viernes, 8 de enero de 2016

TAFAKARI: JUMAMOSI BAADA YA EPIFANIA KIPINDI CHA NOELI

JUMAMOSI BAADA YA EPIFANIA, KIPINDI CHA NOELI
9/1/2016
Somo: 1Yoh 5:14-21
Zab: 149: 1-2, 3-4, 5-6a, 9b
Injili: Yoh 3:22-30
Nukuu:
Na huu ndio ujasiri tulio nao kwake, ya kuwa, tukiomba kitu sawasawa na mapenzi yake, atusikia,” 1Yoh 5:14 

Mtu akimwona ndugu yake anatenda dhambi isiyo ya mauti, ataomba, na Mungu atampa uzima kwa ajili ya hao watendao dhambi isiyo ya mauti. Iko dhambi iliyo ya mauti. Sisemi ya kwamba ataomba kwa ajili ya hiyo,” 1Yoh 5:16 

Kila lisilo la haki ni dhambi, na dhambi iko isiyo ya mauti,” 1Yoh 5:17

Twajua ya kuwa kila mtu aliyezaliwa na Mungu hatendi dhambi; bali yeye aliyezaliwa na Mungu hujilinda, wala yule mwovu hamgusi,” 1Yoh 5:18 

Nasi twajua kwamba Mwana wa Mungu amekwisha kuja, naye ametupa akili kwamba tumjue yeye aliye wa kweli, nasi tumo ndani yake yeye aliye wa kweli, yaani, ndani ya Mwana wake Yesu Kristo. Huyu ndiye Mungu wa kweli, na uzima wa milele,” 1Yoh 5:20

Watoto wadogo, jilindeni nafsi zenu na sanamu,” 1Yoh 5:21

Basi palitokea mashindano ya wanafunzi wa Yohana na Myahudi mmoja juu ya utakaso,” Yoh 3:25

Yohana akajibu, akasema, Hawezi mtu kupokea neno lo lote isipokuwa amepewa kutoka mbinguni,” Yoh 3:27 

Ninyi wenyewe mwanishuhudia ya kwamba nalisema, Mimi siye Kristo, bali nimetumwa mbele yake,” Yoh 3:28 

Aliye naye bibi arusi ndiye bwana arusi; lakini rafiki yake bwana arusi, yeye anayesimama na kumsikia, aifurahia sana sauti yake bwana arusi,” Yoh 3:29 

Basi hii furaha yangu imetimia. Yeye hana budi kuzidi, bali mimi kupungua,” Yoh 3:30

TAFAKARI:Watoto wadogo, jilindeni nafsi zenu na sanamu. Yeye hana budi kuzidi (Kristo), bali mimi kupungua.”

Wapendwa wana wa Mungu, masomo yetu yote mawili wanatutaka tutafakari fadhila ya ‘unyenyekevu.’ Hivyo, “Watoto wadogo, jilindeni nafsi zenu na sanamu. Yeye hana budi kuzidi (Kristo), bali mimi kupungua.” Neno ‘watoto wadogo’ limebeba umbo la ‘unyenyekevu,’ na wito wa kuishi fadhila hiyo. Sifa chache za utoto katika udogo ni ule utayari kwa kupokea pasipo shaka yale aambiwayo na wazazi wake. Utoto katika udogo ni ile hali ya kuamini pasipo shaka. Na utoto katika udogo ni ile hali ya kuwa wazi katika kweli na haki.

Neno ‘kujilinda nafsi na sanamu,’ linakutaka uelewa mwegemeo wa nafsi yako upo wapi. Hivyo basi kabla ya kujua nafsi yako imeegemea wapi ni vyema tukaitazama NAFSI katika uhusiano wake kati ya MWILI na ROHO kadiri ya Maandiko Matakatifu. Mtu kamili anakuwa katika sehemu kuu tatu:- Nafsi, Roho, na Mwili. “Mungu wa amani mwenyewe awatakase kabisa; nanyi Nafsi zenu na Roho zenu na Miili yenu mhifadhiwe mwe kamili, bila lawama, wakati wa kuja kwake Bwana wetu Yesu Kristo.” I The 5:23

Katika hili Roho na Nafsi huwa pamoja na ndizo wewe mwenyewe. Mwili ni nyumba ya roho na nafsi. Katika uumbaji Mungu aliumba mwili kwa udongo halafu akapulizia pumzi puani ambayo ni roho yake ndipo mtu huyo akawa nafsi iliyo hai. “Bwana Mungu akamfanya mtu kwa mavumbi ya ardhi, akampulizia puani pumzi ya uhai; mtu akawa nafsi hai.” Mwa. 2:7. Miili tuliyonayo ni nyumba ya Nafsi na Roho. Kwa hali hii sisi binadamu ni wawili. Kuna mtu wa ndani na mtu wa nje. Mtu wa ndani ni Nafsi na Roho, na mtu wa nje ni Mwili lakini watu hawa wapo pamoja hatuwezi kuwatenganisha wala kumwona kwa macho ya nyama huyu mtu wa ndani, ila yupo.

Katika hili twaona haya yafuatayo:- Huyu mtu wa nje hukua, kuzeeka na kufa. Mtu wa ndani hakui, hazeeki, wala hafi. Mtu wa ndani hubadilika kwa kuchakaa kunakotokana na kujeruhiwa na kuumizwa kunakosababishwa na dhambi na matukio mbalimbali yanayomsibu binadamu. Mtu wa ndani alianza tangu pale kutungwa mimba siku ya kwanza wakati yai na mbegu na pumzi ya Mungu alipoweka roho yake. Mtu huyu wa ndani hakui wala haongezeki ila hufanywa upya. “Kwa hiyo hatulegei, bali ijapokuwa utu wetu wa nje unachakaa, lakini utu wetu wa ndani unafanywa upya siku kwa siku,” 2Kor 4:16. Kwa hiyo huyu mtu wa nje akifa mtu wa ndani huenda mahali atakapokuwa amejiandalia ama Mbinguni au motoni.

Wapendwa wana wa Mungu, kwenye Nafsi ndipo penye tatizo lenyewe kwani ni katikati ya Roho na Mwili. Nafsi hutawaliwa na Hisia, mfano:- Hofu, Chuki, Hasira, Kujihukumu, Kujikataa, Kukosa furaha, Kukosa upendo, Kukosa amani, n.k. Ni muhimu sana mtu atawale hisia zake. Nafsi ikiegemea rohoni huleta matunda mazuri. “Lakini tunda la Roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, upole, kiasi; juu ya mambo kama hayo hakuna sheria.” Gal. 5:22-23. Ila nafsi inapoegemea Mwili mambo huwa mabaya kwani ufanya matendo ya mwili kama tusomavyo katika maandiko matakatifu, “basi matendo ya mwili ni dhahiri, ndiyo haya: uasherati, uchafu, ufisadi, ibada ya sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, faraka, uzushi husuda, ulevi, ulafi, na mambo yanayofanana na hayo; katika hayo nawaambia mapema, kama nilivyokwisha kuwaambia, ya kwamba watu watendao mambo ya jinsi hiyo hawataurithi ufalme wa Mungu.” Gal.5:19-21. Ni vizuri kujua nafsi yako imeegemea wapi. Ikiegemea rohoni utaenda Mbinguni, ikiegemea mwilini utaenda motoni.

Hivyo wapendwa katika Kristo, kujilinda nafsi na sanamu ni kuiruhusu nafsi yako kuegemea katika matendo ya mwili. Sanamu hizo ambazo tunapewa angalizo leo ni hizi: uasherati, uchafu, ufisadi, ibada ya sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, faraka, uzushi husuda, ulevi, ulafi, na mambo yanayofanana na hayo mfano: fedha, sifa, mamlaka na kujiinua zaidi ya Muumba wako, na kujulikana kunakofifisha utukufu wa Mungu. Hizi zote ni sanamu. Mambo haya yakiwa ndiyo dira ya maisha yako kamwe Kristo hawezi kupata nafasi katika maisha yako hata kama utafanya mambo mazuri kupitia miwani ya Kanisa au Vyama vya kitume. Yote hayo utakayoyafanya yatakuwa na lengo la kujitukuza mwenyewe ukimwinua sanamu SIFA.

Ili niepukane sanamu hizi yanipasa niielekeze nafsi yangu katika tunda la Roho. Tunda hili la Roho litabadili mfumo mzima wa maisha yangu kutoka hali ya kujitukuza na kuelekea hali ya kujinyenyekeza. Tunda la Roho ni hili: upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, upole, kiasi; juu ya mambo kama hayo hakuna sheria. Katika hali hii Kristo atapata nafasi katika maisha yangu kwa sababu, “Yeye hana budi kuzidi, bali mimi kupungua,” Yoh 3:30b. Yohane Mbatizaji ni mfano hai wa yule aliyeishi tunda la Roho. Yohane Mbatizaji anajua mipaka yake na kile kimpasacho kufanya kadiri ya mipaka hiyo. Ninyi wenyewe mwanishuhudia ya kwamba nalisema, Mimi siye Kristo, bali nimetumwa mbele yake,” Yoh 3:28. Huku ndiko kuishinda nafsi na kukumbatia tunda la Roho.

Anayeishi katika tunda la Roho ni  Mtu yule amwonaye ndugu yake anatenda dhambi isiyo ya mauti, ataomba, na Mungu atampa uzima kwa ajili ya hao watendao dhambi isiyo ya mauti,” 1Yoh 5:16a. Moja ya dhambi isiyo ya mauti ni dhambi ile tunayoikiri katika sala ya ‘Nakuungamia Mungu Mwenyezi…,’ yaani dhambi ya “kutotimiza wajibu.” Tunapoishi katika tunda la Roho, nafsi yetu ukiri uwepo wa Kristo kwa kila tunayekutana naye. Hivyo, Nasi twajua kwamba Mwana wa Mungu amekwisha kuja, naye ametupa akili kwamba tumjue yeye aliye wa kweli, nasi tumo ndani yake yeye aliye wa kweli, yaani, ndani ya Mwana wake Yesu Kristo. Huyu ndiye Mungu wa kweli, na uzima wa milele,” 1Yoh 5:20. Ufunuo huu wa nafsi katika uwepo wa Kristo ndani na katika  maisha yetu unatupeleka karibu zaidi na Mungu na kututenga na dhambi. Twajua ya kuwa kila mtu aliyezaliwa na Mungu hatendi dhambi; bali yeye aliyezaliwa na Mungu hujilinda, wala yule mwovu hamgusi,” 1Yoh 5:18.

Ndugu yangu tuliyesafiri wote katika tafakari hii nikuombe ufanye tafiti NAFSI yako ili uweze kubaini egemeo la nafsi lako lipo wapi. Na utakapo gundua nafsi yako ilipoegemea na hasa katika tunda la Roho utajawa na furaha na kusema kama alivyosema Yohane Mbatizaji, Aliye naye bibi arusi ndiye bwana arusi; lakini rafiki yake bwana arusi, yeye anayesimama na kumsikia, aifurahia sana sauti yake bwana arusi. Basi hii furaha yangu imetimia. Yeye hana budi kuzidi, bali mimi kupungua,” Yoh 3:29-30. Bwana harusi wetu ni Kristo mwenyewe. Kiti chake cha Kifalme ni Msalaba wake Mtakatifu, na Kofia yake ya Kifalme ni taji lile la miiba. Haya ndiyo ya kujisifia katika maisha yangu kila siku ninapompa Kristo nafasi ndani ya maisha yangu kama Mkristo-mfuasi wa Kristo. AMINA.

Tumsifu Yesu Kristo!


Lakini mimi, hasha, nisione fahari juu ya kitu cho chote ila msalaba wa Bwana wetu Yesu Kristo, ambao kwa huo ulimwengu umesulibishwa kwangu, na mimi kwa ulimwengu,” Gal 6:14

No hay comentarios:

Publicar un comentario