SIKUKUU
YA BIKIRA MARIA MAMA WA MUNGU
1/1/2016
Somo I: Hes 6:22-27
Zab: 67:2-3, 5, 6, 8
Somo II: Gal 4:4-7
Injili: Lk 2:16-21
Nukuu:
“Ndivyo watakavyoweka
jina langu juu ya wana wa Israeli; nami nitawabarikia,” Hes 6:27
“Hata ulipowadia
utimilifu wa wakati, Mungu alimtuma Mwanawe ambaye amezaliwa na mwanamke,
amezaliwa chini ya sheria,” Gal 4:4
“Kama ni hivyo, wewe si mtumwa tena bali u mwana; na kama u
mwana, basi, u mrithi kwa Mungu,” Gal 4:7
“Wakaenda kwa haraka wakamkuta Mariamu na Yusufu, na yule
mtoto mchanga amelala horini,” Lk 2:16
“Lakini Mariamu akayaweka maneno hayo yote, akiyafikiri
moyoni mwake,” Lk 2:19
“Wale wachungaji wakarudi, huku wanamtukuza Mungu na kumsifu
kwa mambo yote waliyosikia na kuyaona, kama walivyoambiwa,” Lk 2:20
“Hata zilipotumia siku nane za kumtahiri, aliitwa jina lake
Yesu; kama alivyoitwa na malaika kabla hajachukuliwa mimba,” Lk 2:21
TAFAKARI:
“Lakini Mariamu akayaweka maneno
hayo yote, akiyafikiri moyoni mwake.”
Wapendwa wana wa Mungu,
Leo ni mwaka Mpya. Tulio hai tuna kila sababu ya kumshukuru Mungu kwa yale yote
aliyotujalia na hasa yale tuliyokutana nayo kwa mwaka tuliouaga, tukijua kwamba
kila jambo lilikuwa na sababu yake na mapenzi ya Mungu ndani yake. Leo
tunapouanza mwaka kwa namna ya pekee Mama Kanisa anaadhimisha siku hii kwa
Heshima ya Mama Bikira Maria Mama wa Mungu. Kuuanza mwaka Mpya twahitaji baraka
za Mungu, tukisafiri pamoja na Mama Bikira Maria Mama wa Mungu kama mfano hai
wa kuiga na kufuata.
Kadiri ya somo letu la
kwanza, wana wa Israeli iliwapasa kuliweka jina la Bwana juu ya mambo yote na
ndivyo walivyobarikiwa. “Ndivyo watakavyoweka jina langu juu ya wana wa Israeli;
nami nitawabarikia,” Hes 6:27. Wana wa Israeli walilishika na kulibeba jina la
Mungu kama ilivyo uhusiano kati ya mke na mume. Jina hili la Bwana liliathiri
kwa kiasi kikubwa mafanikio yao, wakati mwingine ilikuwa balaa walipoliasi jina
hili. Hivyo hatima ya maisha yao ilitegemea namna walivyolichukulia jina hili
la Mungu aliye hai. Ndivyo hivyo basi wakati wana wa Israeli walipokuwa
uhamishoni na katika unyonge wao, jina la Mungu lilinajisiwa katika mataifa,
Eze 36. Ni kwa namna hiyo hiyo tunaona kwamba wana wa Israeli walipowekwa huru
kwa maajabu makubwa ya Mungu, jina la Mungu lilitakatifuzwa, liliinuliwa juu
kabisa kutoka unyonge na kudhalilishwa, na kutakatifuzwa, Eze 36. Ni kutoka
katika mtazamo huu kulitaja jina la Mungu na watu wake ni chanzo cha baraka na
dhana ya ukarimu. Hivyo kuuanza mwaka na kuumaliza yatupasa kuweka vipauwa
mbele muhimu na hasa kwa maisha ya kiroho.
Kipauwa
mbele namba moja ni kukaa ndani ya jina la Mungu na neno lake. Huko ndiko
kwenye uzima wa kweli. Kristo ni Mzabibu nasi ni matawi. “Mimi ni mzabibu; ninyi ni matawi, akaaye ndani yangu nami ndani
yake, huyo huzaa sana; maana pasipo mimi ninyi hamwezi kufanya neno lo lote,”
Yoh 15:5. Uzima huu twaupata pia kwa kulishika neno lake; kulisoma, kulipokea,
kulitafakari, kulitafiti, na kulikumbuka kusiko kikomo. “Amin, amin, nawaambia, Yeye alisikiaye neno
langu na kumwamini yeye aliyenipeleka yuna uzima wa milele; wala haingii
hukumuni, bali amepita kutoka mautini kuingia uzimani,” Yoh 5:24.
Kipauwa mbele namba mbili ni kulishwa na kuhuishwa kila
mara kwa kupokea Masakramenti katika hali iliyo safi, hasa Sakramenti ya
Ekaristi Takatifu. Ndani ya Sakramenti hii ya Ekaristi Takatifu, tunakaa ndani
na katika Kristo, na kupata uzima wa milele. Mwili na damu ya Kristo ni chakula
na kinywaji cha kweli. Naye Yesu
anasema, “Aulaye mwili wangu na kuinywa damu yangu anao uzima wa milele;
nami nitamfufua siku ya mwisho. Kwa
maana mwili wangu ni chakula cha kweli, na damu yangu ni kinywaji cha kweli. Aulaye mwili wangu na kuinywa damu
yangu hukaa ndani yangu, nami hukaa ndani yake,” Yoh 6:54-56. Pamoja na makuu
tuyachotayo kutoka Sakramenti hii, neema na baraka zake, Mtume Paulo anatupa
angalizo juu ya Mwili huu na Damu hii ya Kristo. “Basi kila aulaye
mkate huo, au kukinywea kikombe hicho cha Bwana isivyostahili, atakuwa
amejipatia hatia ya mwili na damu ya Bwana,” 1Kor 11:27. Ndugu yangu, kabla ya
kuijongea meza hii ya Bwana jihoji kwanza nafsini mwako. Je, nastahili kwa hali
niliyo nayo? “Lakini mtu ajihoji mwenyewe, na hivyo aule mkate, na kukinywea
kikombe,” 1Kor 11:28. Tusiogope
macho ya watu, na wala tusipende kushiriki Sakramenti hii na Karamu hii ya
Upendo kwa mazoea.
Kipauwa mbele namba tatu
tusiache kwamwe kupatanishwa kwanza na Mungu kwa Sakramamenti ya Upatanisho au
Kitubi o. Kwa namna ya pekee Mama
Kanisa ameutenga mwaka huu kama mwaka pekee wa Huruma ya Mungu. Jambo la
kusikitisha leo Sakramenti hii ya Upatanishao imekuwa kama ‘kituo cha polisi.’
Walio wengi leo wanataka kuhalalisha dhambi. Sakramenti hii ya Upatanisho
imewekwa rasmi na Kristo mwenyewe katika Kanisa, na wahudumu wake ni wale
walioteuliwa {kuhesabiwa haki na Mama Kanisa}, kupakwa mafuta, na kuwekwa wakfu, {Mapandre na Maaskofu} na
kwa ajili hiyo huadhimisha Sakramenti hiyo. Hapa tunakutana na Huruma ya Mungu,
Msamaha wa Mungu, na Kupatanishwa na Mungu. Naye Yesu anasema, “Wo wote mtakaowaondolea dhambi, wameondolewa; na wo wote
mtakaowafungia dhambi, wamefungiwa,” Yoh 20:23. Ndugu yangu tuijongee Huruma ya
Mungu, Msamaha wa Mungu, na Kupatanishwa naye {nafsi, jirani, na mazingira}.
Mwaka huu tunaouanza unatudai kuishi katika ukweli huu kama kweli twautaka
uzima ndani yetu.
Somo letu
la pili na Injili linafafanua fumbo zima la kumwilishwa, Neno akafanyika mwili
akakaa kwetu, Yoh 1:14. Na hapa ndipo tunapoona nafasi ya Mama Bikira Maria
Mama wa Mungu tunaye msherehekea leo katika tendo hili zima. Tendo hili
limetokea katika utimilifu wa wakati, baada ya muda mrefu wa kusubiri. “Hata ulipowadia utimilifu wa wakati, Mungu alimtuma Mwanawe
ambaye amezaliwa na mwanamke, amezaliwa chini ya sheria,” Gal 4:4. Tendo hili
limebeba sehemu kuu mbili kwa wakati mmoja; kwanza linawapa watu uwana wa Mungu
kwa kuwafungua kutoka sheria ya Musa. “Wewe si mtumwa tena bali u mwana; na kama u mwana, basi, u
mrithi kwa Mungu,” Gal 4:7. Sehemu ya
pili, kumwilishwa kwa neno kumefanyika katika hali ya kibinadamu na kwa sheria,
yaani, kwa Kristo kuzaliwa na mwanamke
chini ya sheria ili kumkomboa huyo mwanadamu aliye katika sheria. Sheria inamweka Kristo katika historia ya wokovu,
yaani katika historia ya watu wake. Mwanamke ni kati ya watu, yaani, ndugu zake
Kristo aliokuja kuwaweka huru na kuwakomboa kwa kuwafanya kama yeye, yaani,
wana wa Baba. Kwa maana hiyo, “Kwa kuwa hamkupokea
tena roho wa utumwa iletayo hofu; bali mlipokea roho ya kufanywa wana, ambayo
kwa hiyo twalia, Aba, yaani, Baba. Roho
mwenyewe hushuhudia pamoja na roho zetu, ya kuwa sisi tu watoto wa Mungu,” Rum
8:15-16.
Katika
hali hii ya kumwilishwa, tunaona katika Injili yetu ya leo kwamba waamini wa
kwanza wa tukio hili ni wachungaji ambao wapo karibu ya Maria Mama yake
Yesu na Mtoto Yesu, walio jiachia wazi
kwa Mungu. Hapa Bikira Maria ni Mama kwa utayari na NDIYO yake kwa Neno la
Mungu, kwa uamini wake na ukimya ambao unamfanya kupokea fumbo hili: “Hapo mwanzo kulikuwako
Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu. Naye Neno
alifanyika mwili, akakaa kwetu; nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama wa
Mwana pekee atokaye kwa Baba; amejaa neema na kweli,” Yoh 1:1,14. Mapaswa na
ubora wa wana wa Israeli ulikuwa ‘kusikiliza Neno la Mungu.’ Katika tendo hili,
Bikira Maria ndiyo kielelezo cha ukamilifu na utimilifu wa Neno hili la kumwilishwa
kwa NDIYO yake. “Mariamu akasema, Tazama, mimi
ni mjakazi wa Bwana; na iwe kwangu kama ulivyosema,” Lk 1:38a. Fumbo
hili ndilo linalomwinua Bikira Maria katika nafasi hii ya juu kabisa Binadamu
kuwekwa. Hivyo katika shina la Daudi limetoka chipukizi ambalo ndilo tumaini na
jibu la Mungu kwa watu wake.
Nafasi ya
Maria katika tendo hili la utayari wake, yaani Neno kumwilishwa ni uchungu na
mateso na furaha. Yusufu mumewe katika sintofahamu hii anataka kumwacha kwa
siri. “Naye
Yusufu, mumewe, kwa vile alivyokuwa mtu wa haki, asitake kumwaibisha, aliazimu
kumwacha kwa siri,” Mt 1:19. Ndiyo ya Bikira Maria kwa Mungu inakuwa mwanzo wa
aibu, ugumu wa kueleweka na mumewe, na maumivu. Hata pamoja na hali hii Bikira
Maria hakuwa sababu ya kuzuia mapenzi ya Mungu yasitendeke kwa sifa na Utukufu
wa Mungu na watu wake aliowaridhia. Sauti ya Mungu ilimfikia Mama Maria kupitia
mwanaye Yesu Kristo aliyemzaa, Simeoni, na wachungaji. Maria aliyaweka yote
haya na kuyatafakari moyoni mwake. U
Mama wa Bikira Maria na upana wa kifua chake wa kuyabeba mambo makuu na mazito
haukuishia pale horini tu, bali aliendelea kuubeba U Mama huo wa Mungu na hali
hiyo hadi Msalabani. Hapa ndipo aliposhuhudia kifo katili dhidi ya mwanaye
mpenzi ambaye hakuwa na kosa lolote zaidi ya wema aliyotutendea.
Hakika
Mama Bikira Maria aliyastahimili na kuyashiriki kikamilifu mateso ya mwanaye
Yesu Kristo. “Na penye msalaba wake Yesu walikuwa wamesimama mamaye, na
umbu la mamaye, Mariamu wa Klopa, na Mariamu Magdalene,” Yoh 19:25. Pamoja na
huzuni na uchungu aliokuwa nao Mama Bikira Maria na Yesu ambaye kwa sasa
alikuwa tayari kesha wambwa juu msalabani, Yesu analikabidhi Kanisa (kwa
mitume) na jumuiya yote ya waamini kwa Mama yake. “Basi Yesu alipomwona mama yake, na yule mwanafunzi
aliyempenda amesimama karibu, alimwambia mama yake, Mama, tazama, mwanao. Kisha
akamwambia yule mwanafunzi, Tazama, mama yako. Na tangu saa ile mwanafunzi yule
akamchukua nyumbani kwake,” Yoh 19:26-27. Huyu ndiye Mama Bikira Maria Mama wa
Mungu tunaye msheherekea leo. Huyu ndiye tunayetaka kuanza naye mwaka huu mpya
tukiwa na imani pasipo shaka kwamba tutamaliza naye mwaka huu salama kama
iliyokuwa NDIYO yake wakati ulipotimia pale horini, na kuendelea na NDIYO yake
hadi mwisho pale msalabani ulipotundikwa wakovu
wetu na UTUKUFU wa Kristo na wetu. Hakika
yatupasa kumshangilia Mama Yetu Bikira Maria, Mama wa Mungu.
Mwaka
huu nilipokuwa likizo nyumbani mwezi wa saba hadi wa tisa mwanzoni, nilikumbuka
tukio la miaka 23 iliyopita mara baada ya kumaliza mwaka wa Malezi huko Mahanje
Songea. Nilikuwa na furaha kubwa sana ya kuchaguliwa na kuendelea na masomo ya
sekondari katika Seminari ya watawa wa Mt. Fransisco wa Assis huko Maua
Seminary-Moshi.
Nikiwa
nyumbani Arusha-Njiro najiandaa kwa kuanza masomo hayo ya kidato cha kwanza,
niliugua homa ya miguu na kuhisi kupooza na kutoweza kutembea tena. Niliona
kama vile ndoto yangu ya kuwa siku moja Mtawa na Padre kuanza kutoweka. Mama
yangu Mzazi alinihudumia kwa upendo mkubwa; kuniogesha na kunisaidia hudumu
nyingine nilizohitaji kwa hali ile niliyokuwa nayo. Nakumbuka alinibeba
mgongoni mwake umbali usiopungua zaidi kilomita 15 hivi kwenda na kurudi, kwani
wakati ule hapakuwa na usafiri wa daladala na bodaboda kama ilivyo sasa. Safari
hii tulikuwa tunaelekea hospitali ya KCMC-Moshi kwa vipimo zaidi. Hakika Mama
yangu alitaabika sana nami. Jambo la ajabu sikuona kukerwa na hali ile niliyokuwa
nampatia.
Nilipata
vipimo na kurejea nyumbani Arusha-Njiro. Mungu alivyomwema kwa watu wote na
nyakati zote, baada ya wiki kama mbili hivi nilianza kupata hauweni. Tarehe za
kufungua Seminari zilipowadia nilikuwa tayari kwa masomo na mwenye afya ya kutosha.
Hivyo
mwaka huu baada ya miaka hiyo 23 kupita, Mama yangu Mzazi naye alipatwa na homa
ya miguu kama ilivyokuwa kwangu ila kwa tatizo tofauti. Nikiwa likizo ilinipasa
kumuhudumia, hasa kumwinua kitandani na kumkominisha kila siku mara baada ya
kuadhimisha Misa kigangoni kwetu St. Josephina Bakhita Korona-Njiro. Ilinipasa
pia kumpikia kwani karibu ndugu zangu wote wameolewa na kuoa hivyo wanamiji
yao. Wajukuu aliokuwa anaishi nao Mama yangu nyumbani asubuhi hadi jioni
iliwapasa kuwa shuleni {shule ya upili}. Hivyo muda mwingi nilikuwa naye.
Nilimbeba ingawa siyo mgongoni hadi KCMC kwa matibabu. Nilitumia muda mwingi
kumfurahisha kwa kumchezea gitaa na kuimba. Kwa kweli nilijaribu kurudisha
shukrani zangu japo kwa uchache aliyonitendea miaka 23 iliyopita.
Leo
ninamshukuru Mungu Mama yangu anaendelea vizuri licha kwamba hajapona kabisa.
Huu upendo ni sehemu tu ya upendo niliouonja kwa Mama kwa namna alivyotesema na
kutaabika nami bila kuchukizwa na karaha nilizompatia. Hakika kama nikiambiwa
leo nilipe alichonitendea sintoweza kufanya hivyo hata nikipewa miaka 1000 na
Mungu ya kuishi nikiwa nafanya kazi usiku na mchana. Sintoweza kulipa kwa
sababu kadiri nitakavyoishi na kuwa hai, ni kwa kipimo hicho hicho deni hili
litakavyoongezeka hata kama yeye atakuwa kesha kufa.
Wapendwa
wana wa Mungu, kwa sadaka na matojitoleo ya Mama Maria, Mama wa Mungu na hasa
kwa NDIYO yake katika fumbo hili la kumwilishwa, mimi na wewe tuna deni kubwa
sana la lipa licha ya kwamba Mwanaye Yesu Kristo kesha tulipia deni letu,
dhambi zetu kwa sadaka yake pale msalabani. Kwa upande wa kwanza, deni hili ni
kuishi upendo wa kweli na haki kwa kila aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.
Ni kwa sababu ya upendo huu Kristo alikubali kuyatoa maisha yake kwa ajili yako
na yangu. “Amri yangu ndiyo hii, Mpendane, kama nilivyowapenda ninyi. Hakuna aliye na upendo
mwingi kuliko huu, wa mtu kuutoa uhai wake kwa ajili ya rafiki zake,” Yoh
15:12-13. Ni kwa kumkomboa huyu aliyeumbwa kwa sura na mfano
wake, Mungu anaruhusu mwanaye ateseke kwa ajili yangu na yako, na Mama Bikira
Maria kushiriki mateso haya ya mwanaye. Na sehemu ya pili ya deni hili ni kuwa
watakatifu kama Baba yetu wa Mbinguni alivyo Mtakatifu. Utakatifu huu tunaupata
kwa kuishi vyema na kuzitumia vyema karama zetu kila mmoja kadiri ya wito wake,
kwa kutimiza utume wake vyema.
Tumsifu
Yesu Kristo!
“Basi ninyi mtakuwa wakamilifu, kama Baba yenu wa mbinguni
alivyo mkamilifu,”
Mt
5:48
No hay comentarios:
Publicar un comentario