ALHAMISI WIKI YA 1 YA MWAKA-C
14/1/2016
Somo: 1Sam 4:1-11
Zab: 44:10-11, 14-15, 24-25
Injili: Mk 1:40-45
Nukuu:
“Nao Wafilisti wakajipanga juu ya Israeli; na walipopigana,
Israeli wakapigwa mbele ya Wafilisti; wakauawa watu wa jeshi lao lililokuwa uwandani
wapata watu elfu nne,” ISam 4:2
“Hata watu walipofika kambini, wazee wa Israeli wakasema,
Mbona Bwana ametupiga leo mbele ya Wafilisti? Twende tukalilete sanduku la
agano la Bwana toka Shilo hata huku, lije kati yetu, na kutuokoa katika mikono
ya adui zetu,” 1 Sam 4:3
“Basi wakatuma watu kwenda Shilo, nao wakalileta toka huko
sanduku la agano la Bwana wa majeshi, akaaye juu ya makerubi; na Hofni na
Finehasi, wana wawili wa Eli, walikuwako huko pamoja na sanduku la agano la
Mungu,” 1Sam 4:4
“Na sanduku la agano la Bwana lilipoingia kambini, Israeli
wote wakapiga kelele kwa sauti kuu, hata nchi ikavuma,” 1Sam 4:5
“Ole wetu! Ni nani atakayetuokoa na mkono wa
miungu hawa walio hodari? Hawa ndio miungu waliowapiga Wamisri kwa mapigo ya
kila namna jangwani,” 1Sam 4:8
“Iweni hodari, na kufanya kiume enyi Wafilisti, msije mkawa
watumwa wa Waebrania, kama wao walivyokuwa watumwa wenu; fanyeni kiume,
mkapigane nao,” 1Sam 4:9
“Wafilisti wakapigana nao, Israeli wakapigwa, wakakimbia kila
mtu hemani kwake; wakauawa watu wengi sana; maana katika Israeli walianguka
watu thelathini elfu wenye kwenda vitani kwa miguu,” 1Sam 4:10
“Akaja kwake mtu mwenye ukoma, akamsihi na kumpigia magoti, na
kumwambia, Ukitaka, waweza kunitakasa,” Mk 1:40
“Naye akamhurumia, akanyosha mkono wake, akamgusa, akamwambia,
Nataka, takasika. Na mara ukoma wake ukamtoka, akatakasika,” Mk 1:41-42
“Akamkataza kwa nguvu, akamwondoa mara, akamwambia, Angalia,
usimwambie mtu neno lolote, ila enenda zako ukajionyeshe kwa kuhani, ukatoe alivyoamuru
Musa kwa kutakasika kwako, iwe ushuhuda kwao,” Mk 1:43-44
TAFAKARI: “Mungu
wetu si wakuchezewa na wala si wamajaribio. Mungu hutenda kadiri unavyojiachia
kwake bila kujibakiza.”
Wapendwa
wana wa Mungu, pamoja na uovu tulionao, hali hiyo isiwe kibali cha kuendelea
kufanya uovu tukijidanganya kuwa Mungu hayaoni matendo yetu. Mungu wetu ni
Huruma, Upendo, Msahama, Haki na Kweli. Kukaa kwake kimya pale tunapomkosea
kunathibitisha mambo makuu mawili: kwanza, kunathibisha ukweli wa sifa hizo
nilizozitaja kuhusu Mungu. Pili, Mungu hataki tuangamie bali tuongoke na
kumrudia. Mungu hutupa muda wa kutosha kwa ajili ya wongofu wetu. Bwana wa
Majeshi asema hivi, “Tena, mtu mwovu atakapoghairi, na kuuacha uovu wake
alioutenda, na kutenda yaliyo halali na haki, ataponya roho yake, nayo itakuwa
hai. Kwa sababu atafakari, na
kughairi, na kuyaacha makosa yake yote aliyoyatenda, hakika ataishi, hatakufa,”
Eze 18:27-28. Hivyo Mungu hafurahii hata kidogo kuangamia kwa mtu kutokana na
dhambi zake. Tatizo ni pale tunapocheza na Mungu.
Wana wa Israeli wanashindwa katika vita dhidi ya Wafilisti
kwa sababu wanacheza na Mungu. Wanatumia vibaya Upendo wa Mungu na Huruma yake.
Watoto wa Eli ambao kwa kiasi kikubwa ndiyo walikuwa daraja kati ya watu na
Mungu, hawakutenda sawa sawa na mapenzi ya Mungu. Walipatumia vibaya patakatifu
pa Mungu kwa tamaa zao za mwili na ibada haikufanyika kadiri ya uchaji wa
Mungu. Kushindwa kwa wana wa Israeli katika vita kunatokana na historia yao
mbaya, tena ikiongozwa na makuhani wao, yaani watoto wa Eli, Hofni na Finehasi.
“Basi Eli alikuwa mzee sana; naye alisikia habari za mambo yote
ambayo wanawe waliwatenda Waisraeli; na jinsi walivyolala na wanawake waliokuwa
wakitumika mlangoni pa hema ya kukutania. Akawaambia,
Mbona mnatenda mambo kama hayo? Maana nasikia habari za matendo yenu mabaya kwa
watu hawa wote,” 1Sam 2:22-23. Kwa mtindo huu wa maisha, kifo cha watoto wa Eli
kinatabiriwa. Mungu wetu si wakuchezewa hata kama yupo kimya pale tunapotenda
maovu. “Na hii ndiyo ishara itakayokuwa kwako, itakayowapata wana wako
wawili, Hofni na Finehasi; watakufa wote wawili katika siku moja,” 1Sam 2:34
Mungu
wetu siyo Edgar wala Athmani. Hasira ya Mungu ikiwaka hakuna wa kuizuia. Je,
Mungu wakulaumiwa? La Hasha! Adhabu ya Mungu kwetu ni matokeo ya kukaidi kwetu.
Uhusiano wetu na Mungu hupaswi kuwa ule wa matukio tu. Kama Mungu ni uhai kwetu
ni kwa maana hiyo hiyo hatuwezi kuishi bila Mungu. Wana wa Israeli wanamkumbuka
Mungu wakati wa shida ilhali hawakuwa waaminifu mbele zake. Mungu anaruhusu
wapigwe na hata kupoteza maisha ili liwe somo na fundisho kwao na kwa wengine
wenye hofu ya Mungu. “Nao Wafilisti wakajipanga juu ya Israeli; na walipopigana,
Israeli wakapigwa mbele ya Wafilisti; wakauawa watu wa jeshi lao lililokuwa
uwandani wapata watu elfu nne,” ISam 4:2. Wana wa Israeli wanachukua sanduku la Agano
kama kinga yao juu ya adui zao. “Hata watu walipofika kambini, wazee wa Israeli wakasema,
Mbona Bwana ametupiga leo mbele ya Wafilisti? Twende tukalilete sanduku la
agano la Bwana toka Shilo hata huku, lije kati yetu, na kutuokoa katika mikono
ya adui zetu,” 1 Sam 4:3. Tendo hili ni sawa na kufanya USHIRIKINA. Ushirikina ni
kutegemea nguvu fulani kutoka kitu fulani ambacho kwa kweli hakuna uhusiano
nawe kati ya uaminifu wako kimaisha na kitu hicho. “Basi wakatuma watu kwenda Shilo, nao wakalileta toka huko
sanduku la agano la Bwana wa majeshi, akaaye juu ya makerubi; na Hofni na
Finehasi, wana wawili wa Eli, walikuwako huko pamoja na sanduku la agano la
Mungu,” 1Sam 4:4
Pamoja na ushirikina huu, wakujifanya wanautambua uwepo wa
Mungu, wana wa Israeli walipigwa vibaya na kuuwawa. “Wafilisti wakapigana nao, Israeli wakapigwa, wakakimbia kila
mtu hemani kwake; wakauawa watu wengi sana; maana katika Israeli walianguka
watu thelathini elfu wenye kwenda vitani kwa miguu,” 1Sam 4:10. Mungu wetu hachezewi rafu wala hapewi rushwa.
Yanipasa kuishi kweli ndani yangu mwenyewe na kweli hiyo ijithihirishe kwa
Mungu kwa matendo yangu mema na yanayompendeza Mungu. Yesu mwenyewe anatukumbusha
kweli hii na kusema, “Si kila mtu
aniambiaye, Bwana, Bwana, atakayeingia katika ufalme wa mbinguni; bali ni yeye
afanyaye mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni,” Mt 7:21. Hivyo tuonje moyoni
tunayotamka mdomoni. Hakika tusipoyafanya mapenzi ya Mungu tujiandaye kwa
kupigwa mshangao kama walivyopingwa na mshangao wana wa Israeli. “Wafilisti wakapigana nao, Israeli wakapigwa, wakakimbia kila
mtu hemani kwake; wakauawa watu wengi sana; maana katika Israeli walianguka
watu thelathini elfu wenye kwenda vitani kwa miguu. Hilo sanduku la Mungu Likatwaliwa; na Hofni
na Finehasi, wale wana wawili wa Eli, wakauawa,” 1Sam 4:10-11. Na hapa ndipo
ule unabii ulipotimilika kwamba watoto wote wa Eli watakufa pamoja siku moja.
Wapendwa
wana wa Mungu, tumeona kwa undani kwamba Mungu wetu si wakuchezewa na wala si
wamajaribio. Sehemu yetu ya pili tumtazame Mungu wetu katika kutenda kwake.
Mungu wetu hutenda kadiri unavyojiachia kwake bila kujibakiza. Hivyo Injili
yetu ya leo inathibisha jambo hili. “Akaja kwake mtu mwenye ukoma, akamsihi na kumpigia magoti, na
kumwambia, Ukitaka, waweza kunitakasa,” Mk 1:40. ‘Ukitaka, waweza kunitakasa.’
Maneno haya yamebeba kauli ya kujiachia pasipo shaka. Ni kumruhusu Mungu atende
kadiri aonavyo na kumpendeza. Nasi waja wake tunajua wazi kabisa hawezi
kutupatia kile kisicho uzuri wake. “Ombeni, nanyi mtapewa; tafuteni, nanyi
mtaona; bisheni, nanyi mtafunguliwa; kwa
maana kila aombaye hupokea; naye atafutaye huona; naye abishaye atafunguliwa. Au kuna mtu yupi kwenu, ambaye, mwanawe akimwomba mkate,
atampa jiwe? Au akiomba samaki,
atampa nyoka? Basi ikiwa ninyi,
mlio waovu, mnajua kuwapa watoto wenu vipawa vyema, je! Si zaidi sana Baba yenu
aliye mbinguni atawapa mema wao wamwombao?” Mt 7:7-11
Kwa kuona nia ya mtu yule na kujiachia kwake pasipo
shaka, Yesu “akamhurumia, akanyosha mkono wake, akamgusa, akamwambia, Nataka,
takasika. Na mara ukoma wake ukamtoka,
akatakasika,” Mk 1:41-42. Ndugu yangu tuliyesafiri wote katika tafakari hii,
wamwamini Yesu wana wa Mungu? Baada ya uponyaji huu, Yesu anamwamuru mtu huyu
aende kwa makuhani kujitambulisha. Kujitambulisha kwa makuhani ilikuwa ni
wajibu wa lazima ili kupata kibali cha kushiriki tena maisha katika jamii. Wale
wote ambao walifikwa na ukoma walitengwa na jamii na kuishi sehemu yao wenyewe.
Makuhani ndio waliokuwa na uwezo kisheria wa kuwatenga hawa wenye ukoma na
kuwarudishia stahiki zao pale wanapopona ugongwa huu. “Akamkataza kwa nguvu, akamwondoa mara, akamwambia, Angalia, usimwambie mtu neno
lolote, ila enenda zako ukajionyeshe kwa kuhani, ukatoe alivyoamuru Musa kwa
kutakasika kwako, iwe ushuhuda kwao,” Mk 1:43-44. Yesu anathibitisha kweli yeye ni Masiha na Mfalme wa Upendo na
Amani, na Haki. Yesu anaturudishia heshima na kutambulika kwetu tena kati ya
watu. Hakika “wala yaliyo juu, wala yaliyo chini, wala kiumbe kinginecho chote
hakitaweza kututenga na upendo wa Mungu ulio katika Kristo Yesu Bwana wetu,”
Rum 8:39. AMINA!
Tumsifu
Yesu Kristo!
“Kwa kuwa Bwana ndiye mwenye haki, Apenda matendo ya haki,
Wanyofu wa moyo watamwona uso wake,” Zab 11:7
No hay comentarios:
Publicar un comentario