a.

Je, njia bora ya kujisalimisha ni ipi?
Kila mtu hatimaye hujisalimisha kwa mtu au kitu fulani. Kama sio kwa Mungu, utajisalimisha kwa matarajio au maoni ya watu wengine, au pesa, chuki, hofu, au kwa kiburi chako au tamaa mbaya, au ubinafsi. Uliumbwa kumwabudu Mungu na kama utashindwa kumwabudu, utatengeneza vitu vingine (sanamu) ili uvipe maisha yako.

Ndugu yangu na Mtawa mwenzangu, nawe mwenye hofu ya Mungu, unao uhuru wa kuchagua usalimishe maisha yako, lakini huko huru na matokeo ya uchaguzi huo. E. Stanly Jones alisema, "kama hujajisalimisha kwa Kristo, utajisalimisha kwa machafuko." Kijisalimisha si njia bora ya kuishi; ni njia pekee ya kuishi. Hakuna kitu kingine cha kukufanikisha. Njia nyingine zote hukuongoza kwenye kukutatisha tamaa, na kuziangamiza nafsi. Tafsiri ya King James huita kujisalimisha "huduma yenu yenye maana," Rum 12:1. Tafsiri nyingine inasema, "njia yenye maana zaidi ya kumtumikia." Rum 12:1.

Kusalimisha maisha yako si hisia za kipumbavu kama wengu watuonavyo leo sisi Watawa,  bali ni tendo la akili na busara ambalo unaweza kulifanya kwa ajili ya maisha yako. Ndiyo maana Mtume Paulo anasema, "kwa hiyo tena, ikiwa tupo hapa, au ikiwa hatupo hapa, twajitahidi kumpendeza yeye," 2Kor 5:9. Nyakati zako za busara zitakuwa zile ambazo unasema ndiyo kwa Mungu.

Wakati mwingine huchukua miaka, lakini hatimaye unagundua kwamba kizuizi kikubwa kwa Baraka za Mungu maishani mwako sio watu wengine, ni wewe mwenyewe-matakwa yako binafsi, kiburi cha hali ya juu, na matarajio yako. Huwezi kutimiza lengo la Mungu kwa maisha yako huku ukikazania malengo yako binafsi.

Kama ataenda kufanya kazi ndani yako, itaanza hivyo. Kwa hiyo mpe yote Mungu: kushindwa kwako hapo nyuma, matatizo yako ya sasa, matarajio yako ya mbele hofu zako, ndoto, udhaifu, tabia, maumivu, na madhara yoyote uliyo nayo. Mtawa mwenzangu, nawe mwenye hofu ya Mungu, mweke Yesu katika kiti cha dereva wa maisha yako na uondoe mikono yako toka kwenye usukani. Usiogope; hakuna chochote katika uongozi wake kinaweza kupoteza dira. Chini ya uongozi wa Kristo unaweza kudumu chochote. Utakuwa na Mtume Paulo, "Nayaweza mambo yote katika yeye anitiaye nguvu," Flp 4:13

Wapendwa wana wa Mungu, kujisalimisha kwa Paulo kulitokea katika njia ya Dameski alipoangushwa chini na mwanga mkali uliompofusha. Kwa watu wengine, Mungu anapata mwitikio wetu bila kutumia njia ya ajabu sana. Pamoja na hayo kujisalimisha siyo tukio la wakati mmoja tu. Kuna wakati wa kujisalimisha, na kuna tendo la kujisalimisha, ambalo ni la muda-hadi-muda na maisha yote. Tatizo la sadaka iliyo hai ni kwamba inaweza kutambaa na kutoka madhabahuni, hivyo unaweza kutakiwa kujisalimisha hata mara hamsini kwa siku. Ni lazima ufanye jambo hili kuwa tabia yako ya kila siku. Yesu anasema, "mtu ye yote akitaka kunifuata, na ajikane mwenyewe, ajitwike msalaba wake kila siku, anifuate," Lk 9:23

Ngoja nikuonye: unapoamua kuishi maisha ya kujisalimisha kikamilifu, uamuzi huo utapimwa. Wakati mwingine itamaanisha kufanya mambo yasiyostahili, ya gharama, au yanayoonekana hayawezekani. Mara nyingi itamaanisha kufanya kinyume cha unavyojisikia kufanya. Mmoja ya viongozi wakuu wa Kikristo wa karne ya ishirini alikuwa Bill Bright, mwanzilishi wa Campus Crusade for Christ. Kwa kutumia watumishi wa shirika hili duniani pote, kipeperushi cha sheria nne za kiroho, na filamu ya Yesu (iliyoonwa na watu zaidi ya bilioni nne), zaidi ya watu milioni 150 wamekuja kwa Yesu.

Siku moja mtu mmoja alimuuliza Bill, "Kwa nini Mungu anakutumia na kukubariki maisha yako kiasi kikubwa hivyo? Alisema, "Nilipokuwa kijana mdogo, nilifanya mkataba na Mungu. Niliandika na kutia sahihi ya jina langu chini yake. Mkataba huo ulisema. 'Tangu siku hii ya leo na kuendelea, mimi ni mtumwa wa Kristo.'"

Je, umewahi kusaini mkataba kama huo na Mungu?  Au bado unabishana na kupambana na Mungu juu ya haki yake kufanya lolote apendalo kwa maisha yako? Ndugu na Mtawa mwenzangu, sasa ni wakati wako kujisalimisha-kwa neema ya Mungu, upendo na hekima yake.

Tumsifu Yesu Kristo!


Basi wewe, mwanangu, uwe hodari katika neema iliyo katika Kristo Yesu,” 2Tim 2:1

No hay comentarios:

Publicar un comentario