JUMATANO WIKI YA 3 YA MWAKA-C
Somo: 2Sam 7:4-17
Zab: 88:4-5, 27-28, 29-30
Injili: Mk 4:1-20
Nukuu:
“Kwa maana mimi sikukaa ndani ya nyumba, tangu siku ile
niliyowatoa wana wa Israeli katika Misri, hata leo, lakini nimekaa katika hema
na maskani,” 2Sam 7:6
“Basi, sasa, mwambie mtumishi wangu, Daudi, maneno haya, Bwana
wa majeshi asema hivi, Nalikutwaa katika zizi la kondoo, katika kuwaandama
kondoo, ili uwe mkuu juu ya watu wangu, juu ya Israeli,” 2Sam 7:8
“nami nimekuwa pamoja nawe kila ulikokwenda, na kuwakatilia
mbali adui zako wote mbele yako; nami nitakufanyia jina kuu, kama jina la wakuu
walioko duniani,” 2Sam 7:9
“Yeye ndiye atakayejenga nyumba kwa jina langu, nacho kiti cha
enzi cha ufalme wake nitakifanya imara milele,” 2Sam 7:13
“lakini fadhili zangu hazitamwondoka, kama vile
nilivyomwondolea Sauli, niliyemwondoa mbele yako,” 2Sam 7:15
“Na nyumba yako, na ufalme wako, vitathibitishwa milele mbele
yako. Nacho kiti chako kitafanywa imara milele,” 2Sam 7:16
“Mpanzi huyo hulipanda
neno,” Mk 4:14
“Hawa ndio walio kando
ya njia lipandwapo neno; nao, wakiisha kusikia, mara huja Shetani, akaliondoa
lile neno lililopandwa mioyoni mwao,” Mk 4:15
“Kadhalika na hawa
ndio wapandwao penye miamba, ambao kwamba wakiisha kulisikia lile neno, mara
hulipokea kwa furaha; ila
hawana mizizi ndani yao, bali hudumu muda mchache; kisha ikitokea dhiki au
udhia kwa ajili ya lile neno, mara hujikwaa,” Mk 4:16-17
“Na hawa ndio wale
wapandwao penye miiba; ni watu walisikiao lile neno, na shughuli za dunia,
na udanganyifu wa mali, na tamaa za mambo mengine zikiingia, hulisonga lile
neno, likawa halizai,” Mk 4:18-19
“Na hawa ndio
waliopandwa penye udongo ulio mzuri; ni watu walisikiao lile neno na kulipokea,
na kuzaa matunda, mmoja thelathini, mmoja sitini, na mmoja mia,” Mk 4:20
TAFAKARI: “Na tuutafute udongo mzuri ili tuzae matuma. Nalo ndilo
neno la uzima.”
Wapendwa wana wa Mungu,
ulimwengu wetu wa leo umekamatwa na vipaumbele vyake ambavyo ukichunguza kwa
undani havina uhai ndani yake. Miaka kumi na tano iliyopita kwa mkristo kwenye
hofu ya Mungu kabla ya kuanza safari yake
hakuweza kuondoka nyumbani bila kuhakikisha Rozali yake ipo mfukoni. Leo
jambo la kwanza kabla yote kuweka mfukoni ni simu ya mkononi. Na wakati
mwingine mtu yupo tayari hata kulala njaa lakini simu yake iwe na salio.
Leo siyo kwamba watu
hawaamini uwepo wa Mungu tu, bali hawataki kabisa kusikia habari zake. Mungu
aliye Upendo, Huruma, Haki na Amani, amejeuzwa kuwa adui kwa wale
walioutanguliza mbele ulimwengu na malimwengu yake. Na pale Mungu anapotafutwa
lengo lake ni kumtaka Mungu afanye kadiri ya mapenzi yetu. Mungu huyu
tunamtafuta kwa bidii pale mipango yetu inapokwama na hatuna namna ya
kujikwamua katika matatizo yetu. Tunamjeuza Mungu wetu kuwa kama Shirika la
Msalaba mwekundu.
Leo Yesu anatupa mfano wa
Mpanzi akitutaka kuujenga uhusiano mzuri na Mungu kupitia neno lake. Neno la
Bwana ni uzima kwetu na neno hilo hututoa mautini na kuingia uzimani. “Amin, amin, nawaambia, Yeye alisikiaye neno
langu na kumwamini yeye aliyenipeleka yuna uzima wa milele; wala haingii
hukumuni, bali amepita kutoka mautini kuingia uzimani,” Yoh 5:24. Maadui wa
neno la Mungu wa kwanza ni shetani na hila zake. Ila shetani wa mtu ni mtu
mwenyewe. Unaporuhusu hali ya ukavu ndani ya maisha yako ndivyo hivyo hivyo
unavyo yapalilia makazi ya shetani ndani ya nafsi yako. “Hawa ndio walio kando ya njia lipandwapo neno; nao, wakiisha
kusikia, mara huja Shetani, akaliondoa lile neno lililopandwa mioyoni mwao,” Mk
4:15. Ni vyema kila siku ukawa hata na dakika
15 za kulisoma neno la Mungu na kulifanya lako. Usomapo neno hilo jiulize
linasema nin juu ya maisha yako.
Adui wa pili kuhusu neno la Mungu ni dhiki na udhia katika
maisha yetu. Katika dhiki za maisha na udhia Yesu anatuambia neno la uzima
kwamba Yeye kesha ushinda ulimwengu hivyo tuwe na imani ndani yake. Naye Yesu
anasema, “Tazama, saa yaja, naam, imekwisha kuja, ambapo mtatawanyika kila
mmoja kwao kwao, na kuniacha mimi peke yangu; walakini mimi si peke yangu, kwa
kuwa Baba yupo pamoja nami. Hayo
nimewaambieni mpate kuwa na amani ndani yangu. Ulimwenguni mnayo dhiki; lakini
jipeni moyo; mimi nimeushinda ulimwengu,” Yoh 16:32-33. Ndugu yangu bila
kushikamana na Kristo aliyeushinda ulimwengu katika dhiki na udhia hutaweza
kuushinda ulimwengu huu kwa nguvu zako mwenyewe. Kuzitumainia nguvu zako ni
kuelekea kushindwa kabisa. “Kadhalika na hawa ndio wapandwao penye miamba, ambao
kwamba wakiisha kulisikia lile neno, mara hulipokea kwa furaha; ila hawana mizizi ndani yao,
bali hudumu muda mchache; kisha ikitokea dhiki au udhia kwa ajili ya lile neno,
mara hujikwaa,” Mk 4:16-17
Adui wa
tatu wa neno la Mungu ni shughuli za dunia, na udanganyifu wa mali, na tamaa za
mambo mengine. Leo watu wengi lengo la maisha yao yote huongozwa na tamaa ya kupata vitu. Msukumo huu wa
kutaka zaidi kila siku una misingi yake katika udanganyifu wa kuwa nikiwa na
vingi nitakuwa na furaha zaidi, nitakuwa wa muhimu, na nitakuwa salama; lakini
mawazo hayo yote matatu si ya kweli. “Na hawa
ndio wale wapandwao penye miiba; ni watu walisikiao lile neno, na shughuli za dunia, na
udanganyifu wa mali, na tamaa za mambo mengine zikiingia, hulisonga lile neno,
likawa halizai,” Mk 4:18-19. Mali
huleta furaha ya "muda mfupi tu." Na sababu kubwa ndugu yangu, vitu
havibadiliki, hivyo vinatuchosha na tunataka vipya, vikubwa, na bora zaidi.
Kuna imani pia kwamba
nitapata mali nyingi nitakuwa wa muhimu. Umuhimu wako na mali ni vitu viwili
tofauti. Thamani yako haitegemei mali zako, Mungu anasema kitu cha muhimu maishani
mwako si vitu! Imani ya watu wengi kuhusu fedha ni kwamba kuwa nazo nyingi
kutanipa usalama. Huwezi! Yesu anawaambia wale wafuasi wa Yohane Mbatizaji,
“Mnatafuta nini?” Wanafunzi wale wakamjibu,
Rabi, (maana yake, Mwalimu), unakaa wapi?”
Yoh 1:38. Anapokaa Yesu ndipo kwenye usalama kupita vitu vyote na hali zote
tunazoweza kufikiria. Mt. Augustino anasema, “mioyo yetu haitulii mpaka
itakapotulia kwako Ee Bwana.”
Ndugu yangu, utajiri
unaweza kupotezwa mara moja kwa sababu zisizozuilika. Usalama halisi unaweza
kupatikana katika kile ambacho huwezi kunyang'anywa yaani uhusiano wako na
Mungu. “Na hawa ndio waliopandwa penye udongo ulio mzuri; ni watu
walisikiao lile neno na kulipokea, na kuzaa matunda, mmoja thelathini, mmoja
sitini, na mmoja mia,” Mk 4:20. Mt.
Augustino anatuwasa kutoka kwenye kanuni yake, "kuna furaha kubwa kuwa na
vichache kuliko kuwa na vingi." Hata hivyo tatizo hapa ni kipimo cha huo
uchache na huo wingi. Uzima wetu upo katika neno la uzima nalo ndilo ngao yetu
katika ulimwengu huu kigeugeu.
Usalama wa Mfalme Daudi
upo katika kuujenga uhusiano mzuri na wakaribu na Mungu. Nabii Nathani anampa
Mfalme Daudi ujumbe wa Mungu kuhusu hamu yake, yaani, kumjengea nyumba naye
hatamwacha kamwe. “Kwa
maana mimi sikukaa ndani ya nyumba, tangu siku ile niliyowatoa wana wa Israeli
katika Misri, hata leo, lakini nimekaa katika hema na maskani,” 2Sam 7:6. Na wakuifanya kazi hii ni Mfalme Daudi na si
mwingine. “Yeye ndiye atakayejenga nyumba kwa jina langu, nacho kiti cha enzi cha
ufalme wake nitakifanya imara milele,” 2Sam 7:13. Ndugu yangu, yapo mambo mengi
katika maisha yetu yanayofanana na hili jukumu alilopewa Mfalme Daudi. Bila
shaka yoyote Kanisa letu la Tanzania leo takribani kila Parokia kuna ujenzi wa
Nyumba ya Mungu au Shule. Jukumu hilo ni la kila mbatizwa pale alipo. Kwa
kufanya hivyo bila kujibakiza ndivyo tunavyopewa baraka kama alivyohaidiwa
Mfalme Daudi.
Shughuli hii ya kujenga Nyumba ya Mungu, yaani, Kanisa
ifanywe bila malalamko na manung’uniko kwa sababu Kanisa hili ni baraka kwako
kwa milele yote. Watu wataendelea kumsifu na kumwabudu Mungu vizazi na vizazi
hata kama hautakuwepo tena katika ulimwengu huu. Baraka hizi hazina kipimo.
Mchango wako leo katika ujenzi wa Kanisa au Shule ni hazima kubwa sana, na hasa
pale unapojitoa bila kujibakiza kwa hali na mali. Haya ndiyo aliyohaidiwa Mfalme Daudi na ndiyo
unayohaidiwa wewe na mimi tutakapotimiza wajibu huu muhimu wa kumjengea Mungu
Nyumba-Kanisa. “Lakini fadhili zangu hazitamwondoka, kama vile
nilivyomwondolea Sauli, niliyemwondoa mbele yako. Na nyumba yako, na ufalme
wako, vitathibitishwa milele mbele yako. Nacho kiti chako kitafanywa imara
milele,” 2Sam 7:15-16. Wakati ndio sasa na
timiza wajibu wako huo muhimu mbele za Mungu.
Tumsifu
Yesu Kristo
“Katika shida za moyo wangu unifanyie nafasi, Na kunitoa
katika dhiki zangu,” Zab 25:17
No hay comentarios:
Publicar un comentario