sábado, 9 de enero de 2016

TAFAKARI: UBATIZO WA BWANA

SIKUKUU YA UBATIZO WA BWANA
10/1/2016
Somo I: Isa 42:1-4, 6-7
Zab: 29:1-2, 3-4, 3, 9-10
Somo II: Mdo 10:34-38
Injili: Lk 3:15-16, 21-22
Nukuu:
Tazama mtumishi wangu nimtegemezaye; mteule wangu, ambaye nafsi yangu imependezwa naye; nimetia roho yangu juu yake; naye atawatolea mataifa hukumu,” Isa 42:1 

Mwanzi uliopondeka hatauvunja, wala utambi utokao moshi hatauzima; atatokeza hukumu kwa kweli,” Isa 42:3

Mimi, Bwana, nimekuita katika haki, nami nitakushika mkono, na kukulinda, na kukutoa uwe agano la watu, na nuru ya mataifa,” Isa 42:6

kuyafunua macho ya vipofu, kuwatoa gerezani waliofungwa, kuwatoa wale walioketi gizani katika nyumba ya kufungwa,” Isa 42:7 

Petro akafumbua kinywa chake, akasema, Hakika natambua ya kuwa Mungu hana upendeleo; bali katika kila taifa mtu amchaye na kutenda haki hukubaliwa na yeye,” Mdo 10:34-35

habari za Yesu wa Nazareti, jinsi Mungu alivyomtia mafuta kwa Roho Mtakatifu na nguvu naye akazunguka huko na huko, akitenda kazi njema na kuponya wote walioonewa na Ibilisi; kwa maana Mungu alikuwa pamoja naye,” Mdo 10:38

Yohana alijibu akawaambia wote, Kweli mimi nawabatiza kwa maji; lakini yuaja mtu mwenye nguvu kuliko mimi, ambaye mimi sistahili kuilegeza gidamu ya viatu vyake; yeye atawabatiza kwa Roho Mtakatifu na kwa moto,” Lk 3:16

Ikawa, watu wote walipokwisha kubatizwa, na Yesu naye amebatizwa, naye anaomba, mbingu zilifunuka,” Lk 3:21

Roho Mtakatifu akashuka juu yake kwa mfano wa kiwiliwili, kama hua; sauti ikatoka mbinguni, Wewe ndiwe Mwanangu, mpendwa wangu; nimependezwa nawe,” Lk 3:22 

TAFAKARI:Wewe ndiwe Mwanangu, mpendwa wangu; nimependezwa nawe.”

Wapendwa wana wa Mungu, leo kwa furaha kubwa Mama Kanisa anaadhimisha Sikukuu ya Ubatizo wa Bwana. Swali ambalo hutujia hata kama hatutaki ni hili: Je, Yesu alihitaji kubatizwa? Jibu ni ndiyo na hapana! “Ndiyo” ya ubatizo wa Yesu imelenga katika “kielelezo,” “Mfano wa kufuata,” yaani kupitia mfano huo tunao uthibitisho pasipo shaka wa maneno haya Yesu, kwamba, “Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi,” Yoh 14:6. Mamlaka ya Maneno haya ya Yesu (Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima) yanawekwa wazi na nafsi ya tatu na ya kwanza ya Mungu mwenyewe pale Mbingu zilipofunguka, Roho Mtakatifu akashuka kama kiwiliwili, na sauti kutoka mbinguni ikasikika, “Wewe ndiwe Mwana wangu, mpendwa wangu; nimependezwa nawe,” Lk 3:22b.

Ubatizo aliokuwa anaufanya Yohane Mbatizaji ulikuwa ubatizo wa maji kama ishara ya toba ya kweli ikiwa ndiyo, maandalizi ya ubatizo wenyewe wa Roho Mtakatifu na Moto. Yohane Mbatizaji anaweka jambo hili wazi kwa kusema, “Kweli mimi nawabatiza kwa maji; lakini yuaja mtu mwenye nguvu kuliko mimi, ambaye mimi sistahili kuilegeza gidamu ya viatu vyake; yeye atawabatiza kwa Roho Mtakatifu na kwa moto,” Lk 3:16. Je, ubatizo wa Yohane Mbatizaji ulikuwa ni kupoteza muda? La hasha! Kwa neno “maandalizi,” linabeba dhana nzima ya uwepo wetu hapa duniani. Mahali hapa siyo sehemu ya kudumu, bali tunapita kuelekea umilele. Hivyo kuufikia umilele ambao sasa unawezekana ndani na katika Kristo, maandalizi ni muhimu ikiwa ni pamoja na kuishi katika hali ya neema. Huku ndiko kufanya toba ya kweli kama ilivyo ubatizo ule wa maji ambao ulikuwa ni kuwaandaa watu katika kweli na haki ambayo ukamilifu wake upo kwa Kristo mwenyewe. Lengo la toba ni ondoleo la dhambi. Hivyo, Yohana alitokea, akibatiza nyikani, na kuuhubiri ubatizo wa toba liletalo ondoleo la dhambi,” Mk 1:4

Wapendwa wana wa Mungu, ahadi za Mungu kwetu zinatufikia pale tunapofanya toba ya kweli. Bwana hakawii kuitimiza ahadi yake, kama wengine wanavyokudhani kukawia, bali huvumilia kwenu, maana hapendi mtu ye yote apotee, bali wote wafikilie toba,” 1Pet 3:9. Mungu leo ametimiza ahadi yake kwa uvumilivu wa watu wake kwa kazi iliyofanywa na Yohane Mbatizaji. Kristo Yesu ndiye kielezo halisi cha Ubatizo wa Roho Mtakafu na Moto. Hizi ndizo habari za Yesu wa Nazareti, jinsi Mungu alivyomtia mafuta kwa Roho Mtakatifu na nguvu naye akazunguka huko na huko, akitenda kazi njema na kuponya wote walioonewa na Ibilisi; kwa maana Mungu alikuwa pamoja naye,” Mdo 10:38. Wewe ndiwe Mwanangu, mpendwa wangu; nimependezwa nawe!

Tangu sasa neema na baraka zimefunguliwa kwa watu wote. Mlango huu umefunguliwa hata kwa wale walioonekana ni wapagani kwa njia ya maono ya Petro alipokuwa akisali na mbingu zikafunguka, na chombo kikashuka kama nguo kubwa, wakiwemo aina zote za wanyama wenye miguu minne, watambaao, na ndege wa angani, Mdo 10:11-12. Kadiri ya maono haya Petro alisita kupokea maagizo ya Mungu kwa sababu ndani yake walikuwepo wanyama wale waliokatazawa kuliwa nao ni najisi, Mdo 10:14. Pamoja na hayo, wanyama hawa hamtawala katika wale wenye kucheua, na katika wale walio na kwato; ngamia, kwa sababu yuacheua lakini hana kwato, yeye ni najisi kwenu. Na wibari, kwa sababu yeye hucheua lakini hana kwato, yeye ni najisi kwenu. Na sungura, kwa sababu hucheua, lakini hana kwato, yeye ni najisi kwenu. Na nguruwe, kwa sababu yeye anazo kwato, ni mwenye miguu iliyopasuka kati, lakini hacheui, yeye ni najisi kwenu. Msiile nyama yao, wala msiiguse mizoga yao; hao ni najisi kwenu,” Law 11:4-8.

Wapagani hawakuchangamana na Wayahudi, na mbaya kazaidi Wayahudi wale ambao kwa namna ya pekee ndio walikuwa Kanisa la Mwanzo. Hizi ni changamoto ambazo zitapelekea kuwepo kwa Mkutano/Mtaguso huko Yerusalemu, Mdo 15:1-41. Kuchangamana kwao ni najisi kama ilivyokuwa kula nyama za wanyama hawa au kugusa mizoga yake. Badala yake  “sauti ikamjia, kusema, Ondoka, Petro, uchinje ule. Sauti ikamjia mara ya pili, ikimwambia, Vilivyotakaswa na Mungu, usiviite wewe najisi,” Mdo 10: 13, 15. Neno “Ondoka uchinje ule,” linatupa uthibitisho wa kufunguliwa neema na baraka kwa watu wote wenye hofu ya Mungu. Tendo hili linathibitishwa na Petro mwenyewe huko Kaisaria kwa ujumbe uliotumwa kwake na  Kornelio akida, mtu mwenye haki, mchaji wa Mungu, aliye na sifa njema kwa taifa lote la Wayahudi, Mdo 10:22. Mtume Petro kwa kuona tendo hili kubwa likitokea hata kwa wapagani kushukiwa na Roho Mtakatifu, anatoa hitimisho la Imani na kusema, “Hakika natambua ya kuwa Mungu hana upendeleo; bali katika kila taifa mtu amchaye na kutenda haki hukubaliwa na yeye,” Mdo 10:34-35. Hivyo kumcha Mungu na kutenda haki ndicho kibali chakukubaliwa na Mungu. Kibali hiki ndicho kielelezo cha utakatifu wetu. Na utakatifu huu ndio cheo chetu mbele ya Mungu licha ya utofauti rangi zetu, familia zetu, koo zetu, makabila yetu, na utaifa wetu. Haya yote yaliyo ya kibinadamu bila utakatifu wa Mungu katika kumcha na kutenda haki hayana fadhila yoyote mbele za Muumba wetu.

Kwa maana hiyo, ubatizo wa Bwana leo ni kielelezo na mfano wa hayo yote niliyoyasema. Kwa maneno mengine Yesu kama Yesu hakuhitaji ubatizo huo katika maana ya ubatizo wa toba liletalo ondoleo la dhambi, Mk 1:4. Na huu ndio ule utabiri aliousema Nabii Isaya kwa mtumishi yule atakayepewa Mamlaka na Mungu juu ya watu wake waliomridhia. Tazama mtumishi wangu nimtegemezaye; mteule wangu, ambaye nafsi yangu imependezwa naye; nimetia roho yangu juu yake; naye atawatolea mataifa hukumu,” Isa 42:1. Mamlaka yake ni pamoja na kutoa hukumu ya haki na kweli. Mimi, Bwana, nimekuita katika haki, nami nitakushika mkono, na kukulinda, na kukutoa uwe agano la watu, na nuru ya mataifa,” Isa 42:6. Je, ujio wa Mjumbe huyu wa Mungu ni mabadiliko ya kila kitu ambacho kilikuwa hapa mwanzo? La hasha! Mwanzi uliopondeka hatauvunja, wala utambi utokao moshi hatauzima; atatokeza hukumu kwa kweli,” Isa 42:3.

Je, Mjumbe huyu wa Mungu atafanya nini basi kwa hali yetu ya kila siku? Kuhusu ukweli wa jambo hili, Yesu akiwa ndiye Mjumbe halisi wa Mungu, (Wewe ndiwe Mwanangu, mpendwa wangu; nimependezwa nawe) mwenyewe anasema hivi, Msidhani ya kuwa nalikuja kuitangua torati au manabii; la, sikuja kutangua, bali kutimiliza. Kwa maana, amin, nawaambia, Mpaka mbingu na nchi zitakapoondoka,yodi moja wala nukta moja ya torati haitaoondoka ,hata yote yatimie,” Mt 5:17-18. Ndugu yangu, amri za Mungu ni zile zile na mafundisho ya Kristo ni yale yale yanayotuongoza kumjua Mungu, kumpenda Mungu, kumtumikia Mungu, na Mwisho turudi kwake Mbinguni. Mimi na wewe yatupasa kuwa waaminifu kwa amri hizi na kuziishi ikiwa ni pamoja na mafundisho tunayopewa kila siku. Hii ndiyo maana ya kutimiliza torati. Wayahudi wakati wa Yesu hawakuwa waaminifu kuhusu Torati. Badala yake waliitafsi ili ikidhi mahitaji na malengo yao. Waliishi tafsiri hii-TALMUD, kama ukweli wa Mungu uliopotoshwa. Yesu anawarudisha kwa mizizi la sheria ya Mungu, yaani Torati itimizwe kama yalivyokuwa makusudi ya Mungu na siyo ya mwanadamu.

Kazi hii ya Yesu ni kuweka wazi yale yote yaliyo giza, na kuwaweka watu wote huru. Na haya ndiyo yaliyotabiriwa na Nabii Isaya juu wa Mtumishi huyu wa Mungu kwamba, kuyafunua macho ya vipofu, kuwatoa gerezani waliofungwa, kuwatoa wale walioketi gizani katika nyumba ya kufungwa,” Isa 42:7. Maneno haya ya Nabii Isaya yanarudiwa na Yesu mwenyewe alipoianza kazi yake rasmi ya kupambana na giza ili sote kutuweka huru. Naye Yesu anasema, Roho wa Bwana yu juu yangu, Kwa maana amenitia mafuta kuwahubiri maskini habari njema. Amenituma kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao, Na vipofu kupata kuona tena, Kuwaacha huru waliosetwa, Na kutangaza mwaka wa Bwana uliokubaliwa,” Lk 4:18-19. Ndugu yangu niliyesafiri nawe katika tafakari hii, leo tunapofanya Sikukuu ya Ubatizo wa Bwana, ni wakati wa kukumbuka maneno haya ya Yesu unapoutazama ubatizo wako wenyewe. Kwa ubatizo wako haya aliyoyasema Yesu yametimia ndani ya moyo wako. “Leo Maandiko haya yametimia masikioni mwenu,” Lk 4:21b. Ndugu yangu wauthamini ubatizo wako?

Marieta ni mwanafunzi wa dini ambaye mara baada ya mafundisho yake alibahatika kupata Sakramenti tatu kwa wakati mmoja, yaani, Sakramenti ya ubatizo, Kimpaimara/kuimarishwa, na Ekaristi Takatifu. Kwa Sakramenti ya ubatizo alipakwa Mafuta Matakatifu utosini na kifuani. Na kwa Sakramenti ya Kipaimara alipakwa mafuta Matakatifu ya Krisma kwenye paji la uso. Na baadaye alipokea Sakramenti ya Ekaristi Takatifu.

Baada ya tukio hili, Marieta hakuonekana tena Kanisani. Sakramenti hizi za mkupuo zilikuwa ndiyo tiketi ya ‘bye bye.’ Marieta alijichanganya sana na malimwengu na kwa waganga wa kienyeji ndiko kulikokuwa hija yake. Waganga hawa walimtengeneza kweli kweli. Alipewa chale utosini, paja la uso, kifuani na kiunoni kama mkanda wa Rombo mcheza filamu.

Lakini pamoja na kinga hii kama alivyoambiwa na magwiji hawa, Marieta hakuacha kuweweseka na kupandisha maruhani kila mara. Marafiki zake walimshauri awe anakwenda Kanisani kusali. Hata hivyo maruhani haya huwangusha chini na kugaagaa wakati ule wa kufukiza ubani na Mageuzo. Je, tatizo lipo wapi?

Ndugu yangu, wewe uliyebatizwa umeingia mkataba na Mungu na kuwa kiungo cha Kristo. Unapousaliti ubatizo wako kwa kwenda kwa waganga wa kienyeji, na kupigwa chale sehemu zile ulizopakwa Mafuta Matakatifu ya Krisma unausaliti ubatizo wako na kujiweka wakfu kwa shetani. Kwa tendo hili unakosa kinga kwani hata malaika mlinzi wako anaondoka kwa sababu mwili wako kama hekalu la Roho Mtakatatifu ni chafu, 1Kor 6:19. Hivyo utembeapo njiani mwili wako unakuwa kama mnara wa simu, yaani, “network ni full.” Pepo yeyote anayerandaranda lazima akuingie kwa sababu huna kinga tena. Haya ndiyo mateso ya wengi leo.

Ponya yako katika tatizo hili lazima ufanye ukiri kwa toba ya kweli, na kuziungama dhambi zako ili upate uponyaji ndani yako. Kiti cha huruma ya Mungu kipo muda wote na hasa kwa namna ya pekee mwaka huu wa huruma ya Mungu Kikanisa.

Tumsifu Yesu Kristo!

Basi tulizikwa pamoja naye kwa njia ya ubatizo katika mauti yake, kusudi kama Kristo alivyofufuka katika wafu kwa njia ya utukufu wa Baba, vivyo hivyo na sisi tuenende katika upya wa uzima,” Rum 6:4


No hay comentarios:

Publicar un comentario