domingo, 10 de enero de 2016

TAFAKARI: JUMATATU WIKI YA 1 YA MWAKA-C

JUMATATU WIKI YA 1 YA MWAKA-C
11/1/2016
Somo: 1Sam 1:1-8
Zab: 116: 12-13, 14-19
Injili: Mk 1:14-20
Nukuu:
Elkana mumewe akamwambia, Hana, unalilia nini? Kwani huli chakula? Kwa nini moyo wako una huzuni? Je! Mimi si bora kwako kuliko watoto kumi?” Isam 1:8

akisema, Wakati umetimia, na ufalme wa Mungu umekaribia; tubuni, na kuiamini Injili,” Mk 1:15

Yesu akawaambia, Njoni mnifuate, nami nitawafanya kuwa wavuvi wa watu,” Mk 1:17

Mara wakaziacha nyavu zao, wakamfuata,” Mk 1:18

TAFAKARI:Wakati umetimia, na ufalme wa Mungu umekaribia; tubuni, na kuiamini Injili.”

Wapendwa wana wa Mungu, maisha yanayoongozwa na malengo lazima yasukumwe na kauli mbiu yenye mwelekeo wa umilele. Ufupisho wa kile ambacho Kristo anakifanya ndani ya maisha yetu kimejumuishwa katika kauli mbiu hii: “Wakati umetimia, na ufalme wa Mungu umekaribia; tubuni, na kuiamini Injili,” Mk 1:15. Kauli mbiu hii ya Yesu imeweka wazi muda maalum wa kuanza mradi huu wa umilele, kudumu kwa mradi huu kabla ya kufikia umilele, mapaswa ya mradi huu, na  kielelezo kinacho sadifu mradi huu.

Kwa ujumla maisha ya hapa duniani ni ya muda mfupi ukilinganisha na umilele. Hivyo kauli mbiu hii ya Yesu inatutaka kutambue ukweli huu wa uchache wa muda tungali hapa duniani. Ninapopata nafasi ya kuishi hata kwa dakika moja nielewa muda huo haujirudii tena na nishapunguza muda wa maandalizi kuelekea umilele. Kwa maana nyingine yanipasa kuishi nikijua nina muda na wakati huu tu katika maisha yangu.

Wakati kwa Mkristo umetimilizwa na Kristo mwenyewe kwa tendo la Neno kufanyika mwili na kukaa kwetu, Yoh 1.14. Mungu, ambaye alisema zamani na baba zetu katika manabii kwa sehemu nyingi na kwa njia nyingi, mwisho wa siku hizi amesema na sisi katika Mwana, aliyemweka kuwa mrithi wa yote, tena kwa yeye aliufanya ulimwengu,” Ebr 1:1-2. Hivyo Kristo ndiye dira ya maisha yako na yaliyo mafupi hapa duniani katika dhana nzima ya kujiandaa na umilele. Ufalme wa Mungu umekaribia kwa sababu Neno huyu, yaani, Emmanueli, ni Mungu pamoja nasi, Mt 1:23. Mungu ambaye hapo mwanzo alioneka yupo mbali sana na watu sasa kamwilishwa na kuwa sawa na sisi isipokuwa hakutenda dhambi, 1Pet 2:22.

Pamoja na ukweli kwamba sasa tupo karibu sana na Mungu kupitia mwanaye Yesu Kristo, hiyo haimaanishi wakovu ni bwerere! La hasha! Yatupasa kutubu na kuamini habari njema, yaani Injili. Toba yetu ni kuanza upya na Mungu kupitia mwanaye Mpenzi Yesu Kristo. Ni kuuvua utu wetu wa zamani na kuuvaa utu mpya kama asemavyo Paulo Mtume. Ikiwa mlimsikia mkafundishwa katika yeye, kama kweli ilivyo katika Yesu, mvue kwa habari ya mwenendo wa kwanza utu wa zamani, unaoharibika kwa kuzifuata tamaa zenye kudanganya; na mfanywe wapya katika roho ya nia zenu; mkavae utu mpya, ulioumbwa kwa namna ya Mungu katika haki na utakatifu wa kweli,” Efe 4:22-24. Habari njema iwe kweli habari njema kwako na wote wale waliokata tamaa katika maisha yao, wewe ukiwa mjumbe wa habari hiyo yenye matumaini. Kristo ndiye tumaini jipya kwetu sote katika safari yetu hii kuelekea maisha ya umilele.

Hivyo ishi yetu leo siyo tena ishi ile inayosukumwa na mitazamo ya watu, ikiwa ni pamoja na mila na desturi zetu zilizopotofu. Kuishi kwetu leo ndani na katika Kristo siyo kuwapendezesha wanadamu, bali Mungu mwenyewe, Gal 1:10. Tatizo hili tunaliona katika somo letu la kwanza Hana mke wa Halkana anakosa furaha na kuhuzunika kwa vile hakuwa na mtoto. Ni kweli kabisa kama mama ilimpasa kuwa na mtoto kadiri mitizamo, mila na desturi. Hata leo zipo ndoa nyingi hazina amani kwa vile tu hawakubahatika kupata watoto. Ndoa Takatifu haikamilishwi kwa kuwa na watoto. Watoto ni matunda ya Ndoa Takatifu, na hata bila watoto ndoa hiyo hubaki kuwa Takatifu. Kitu cha muhimu katika ndoa ni upendo wa dhati kati ya mume na mke na kusindikizana katika Utakatifu. Halkana anamkumbusha mkewe Hana msingi huu wa ndoa ambao wengi uingiwa upofu na kutokuuona. Elkana mumewe akamwambia, Hana, unalilia nini? Kwani huli chakula? Kwa nini moyo wako una huzuni? Je! Mimi si bora kwako kuliko watoto kumi?” Isam 1:8.

Vile vile ishi letu leo siyo tena ile kwamba ulimwengu huu ndiyo kikomo cha kila kitu na kutufanya kuwekeza hapa duniani. Yote tuyafanyayo, tena kwa ukamilifu wake, yawe ni moja ya njia ya kutufikisha katika umilele ambao ndio kikomo cha kila kitu. Tumeumbwa na Mungu tuishi milele kama Yeye alivyo wa milele. Ukitizama kwa makini chagua ya Yesu kwa wale Mitume wake utaona ukweli huu. Ni kama vile Yesu anataka kusema hivi, “najua kazi yako ndiyo kila kitu kwako, ila hili nikuambialo ni muhimu na lina umilele ndani yako.” Yesu hakudharau waliyokuwa wanayafanya kabla wale aliowachagua, bali aliwaonyesha lililomuhimu na lakudumu katika kufanya. Yesu akawaambia, Njoni mnifuate, nami nitawafanya kuwa wavuvi wa watu,” Mk 1:17. Pamoja na sintofahamu hii, Mitume na wanafunzi hawa wa Yesu wanaacha kazi zao na kumfuata Yesu. Mara wakaziacha nyavu zao, wakamfuata,” Mk 1:18. Nani kati yetu leo atakuwa tayari kuacha mkate wake, kazi yake nzuri na yenye mshahara ulio nona na kumfuata mtu tu asiyemjua vizuri?  Ni changamoto kubwa sana!

Ila ndugu yangu tuliyesafiri wote katika tafakari hii, kama unataka kuishi katika umilele, yakupasa kuiisikia sauti ya Mungu. Yote tuliyonayo hapa duniani licha ya umuhimu wake, hayana umilele. Tunaangaika sana kuvipata vitu hivyo tena kwa jasho na gharama kubwa, ila ukweli ni kwamba ipo siku tutaviacha na kwenda bila kitu. Kumbe tumia muda wako vizuri katika utume wako kwa sababu hilo litadumu milele hata baada ya maisha yako hapa duniani.

Tumsifu Yesu Kristo!


Msijiwekee hazina duniani, nondo na kutu viharibupo, na wevi huvunja na kuiba; bali jiwekeeni hazina mbinguni, kusikoharibika kitu kwa nondo wala kutu, wala wevi hawavunji wala hawaibi; kwa kuwa hazina yako ilipo, ndipo utakapokuwapo na moyo wako,” Mt 6:19-21

No hay comentarios:

Publicar un comentario