domingo, 3 de enero de 2016

TAFAKARI: SIKUKUU YA EPIFANIA, TOKEO LA BWANA

3/1/2016
Somo I: Isa 60:1-6
Zab: 71: 2, 7-8, 10-11, 12-13
Somo II: Efe 3:2-3a, 5-6
Injili: Mt 2:1-12
Nukuu:
Ondoka, uangaze; kwa kuwa nuru yako imekuja, Na utukufu wa Bwana umekuzukia,” Isa 60:1 

Na mataifa wataijilia nuru yako, Na wafalme kuujia mwanga wa kuzuka kwako,” Isa 60:3

"Ndipo utakapoona na kutiwa nuru, Na moyo wako utatetemeka na kukunjuka; Kwa kuwa wingi wa bahari utageuzwa kukujia, Utajiri wa mataifa utakuwasilia,” Isa 60:5 

ikiwa mmesikia habari ya uwakili wa neema ya Mungu niliyopewa kwa ajili yenu; ya kwamba kwa kufunuliwa nalijulishwa siri,” Efe 3:2-3a

Siri hiyo hawakujulishwa wanadamu katika vizazi vingine; kama walivyofunuliwa mitume wake watakatifu na manabii zamani hizi katika Roho; ya kwamba Mataifa ni warithi pamoja nasi wa urithi mmoja, na wa mwili mmoja, na washiriki pamoja nasi wa ahadi yake iliyo katika Kristo Yesu kwa njia ya Injili,” Efe 3:5-6

Yesu alipozaliwa katika Bethlehemu ya Uyahudi zamani za mfalme Herode, tazama, mamajusi wa mashariki walifika Yerusalemu, wakisema, Yuko wapi yeye aliyezaliwa mfalme wa Wayahudi? Kwa maana tuliiona nyota yake mashariki, nasi tumekuja kumsujudia,” Mt 2:1-2 

Basi mfalme Herode aliposikia hayo, alifadhaika, na Yerusalemu pia pamoja naye,” Mt 2:3
“Akawapeleka Bethlehemu, akasema, Shikeni njia, mkaulize sana mambo ya mtoto; na mkiisha kumwona, nileteeni habari, ili mimi nami niende nimsujudie,” Mt 2:8

Wakaingia nyumbani, wakamwona mtoto pamoja na Mariamu mamaye, wakaanguka wakamsujudia; nao walipokwisha kufungua hazina zao, wakamtolea tunu; dhahabu na uvumba na manemane,” Mt 2:11 

Nao wakiisha kuonywa na Mungu katika ndoto wasimrudie Herode, wakaenda zao kwao kwa njia nyingine,” Mt 2:12

TAFAKARI:Mataifa wataijilia nuru yako, Na wafalme kuujia mwanga wa kuzuka kwako.”

Wapendwa wana wa Mungu, leo Mama Kanisa anaadhimisha Dominika ya Epifania, yaani, Toleo la Bwana. Leo Mama Kanisa anatukumbusha mambo makuu matatu muhimu. Kwanza, ni ufunuo na udhihirisho wa Kristo katika ulimwengu. Ni ufunuo wa Kristo kwa Mataifa yote ya ulimwengu ambapo kunajidhihirisha kwa wataalamu wa nyota-Mamajusi wakiongozwa na nyota ile ya ajabu.Na mataifa wataijilia nuru yako, Na wafalme kuujia mwanga wa kuzuka kwako,” Isa 60:3. Wokovu wa Yesu Kristo unajionyesha kama nuru au mwanga  wa alfajiri unaoliondoa jiza na uvuli wa mauti ambao unautawala ulimwengu. Mungu mwenyewe ndiye pambazuko. Siku ya leo inadhihirika wazi machoni mwa wanadamu kwamba Kristo ndiye Mfalme wa ulimwengu wote, kwa ajili ya watu wote, na mmiliki wa utajiri wote. "Ndipo utakapoona na kutiwa nuru, Na moyo wako utatetemeka na kukunjuka; Kwa kuwa wingi wa bahari utageuzwa kukujia, Utajiri wa mataifa utakuwasilia,” Isa 60:5. Ukweli huu unajifunua kwa tunu zile alizopewa mtoto Yesu. Wakaingia nyumbani, wakamwona mtoto pamoja na Mariamu mamaye, wakaanguka wakamsujudia; nao walipokwisha kufungua hazina zao, wakamtolea tunu; dhahabu na uvumba na manemane,” Mt 2:11.

Toleo hili la Bwana la dhihirisha ukuhani wa Kristo kwa tunu ile ya uvumba. Huyu ndiye kwa huduma yake atavitakatifuza vyote katika ulimwengu huu na kuvikomboa. Tendo hili linakwenda sambamba na sadaka ile atakayo itoa pale Msalabani. Tendo hili la upendo mkubwa wa Mungu kwa wanadamu leo linajifunua kwa tunu hii ya manemane. Manemane yanatabiri kifo chake kama ilivyo taratibu za Wayahudi kuhifadhi Maiti na kuzika. Akaenda Nikodemo naye, (yule aliyemwendea usiku hapo kwanza), akaleta machanganyiko ya manemane na uudi, yapata ratli mia. Basi wakautwaa mwili wake Yesu, wakaufunga sanda ya kitani pamoja na yale manukato, kama ilivyo desturi ya Wayahudi katika kuzika,” Yoh 19:39-40. Mambo haya makuu matatu yanajifunua kwetu leo.

Pili, toleo hili la Bwana, Epifania, linatupa namna ya kuishi kama Wakristo-wafuasi wa Kristo. Tendo hili ya kufunuliwa na kudhihishwa kwa Kristo ulimwenguni pote kunatuondoa katika hali ile ya kuwa wakristo wa kidunia na kutufanya Wakristo wa ulimwengu-wamishionari. Leo tunafanywa Wakristo wa tabaka la ulimwengu wote na siyo Mkristo wa kidunia. Wakristo wa kidunia kadiri ya Rich Warren, humtazama Mungu kwanza kwa ajili ya kukidhi haja zao binafsi. Wanapenda kuhudhuria mikutano na semina za kujenga, lakini hutawakuta katika mkutano wa umisheni kwa sababu hawaupendelei. Maombi yao yanajali mahitaji yao binafsi, baraka, na furaha yao. Ni ile imani ya ‘mimi kwanza.’ Husukumwa mara zote na swali hili: Je, Mungu anawezaje kufanya maisha yangu kuwa na furaha? Wanapenda kumtumia Mungu kwa malengo yao badala ya wao kutumiwa kwa malengo yake.

Wapendwa wana wa Mungu, kinyume cha hapo, Wakristo wa tabaka la ulimwengu mzima wanajua waliokolewa ili watumike na kutayarishwa kwa ajili ya utume. Wako tayari kupokea jukumu la mtu binafsi na wanafurahia upendeleo huo wa kutumiwa na Mungu. Wakristo wa tabaka la ulimwengu wote ndio watu pekee walio hai kikamilifu katika sayari hii. Furaha yao, uhakika na hamasa yao vinaambukiza kwa sababu wanajua wanafanya tofauti. Wanaamka asubuhi wakitazamia Mungu kufanya kazi kuwapita katika njia mpya. Je, unataka kuwa Mkristo wa aina gani? Leo katika toleo la Bwana, Mungu anakualika kushiriki katika tendo kubwa kuliko yote, la aina yake na la muhimu sana katika historia-ufalme wake. Hivi ndivyo Yesu alivyowaambia wanafunzi wake kabla ya kapaa, “Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani. Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu; na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi; na tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote, hata ukamilifu wa dahari,” Mt 28:18-20. Tendo hili linamfanya Kristo kuendelea kudhihika ulimwenguni kote.

Tatu, toleo hili la Bwana leo linatukumbusha kwamba Uinjilishaji hapa duniani ni jambo la pekee. Yapo malengo matano ya Mungu kwa maisha yako hapa duniani. Mungu alikuumba ili uwe mshiriki katika jamii yake, kielelezo cha tabia yake, mtu anayetukuza utukufu wake, mtumishi wa neema yake, na mjumbe wa Habari zake Njema. Katika malengo haya matano, hii la tano linaweza tu kutendwa hapa duniani. Yale mengine manne utaendelea kuyafanya milele kwa namna fulani. Hivyo kutangaza Habari Njema ni muhimu sana; una muda mfupi tu wa kushirikisha wengine ujumbe wa maisha yako na kutimiza utume wako.

Ujumbe wa Mtume Paulo kwa watu wa mataifa anaonyesha mpango wa wokovu wa Mungu umejifunua wazi kwa Watakatifu, Mitume wake na Manabii. Hata hivyo watu hawa wa mataifa wameupokea wokovu wa Mungu kwa ufunuo wa Roho. Watu hawa wa Mataifa ni warithi pia wa ahadi hizi za Mungu. Katika mpango huu wa wokovu hakuna tena matabaka. Hii ndiyo siri kubwa inayoibuliwa leo kwa tendo hili la toleo la Bwana. Siri hiyo hawakujulishwa wanadamu katika vizazi vingine; kama walivyofunuliwa mitume wake watakatifu na manabii zamani hizi katika Roho; ya kwamba Mataifa ni warithi pamoja nasi wa urithi mmoja, na wa mwili mmoja, na washiriki pamoja nasi wa ahadi yake iliyo katika Kristo Yesu kwa njia ya Injili,” Efe 3:5-6. Sote tu huru ndani na katika Kristo. Hivyo tuna mwili mmoja tu wa Kristo, nalo ndilo Kanisa. Sote tu viungo vya mwili huo mmoja na Kanisa hilo moja yaani Kanisa la Kristo. Kwa utarajibu na mwono huu, sote tunashiriki fumbo la Kristo kwa Sakramenti ya Ubatizo. Kristo katika mtazamo huu ndiye mrithi wa kweli wa ahadi zile za Mungu. Basi ahadi zilinenwa kwa Ibrahimu na kwa mzao wake. Hasemi, Kwa wazao, kana kwamba ni wengi, bali kana kwamba ni mmoja, Kwa mzao wako, yaani, Kristo,” Gal 3:16

Yesu Kristo Mfalme na Masiha kwa mara ya kwanza anakutana na wana wa ulimwengu wote. Injili ya Matayo inatajirisha simulizi la toleo la Bwana kwa vielelezo vya Kibiblia-Maandiko Matakatifu. Unabii ule wa Nabii Mika unatimia, yaani; (nyota Yakobo, zawadi za dhahabu na uvumba). Kristo ndiye Mfalme Mpya wa Wayahudi, na Musa mpya, mwakilishi wa ulimwengu mzima. Tendo hili la toleo la Bwana ni tishio kwa falme nyingine la ulimwengu huu. Basi mfalme Herode aliposikia hayo, alifadhaika, na Yerusalemu pia pamoja naye,” Mt 2:3. Habari za ufalme huu mpya ni habari njema wa masikini na wenye hofu ya Mungu. Wale wote wasio na hofu ya Mungu huongozwa na mipango miovu ya shetani. Mungu hata hivyo uiweka mipango yao miovu wazi kwa ajili ya kuwanusuru wanyonge na waadilifu wake. Nao wakiisha kuonywa na Mungu katika ndoto wasimrudie Herode, wakaenda zao kwao kwa njia nyingine,” Mt 2:12. Huyu ndiye Mungu asiyeshindwa katika mipango yake kwa wapendwa wake. Na huyu ndiye tunayesujudia leo siku ya Epifania, toleo la Bwana.

Je, ungepata leo nafasi ya kumtolea Yesu tunu ungempa kitu gani? Mathias Makyadi kutoka Kongo alikuwa ni mmoja wa wanavisi kati ya wanovisi kumi wa shirika fulani la kimisionari. Kila wiki mmoja wa wanovisi hupewa muda wa saa moja kutafakari mbele ya Ekaristi Takatifu. Waweza kutumia muziki wa ala ukuongoze katika tafakuri yako au ukimya tulivu.

Tendo la kufanya tafakuri lilikuwa gumu sana kwa Mathias Makyadi. Hivyo ilipofika zamu yake ulikuwa mtihani mkubwa sana. Hata hivyo Mathias alimwambia Yesu wa Ekaristi hivi, “kutafakari kwa ukimya kadiri ya utaratibu uliozoeleka mimi siwezi. Hivyo naomba nikupe kile nilichonacho kama shukrani na upendo wangu kwako.” Mathias aliondoka na kwenda chumbani mwake akachukua redio kaseti yake na kuweka mziki wa kwao “ndombolo” na kucheza kwa nguvu zake sote, kwa kutumia akili yake yote, na moyo wake wote.

Mara aliingia Mlezi wake kwenye kile kikanisa  kwani kelele zele zilisikika kila mahali katika nyumba ile ya Unovisi. “Kwa nini unafanya kelele mahali hapa na kucheza mbele ya Yesu wa Ekaristi?” Mlezi wa wanavisi alisema kwa jazba na hasira. “Baba, hiki ndicho ninachoweza kumpa Yesu wa Ekaristi kilicho cha thamani kubwa na ninachoweza kumpa kwa moyo wangu wote,” Mathias amjibu Mlezi wake kwa upole. Baada ya kuyatafakari maneno yale ya Mathias, Mlezi wake aliondoka bila ya kusema neno.

Wapendwa wana wa Mungu, kila mmoja wetu anacho cha kumpa Yesu leo kama walivyofanya Mamajusi na alivyofanya Mathias. Lakini zaidi ya yote, mimi na wewe tunaweza kumpa dhambi zetu kwani ndiyo mali yetu halali. Tunapoutazama mwaka huu wa huruma ya Mungu, tutazame mali hii halali tuliyonayo. Kristo Mfalme, ni Huruma, Upendo, Msamaha, Haki, na Kweli. Zawadi hii ataibadilisha na kuwa nyeupe kama sufu. Haya, njoni, tusemezane, asema Bwana. Dhambi zenu zijapokuwa nyekundu sana, zitakuwa nyeupe kama theluji; zijapokuwa nyekundu kama bendera, zitakuwa kama sufu,” Isa 1:18

Tumsifu Yesu Kristo!


“Na majeshi yaliyo mbinguni wakamfuata, wamepanda farasi weupe na kuvikwa kitani nzuri, nyeupe, safi,” Ufu 19:14

No hay comentarios:

Publicar un comentario