JUMATANO WIKI YA 1 YA MWAKA-C
13/1/2016
Somo: 1Sam 3:1-10, 19-20
Zab: 40:2, 5, 7-8a, 8b-9, 10
Injili: Mk 1:29-39
Nukuu:
“Basi Samweli alikuwa
hamjui Bwana bado, na neno la Bwana lilikuwa bado halijafunuliwa kwake,” 1Sam
3:7
“Bwana akamwita Samweli mara ya tatu. Naye akaondoka
akamwendea Eli, akasema, Mimi hapa; kwa maana uliniita. Ndipo Eli akatambua ya
kuwa Bwana ndiye aliyemwita yule mtoto,” 1Sam 3:8
“Kwa hivyo Eli akamwambia Samweli, Enenda, kalale; itakuwa,
akikuita, utasema, Nena, Bwana; kwa kuwa mtumishi wako anasikia. Basi Samweli
akaenda akalala mahali pake,” 1Sam 3:9
“Bwana akaja, akasimama, akaita vile vile kama kwanza,
Samweli! Samweli! Ndipo Samweli akasema, Nena, Bwana; kwa kuwa mtumishi wako
anasikia,” 1Sam 3:10
“Naye mkwewe Simoni, mamaye mkewe, alikuwa kitandani, hawezi
homa; na mara wakamwambia habari zake,” Mk 1:30
“Akamkaribia, akamwinua kwa kumshika mkono, homa ikamwacha,
akawatumikia,” Mk 1:31
“Akawaambia, Twendeni mahali pengine, mpaka vijiji vilivyo
karibu, nipate kuhubiri huko nako; maana kwa hiyo nalitokea,” Mk 1:38
TAFAKARI: “Samweli
alikuwa hamjui Bwana bado, na neno la Bwana lilikuwa bado halijafunuliwa
kwake.”
Wapendwa wana wa Mungu, pamoja na kwamba kumjua Mungu ni
hatua kama tulivyoona kwa Samweli, zipo njia mbili zinazoweza kutupeleka katika
uwepo wa Mungu na ufahamu wake. Njia ya kwanza ni ‘kukisia.’ Eli anakuwa msaada
kwa Samweli katika kutafsiri tendo lile la kusikia sauti ikimwita mara tatu. “Kwa hivyo Eli akamwambia Samweli, Enenda,
kalale; itakuwa, akikuita, utasema, Nena, Bwana; kwa kuwa mtumishi wako
anasikia,” 1Sam 3:9a. Namna
ya kuita kwake Mungu kulivyo kwa pekee, Eli moja kwa moja anakisia kwa namna
hiyo huyo atakuwa Mungu.
Kwa kiasi kikubwa kila siku ya maisha yetu tunakumbana na
matukia mbalimbali na mengine hatuelewi sawa sawa. Mungu anapenda tumtafute
wenyewe hadi tumpate. Tukimpata Mungu kwa kumtafuta si rahisi kuachana naye. Na
Mungu hupenda kukutana nasi katika matukio mbalimbali, na wakati mwingine
matukio hayo huwa ya huzuni na kukata tamaa. Mungu kwa kufanya hivyo siyo
kwamba haoni wala hatujui, la hasha! Mungu anatujua hata kabla ya kuzaliwa
kwetu. Hivyo uwepo wako leo ni kusudi kubwa sana la Mungu. Mungu anataka katika
mahangaiko hayo sasa umtafute ili ufanye kazi naye.
Kila tukio linalotokea katika maisha yako lichukulie kama
somo la kumfahamu Mungu zaidi na vizuri. Usikubali kamwe lawama ikawa ndiyo
salamu yako ya kwanza unapokabiliana na tatizo lolote lile. Salamu yako ya
kwanza muulize Mungu hivi: katika tukio hili wataka kunifundisha nini Ee Mungu
wangu? Kumbe jambo la kwanza yatupasa kupokea hali hiyo. Kwa msaada wa Eli,
Samweli anapokea hali ile kwanza. “Bwana akaja, akasimama, akaita vile vile kama kwanza,
Samweli! Samweli! Ndipo Samweli akasema, Nena, Bwana; kwa kuwa mtumishi wako
anasikia,” 1Sam 3:10.
Ndugu yangu, usipolipokea NENO hutoweza kulitafakari,
kulitafiti, kulikumbuka, na kulishirikisha kwa wengine kama moja ya utume wako.
Ni muhimu kuelewa ni Mungu tu anayetuita kwa sababu ilimpendeza kutuumba kwa
sura na mfano wake, Mwa 1:27. Kazi yangu na yako ni kuwasaidia wengine waelewe
sauti ile ya Mungu anamwita au kuwaita. Tusiwe wepesi wa kukatisha safari za
wito kwa wengine kwa vigezo ambavyo wakati mwingine ni ubinadamu wetu tena usio
na chembe ya umungu ndani yake.
Njia ya pili ya kutupeleka katika uwepo wa Mungu na ufahamu
wake ni ‘ufunuo.’ Kwa namna yoyote ile na kwa yeyote yule, Mungu huweza
kujifunua kwake. Kwa vile kila mmoja wetu yupo duniani hapa kwa kusudi maalum
kadiri ya mpango wa Mungu, ni Mungu huyo huyo ujifunua kwake kwa lengo la
kumshirikisha makuu yake. Tendo hili la UFUNUO ndilo lililoibeba historia nzima
ya wokovu wetu.
Wapendwa
wana wa Mungu, kuwepo pale Mungu alipo ni kuwa ndani na katika Kristo kwa
sababu ya kile akisemacho Mungu kuhusu mwanaye, na kile mwana akisemacho kuhusu
Mungu Baba. Siku ya Ubatizo wa Bwana tuliona kile Mungu alichokisema kuhusu
mwana wake. “Kisha likatokea wingu, likawatia uvuli; sauti ikatoka katika
lile wingu, Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, msikieni yeye,” Mk 9:7. Je, ni
nani unayemsikiliza? Kwa upande wa pili kile asemacho Mwana, yaani Yesu kuhusu
Baba yake tunaweza kusoma, Yoh 8:12-59. Katika mahusiano ya Mwana na Baba, Yesu
anasema nini kuhusu hukumu? “Nami nijapohukumu,
hukumu yangu ni kweli; kwa kuwa mimi si peke yangu, bali ni mimi na yeye
aliyenipeleka,” Yoh 8:16. Kumbe kujua pale Mungu alipo pamoja na ufahamu wake
ni kuwa na Kristo Yesu.
Ufunuo
huo wa Mungu wajionyesha moja kwa moja ndani na katika Kristo katika Injili ya
leo. Tunaona uponyaji wa Mama Mkwe wa Simoni Petro ulivyokuwa. “Naye mkwewe Simoni, mamaye
mkewe, alikuwa kitandani, hawezi homa; na mara wakamwambia habari zake. Akamkaribia, akamwinua kwa
kumshika mkono, homa ikamwacha, akawatumikia,” Mk 1:30-31. Je, ulipoguswa na
Mungu na kuponywa, ulikuwa tayari kutumika kama shukrani kwa Mungu? Huyu ndiye
Mungu aliye hai na atupaye uzima. Mungu huyu anayo mamlaka pia ya kuuchukua
uzima huo. “Bwana huua, naye hufanya kuwa hai; Hushusha hata kuzimu, tena
huleta juu. Bwana hufukarisha
mtu, naye hutajirisha; Hushusha chini, tena huinua juu,” 1Sam 2:6-7.
Pamoja na
ufunuo huo wa wazi wa Neno kufanyika mwili na kukaa kwetu, lengo kubwa sasa ni
sisi kumjua Mungu na kumwelekea yeye katika umilele. Pamoja na ishara zote
alizozifanya kwa kuwaponya watu wenye shida mbalimbali, Mk 1:34, Yesu
anawakumbusha wanafunzi wake, na kwa upande mwingine tukiwa wewe na mimi kile
alichokijia hapa duniani. Naye “Akawaambia, Twendeni mahali pengine, mpaka vijiji vilivyo
karibu, nipate kuhubiri huko nako; maana kwa hiyo nalitokea,” Mk 1:38. Kwa
ubatizo wako wewe ni mmisionari. Hivyo peleka habari njema ya wokovu ukianza
hapo ulipo.
Tumsifu
Yesu Kristo!
“Kwa hiyo ndugu, jitahidini zaidi kufanya imara kuitwa kwenu na
uteule wenu; maana mkitenda hayo hamtajikwaa kamwe,” 2Pet 1:10
No hay comentarios:
Publicar un comentario