IJUMAA WIKI YA 3 YA MWAKA-C
Somo: 2Sam 11:1-4a, 5-10a, 13-17
Zab: 51:3-6a, 6bcd-7, 10-11
Injili: Mk 4:26-34
Nukuu:
“Ikawa wakati wa jioni, Daudi akaondoka kitandani, akatembea
juu ya dari ya jumba la mfalme; na alipokuwa juu ya dari aliona mwanamke
anaoga; naye huyo mwanamke alikuwa mzuri sana, wa kupendeza macho,” 2Sam 11:2
“Naye Daudi akapeleka, akauliza habari za yule mwanamke. Mtu
mmoja akasema, Je! Huyu siye Bath-sheba, binti Eliamu, mkewe Uria, Mhiti? Basi Daudi akapeleka wajumbe, akamtwaa,”
2Sam 11:3-4
“Yule mwanamke akachukua mimba; basi akapeleka na kumwambia
Daudi, akasema, Ni mja-mzito,” 2Sam 11:5
“Ndipo Daudi akapeleka kwa Yoabu, akisema, Unipelekee Uria,
Mhiti. Naye Yoabu akampeleka Uria kwa Daudi,” 2Sam 11:6
“Lakini Uria akalala mlangoni pa nyumba ya mfalme, pamoja na
watumishi wote wa bwana wake, wala hakushuka nyumbani kwake,” 2Sam 11:9
“Akaandika katika waraka huo, kusema, Mwekeni Uria mbele ya
watu penye vita vikali, kisha ondokeni, mmwache, ili apigwe akafe,” 2Sam 11:15
“Watu wa mji wakatoka, wakapigana na Yoabu; na baadhi ya watu,
watumishi wa Daudi, wakaanguka; Uria Mhiti naye akafa,” 2Sam 11:17
“Akasema, Ufalme wa
Mungu, mfano wake ni kama mtu aliyemwaga mbegu juu ya nchi,” Mk 4:26
“Ni kama punje ya
haradali, ambayo ipandwapo katika nchi, ingawa ni ndogo kuliko mbegu zote
zilizo katika nchi, lakini
ikiisha kupandwa hukua, ikawa kubwa kuliko miti yote ya mboga, ikafanya matawi
makubwa; hata ndege wa angani waweza kukaa chini ya uvuli wake,” Mk 4:31-32
TAFAKARI: “Madhara ya kuficha
na kutokukiri kosa ni kujiangamiza zaidi katika uovu.”
Wapendwa
wana wa Mungu, hakuna kati yetu asiyekuwa na mapungufu yake. Mapungufu yako
yanathibitisha ubinadamu wako. Kuyatambua mapungufu yako ni hatua muhimu sana
kuelekea ukamilifu ambao ndio wito wa kila mmoja wetu. “Basi ninyi mtakuwa wakamilifu, kama Baba yenu
wa mbinguni alivyo mkamilifu,” Mt 5:48. Jambo la kushangaza ni kwamba kati yetu
wapo ambo hawapendi na hawayakubali mapungufu yao na kuchukua hatua kuelekea
ukamilifu. Badala yake huvaa vinyago ambavyo huwaharibu kabisa na kupoteza sura
yao halisi. Wengi kati yetu tunaisha maisha ya kuigiza ilhali kwa uhakika
tunasutwa na nafsi zetu.
Kuvutwa na kuwashwa kwa tamaa hasa za mwili ni jambo la
kawaida kwa binadamu yeyote. Tumeumbwa na hali hiyo ndani ya miili yetu. Hata
hivyo tatizo lipo hapa; pale ambapo tunapozifurahia hisia hizo na kukubali
kuendeshwa nazo. Ni katika hali hii tunazungumzia matendo ya mwili, ikimaanisha
nafsi kuegemea mwili na siyo roho. “Basi matendo ya mwili
ni dhahiri, ndiyo haya, uasherati, uchafu, ufisadi, ibada ya sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina,
faraka, uzushi, husuda, ulevi,
ulafi, na mambo yanayofanana na hayo, katika hayo nawaambia mapema, kama
nilivyokwisha kuwaambia, ya kwamba watu watendao mambo ya jinsi hiyo
hawataurithi ufalme wa Mungu,” Gal 5:19-21. Hakika kwa matendo haya hakuna
mbingu!
Mfalme
Daudi katika tembeatembea yake jioni katika hekalu lake anakutana na changamoto
ndani ya nafsi yake. “Ikawa wakati wa jioni, Daudi akaondoka kitandani, akatembea
juu ya dari ya jumba la mfalme; na alipokuwa juu ya dari aliona mwanamke
anaoga; naye huyo mwanamke alikuwa mzuri sana, wa kupendeza macho,” 2Sam 11:2.
Ndugu yangu, macho huweza kupendezwa na kitu chochote kile, ila sio kila kitu
kipendezacho macho yetu cha faa katika makuzi ya roho na mwili hasa pale
tunapojifurahisha nacho kwa kuwashwa tamaa za mwili pasipo kujizuia. Si vibaya
kuona uzuri na kuvutwa nao katika maana ya kuusifu uzuri wa uumbaji wa Mungu.
Mfalme Daudi hakuishia kuona tu na kumsifu Mungu kwa uumbaji wake, bali
alifanyia kazi tazamo lile. “Naye Daudi akapeleka, akauliza habari za yule mwanamke. Mtu
mmoja akasema, Je! Huyu siye Bath-sheba, binti Eliamu, mkewe Uria, Mhiti? Basi Daudi akapeleka wajumbe, akamtwaa,” 2Sam 11:3-4.
Kosa la kwanza la Daudi ni hili; hata baada ya kupata taarifa
kwamba mwanamke yule alikuwa Bath-sheba, binti Eliamu, mke wa Uria-ambaye ni
mmoja wa askari wake, hakuweza kuishinda tamaa yake. Bila shaka Daudi kama
mfalme alikuwa na fursa ya kuwa na wanawake wote ambao hawakuwa wameolewa.
Mamlaka yake na uwezo wake uliruhusu uwezekano huo. Hata hivyo anatimiza hamu
na tamaa ya mwili wake kwa mke wa mjakazi wake Uria. Kila tendo ufanyalo katika
maisha yako ndugu yangu linatokeo lake, liwe zuri au baya. Na hakuna kilicho
siri chini ya jua hata kama utakuwa mwenyewe au wawili katika jambo hilo. Mtu
wa pili ukiwa mwenyewe ni Mungu. Na mtu wa tatu mkiwa wawili ni Mungu pia.
Nafasi ya Mungu ni kama kivuli unachotemba nacho, au mnachotembea nacho. Ndivyo
ilivyokuwa kwa Daudi. Matokea ya tendo lile la uzinifu la Daudi, ilikuwa ni
mimba. “Yule mwanamke akachukua mimba; basi akapeleka
na kumwambia Daudi, akasema, Ni mja-mzito,” 2Sam 11:5. Tokeo hili la uzinifu
linakuwa shitusho la kile alichokifanya. Mfalme Daudi hakuona uovu wake hadi
katika tokeo hili la mimba.
Salama ya Mfalme Daudi hadi hatua hii ilikuwa kukiri kosa
lake na kuanza upya katika upya na Mungu ambaye ndiye shahidi asiyefichwa
chochote. Badala yake, Daudi anautazama ufalme wake, na nafasi yake, hivyo
anaficha kosa lake kwa kufanya kosa lingine ambalo ni kubwa zaidi. Daudi
anatoka kwenye uzinifu na kuelekea umauti. Hivi ndivyo tufanyavyo pale
tunapotaka kula “keki na kuishikilia wakati huo huo.” “Ndipo Daudi akapeleka kwa Yoabu, akisema, Unipelekee Uria,
Mhiti. Naye Yoabu akampeleka Uria kwa Daudi,” 2Sam 11:6. Lengo la kuitwa Uria
nyumbani na Daudi ni kutaka kudanganya kuhusu mimba ile. Alijua Uria akilala na
mke wake ni rahisi kuhalalisha kosa lake. Je, haya yana tofauti na yatendekayo
katika familia zetu? Anayemjua baba wa mtoto ni mama. Hivyo akina baba wengi
katika familia zetu leo wamekuwa wakiuziwa mbuzi kwenye gunia. Kwa kweli
inasikitisha sana!
Uria akijua vigezo na masharti ya kazi yake hasa nyakati za
vita, haikuwa busara kulala na mke wake. Uria ni mtiifu kwa viapo vya kazi yake
kama askari. Haikuruhusiwa askari kulala na mke wake nyakati za vita. Hivyo,
“Uria akalala mlangoni pa nyumba ya mfalme, pamoja na watumishi wote wa bwana
wake, wala hakushuka nyumbani kwake,” 2Sam 11:9. Mfalme alifanya mbinu zote
hata kumlewesha ili Uria ajichanganye na kulala na mke wake ila Uria alikuwa
dhabiti katika viapo vyake kama askari.
Baada ya zoezi kugonga ukuta, Mfalme anabuni mbinu nyingine.
Daudi anamrudisha Uria vitani na kutoa maelekezo kwa waraka kwa Yoabu kiongozi
wa vita na askari wa vita, “akaandika katika waraka huo, kusema, Mwekeni Uria mbele ya
watu penye vita vikali, kisha ondokeni, mmwache, ili apigwe akafe,” 2Sam 11:15.
Hapa tunaona tamaa ya Mfalme Daudi inazaa mauti. Tuelewe wazi kwamba “kila mmoja hujaribiwa na tamaa yake mwenyewe huku akivutwa na
kudanganywa. Halafu ile tamaa ikiisha kuchukua mimba huzaa dhambi, na ile
dhambi ikiisha kukomaa huzaa mauti,” Yok 1:14-15. Kweli Uria asiyejua hili wala
lile anawekwa mstari wa mbele na kupoteza maisha yake. “Watu wa mji wakatoka, wakapigana na Yoabu; na
baadhi ya watu, watumishi wa Daudi, wakaanguka; Uria Mhiti naye akafa,” 2Sam
11:17. Kwa tendo hili Daudi anapata amani ya muda mfupi tu. Daudi anaendelea
kuteswa na dhamiri yake mbaya. Mfalme Daudi kuanzia sana anaishi katika hatia.
Wapendwa katika Kristo, hakuna shaka kabisa kati yetu wapo
ambao maisha yao wanaongozwa na hatia. Watu hawa hutumia muda
wa maisha yao yote wakiepuka lawama na kuficha aibu. Watu wanaoongozwa na hatia
wanaonewa sana na kumbukumbu. Wanaruhusu mambo yaliyopita kutawala mambo yao ya
usoni.Wanajiadhibu bila kujua kwa kuharibu mafanikio yao. Kaini alipotenda
dhambi, hatia yake ilimtenga na Mungu, na Mungu akasema, "utakapoilima
ardhi haitakupa mazao yake; utakuwa mtoro na mtu asiye na kikao duniani,"
Mwa 4:12. Hali hii inawaeleza jinsi watu wengi walivyo siku hizi-wanatangatanga
katika maisha bila lengo.
Ndugu yangu, sisi ni
matokeo ya muda wetu uliopita lakini hatupaswi kuwa wafungwa wa muda huo.
Kusudi la Mungu halifungwi na muda wako uliopita. Ona! Alimbadilisha muuaji
Musa na kuwa kiongozi mzuri; akambadilisha Gidioni aliyekuwa mwoga akawa shujaa
na hodari; anaweza kufanya mambo ya ajabu na maisha yako yaliyobaki. Tazama pia
maisha ya Mt. Augustino wa Hippo kabla na baada ya kuongoka kwake.
Mungu ni mtaalam wa
kutupa mawazo mapya. "Heri aliyesamehewa dhambi, na kusitiriwa makosa
yake," Zab 32:1. Kwa maana nyingine twaweza kusema, "wana furaha
kubwa wale waliosamehewa hatia zao. Na wana amani wale waliotubu dhambi zao na
Mungu amefuta mashtaka yao."
Ndugu yangu unayesafiri nami katika tafakari hii, toba ya
kweli kwa dhambi zako ndiyo njia pekee ya kuishi katika amani ya kweli. Bila
kufanya toba ya kweli mbingu ni ndoto kuifikia. Yesu leo anatupa aina mbili za
mfano wa Ufalme wa Mungu. “Akasema, Ufalme wa Mungu, mfano wake ni kama mtu aliyemwaga
mbegu juu ya nchi,” Mk 4:26. Maana yake, anayezikuza mbegu hizo na kuwa kile
kilichokusudiwa na Mungu mwenyewe. Na katika makuzi haya yaani maisha yako kila
siku ni wakati wa wewe kuwa kile Mungu alichokusudia uwe. Hivyo ni wazi Mungu
anapenda tuwe wanadamu kama alivyotuumba kwa sura na mfano wake. Tunapojaribu
kuwa kitu kingine ni chukizo kwa Mungu na hapo tunakuwa wabaya kuliko hata
shetani.
Mfano wa pili wa Ufalme wa Mungu ni huu; “Ni kama punje ya haradali, ambayo ipandwapo katika nchi, ingawa
ni ndogo kuliko mbegu zote zilizo katika nchi, lakini ikiisha kupandwa
hukua, ikawa kubwa kuliko miti yote ya mboga, ikafanya matawi makubwa; hata
ndege wa angani waweza kukaa chini ya uvuli wake,” Mk 4:31-32. Hapa
tunakumbushwa kwamba hakuna kisicho na umaana mbele ya Mungu katika mwonekano
wake, iwe ukubwa au udogo. Vyote vinaudhihirisha Utukufu na Uzuri wa Mungu, na
kwayo kwa kuwa kile kilicho ufikia ukamilifu wake ambao ndio kusudio la kuumbwa
kwake. Hivyo ndugu yangu jipokee ulivyo na yakamilishe yaliyo ndani yako kadiri
ya mpango wa Mungu katika ukamilifu wake.
Tumsifu
Yesu Kristo!
“Mikono yako ilinifanya ikanitengeneza, Unifahamishe
nikajifunze maagizo yako,” Zab 119
No hay comentarios:
Publicar un comentario