IJUMAA BAADA YA EPIFANIA, KIPINDI CHA NOELI
8/1/2016
Somo: 1Yoh 5:5-13
Zab: 142:12-13, 14-15, 19-20
Injili: Lk 5:12-16
Nukuu:
“Mwenye kuushinda
ulimwengu ni nani, isipokuwa ni yeye aaminiye ya kwamba Yesu ni Mwana wa Mungu?” 1Yoh 5:5
“Huyu ndiye aliyekuja
kwa maji na damu, Yesu Kristo; si katika maji tu, bali katika maji na katika
damu,” 1Yoh 5:6
“Naye Roho ndiye
ashuhudiaye, kwa sababu Roho ndiye kweli,” 1Yoh 5:7
“Yeye amwaminiye Mwana
wa Mungu anao huo ushuhuda ndani yake. Asiyemwamini Mungu amemfanya kuwa
mwongo, kwa kuwa hakuuamini huo ushuhuda ambao Mungu amemshuhudia Mwanawe,”
1Yoh 5:10
“Yeye aliye naye
Mwana, anao huo uzima; asiye naye Mwana wa Mungu hana huo uzima,” 1Yoh 5:12
Bwana, ukitaka, waweza kunitakasa,” Lk 5:12c
“Naye akaunyosha mkono wake, akamgusa akisema, Nataka;
takasika. Na mara ukoma wake ukamwondoka,” Lk 5:13
“Akamkataza asimwambie mtu, ila, Nenda ukajionyeshe kwa
kuhani; ukatoe kwa ajili ya kutakasika kwako kama Musa alivyoamuru, iwe
ushuhuda kwao,” Lk 5:14
“Lakini habari zake zikazidi kuenea, wakakutanika makutano
mengi wamsikilize na kuponywa magonjwa yao,” Lk 5:15
“Lakini yeye alikuwa akijiepua, akaenda mahali pasipokuwa na
watu, akaomba,” Lk 5:16
TAFAKARI: “Bwana, ukitaka, waweza kunitakasa.”
Wapendwa wana wa Mungu, neema za Mungu zipo wakati wote
katika maisha yetu. Tatizo langu na lako ni kwamba hatujiachii na kujifunua kwa
neema hizo. Haturuhusu kuguswa na neema
hizo. Ni sawa na kwenda bafuni kuoga huku ukiwa na mwamvuli. Je, utaguswa na
maji hayo? Ndiyo ya Bwana kwetu ni kujiachia kwake pasipo shaka yoyote. Hali
hii ya kujiachia kwa Bwana hupaswi kutazama shindwa yako ya nyakati zilisopita.
Mungu hututazama kila siku katika upya wetu. Tunapojisalimisha kwake, Mungu
hahesabu makaosa yetu yaliyopita. Rejea habari ya mwana mpotevu (Lk 15:11-32).
Hakika angefanya hivyo hakuna ye yote kati yetu angeweza kusimama mbele
yake. Naye Mzaburi anasema, “Bwana, kama
wewe ungeheabu maovu, Ee Bwana, nani angesimama?” Zab 130:3
Leo uponyaji wa mtu huyu mwenye ukoma kama tusomavyo katika
Injili yetu leo, unafanyika mara baada ya ndugu huyu kujiachia kwa Yesu bila
shaka. “Naye alipomwona Yesu alianguka kifudifudi, akamwomba akisema, Bwana,
ukitaka, waweza kunitakasa,” Lk 5:12bc. Ni mara ngapi tunaanguka kifudifudi
mbele ya Yesu na kujiachia kwake kwa yale yanayotusonga? Hakuna jambo lolote
tumwombalo Yesu naye akatupiga kisogo. Yesu anatuambia hivi, “Ninyi mkikaa
ndani yangu, na maneno yangu yakikaa ndani yetu, ombeni mtakalo lote nanyi
mtatendewa,” Yoh 15:7. Ndugu yangu tunayesafiri wote katika tafakari hii,
huwezi kuushinda ulimwengu wa roho bila kuwa na Yesu Mwana wa Mungu. Mtume Yohane analiona hilo na kuhoji
nafsi zetu kwa kusema, “Mwenye kuushinda ulimwengu ni nani, isipokuwa ni yeye aaminiye
ya kwamba Yesu ni Mwana wa Mungu?” 1Yoh 5:5.
Ni kweli isiyoshaka kwamba yapo mambo mengi katika maisha yetu tunakumbana nayo
na hatuna majibu ya moja kwa moja. Bila kuwa na Yesu ndani yako ambaye ndiye
njia, kweli na uzima, Yoh 14:6, ni vigumu sana kushinda sintofahamu zako.
Yesu Kristo ndiye
kielelezo chetu katika sintofahamu zote zile katika maisha yetu. Huyu ndiye
aliyekuja kwetu katika maji na katika damu. Hivyo katika ubatizo wetu
tumefanywa wana wa Mungu kupitia kwake, yaani maji, na katika sadaka yake pale
msalabani, yaani katika damu, tumefanywa huru kutoka utumwa wa dhambi. Hivyo, “Huyu ndiye aliyekuja kwa maji na damu, Yesu Kristo; si katika
maji tu, bali katika maji na katika damu,” 1Yoh 5:6. Kwake Yesu ndiko kwenye utoshelevu wote katika
mahangaiko yetu. Kweli hii ya Yesu ndani yetu imeshuhudiwa na Roho mwenyewe.
Yesu anatoa ushuhuda huu wa Roho wa Mungu ndani yake kwa kusema, “Roho
wa Bwana yu juu yangu, Kwa maana amenitia mafuta kuwahubiri maskini habari
njema. Amenituma kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao, Na vipofu kupata kuona
tena, Kuwaacha huru waliosetwa, Na
kutangaza mwaka wa Bwana uliokubaliwa,” Lk 4:18-19. Alisemalo Kristo ndiye
kweli, na alishuhudialo Roho ndiyo utakaso wenyewe. “Naye
Roho ndiye ashuhudiaye, kwa sababu Roho ndiye kweli,” 1Yoh 5:7. Ndugu yangu wayaamini haya?
Ushuhuda huu wa Kristo kwa
kinywa chake kuhusu Roho huyu wa Bwana ndani yake ni ushuhuda wetu pale
tunapomwamini Kristo. Yote ayafanyayo Kristo si kwa faida yake bali ni faida
yako na yangu. Hivyo amini yetu kuhusu Kristo ndiyo pona yetu kwa sababu
misioni ya Kristo hapa duniani ni kwa ajili ya wokovu wako na wangu. Hivyo, “Yeye amwaminiye Mwana wa Mungu anao huo ushuhuda ndani yake.
Asiyemwamini Mungu amemfanya kuwa mwongo, kwa kuwa hakuuamini huo ushuhuda
ambao Mungu amemshuhudia Mwanawe,” 1Yoh 5:10. Ni vigumu sana kupata neema hizi
za Mungu kama hatujiachii kwa Kristo katika kumwamini na kukaa ndani yake ili
uzima wake uwe ndani yetu. Mpendwa katika Kristo, “Yeye aliye naye
Mwana, anao huo uzima; asiye naye Mwana wa Mungu hana huo uzima,” 1Yoh 5:12. Hivyo uzima wa kweli ni ndani katika Kristo.
Wapendwa wana wa Mungu, bado hatujachelewa. Sote mbele
ya Mungu tu wapya na Yeye bila kuhesabu makosa yetu, huanza upya nasi kwani
lengo lake ni kutupata kuliko kutupoteza. Hii ndiyo huruma ya Mungu kwetu.
Hivyo ninapotambua huruma hii ya Mungu katika maisha yangu iwe nafasi ya
kubadilika na kubadili mfumo mzima wa maisha yangu kama kweli nataka kuishi
katika umilele. Hofu yangu iwe kwa Mungu aliye kila kitu katika maisha yangu.
Tumsifu Yesu Kristo!
“Mtu mbaya na aache njia
yake, Na mtu asiye haki aache mawazo yake; Na amrudie Bwana, Naye atamrehemu;
Na arejee kwa Mungu wetu, Naye atamsamehe kabisa,” Isa 55:7
No hay comentarios:
Publicar un comentario