SIKUKUU YA WATAKATIFU TIMOTEO NA TITO MAASKOFU
26/1/2016
Somo: 2Tim 1:1-8
Zab: 96:1-2ab, 3, 7-8a, 10
Injili: Mk 3:31-35
Nukuu:
“kwa Timotheo, mwanangu mpendwa. Neema na
iwe kwako, na rehema, na amani, zitokazo kwa Mungu Baba na kwa Kristo Yesu
Bwana wetu,” 2Tim 1:2
“nikiikumbuka imani uliyo nayo isiyo na
unafiki, ambayo ilikaa kwanza katika bibi yako Loisi, na katika mama yako
Eunike, nami nasadiki wewe nawe unayo,” 2Tim 1:5
“Maana Mungu hakutupa roho ya woga, bali ya nguvu na ya upendo na
ya moyo wa kiasi,” 2Tim 1:7
“Basi usiuonee haya ushuhuda wa Bwana wetu, wala usinionee haya
mimi mfungwa wake, bali uvumilie mabaya pamoja nami kwa ajili ya Injili, kwa
kadiri ya nguvu ya Mungu,” 2Tim 1:8
“Akawatazama wale
walioketi wakimzunguka pande zote, akasema, Tazama, mama yangu na ndugu zangu!” Mk 3:34
“Kwa maana mtu ye yote
atakayeyafanya mapenzi ya Mungu, huyo ndiye ndugu yangu, na umbu langu, na mama
yangu,” Mk 3:35
TAFAKARI: “Usiuonee haya
ushuhuda wa Bwana wetu.”
Wapendwa
wana wa Mungu, leo Mama Kanisa anaadhimisha Sikukuu ya Watakatifu Timeteo na
Tito Maaskofu. Timoteo na Tito, wanafunzi na washirika wa Mtume Paulo walikuwa
mstari wa mbele kwa kulijenga na kuliimarisha Kanisa la Efeso, na baadaye huko
Crate. Wote wawili walielekezwa na Mtume Paulo kwa barua zilizojulikana kama
barua za kichungaji. Ndani ya maelekezo ya barua hizi kulikuwa na matamko hasa
pale kulipotokea upotoshwaji wa jambo fulani, na maonyo kwa mafundisho ya
waamini na wachungaji.
Somo letu la kwanza tunaona Mtume Paulo
akiandika barua hii angali gerezani. Na hapa inaonyesha yale aliyowaandikia
Wafilipi sasa yameshatokea. Hivyo Paulo Mtume anamtuma Timoteo kwao ili naye
apata habari zao. “Walakini natumaini katika Bwana Yesu kumtuma Timotheo afike
kwenu karibu, nifarijiwe na mimi, nikiijua hali yenu. Maana sina mtu mwingine mwenye nia moja
nami, atakayeiangalia hali yenu kweli kweli. Maana wote wanatafuta vyao wenyewe, sivyo vya Kristo Yesu. Ila mwajua sifa yake, ya kuwa ametumika pamoja nami kwa ajili ya
Injili, kama mwana na baba yake. Basi,
natumaini kumtuma huyo mara, hapo nitakapojua yatakayonipata,” Flp 2:19-23
Ni kweli
kwamba Mtume Paulo alipendezwa sana na utendaji, ushiriki, na ushupavu wa imani aliokuwa nao Timeoteo. Mtume Paulo
anamchukulia Timoteo kama mwanaye. “Kwa Timotheo, mwanangu mpendwa. Neema na iwe kwako, na rehema,
na amani, zitokazo kwa Mungu Baba na kwa Kristo Yesu Bwana wetu,” 2Tim 1:2.
Imani aliyokuwa nayo Timoteo ilikuwa thabiti, na kamwe hakutetereshwa na jambo
lolote. Akiwa gerezani Paulo anayasema haya juu ya Timoteo, “nikiikumbuka imani uliyo
nayo isiyo na unafiki, ambayo ilikaa kwanza katika bibi yako Loisi, na katika
mama yako Eunike, nami nasadiki wewe nawe unayo,” 2Tim 1:5
Kama
ilivyokuwa uhusiano wa karibu wa Mtume Paulo na Timoteo, ndivyo ilivyokuwa kwa
Tito. Barua ndogo kwa Tito tunaona Mtume Paulo anakutana kwa mara ya kwanza na
Tito huko Antiokia bila shaka mwaka (48 bk), na Tito alimsindikiza Mtume Paulo
kwenye ule mtaguso wa Yerusalemu, Mdo 15. “Kisha, baada ya miaka
kumi na minne, nalipanda tena kwenda Yerusalemu pamoja na Barnaba, nikamchukua
na Tito pamoja nami,” Gal 2:1. Kwa nyakati mbalimbali Tito anawatembelea
Wakristo wa Korintho. “Lakini ahimidiwe Mungu atiaye bidii ile ile kwa ajili yenu
katika moyo wa Tito. Maana
aliyapokea kweli yale maonyo; tena, huku akizidi kuwa na bidii, alisafiri
kwenda kwenu kwa hiari yake mwenyewe,” 2Kor 8:16-17. Mtume Paulo alimtuma huko kwa sababu kuu mbili;
kwanza, kuimarisha maisha ya imani ya jumuiya hiyo ya Korintho. Na pili, kwa
shughuli za kimisionari.
Uinjilishaji huu ulikuwa
mgumu sana kwa sababu walipambana na kila aina ya upinzani kwa ajili ya habari
njema ya wokovu. Mtume Paulo anajua taabu zote hizo na anasema, “Mungu hakutupa roho ya
woga, bali ya nguvu na ya upendo na ya moyo wa kiasi,” 2Tim 1:7. Ni kwa kuushinda
woga habari njema zilienea kila pande za dunia. Nasi leo tunajionea na
kujivunia majitoleo yao katika kulihubiri neno la Mungu. Ujumbe anaotupatia leo
Mtume Paulo kuhusu habari njema ya wokovu ni huu: “Basi usiuonee haya
ushuhuda wa Bwana wetu, wala usinionee haya mimi mfungwa wake, bali uvumilie
mabaya pamoja nami kwa ajili ya Injili, kwa kadiri ya nguvu ya Mungu,” 2Tim
1:8. Yanipasa mimi na wewe kusimama imara katika imani dhabiti pale nilipo.
Anza umisionari huo hapo ulipo kwa kuona kama Kristo, kuwaza kama Kristo,
Kuamua kama Kristo, na kutenda kama Kristo.
Tumsifu
Yesu Kristo!
Watakatifu
Timoteo na Tito Maaskofu. Mtuombee
“Maana, ijapokuwa
naihubiri Injili, sina la kujisifia; maana nimewekewa sharti; tena ole wangu
nisipoihubiri Injili!” 1Kor 9:16
No hay comentarios:
Publicar un comentario