viernes, 15 de enero de 2016

TAFAKARI: JUMAPILI YA 2 YA MWAKA-C

JUMAPILI WIKI YA 2 YA MWAKA-C
17/1/2016
Somo I: Isa 62:1-5
Zab: 96: 1-3, 7-8, 9-10
Somo II: 1Kor 12:4-11
Injili: Yoh 2:1-12
Nukuu:
Kwa ajili ya Sayuni sitanyamaza, na kwa ajili ya Yerusalemu sitatulia, hata haki yake itakapotokea kama mwangaza, na wokovu wake kama taa iwakayo,” Isa 62:1 

 “Basi pana tofauti za karama; bali Roho ni yeye yule,” 1Kor 12:4 

Lakini kila mmoja hupewa ufunuo wa Roho kwa kufaidiana,” 1Kor 12:7 

lakini kazi hizi zote huzitenda Roho huyo mmoja, yeye yule, akimgawia kila mtu peke yake kama apendavyo yeye,” 1Kor 12:11 

Yesu naye alikuwa amealikwa arusini pamoja na wanafunzi wake,” Yoh 2:2 

Hata divai ilipowatindikia, mamaye Yesu akamwambia, Hawana divai,” Yoh 2:3 

Yesu akamwambia, Mama, tuna nini mimi nawe? Saa yangu haijawadia,” Yoh 2:4

Mamaye akawaambia watumishi, Lo lote atakalowaambia, fanyeni,” Yoh 2:5 

Basi kulikuwako huko mabalasi sita ya mawe, nayo yamewekwa huko kwa desturi ya Wayahudi ya kutawadha, kila moja lapata kadiri ya nzio mbili tatu,” Yoh 2:6 

Yesu akawaambia, Jalizeni mabalasi maji. Nao wakayajaliza hata juu,” Yoh 2:7

Naye mkuu wa meza alipoyaonja yale maji yaliyopata kuwa divai, (wala asijue ilikotoka, lakini watumishi walijua, wale walioyateka yale maji), yule mkuu wa meza alimwita bwana arusi, akamwambia, Kila mtu kwanza huandaa divai iliyo njema; hata watu wakiisha kunywa sana ndipo huleta iliyo dhaifu; wewe umeiweka divai iliyo njema hata sasa,” Yoh 2:9

TAFAKARI:Mama, tuna nini mimi nawe? Saa yangu haijawadia.”

Wapendwa wana wa Taifa la Mungu, leo Mama Kanisa anaadhimisha Dominika ya 2 ya mwaka ‘C’ wa Kanisa. Leo kwa namna ya pekee Mama Kanisa anatualika kutafakari kwa undani Upendo na Huruma ya Mungu kupitia Mwanaye Mpenzi Yesu Kristo. Pia ni kwa Upendo na Huruma hii ya Mungu inaakisi kilele chake, yaani, sadaka ya Kristo pale Msalabani. Kuuthamini na kuuishi upendo na huruma hii ya Mungu, yanipasa mimi na wewe kuijua “SHAPE” au “KAMOUHUMA” yako. SHAPE ni ufupisho wa maneno haya:- S, ‘Spiritual gifts’-Karama za kiroho ulizo nazo, H, ‘Heart-Moyo, ujue moyo wako, A, ‘Abilities’-Uwezo, jua uwezo wako, P, ‘Personality’-Hulka, jua nafsi na mapungufu yako, E, ‘Experience’-Mang’amuzi, yatumie vyema mang’amuzi yako uliyoyapata katika maisha. Kama ilivyo ‘mwana wa Adamu asivyokuja kutumikiwa, bali kutumika, na kutoa nafsi yake iwe fidia ya wengi, Mt 20:28, nasi kwa kujua ‘SHAPE au KOMOUHUMA’ yetu tutumika kama yeye alivyotumika kwa ajili yetu.

Kwa kujua SHAPE au KAMOUHUMA yako, Mungu huzimimina baraka zake zisizo na kipimo kwako kwa sababu Mungu kamwe habariki pasipo na kitu wala pasipo na juhudi njema za Mtu husika. Leo Mama yake Yesu, Yesu mwenyewe, na wanafunzi wake wanaalikwa kwenye Harusi huko Kana. Wakiwa katikati ya shamrashamra za Harusi ile divai inawaishia. Mama Bikira Maria anakwenda moja kwa moja kwa Yesu na kumwambia hawana divai, Yoh 2:3. Kwa nini Bikira Maria anakwenda kwa Yesu? Mama Bikira Maria anakwenda kwa mwanaye kwa sababu ya ‘mang’amuzi’ aliyonayo juu ya mtoto wake. Bikira Maria anajua ‘uwezo’ wa mtoto wake. Pamoja na ukweli huu, Yesu akamwambia, Mama, tuna nini mimi nawe? Saa yangu haijawadia,” Yoh 2:4. Maneno haya “Mama, tuna nini mimi na nawe,” ni maneno mazito sana na yenye kubeba ujumbe mzito.

Yesu anataka Mama yake na wanafunzi wake waelewe kwamba kwa tukio lile wao ni waalikwa tu kwanye harusi au karamu ile. Tendo hili linawakumbusha Mama Bikira Maria na wanafunzi wake “uwezo” na hali waliyonayo kutokana na ubinadamu wao. Kwa uwezo wao kama wanadamu wanaweza kufanya tu yaliyo ndani ya uwezo huo wa kibinadamu. Nasi kwa namna ya pekee, Yesu anatukumbusha uwezo na ubinadamu wetu. Tuwapo hapa duniani sote ni waalikwa na kwa zawadi ya uhai ni kama harusi au karamu ambayo kwa namna ya kuishi lolote laweza kutokea katika safari yetu hii. Pamoja na ukweli huu ambao mimi na wewe yatupasa kuufahamu, Yesu anaenda mbele zaidi na kusema, “Saa yangu haijawadia.” Maneno haya yanaakisi utimilifu wa kile alichokijia hapa duniani. Ukweli huu utatupeleka kwenye utimifu wa upendo na huruma ya Mungu pale Msalabani ambapo kwenye mti ule wa msalaba ndipo utakapotundikwa wokovu wetu.

Baada ya maneno hayo machache na mazito ya Yesu, Mama Bikira Maria hajibizani na Yesu kwa sababu ndani ya “Moyo” wake Mama Bikira anayajua mang’amuzi juu ya mtoto wake, na uwezo wake. Bikira Maria akijua ujumbe ushafika kwa mwanaye-“Message send and delivered,” na akijua hawezi kumwangusha, Maria Bikira anakwenda moja kwa moja kwa watumishi wa ile harusi na kuwaambia, “Lo lote atakalowaambia, fanyeni,” Yoh 2:5. Mama Bikira Maria hapa anatukumbusha uwezo wa Mwanaye na hakika hatupaswi kuwa na shaka. Yeye kama Mama anamfahamu vizuri mtoto wake kwani ameshiriki kwa namna ya pekee kabisa katika makuzi yake. Tunapotindikiwa katika maisha yetu, tukumbuke ujumbe huu wa Bikira Maria kwa wale watumishi wa Kana, “lo lote atakalowaambia, fanyeni.” Yesu anatuambia mambo sita ya muhimu:-

-Mimi ndimi chakula cha uzima; yeye ajaye kwangu hataona njaa kabisa, naye aniaminiye hataona kiu kamwe,” Yoh 6:35 

-Aniaminiye mimi, kama vile maandiko yalivyonena, mito ya maji yaliyo hai itatoka ndani yake,” Yoh 7:38

-“Mimi ndimi huo ufufuo, na uzima. Yeye aniaminiye mimi, ajapokufa, atakuwa anaishi;  naye kila aishiye na kuniamini hatakufa kabisa hata milele. Je! Unayasadiki hayo?” Yoh 11:25-26 

-Naye Yesu akapaza sauti, akasema, Yeye aniaminiye mimi, haniamini mimi bali yeye aliyenipeleka,” Yoh 12:44

-Mimi nimekuja ili niwe nuru ya ulimwengu, ili kila mtu aniaminiye mimi asikae gizani,” Yoh 12:46

-Amin, amin, nawaambieni, Yeye aniaminiye mimi, kazi nizifanyazo mimi, yeye naye atazifanya; naam, na kubwa kuliko hizo atafanya, kwa kuwa mimi naenda kwa Baba,” Yoh 14:12

Wapendwa wana wa Mungu, haya aliyoyasema Yesu ndiyo anayotukumbusha Mama Bikira Maria tuyafanye, katika maana ya kumwamini pasipo shaka mwanaye Mpendwa Yesu Kristo. Kabla ya kufanya kile Yesu atakachokisema, tunapewa hali halisi ya mazingira yale ya harusi ya Kana ikiwa ni pamoja na mila na desturi zao. Basi kulikuwako huko mabalasi sita ya mawe, nayo yamewekwa huko kwa desturi ya Wayahudi ya kutawadha, kila moja lapata kadiri ya nzio mbili tatu,” Yoh 2:6.  Mungu kupitia Mwanaye Mpenzi Yesu Kristo hutenda kadiri ya hali na mazingira yetu. Mtakatifu Thomas wa Aquina anasema hivi, “neema hufanya kazi katika uhalisi wa kitu.”

Wapendwa katika Kristo, “Mabalasi sita ya mawe,” yanatukumbusha umuhimu na tafsiri ya namba kadiri ya mila na desturi ya Wayahudi. Namba sita inawakilisha udhaifu, isiyo kamili au kutokukamilika, na isiyotosha. Kwa upande mwingine, namba kama 7, 14, na 40, huwakilisha ukamilifu, utoshelevu, na yakutosha.

Fundisho la kwanza hapa ni kwamba licha la udhaifu ule na kutokutosheleka kule kutokana na hali na ubinadamu wetu, kwa Upendo na Huruma aliokuwa nao Mungu,  Yesu anafanya kitu licha ya kwamba saa yake bado, yaani ukamilifu wa sadaka yake pale msalabani. Naye  Yesu akawaambia, Jalizeni mabalasi maji. Nao wakayajaliza hata juu,” Yoh 2:7. Tunapomwelekea Mungu kwa unyenyekevu licha ya mapungufu yetu kibinadamu, hawezi kukaa kimya. Kwa ajili ya Sayuni sitanyamaza, na kwa ajili ya Yerusalemu sitatulia, hata haki yake itakapotokea kama mwangaza, na wokovu wake kama taa iwakayo,” Isa 62:1.

Fundisho la pili katika tendo hili tunafundishwa ukweli huu kama asemavyo Mt. Augustino, “Aliyekuumba wewe, pasipo wewe, hatokusaidia wewe, pasipo wewe.” Mungu anahitaji ushirikiano wako kukamilisha uwezo wake juu yako. Mungu ulifanya hilo endapo utagundua “SHAPE au KAMOUHUMA” yako. Mungu kamwe habariki kisichokuwepo. Siyo kwamba Mungu hawezi kufanya hivyo, ila anapenda ushiriki wako katika jambo hilo kama kiumbe shirikishwa katika uumbaji na Mungu. Uumbaji wa kwanza Mungu aliumba vyote kutoka kisichokuwepo. Uumbaji huu wa pili Mungu anapenda kutushirikisha kama viumbe vyake shirikishwa katika uumbaji naye. Muujiza huu wa maji kujeuka kuwa divai, binadamu anashiriki kwa tendo la kuyajaliza yale mabalazi maji hadi juu. Hivyo haitoshi kuuomba tu ili ufanikishwe na Mungu, bali yakupasa pia kufanya kitu kadiri ya “SHAPE au KAMOUHUMA yako.

Moja ya “SHAPE au KAMOUHUMA yako ni karama zako za kiroho ulizojaliwa na Mungu. Mtume Paulo amezichambua vizuri karama hizi katika somo letu la pili. Sisi tunapobatizwa tunampokea roho huyu wa Mungu, Roho Mtakatifu. Anatufanya kuwa wana wa Mungu na wana wa Kanisa. Kwa sakramenti ya Kipaimara, Roho Mtakatifu anatufanya kuwa askari hodari wa Yesu Kristo kwa njia ya mapaji yake saba tunayopokea. Kuwa tayari kutoa ushuhuda juu ya Yesu.

Ni katika Kanisa tunapewa karama ya Roho Mtakatifu. “Na Mungu ameweka wengine katika Kanisa, wa kwanza mitume, wa pili manabii, wa tatu waalimu, kisha miujiza, kisha karama za kuponya wagonjwa, na masaidiano, na maongozi, na aina za lugha,” 1Kor 12:28.  Anatoa karama mbalimbali kwa wafuasi wa Kristo. Karama hizi ni kwa ajili ya manufaa ya Kanisa lote, ingawa zinaweza kuwa na msaada kwa aliyepewa. “Lakini kila mmoja hupewa ufunuo wa Roho kwa kufaidiana. Maana mtu mmoja kwa Roho apewa neno la hekima; na mwingine neno la maarifa, apendavyo Roho yeye yule; mwingine imani katika Roho yeye yule; na mwingine karama za kuponya katika Roho yule mmoja; na mwingine matendo ya miujiza; na mwingine unabii; na mwingine kupambanua roho; mwingine aina za lugha; na mwingine tafsiri za lugha; lakini kazi hizi zote huzitenda Roho huyo mmoja, yeye yule, akimgawia kila mtu peke yake kama apendavyo yeye,” 1Kor 12:7-11.  Kanisa lina wajibu wa kupima kwamba karama inapojitokeza kama kweli ni kutoka kwa Roho Mtakatifu. Kama si kutoka kwa Roho Mtakatifu, hii si karama bali ni kitu kingine. “Basi pana tofauti za karama; bali Roho ni yeye yule,” 1Kor 12:4 

Kama wafuasi wa Yesu, tunapojaliwa karama na Roho Mtakatifu, tunavutwa daima kumtazama yule waliyemchoma, Yoh 19:28-37. Yohani Mtakatifu anaunganisha tukio la kifo cha Yesu na kutukuzwa kwake. Yesu anaonyeshwa akiwa anaiendea saa yake, ndio saa ya kutukuzwa kwake, kwa kifo, ufufuko na kupaa kwake Mbinguni. Anamwonyesha Yesu anatoka kwa Baba na anarudi kwa Baba.

Yesu anapokufa msalabani anatoa roho yake, anatupa roho huyu aliyempokea wakati anaanza kazi yake, aliposema, “Roho wa Bwana yu juu yangu, Kwa maana amenitia mafuta kuwahubiri maskini habari njema. Amenituma kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao, Na vipofu kupata kuona tena, Kuwaacha huru waliosetwa, Na kutangaza mwaka wa Bwana uliokubaliwa,” Lk 4:18-19. Yohani anaunganisha tukio la kifo cha Yesu, tukio la msalaba na Pentekoste. Pale msalabani Yesu anatoa roho wake, nasi tunampokea kutoka ubavuni mwake tunapopokea sakramenti zake, “damu na maji”, katika Kanisa lake. “Lakini askari mmojawapo alimchoma ubavu kwa mkuki; na mara ikatoka damu na maji,” Yoh 19:34

Hivyo, tunapojaliwa karama na Roho Mtakatifu, tunavutwa daima kumtazama yule waliyemchoma. Tukifanya hivyo karama na vipaji vyetu havitakosa kuwa vya manufaa kwa Kanisa zima. Tunapomtazama tunatambua kweli tuna karama. Je, tutamtazama namna gani? Katika Kanisa lake hasa anapotufundisha kwa njia ya neno lake alilowakabidhi mitume, viongozi wa Kanisa ambao ndio wenye madaraka ya kututafsiria neno la Mungu na karama mbalimbali katika Kanisa na kuona kama kweli ni karama au ni hisia au maigizo au mahangaiko ya  kisaikolojia n.k.

Wapendwa wana wa Mungu, Karismatiki katoliki ni karama ya Roho Mtakatifu katika Kanisa. Ni tofauti na karismati za kilokole na madhehebu mengine au dini nyingine. Ipo hatari ya kuchanganya Karismatiki katoliki na hasa karismatiki ya kilokole. Siku hizi katika Karismatiki Katoliki wengi wanaiga mambo mengi ya kilokole kama nyimbo, namna ya kucheza, namna ya kuongea na kuhubiri, namna ya kusalimiana na kufurahi, namna ya uponyaji na kukemea uovu n.k. Je, haya hapa kwetu hayapo? Si tu Karismatiki Katoliki wamekumbwa na tamaa hii ya kuiga na kutumia mambo ya wengine, bali hata wakatoliki wengi hutumia nyimbo, muziki, na hisia za kilokole katika tafrija, sherehe, mikutano na semina zao. Kweli sisi wakatoliki tumechuja kiasi hicho kwamba tulivyo navyo, mathalani nyimbo zetu hazigusi nafsi na hisia zetu? Kuna kila dalili ya kuweka vya kwetu chini, au kuvichimbia na kukumbatia vya wengine na kuwasaidia kuvieneza hata ndani ya Kanisa Katoliki.

Tufanyeje basi? Tuanze kumtazama yule waliyemtoboa, tuliyemtoboa, ndio kutumia vile ambavyo kweli ni mapokeo sahihi ya Kanisa na kuacha kuwasaidia walokole kueneza ibada zao na namna zao za kusali. Tutafanikiwa hili tukiwa na ushirikiano sisi wenye, na viongozi halali wa Kanisa, tukiwatumia wataalamu wetu [kwaya zetu, waalimu wa kwaya, makatekista wetu] na pia tukitumia vipawa tulivyopewa kama wakatoliki na si kama walokole au wanakarismatiki wa dini nyingine. Yapo mengi tunaweza kuiga toka kwa wenzetu yakatusaidia lakini hii inahitaji umakini wa hali ya juu na ruhusa ya Kanisa. Si kila mtu anajiamulia kitu chake na kukileta katika Kanisa Katoliki, kuna utaratibu tangu enzi za mitume ambao unaongozwa na Roho Mtakatifu. Kila mtu akileta utaratibu wake au kitu chake itakuwa ni fujo na hakutakuwa na umoja ambao unaletwa na Roho Mtakatifu. Penye migogoro, ubinafsi na hali ya kupenda kuwa juu ya mamlaka ya Kanisa, ambapo hakuna utii, hakuna karama, bali kiburi na majivuno ndio vinatawala.

Wapendwa wana wa Mungu, Maria Kasumuni ni mwana Legio Maria aliye hai. Kipindi fulani miaka michache iliyopita kulikuwa na shindano la “voda fasta jishindie milioni 100.” Kutokana na uhitaji wa fedha hizi, Maria Kasumuni alifanya novena ya siku 90 kupitia maombezi ya Bikira Maria aweze kushinda shindano hili.

Hivyo Maria Kasumuni alifanya Novena hii kwa uaminifu Mkubwa kwa mambo makuu matatu aliyojiwekea: kuhudhuria Misa Tatatifu kila siku, kuwatembelea wagonjwa, na kuijongea Sakramenti ya kitubio kila wiki. Siku tisini ziliisha na Yasinta Masikio alitangazwa kama mshindi. Maria Kasumuni alihuzunika sana na kwenda kwenye Pango la Mama Bikira Maria na kumlilia.

Mara Maria Kasumuni alichukuliwa katika njozi na alimwona Bikira Maria katika hali ya tabasamu na alimwambia, “Maria Kasumuni usinilaumu kwa sababu mimi nilifanya kazi yangu vyema na nilikuwakilisha vizuri kwa mwanangu Yesu Kristo. Tatizo lilikuwa kwako kwa sababu hukufanya kadiri alivyokuambia.”

Maria Kasumuni alimjibu Bikira Maria na kusema, “mbona nilifanya yote kwa uaminifu mkubwa Mama wa Mungu?” Bikira Maria akamjibu kwa kumwelewesha na kusema, “Mwanangu Yesu Kristo huongea nasi kadiri ya hali, mazingira, na desturi zetu. Ulikuwa mpango wake pia kuamsha hari ya Kampuni hii ya VODA kuandaa shindano hilo ili nawe ushinde. Ila wewe hukufanya kadiri ya vigezo na masharti ya kampuni hii ya voda. Je, unatumia ‘line’ gani ya simu?”

Akiwa ameinamisha kichwa chake, Maria Kasumuni akamjibu Mama Bikira Maria na kusema, “natumia ‘line’ ya TIGO.”  Bikira Maria akamwambia Maria Kasumuni, “Ni kwa sababu hiyo hukuweza kushinda shindano la kampuni ya VODA.”

Tumsifu Yesu Kristo!

“Lo lote atakalowaambia, fanyeni,” Yoh 2:5

No hay comentarios:

Publicar un comentario