martes, 5 de enero de 2016

TAFAKARI: JUMATANO BAADA YA EPIFANIA, KIPINDI CHA NOELI

JUMATANO BAADA YA EFANIA, KIPINDI CHA NOELI
6/1/2016
Somo: 1Yoh 4:11-18
Zab: 72:1-2, 10-13
Injili: Mk 6:45-52
Nukuu:
Wapenzi ikiwa Mungu alitupenda sisi hivi, imetupasa na sisi kupendana,” 1Yoh 4:11

Hakuna mtu aliyemwona Mungu wakati wo wote. Tukipendana, Mungu hukaa ndani yetu, na pendo lake limekamilika ndani yetu,” 1Yoh 4:12

Kila akiriye ya kuwa Yesu ni Mwana wa Mungu, Mungu hukaa ndani yake, naye ndani ya Mungu,” 1Yoh 4:15

Katika pendo hamna hofu; lakini pendo lililo kamili huitupa nje hofu, kwa maana hofu ina adhabu; na mwenye hofu hakukamilishwa katika pendo,” 1Yoh 4:18

Nao walipomwona anatembea juu ya bahari, walidhani ya kuwa ni kivuli, wakapiga yowe,” Mk 6:49 

kwa kuwa wote walimwona, wakafadhaika. Mara akasema nao, akawaambia, Changamkeni; ni mimi, msiogope,” Mk 6:50 

Akapanda mle chomboni walimo; upepo ukakoma; wakashangaa sana mioyoni mwao,” Mk 6:51

kwa maana hawakufahamu habari za ile mikate, lakini mioyo yao ilikuwa mizito,” Mk 6:52 

TAFAKARI: Katika pendo hamna hofu; na mwenye hofu hakukamilishwa katika pendo.”

Wapendwa wana wa Mungu, hofu tunayotaka kuiongelea hapa si hofu ya nyoka au simba, na vingine kama hivyo. Ni hofu ya vitu vya kawaida kabisa kama asemavyo Mzaburi, “hapo waliingiwa na hofu pasipokuwapo hofu…” Zab. 53:5a. Mfano: Kuogopa giza sana kiasi cha kutothubutu kutoka chumba kimoja kwenda kingine wakati wa usiku. Kuogopa kutembea barabarani mpaka uwe na mtu.  Kuogopa wadudu na viumbe kama mende, chura, panya, kinyonga, mjusi. Kuogopa watoto wachanga na wazee. Mtu akiona kikongwe anapita yupo tayari hata kubadili njia ili asipishane naye.

Kwa upande mwingine kuna hofu ya maisha yatakavyokuwa magumu. Hofu ya maisha ya kesho. Hofu ya kuolewa na kuoa: wakikijiuliza itakuwaje watakapoanza maisha ya ndoa? Hofu ya matukio magumu ya maisha huleta roho yakutufanya tumchukie MUNGU na kutenda dhambi. Hofu huzaa kushtuka shtuka na kufanya mtu kuugua magonjwa ya mwili. Pia hofu ni mbaya zaidi inapokutawala.

 Wanafunzi wa Yesu wanapomwona Yesu akitembea juu ya maji wanaingiwa na hofu. Nao walipomwona anatembea juu ya bahari, walidhani ya kuwa ni kivuli, wakapiga yowe; kwa kuwa wote walimwona, wakafadhaika. Mara akasema nao, akawaambia, Changamkeni; ni mimi, msiogope,” Mk 6:49-50 

Neno “usiogope” lipo mara 366 katika Biblia. Hii ina maana Mungu anatuambia kila siku “usiogope”. Unapokuwa na hofu ya kitu chochote, basi kitu hicho ndicho chenye uwezo wa kuamua hatima yako. Kwa watu wa Mungu tunatakiwa tuelekeze hofu yetu kwa Mungu tu na si kwingineko kwani tutakapoielekeza kwa Mungu yeye ni mwaminifu na atatuelekeza kufanya ya Mbinguni. Huwezi kupenda katika ukamilifu wake kama unatawaliwa na hofu. Je, utapenda vipi kile ulichokuwa na mashaka nacho? Hivyo, katika pendo hamna hofu; lakini pendo lililo kamili huitupa nje hofu, kwa maana hofu ina adhabu; na mwenye hofu hakukamilishwa katika pendo,” 1Yoh 4:18

Maandiko Matakatifu yanasema nini juu ya HOFU? Ndugu yangu, wakuhofia ni Bwana wa majeshi na huyu ndiye apaswaye kuwa hofu yetu. Bwana wa majeshi ndiye mtakayemtakasa; na awe yeye hofu yenu, na awe yeye utisho wenu,”Isa 8:13. Bwana wetu Yesu Kristo anasema vizuri nani inatupasa kumwaogopa. Nami nawaambia ninyi rafiki zangu, msiwaogope hao wauuao mwili, kisha baada ya hayo hawana wawezalo kutenda zaidi. Lakini nitawaonya mtakayemwogopa; mwogopeni yule ambaye akiisha kumwua mtu ana uweza wa kumtupa katika Jehanum; naam, nawaambia, Mwogopeni huyo,” Lk 12:4-5. Wapo kati yetu kutokana na mifumo mbalimbali katika jamii yetu leo wamejawa hofu na mara zote huishi kama wafu. Hatupaswi kuishi katika hali hii. Unapomtoa Mungu katika mfumo wako wa kuishi unakumbatia mauti ya pili kama tusomavyo katika kitabu cha ufunuo. Bali waoga, na wasioamini, na wachukizao, na wauaji, na wazinzi, na wachawi, na hao waabuduo sanamu, na waongo wote, sehemu yao ni katika lile ziwa liwakalo moto na kiberiti. Hii ndiyo mauti ya pili,” Ufunuo 21:8

Wapendwa katika Kristo, hofu haileti madhara ya kiroho tu bali hata ya kimwili. Hofu huleta mshituko na penye hofu pana wasiwasi, palipo na haya huleta magonjwa ya “Organic” {sehemu za mwili zifanyazo kazi maalumu} na hitilafu katika shehemu hizi husababisha vidonda vya tumbo {ulcers} shinikizo la damu, kisukari, magonjwa ya ini, upungufu wa damu mwilini, n.k. Nabii Isaya anatuambia baadhi ya magonjwa yanayosababishwa na hofu: Kwa sababu hiyo viuno vyangu vimejaa maumivu, utungu umenishika, kama utungu wa mwanamke azaaye; ninaumwa sana, nisiweze kusikia; nimefadhaishwa wa hofu, nisiweze kuona. Moyo wangu unapiga-piga, utisho umenitaabisha, gizagiza la jioni nilipendalo limegeuka likanitetemesha,” Isa 21:3-4

Tunaishinda hofu kwa kutambua upendo wa Mungu ndani yetu. Upendo huu wa Mungu ndani yetu hujidhihirisha kwa kuwapenda wengine kama tunavyojipenda wenyewe. Hakika hii ndiyo amri Kuu. “Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa nguvu zako zote, na kwa akili zako zote; na jirani yako kama nafsi yako,” Lk 10:27. Mshikamano huu katika Pendo hutuondolea hofu, kwa sababu hakuna mtu aliyemwona Mungu wakati wo wote. Tukipendana, Mungu hukaa ndani yetu, na pendo lake limekamilika ndani yetu,” 1Yoh 4:12. Ukamilisho wa pendo la Mungu ndani yetu ni pale napompenda mwenzangu bila kipimo. “Kipimo cha upendo ni kupenda bila kipimo,” Mt. Augustino. Tunapotambua upendo wa Mungu ndani yetu, upendo kwa jirani ni wajibu.Wapenzi ikiwa Mungu alitupenda sisi hivi, imetupasa na sisi kupendana,” 1Yoh 4:11.

Kukaa ndani ya pendo la Mungu ni kutambua na kukiri Yesu ni Mwana wa Mungu. Kwa nini?  Kwa sababu hakuna chochote kile kilichofanyika au kuwepo katika ulimwengu huu pasipo Neno ambaye ndiye Kristo. Hapo mwanzo kulikuwako Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu. Huyo mwanzo alikuwako kwa Mungu. Vyote vilifanyika kwa huyo; wala pasipo yeye hakikufanyika cho chote kilichofanyika,” Yoh 1:1-3. Kwenda kwa Baba wa Munguni twamwihitaji Yesu kwa namna yoyote ile. Naye Yesu anasema,  “Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi,” Yoh 14:6. Ni kwa maana hiyo kwamba Yohane Mtume anakazia neno hili KUKIRI. Kila akiriye ya kuwa Yesu ni Mwana wa Mungu, Mungu hukaa ndani yake, naye ndani ya Mungu,” 1Yoh 4:15. Ndugu yangu tuliyesafiri wote kwenye tafakari hii ukiri huo upo ndani yako?

Tumsifu Yesu Kristo!


Kwa pendo la udugu, mpendane ninyi kwa ninyi; kwa heshima mkiwatanguliza wenzenu; kwa bidii, si walegevu; mkiwa na juhudi katika roho zenu; mkimtumikia Bwana,” Rum 12:10-11

No hay comentarios:

Publicar un comentario