domingo, 17 de enero de 2016

TAFAKARI: JUMATATU WIKI YA 2 YA MWAKA-C

JUMATATU WIKI YA 2 YA MWAKA-C

Somo: 1Sam 15:16-23
Zab: 50:8-9, 16bc-17, 21, 23
Injili: Mk 2:18-22
Nukuu:
Basi Samweli akasema, Ingawa ulikuwa mdogo machoni pako mwenyewe, je! Hukufanywa kuwa kichwa cha kabila za Israeli? Naye Bwana akakutia mafuta uwe mfalme wa Israeli,” 1Sam 15:17

Mbona, basi, hukuitii sauti ya Bwana, bali ukazirukia nyara ukafanya yaliyo maovu machoni pa Bwana?” 1Sam 15:19

Sauli akamwambia Samweli, Hakika mimi nimeitii sauti ya Bwana, nami nimemleta Agagi, mfalme wa Waamaleki, tena nimewaangamiza Waamaleki kabisa,” 1Sam 15:20 

Naye Samweli akasema, je! Bwana huzipenda sadaka za kuteketezwa na dhabihu Sawasawa na kuitii sauti ya Bwana? Angalia, kutii ni bora kuliko dhabihu, Na kusikia kuliko mafuta ya beberu,” 1 Sam 15:22 

Kwani kuasi ni kama dhambi ya uchawi, Na ukaidi ni kama ukafiri na vinyago; Kwa kuwa umelikataa neno la Bwana, Yeye naye amekukataa wewe usiwe mfalme,” 1Sam 15:23

Nao wanafunzi wake Yohana na Mafarisayo walikuwa wakifunga; basi walikuja, wakamwambia, Kwani wanafunzi wa Yohana na wanafunzi wa Mafarisayo hufunga, bali wanafunzi wako hawafungi?” Mk 2:18
Yesu akawaambia, Walioalikwa arusini wawezaje kufunga maadamu bwana-arusi yupo pamoja nao? Muda wote walipo na bwana-arusi pamoja nao hawawezi kufunga,” Mk 2:19

Hakuna mtu ashonaye kiraka cha nguo mpya katika vazi kuukuu; ikiwa ashona, kile kipya kilichotiwa huliharibu lile vazi kuukuu, na pale palipotatuka huzidi,” Mk 2:21 

Wala hakuna mtu atiaye divai mpya katika viriba vikuukuu; ikiwa atia, ile divai mpya itavipasua viriba vile, divai ikamwagika, vile viriba vikaharibika. Bali hutia divai mpya katika viriba vipya,” Mk 2:22 


TAFAKARI:Kutii ni bora kuliko dhabihu.”

Wapendwa wana wa Mungu, kutii ni kutambua kuwa kuna kitu zaidi ya kile ulicho ambacho kwa namna moja au nyingine kinaathiri uwepo wako hasi au chanya. Kutii hakuna gharama yoyote kama utatambua kile ulicho na kile kilicho zaidi ambacho kina uhusiano nawe katika kuwa, kutenda, kufikiri na kuamua. Kati ya mambo magumu kufanya binadamu ni kutii. Kutii kunamlazimu mtu wakati mwingine kwenda kinyumbe na ufahamu wake kiakili na kimantiki. Kutii wakati mwingine kutakulazimu kuachilia yake uyafahamuyo kiufasaha. Kutii ni kujisalimisha kuliko kwa hiari kwa kile ukifahamucho kwa undani. Kutii ni kuruhusu jambo lingine lifanyike hata kama lile ulifanyalo una uhakika nalo.

Mfalme Sauli anakosa utii mbele za Mungu kwanza kabisa kwa kutokutambua yeye kama Mfalme yupo pale si kwa sababu yake binafsi bali kwa kuchakuliwa na Mungu na kufanya kazi ya Mungu. Basi Samweli akasema, Ingawa ulikuwa mdogo machoni pako mwenyewe, je! Hukufanywa kuwa kichwa cha kabila za Israeli? Naye Bwana akakutia mafuta uwe mfalme wa Israeli,” 1Sam 15:17. Sauli ni Mfalme wa Israeli kwa mkono wa Mungu mwenyewe.

Ndani yetu Mungu katuwekea kwa namna ya pekee dhamiri yenye kutuongoza katika kuchagua lililo jema. Kwa nafasi uliyonayo katika jamii inakuruhusu na kukuzuia baadhi ya mambo kuyafanya na kutokuyafanya. Utii huja pale unapoweza kuizuia nafsi yako kufanya kile ambacho kwa nafasi na uwezo wako unaweza kukifanya. Kosa la Sauli ni kuruhusu kwa nafasi yake na cheo chake watu wafanye yale yaliyokatazwa kufanyika hata kama uhalalishwaji wake unawezwa kufanywa kutokana na mamlaka ya mtu aliyo nayo. Angalia utetezi wa Sauli katika hili: “Ila watu waliteka nyara, kondoo na ng'ombe walio wazuri, katika vitu vilivyowekwa wakfu, kusudi wavitoe dhabihu kwa Bwana, Mungu wako, huko Gilgali,” 1Sam 15:21.

Yapo mambo mengi ambayo tunaondolewa uhalali wake wa kuwa kile tulicho kwa sababu ya kutokutii. Mfano: Katiba ya nchi ni matokeo ya mapendekezo ya watu ya namna watakavyo kuongozwa, na kujiwajibishwa wenyewe pale wanaposhindwa kufanya yale waliyokubaliana. Tunapowachagua viongozi wetu, mfano Rais, tunategemea ailinde Katiba na awe mfano wa utii katiba hiyo na awe mfano wa kuigwa. Lakini kitu tunachokiona hadi sana na hasa katika Taifa letu la Tanzania, hawa tuliowapa dhamana ya kuilinda na kuitetea katiba ndio wanakuwa wa kwanza kuibadili na kuitafsiri ili kukidhi matakwa yao binafsi au vyama wanavyoviwakilisha. Kwa kufanya hivyo hata kama utaendelea kuwa mtawala kwa nguvu ya mtutu wa bunduki kuwaogopesha watu, hautakuwa halali kwa kile unachokiwakilisha mbele ya umma uliokuweka. “Bwana huzipenda sadaka za kuteketezwa na dhabihu Sawasawa na kuitii sauti ya Bwana? Angalia, kutii ni bora kuliko dhabihu, Na kusikia kuliko mafuta ya beberu,” 1 Sam 15:22. Mtakatifu Agustino aliwahi kusema hivi, “Vox populi, vox Dei,” akimaanisha “Sauti ya watu ni Sauti ya Mungu. Kuendelea kujinasibu kuwa kiongozi katika mazingira kama haya ya ujanja ujanja ni kukataliwa na watu na Mungu pia. Adhabu yake ni Kubwa.

Sauli anakutwa na tatizo hilo nililolisema hapo juu. Hivyo Mungu anamkataa licha ya kwamba anajinasibu kama Kiongozi.Kwani kuasi ni kama dhambi ya uchawi, Na ukaidi ni kama ukafiri na vinyago; Kwa kuwa umelikataa neno la Bwana, Yeye naye amekukataa wewe usiwe mfalme,” 1Sam 15:23. Je, hali ya kisiasa Zanzibar ya leo inatofauti na ule ufalme wa  Sauli? Tutafakari!

Injili ya leo tunaona wanafunzi wa Yesu wanashitumiwa kwa kutokufunga kadiri ya mila na desturi za kiyahudu. Yesu anawakumbusa wasome alama za nyakati. Wazo kuu hapa ni hili: nini hatma ya kile unachokifanya? Kama Yesu ndiye kila kitu, je wale walio karibu naye wafuate lipi? Ni kwa mtazamo huo Yesu anawajibu, “Walioalikwa arusini wawezaje kufunga maadamu bwana-arusi yupo pamoja nao? Muda wote walipo na bwana-arusi pamoja nao hawawezi kufunga,” Mk 2:19. Hivyo kile wasichokijua jibu lake ni Kristo. Wakati wa kuyafanya hayo utakuja kadiri na mila na desturi zetu utakuja. “Lakini siku zitakuja watakapoondolewa bwana-arusi, ndipo watakapofunga siku ile,” Mt 2:20.

Kristo ndiyo kila kitu kwetu. Yesu anataka tuanze yote naye. Yesu hataki habari za historia zetu, bali utayari wetu wa kuanza naye katika kweli na haki. Wala hakuna mtu atiaye divai mpya katika viriba vikuukuu; ikiwa atia, ile divai mpya itavipasua viriba vile, divai ikamwagika, vile viriba vikaharibika. Bali hutia divai mpya katika viriba vipya,” Mk 2:22. Je, upo tayari kuanza yote na Kristo? Basi kuwa wazi kuhusu wewe mwenyewe na jiachie mikoni mwa Kristo.

Tumsifu Yesu Kristo!


Nayaweza mambo yote katika yeye anitiaye nguvu,” Flp 4:13

No hay comentarios:

Publicar un comentario