JUMAPILI WIKI YA 3 YA MWAKA-C
Somo I: Neh 8:2-10
Zab: 18:8-10, 15
Somo II: 1Kor 12:12-30
Injili: Lk 1:1-4, 4:14-21
Nukuu:
“Ezra akakifunua kitabu machoni pa watu wote; (maana alikuwa
juu ya watu wote); na hapo alipokifungua, watu wote walisimama; Ezra akamhimidi Bwana, Mungu Mkuu. Nao
watu wote wakaitika, Amina, Amina, pamoja na kuinua mikono yao; kisha wakainama
vichwa vyao, wakamsujudu Bwana kifudifudi,” Neh 8:5-6
“Kisha akawaambia, Enendeni zenu, mle kilichonona, na kunywa
kilicho kitamu, tena mpelekeeni sehemu yeye asiyewekewa kitu; maana siku hii ni
takatifu kwa Bwana wetu; wala msihuzunike; kwa kuwa furaha ya Bwana ni nguvu
zenu,” Neh 8:10
“Maana kama vile mwili
ni mmoja, nao una viungo vingi, na viungo vyote vya mwili ule, navyo ni vingi,
ni mwili mmoja; vivyo hivyo na Kristo,” 1Kor 12:12
“Kwa maana katika Roho
mmoja sisi sote tulibatizwa kuwa mwili mmoja, kwamba tu Wayahudi, au kwamba tu
Wayunani; ikiwa tu watumwa au ikiwa tu huru; nasi sote tulinyweshwa Roho
mmoja,” 1Kor 12:13
“Kwa maana mwili si
kiungo kimoja, bali ni vingi,” 1Kor 12:14
“Basi ninyi mmekuwa
mwili wa Kristo, na viungo kila kimoja peke yake,” 1Kor 12:27
“Na Mungu ameweka
wengine katika Kanisa, wa kwanza mitume, wa pili manabii, wa tatu waalimu,
kisha miujiza, kisha karama za kuponya wagonjwa, na masaidiano, na maongozi, na
aina za lugha,” 1Kor 12:28
“Je! Wote ni mitume?
Wote ni manabii? Wote ni waalimu? Wote wanatenda miujiza? Wote wana karama za kuponya wagonjwa?
Wote wanena kwa lugha? Wote wafasiri?” 1Kor 12:29-30
“Roho wa Bwana yu juu
yangu, Kwa maana amenitia mafuta kuwahubiri maskini habari njema. Amenituma
kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao, Na vipofu kupata kuona tena, Kuwaacha
huru waliosetwa, Na kutangaza
mwaka wa Bwana uliokubaliwa,” Lk 1: 18-19
“Akaanza kuwaambia,
Leo maandiko haya yametimia masikioni mwenu,” Lk 1:21
TAFAKARI: “Leo maandiko haya
yametimia masikioni mwenu.”
Wapendwa wana wa Mungu, leo Mama Kanisa anaadhimisha
Dominika ya 3 ya Mwaka ‘C’wa Kanisa. Leo Mama Kanisa anatutaka tutafakari
kutimia kwa yale yaliyotabiriwa katika safari nzima ya wokovu wetu. Kristo Yesu
ndiye kilele cha yote na ndiye ufunuo wa kweli wa Mungu. Ni katika historia ya
wokovu wetu ambapo tunaona Mungu akifanya maagano mbalimbali na watu wake-taifa
teule la Israeli. Pamoja na kudondoka kwao mara kwa mara na kutoishika sheria
ya Bwana-Torati kiaminifu, Mungu hakuacha kufanya upya agano nao.
Somo letu la kwanza tunaona Mungu anafanya upya agano na
Waisraeli kupitia Torati kama msingi wa kuishi na kufuata yale apendayo Mungu. “Ezra akakifunua kitabu machoni pa watu wote;
(maana alikuwa juu ya watu wote); na hapo alipokifungua, watu wote walisimama; Ezra akamhimidi Bwana, Mungu Mkuu. Nao
watu wote wakaitika, Amina, Amina, pamoja na kuinua mikono yao; kisha wakainama
vichwa vyao, wakamsujudu Bwana kifudifudi,” Neh 8:5-6. Kwa utii na unyenyekevu
wa wana wa Israeli wanafanya agano jipya na kuanza upya na Mungu. Torati
ilikuwa ndiyo msingi wa kuwaunganisha na Mungu kwa kuzishika sheria zake kwa
uaminifu. Kwa kufanya hivyo, Ezra kuhani anawaahidia neema na baraka kutoka kwa
Mungu. “Enendeni zenu, mle kilichonona, na kunywa kilicho kitamu, tena
mpelekeeni sehemu yeye asiyewekewa kitu; maana siku hii ni takatifu kwa Bwana
wetu; wala msihuzunike; kwa kuwa furaha ya Bwana ni nguvu zenu,” Neh 8:10. Kielelezo na furaha yao ni Bwana mwenye nguvu.
Mungu ambaye ni huruma, upendo, haki, na mwingi wa rehema
aliendelea kujifunua kwa Manabii wake yale ambayo wakati ulipotimia aliyafanya.
Nabii Eliya alifunuliwa yale ambayo leo kwa namna ya pekee yanatendeka katika
sinagogi. “Roho ya Bwana MUNGU i juu yangu; kwa sababu Bwana amenitia
mafuta niwahubiri wanyenyekevu habari njema; amenituma ili kuwaganga
waliovunjika moyo, kuwatangazia mateka uhuru wao, na hao waliofungwa habari za
kufunguliwa kwao,” Isa 61:1. Haya yaliyosemwa na Nabii Isaya miaka mingi
iliyopita Yesu “anatuambia, Leo maandiko haya yametimia masikioni mwenu,” Lk. Ni
kweli pamoja na aliyoyatabiri Nabii Isaya, yote yametimia leo katika maani hii;
Masikini kuhubiriwa habari njema, na kutangaza mwaka wa Bwana uliokubaliwa.
Mwaka wa Bwana unawakilisha wakati na fursa tunayopewa tena kuona bila kipimo
Upendo wa Mungu, Huruma ya Mungu, na Msamaha wa Mungu. Kwa msisitizo Yesu
anasema, “Roho wa Bwana yu juu yangu, Kwa maana amenitia mafuta kuwahubiri
maskini habari njema. Amenituma kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao, Na
vipofu kupata kuona tena, Kuwaacha huru waliosetwa, Na kutangaza mwaka wa Bwana
uliokubaliwa,” Lk 1: 18-19.
Wapendwa wana wa Mungu,
pamoja na sheria ya Bwana, yaani Torati, leo kielelezo chetu kuufikia uzima wa
milele ni Kristo Yesu kwa wote walio na ufahamu juu yake (dhamira safi na hofu
ya Mungu), na kwa namna ya pekee wabatizwa wote. “Kwa maana katika Roho mmoja sisi sote tulibatizwa kuwa mwili
mmoja, kwamba tu Wayahudi, au kwamba tu Wayunani; ikiwa tu watumwa au ikiwa tu
huru; nasi sote tulinyweshwa Roho mmoja,” 1Kor
12:13. Ni katika ukweli huu kwamba wapo wengine kwa dhamiri zao safi na hofu
yao juu ya Mungu watapata wokovu.
Wapendwa
katika Kristo, Mungu wetu ni Mungu wa wanadamu wote licha ya tofauti zetu za
kiimani. Hakuna anayeishi katika ulimwengu huu kwa sababu yake mwenyewe. Kila
mmoja wetu anayo chapa ya Mungu ndani yake. Ulimwengu huu ukiwemo na vyote
vilivyomo ni Mali yake Mungu. “Au je! Mungu ni Mungu wa Wayahudi tu? Siye Mungu
wa Mataifa pia? Naam, ni Mungu wa Mataifa pia; kama kwa kweli Mungu ni mmoja,
atakayewahesabia haki wale waliotahiriwa katika imani, nao wale wasiotahiriwa
atawahesabia haki kwa njia ya imani iyo hiyo,” Rum 3:29-30. Ukweli ni kwamba kila
anayeongozwa na mwenye dhamiri hai na safi ataokolewa siku ya mwisho.
Mafundisho ya Kanisa hasa tunaposoma Katekisimu ya Kanisa
Katoliki, namba 847 inafundisha juu ya dhamiri hai na safi ambapo hata wale
wasiomjua Kristo ndiyo ponya yao. Ukweli huu pia umefafanuliwa vizuri katika
mafundisho ya Mtaguso wa Pili wa Vatikano, Konstitusio ya Kichungaji juu ya
Kanisa katika Ulimwengu wa leo, “Gaudium Et Spesteaches,” “Furaha na
Matumaini,” inaelezea ukweli huu kama ifuatavyo; “Jambo hilo haliwahusu wakristo tu bali pia
wanadamu wote wenye mapenzi mema, ambao neema ya Mungu hufanya kazi mioyoni
mwao, kwa namna isiyoonekana. Maana Kristo alikufa kwa ajili ya watu wote na wito halisi wa binadamu ndio mmoja,
ule wa kimungu. Kwa hiyo lazima tuwe na wazo kwamba Roho Mtakatifu anawajalia
watu wote uwezekano wa kushiriki fumbo la kipasaka, kwa jinsi anayoijua Mungu,”
(no. 22)
Somo letu ya pili Mtume Paulo anaongelea
vizuri sana kuhusu Kristo kama Kanisa nasi tukiwa viungo vyake. Ni kwa
Sakramenti ya ubatizo tunafanywa wana wa Mungu na warithi wa ufalme wake.
Lakini tunaishi na kupata uhai tukiunganika na Kristo kama viungo vya huo mwili
yaani Kanisa. “Maana kama vile mwili ni mmoja, nao una viungo vingi, na viungo
vyote vya mwili ule, navyo ni vingi, ni mwili mmoja; vivyo hivyo na Kristo,”
1Kor 12:12. Kanisa kwa mtazamo huu, ni mwili
wa Kristo, yaani wabatizwa wote, na Sakramenti ya wokovu wetu. Basi tukiwa
viungo vya Kristo vyenye kujenga mwili wa Kristo ambao ni Kanisa, kila kiungo
kina kazi yake na kwa kutimiza kazi yake ndiyo afya ya mwili mzima. “Kwa maana mwili si kiungo kimoja, bali ni vingi,” 1Kor 12:14. Hivyo kila mmoja wetu, yaani mbatizwa ana umuhimu
wake wa pekee kuujenga mwili huu, yaani Kanisa, na kufanya vizuri. “Basi ninyi mmekuwa mwili wa Kristo, na viungo kila kimoja peke
yake,” 1Kor 12:27. Umoja katika utofauti wetu ndio uzuri wa mwili huu wa Kristo
yaani Kanisa. Karama zetu mbalimbali ni kwa ajili ya Kanisa na kufaidiana.
Hivyo, “Mungu ameweka wengine katika Kanisa, wa kwanza mitume, wa pili
manabii, wa tatu waalimu, kisha miujiza, kisha karama za kuponya wagonjwa, na
masaidiano, na maongozi, na aina za lugha,” 1Kor 12:28. Utofauti huo katika huduma na karama ni kwa ajili
ya Kanisa zima la wana wa Mungu. Sote kwa pamoja twaufanya mwili huu, yaani
Kanisa kuwa hai.
Wapendwa katika Kristo, ni
vyema ukajua karama zako na huduma yako katika Kanisa. Si vizuri kupoteza muda
wako kwa kuishi maisha linganishi, yaani ya mfanano na mwingine, bila
kuvitambua vipaji vyako ndiyo njia bora ya kutumika katika mwili huu, yaani
Kanisa. Na kuvijua vipaji na karama zako ni kutokukata tamaa pale unaposhindwa
kufikia lengo lako kusudiwa maisha au huduma unayoitoa. Wote hatuwezi fanana. “Je! Wote ni mitume? Wote ni manabii? Wote ni waalimu? Wote
wanatenda miujiza? Wote wana
karama za kuponya wagonjwa? Wote wanena kwa lugha? Wote wafasiri?” 1Kor
12:29-30. HAPANA! Kila mmoja wetu anakarama yake ambayo Mungu anapenda uitumie
hiyo kuudhihirisha utukufu wake na furaha yake.
Alex
aliyetambulika kwa jina la Parandesi, mwanzoni hakuipokea hali yake na hasa
maumbile yake. Alex alikuwa na matege ya ajabu na kwa sababu hiyo alipewa jina
la utani Parandesi. Kwa upande mwingine Alex alipenda sana kucheza mpira licha
ya kukatishwa tamaa na marafiki zake.
Siku
mmoja mwalimu wake wa michezo alimwambia, “Alex wewe una kipaji cha mpira hivyo
usiwasikileze sana rafiki zake kile wasemacho kuhusu wewe. Jitahidi katika hilo
na utafika mbali.” Maneno haya yalimpa faraja kubwa sana Alex.
Leo Alex
ni mchezaji mzuri sana wa kimataifa. Ndugu yangu, kila mmoja kapewa kipaji
chake. Unachotakiwa kufanya ni kugundua uwezo huo. Tusikubali kuvunjwa moyo
pale tunapojitajidi na kupata mafanikio hata kama ni kidogo. Mwanzo wa kila
kitu huwa mgumu, na kwa maana hiyo unaimarishwa kwa kile utakacho kuwa baadaye.
Tumsifu Yesu Kristo!
“Nawapenda
wale wanipendao, Na wale wanitafutao kwa bidii wataniona,” Mit 8:17
No hay comentarios:
Publicar un comentario