IJUMAA WIKI YA 1 YA MWAKA-C
15/1/2016
Somo: 1Sam 8:4-7, 10-22a
Zab: 89:16-17, 18-19
Injili: Mk 2:1-12
Nukuu:
“Ndipo wazee wote wa
Israeli wakakutana pamoja, wakamwendea Samweli huko Rama; wakamwambia, Angalia, wewe umekuwa
mzee, na wanao hawaendi katika njia zako; basi, tufanyie mfalme atuamue, mfano
wa mataifa yote,” 1Sam 8:4-5
“Lakini neno hilo
likawa baya machoni pa Samweli, waliposema, Tupe mfalme atuamue. Naye Samweli
akamwomba Bwana,” ISam 8:6
“Bwana akamwambia
Samweli, Isikilize sauti ya watu hawa katika kila neno watakalokuambia; kwa
maana hawakukukataa wewe, bali wamenikataa mimi, ili nisiwe mfalme juu yao,”
1Sam 8:7
“Walakini hao watu
wakakataa kuisikiliza sauti ya Samweli; wakasema, Sivyo hivyo; lakini tunataka
kuwa na mfalme juu yetu; ili sisi nasi tufanane na mataifa yote; tena ili mfalme wetu
atuamue, tena atoke mbele yetu na kutupigia vita vyetu,” 1Sam 8:19-20
“Bwana akamwambia
Samweli, Isikilize sauti yao, ukawafanyie mfalme,” 1Sam 8:22
“Wakaja watu
wakimletea mtu mwenye kupooza, anachukuliwa na watu wanne,” Mk 2:3
“Na walipokuwa
hawawezi kumkaribia kwa sababu ya makutano, waliitoboa dari pale alipokuwapo;
na wakiisha kuivunja wakalitelemsha godoro alilolilalia yule mwenye kupooza,”
Mk 2:4
“Naye Yesu, alipoiona
imani yao, akamwambia yule mwenye kupooza, Mwanangu, umesamehewa dhambi
zako,”Mk 2:5
“Na baadhi ya
waandishi walikuwako huko, wameketi, wakifikiri mioyoni mwao, Mbona huyu anasema
hivi? Anakufuru. Ni nani awezaye kusamehe dhambi isipokuwa mmoja, ndiye Mungu?” Mk 2:6-7
“Mara Yesu akafahamu
rohoni mwake kwamba wanafikiri hivyo nafsini mwao, akawaambia, Mbona mnafikiri
hivi mioyoni mwenu?” Mk 2:8
“Vyepesi ni vipi,
kumwambia mwenye kupooza, Umesamehewa dhambi zako, au kusema, Ondoka, ujitwike
godoro lako, uende?” Mk 2:9
“Lakini mpate kujua ya
kwamba Mwana wa Adamu anayo amri duniani ya kusamehe dhambi, (hapo amwambia
yule mwenye kupooza)” Mk 2:10
TAFAKARI: “Mwana wa Adamu anayo amri
duniani ya kusamehe dhambi.”
Wapendwa wana wa Mungu, maisha ni pamoja na kuzikabili
changamoto za kila siku. Ila jambo la kukumbuka ni kwamba changamoto hizi ziwe
sehemu za makuzi yako kimwili na kiroho. Mtu ukua kimwili na kiroho
anapoikamili changamoto husika kwa mwelekeo ulio sahihi na bila kupoteza
malengo yake kuelekea kule kuliko sahihi-uzima wa milele. Wengi wetu hupenda
kuzikabili changamoto kwa njia rahisi na za mikato. Ukweli ni kwamba chochote
kile ‘rahisi’ kwisho wa siku huwa ‘ghali.’
Wapo pia baadhi yetu uzikabili changamoto kwa mtazamo
‘mfanano’ kwa lengo la kujiridhisha nafsi baada ya kutamani kitu hicho kwa muda
mrefu bila kukipata. Mfano kama ulitamani gari kama alilokuwa nalo jirani yako
na hukuwa na uwezo wa kulinunua, inapotokea nafasi ya kupata hata lililo bovu ila
linamfanano na lile jirani yako na lipo chini ya uwezo wako kifedha, mtu huyu
ulinunua tu ili kukidhi tamaa ya moyo wake. Ila vilivyo ‘rahisi’ mwisho huwa
‘ghali.’ Matokeo yake ni kwamba badala ya kusonga mbele kimaisha hurudi nyumba
kwa sababu matunzo ya gari hili bovu ulilolinunua ujeuka kuwa kitafuno cha
fedha na mali zako zote ulizokwisha kukusanya muda mrefu kwa shida na taabu.
Hali hii ndiyo iliyowakuta wana wa Israeli wakiongozwa wa
WAZEE walipomwendea Samweli na kumwambia, “Angalia,
wewe umekuwa mzee, na wanao hawaendi katika njia zako; basi, tufanyie mfalme
atuamue, mfano wa mataifa yote,” 1Sam 8:5.
Maisha ya wana wa Israeli muda wote yalikuwa mikoni mwa Mungu. Mungu ndiye
aliyekuwa kiongozi wao na aliwaongoza vyema ingawa hapa na pale waliweza kumwasi.
Mungu alibaki na amebaki kuwa Upendo na Huruma. Mungu wetu si kama mtu katili
mwenye kuwashurutisha watu kama alivyo kamanda wa vita. Kama mzazi aliyekomaa
kimaadili, Lk 15:11-32 (soma habari ya mwana mpotevu), Mungu uruhusu yale
tuyapendayo ili tujionee wenyewe kama waswahili wasemavyo, ‘mtoto akilia wembe
mpe.’ “Bwana akamwambia Samweli, Isikilize sauti ya watu hawa katika
kila neno watakalokuambia; kwa maana hawakukukataa wewe, bali wamenikataa mimi,
ili nisiwe mfalme juu yao,” 1Sam 8:7. Hata
pamoja na kupewa angalizo la mfalme huyo wanayemtaka kutokuwa mzuri, 1Sam
8:11-18, bado wanang’ang’ania kile wasichokijua. “Walakini hao watu wakakataa kuisikiliza sauti ya Samweli;
wakasema, Sivyo hivyo; lakini tunataka kuwa na mfalme juu yetu; ili sisi nasi tufanane na mataifa yote; tena ili mfalme wetu
atuamue, tena atoke mbele yetu na kutupigia vita vyetu,” 1Sam 8:19-20. Hakika
sikio la kufa halisikii dawa. “Bwana akamwambia
Samweli, Isikilize sauti yao, ukawafanyie mfalme,” 1Sam 8:22. Hivi ndivyo Waisraeli walipotamani kuwa na mfalme
na Mungu aliruhusu. Mfalme atakayechaguliwa ndiye yule aliyejulikana kama
Mfalme Sauli. Chini ya mfalme huyu taifa hili liliyumba sana na kukosa amani na
mwelekeo.
Wapendwa katika Kristo,
nasi kwa namna fulani hupenda kuwa huru ndani ya nafsi zetu na kwa namna hiyo
humtafuta mfalme na kumkabidhi nafsi yako aiongoze. Mfalme huyu aweza kuwa
ulevi, fedha, chuki, majungu, wivu, zinaa, nk. Unapoikubali roho hizi ndani
yako na kuruhusu kuwa roho hiyo kuyaongoza maisha yako, basi ujue ni kwa namna
hiyo hiyo tunamkataa Mungu kuwa kiongozi wa maisha yetu. Hapa hapatakuwa na
usalama hata kidogo.
Somo la Injili leo tunaona
mamlaka aliyokuwa nayo Yesu yanahojiwa. Wengi wanamwona Yesu katika mtazamo
‘mfanano.’ Licha ya ishara nyingi alizozifanya Yesu baadhi ya watu hawakuona
zaidi na ishara zile. Wapo walimchukulia Yesu kama mwana mazingaumbwe fulani
hivi. Lakini Yesu anasema, “Kama sizitendi kazi
za Baba yangu, msiniamini; lakini
nikizitenda, ijapokuwa hamniamini mimi, ziaminini zile kazi; mpate kujua na
kufahamu ya kuwa Baba yu ndani yangu, nami ni ndani ya Baba,” Yoh 10:37-38. Kwa
kutambua ukweli huu, Yesu anayasema maneno haya bila kupepesa macho kutokana na
kutokulipokea tendo lile kama tendo la Mungu baada ya kumponya mtu yule aliyekuwa
amepooza. Kwa kutambua yaliyokuwa mioyoni mwao, Yesu akawaambia, “lakini mpate kujua ya kwamba Mwana wa Adamu anayo amri duniani
ya kusamehe dhambi, (hapo amwambia yule mwenye kupooza)” Mk 2:10. Wapo kati yetu hadi leo hawaambia uwezo wa Yesu
na nafasi yake katika fumbo zima la Utatu Mtakatifu. Utatu Mtakatifu huu, yaani
Mungu Baba, Mwana na Roho Mtakatifu, ni umoja usiogawanyika. Ilipo nafsi moja
katika utendaji na nafsi nyingine uwepo hapa hapa.
Tumsifu Yesu Kristo!
“Mimi na Baba tu
umoja,” Yoh 10:30
No hay comentarios:
Publicar un comentario