SIKUKUU YA FAMILIA TAKATIFU MWAKA-A
Yesu, Maria, na Yosefu
Somo
I: YbS 3:3-7; 12-14
Zab:
128: 1-2, 3, 4-5
Somo
II: Kol 3:12-21
Injili:
Mt 2:13-15, 19-23
Nukuu:
“Amheshimuye baba yake
atafanya upatanisho wa dhambi, naye amtukuzaye mama yake huweka akiba iliyo
azizi,” YbS 3:3-4
“Amheshimuye babaye
atawafurahia watoto wake mwenyewe, na siku ya kuomba dua atasikiwa,” YbS 3:3:5
“Amtukuzaye baba yake
ataongezewa siku zake; akimsikiliza Bwana, atamstarehesha mamaye, na
kuwatumikia wazazi wake kama mabwana. Mwanangu,” YbS 3:6-7
“Mwanangu, umsaidie
baba yako katika uzee wake, wala usipate
kumhuzunisha siku zote za maisha yake,” YbS 3:12
“Akiwa amepungukiwa na ufahamu umwie kwa
upole, wala usimdharau iwapo wewe u mzima sana,” YbS 3:13
Mwenye kumdharau baba
yake ni mfidhuli, naye mwenye kumlaani mama yake amekwisha kulaaniwa na Bwana,”
YbS 3:16
“Basi, kwa kuwa
mmekuwa wateule wa Mungu, watakatifu wapendwao, jivikeni moyo wa rehema, utu
wema, unyenyekevu, upole, uvumilivu, mkichukuliana,
na kusameheana, mtu akiwa na sababu ya kumlaumu mwenzake; kama Bwana alivyowasamehe
ninyi, vivyo na ninyi,” Kol 3:12-13
“Zaidi ya hayo yote
jivikeni upendo, ndio kifungo cha ukamilifu,” Kol 3:14
“Ninyi wake, watiini waume zenu, kama ipendezavyo katika Bwana. Ninyi waume, wapendeni wake zenu msiwe
na uchungu nao,” Kol 3:18-19
“Ninyi watoto, watiini
wazazi wenu katika mambo yote; maana jambo hili lapendeza katika Bwana,” Kol
3:20
“Ninyi akina baba,
msiwachokoze watoto wenu, wasije wakakata tamaa,” Kol 3:21
“Na hao
walipokwisha kwenda zao, tazama, malaika wa Bwana alimtokea Yusufu katika
ndoto, akasema, Ondoka, umchukue mtoto na mama yake, ukimbilie Misri, ukae huko
hata nikuambie; kwa maana Herode anataka kumtafuta mtoto amwangamize,” Mt 2:13
“Ndipo Herode, alipoona
ya kuwa amedhihakiwa na wale mamajusi, alighadhabika sana, akatuma watu akawaua
watoto wote wanaume waliokuwako huko Bethlehemu na viungani mwake mwote, tangu
wenye miaka miwili na waliopungua, kwa muda ule aliouhakikisha kwa wale
mamajusi,” Mt 2:16
TAFAKARI:
“Zaidi ya hayo yote jivikeni upendo, ndio kifungo cha
ukamilifu,” Kol 3:14
Wapendwa wana wa Mungu,
leo tukiwa bado katika kipindi cha kuzaliwa Bwana wetu Yesu Kristo, Mama Kanisa
anaadhimisha Sikukuu ya Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu. Kwa namna ya
pekee leo, masomo yote matatu yanamulika swala zima la Familia, muundo wake,
wajibu wake kwa ujumla na kila mmoja katika familia kadiri ya nafasi yake,
Mahangaiko ya familia, na kutengemaa kwa familia yenye kujali na kuwajibika.
Bila shaka msingi wa familia ni ule moyo ya upendo wenye kuzaa hali ya
kuvumiliana na kutabikiana. Hiki ndicho kifungu cha ukamilifu. Kama asemavyo
Mtume Paulo, “Zaidi ya hayo yote jivikeni upendo,
ndio kifungo cha ukamilifu,” Kol 3:14. Tukiachia mbali hii Familia Takatifu ya
Yesu, Marian na Yosefu, familia zetu si kamili katika maana ya Utakatifu.
Familia yetu zina madhaifu mengi sana. Lakini familia hizi ambazo ni dhaifu
husimama imara pale wanapotazama, jifunza, na kuishi Utakatifu wa Familia
Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu kama mfano ulio hai wa kuiga.
Ni wazi
kwamba familia iliyosimama katika kweli, haki, upendo, huruma, na kusamehana si
kazi rahisi na si kazi ya siku moja. Leo tunaposheherekea Familia Takatifu ya
Yesu, Maria na Yosefu, haikuwa kazi rahisi kwa Maria na wala Yosefu kumlea
mtoto Yesu. Tuelewa kwamba Yesu ni Mungu na Mwanadamu. Asili hizi mbili
zilileta sintofahamu nyingi kwa Maria na Yosefu katika malezi ya Mtoto Yesu.
Uwepo wa
Yesu ulikuwa tishio kubwa sana wa utawala ule wa Herode ambaye mamlaka yalikuwa
kila kitu kwake. Hivyo kwa kusikia yaliyosemwa juu ya Mtoto Yesu, Herede anaingiwa
na hofu na kuruhusu umwagikaji wa damu zisizo na hatia. Njia aliyochukua Herode
haina tofauti na watawala wetu wa leo wanapopatwa na hofu juu tawala zao za
mabavu. Wapo
wengi wanaouwawa kila dakika ulimwenguni na hasa nchi zetu za kiafrika kwa
sababu ya hofu ya madaraka yaliyobebwa na utawala dhalimu.
Hivyo
kuhakikisha anamwangamiza Mtoto Yesu, tangazo linatolewa mara moja baada ya
kujua wale Mamajusi wamemdanganya kadiri ya maagizo aliyokwisha wapa, yaani, “Shikeni njia, mkaulize sana mambo ya mtoto; na
mkiisha kumwona, nileteeni habari, ili mimi nami niende nimsujudie,” Mt 2:8.
Wakijua nia yake mbaya juu ya mtoto Yesu, Mamajusi walishika njia nyingine
baada ya kumsujudu mtoto Yesu na kutoa zawadi zao.
Hapa ndipo lilipotolea tangazo la kuwaangamiza watoto wasio
na hatia. “Ndipo Herode, alipoona ya kuwa amedhihakiwa na wale
mamajusi, alighadhabika sana, akatuma watu akawaua watoto wote wanaume
waliokuwako huko Bethlehemu na viungani mwake mwote, tangu wenye miaka miwili
na waliopungua, kwa muda ule aliouhakikisha kwa wale mamajusi,” Mt 2:16. Nguvu
ya Mungu na mpango wake kwa wale aliorithia nao ni tofauti na mipango yetu
ambayo kwayo haina uzima ndani yake.
Kama
Mungu ndiye mweza wa vyote hakuna chochote kitakachozuia mpango huo, kwani nasi
kama tulivyo na mamlaka tuliyonayo humtegemea Mungu huyu huyu. “Na hao
walipokwisha kwenda zao, (Mamajusi) tazama, malaika wa Bwana alimtokea Yusufu
katika ndoto, akasema, Ondoka, umchukue mtoto na mama yake, ukimbilie Misri,
ukae huko hata nikuambie; kwa maana Herode anataka kumtafuta mtoto
amwangamize,” Mt 2:13. Ni nani kama Mungu wetu? Leo tunajionea wenyewe baadhi
ya tawala ambazo hazipo tayari kuachia dola kwa AMANI, na hivyo kuleta maafa
makubwa ya mauaji ya watu wasio na hatia. Pamoja na ukatili huu, uovu hauwezi
kudumu katika umilele wake, kwa sababu uovu hauna umilele. Wale wote wauteteao
na kuulinda uovu ujichosha kure. Hivyo, “Bwana
asipoijenga nyumba Waijengao wafanya kazi bure. Bwana asipoulinda mji Yeye
aulindaye akesha bure,” Zab 127:1
Hali na mazingira haya yanaleta hofu kubwa sana katika familia
hii Takatifu. Hivyo kama mazingira na hali ya ukimbizi tuionayo leo, hata Yesu
ameipitia. Na yanapotokea maafa kama haya wanaotesema ni akina mama na watoto.
Mama Marian a Yosefu wanayanusuri maisha ya Mtoto Yesu kwa kukimbilia Misri.
Familia hii Takatifu inaishi maisha ya ukimbizi.
Pamoja na sintofahau hizi, na malezi ya Mtoto Yesu, Bikira
Maria alikuwa na muda mwingi wa kutafakari haya asiyoyafahamu. “Lakini Mariamu
akayaweka maneno hayo yote, akiyafikiri moyoni mwake,” Lk 2:19. Kuyaweka moyoni
ni kuyapa nafasi ya tafakari kwa yale tusiyoyajua. Je, wewe kama mzazi mwanao
anapofanya ndivyo sivyo, wajiuliza kwa nini amefanya kama alivyo fanya? Kujua
chanzo cha tatizo ni bora kuliko kukimbilia kulitatua tatizo. Hivyo tafakari ya
Bikira Maria ilimsaidia kufahamu uwezo na kile alicho mwanaye Yesu Kristo.
Muujiza wa kwanza ya Yesu kule Kana unathibitisha ufahamu
wa Maria juu ya mtoto wake. Kulipotokea upungufu wa divai, Bikira Maria alienda
moja kwa moja na kumwambia Yesu, Mwanaye, kwamba hakuna divai. Bikira Maria
hakubaki na jibu la mwanaye, ila alienda moja kwa moja kwa wale wahudumu na
kuwaambia, “Lo lote
atakalowaambia, fanyeni,” Yoh 2:5. Kwa tendo hili hakuna shaka kwamba Mama
Bikira Maria anaufahamu uwezo wa mtoto wake. Je, leo wazazi wangu muna muda wa
kutosha kuwafahamu watoto wenu ikiwa ni pamoja na tabia zao? Basi tujifunze kwa
Mama Bikira Maria. Leo tunapoongelea familia na hasa zenye malengo
na mwelekeo, tunaongelea familia ndani ya ndoa Takatifu yenye kujali na
kuwajibika. Hivyo ni vyema kujua fumbo zima la ndoa na chimbuko la famila kama
tunda na matokeo ya ndoa hiyo.
1. Fumbo zima la ndoa na chimbuko la familia
Wapendwa
wana wa Mungu, upendo huu wa Mungu kwa watu wake yatupasa kuuona katika mambo
yote yenye kutupeleka katika umoja wake, upendo wake, ushirikiano wake na hata
katika maagano yetu katika maisha. Ni kwa kupitia umoja huo, upendo huo, na
ushirikiano huo wa Mungu na mwanaye mpenzi, Yesu Kristo Mungu hujidhihirisha
kwetu kila siku ya maisha yetu hapa duniani. Upendo wa Mungu na mshikamano na
mwanaye tunauona katika masakramenti yake, na hasa leo tunavyotafakari kwa
ukaribu sakramenti hii ya ndoa. Naye Mtume
Paulo anasema, “Enyi wake, watiini waume zenu kama kumtii Bwana
wetu. Kwa maana mume ni kichwa cha mkewe, kama Kristo naye ni kichwa cha
Kanisa; naye ni mwokozi wa mwili,” Efe 5:22-23. Hapa upendo wa Mungu kupitia
Kristo mwenyewe unaonekana kwa utii huu wanaoishi wana ndoa, na hasa kwa mke
kumtiii mumewe. Je, ndoa zetu leo ni salama? Akina mama mnaishi ukweli huu
katika agano lenu la ndoa? Leo baadhi ya wanawake wamefikia kuwaita waume zao
vyuma chakavu. Je, hayo ndiyo makusudio ya Mungu na muungano wenu huo?
Kwa
upande wa wanaume yawapasa kuwapenda wake zao katika kweli na haki. Upendo huu
unafananishwa na upendo wa Kristo na Kanisa lake. “Enyi waume, wapendeni wake
zenu, kama Kristo naye alivyolipenda Kanisa, akajitoa kwa ajili yake; ili
makusudi alitakase na kulisafisha kwa maji katika neno; apate kujiletea
Kanisa tukufu, lisilo na ila wala kunyanzi wala lo lote kama hayo; bali liwe
takatifu lisilo na mawaa,” Efe 5:25-27. Wanaume zieshimuni ndoa zetu kwani ndio
utakatifu wenu mnapoziishi katika kweli na haki. Wake zenu hawahitaji mambo ya
pekee sana zaidi ya kuyasadifu yale wayatendayo kila siku katika familia. Tabia
ya kuwaita wake zetu magoli kipa ni chukizo mbele ya Mungu. Muunganiko wenu ni
makusudio ya Mungu, na ndivyo alivyoona inafaa.
Utii wa
kweli si utumwa kwenu, bali ni ukamilifu wa makusudio ya Mungu katika maisha ya
umilele. Wito wenu wa ndoa ni kuufikia umelele wa maisha yenu mlioandaliwa
kupitia sakramenti hiyo. Hivyo, “kama vile Kanisa limtiivyo Kristo vivyo hivyo
wake nao wawatii waume zao katika kila jambo,” Efe 5:24. Ni kuwa na utii katika
Kristo kwa sababu yeye anayo maneno la uzima wa milele. Ni kwa kupitia NENO
huyu vyote vilifanyika, na kwa kupitia NENO huyu vyote huwa na uzima wa milele,
Yoh 1:3. “Kwa sababu hiyo mtu atamwacha baba yake na mama yake, ataambatana na
mkewe na hao wawili watakuwa mwili mmoja,” Efe 5:31. Tendo hili la ajabu katika
sakramenti hii ya ndoa halimwesabii haki mmoja wa wanandoa kuwa na mambo yake
ya pekee na binafsi tena. Hakuna msamiati huu tena wa kusema hiki changu na
hiki chako. Kwa kufanya hivyo ni kuujeruhi mwili huu mmoja. Je, jambo hili lina
ukweli katika ndoa yako? Je, ni mambo mangapi ya siri unayoyafanya bila
kumuhusisha mwenzi wako wa ndoa? Je, hujui kwa kufanya hayo unaijeruhi ndoa
yako? Ndugu yangu kama unaishi ukweli huu na kinyume cha sakramenti hiyo ya
ndoa, elewa kwamba ndoa hiyo ishakufua katika uhalisia wa mambo na ukweli wa
Kimungu. Kilicho baki ni maagizo kuu, na wote mmekuwa wasanii katika sakramenti
hii Takatifu.
2. Changamoto kwa watoto na wajibu wao katika familia:
Ni ukweli usiotia shaka
kwamba ni wajibu wetu kuwaheshimu wazazi wetu ikiwa ndiyo amri ya nne ya Mungu.
Tokeo hilo linatupa heri na miaka mingi katika maisha ya umilele. “Amtukuzaye
baba yake ataongezewa siku zake; akimsikiliza Bwana, atamstarehesha mamaye, na
kuwatumikia wazazi wake kama mabwana. Mwanangu,” YbS 3:6-7. Tendo la kuwapenda
wazazi ni haki na linapendeza machoni mwa Mungu. Ni haki kama asemavyo Mtume
Paulo, "enyi watoto, watiini wazazi wenu katika Bwana, maana hii ndiyo
haki," Efe 6:1. Pia tendo hilo lapendeza machoni mwa Mungu, "ninyi
watoto, watiini wazazi wenu katika mambo yote; maana jambo hii lapendeza katka
Bwana," Kol 3:20.
Kwa mantiki hiyo, mtume
Paulo anaenda mbali na kutupa angalisho kuhusu kuwatii wazazi wetu, na kusema,
"maana watu watakuwa wenye kujipenda wenyewe, wenye kupenda fedha, wenye
kujisifu, wenye kiburi, wenye kutukana, wasiotii wazazi wao, wasio na shukrani,
wasio safi," 2 Tim 3:2. Kwa hiyo ndugu yangu jambo hilo ni wajibu, ni shukrani
na ni safi kufanya hivyo. “Mwenye kumdharau baba yake ni mfidhuli, naye mwenye
kumlaani mama yake amekwisha kulaaniwa na Bwana,” YbS 3:16. Kwa upande mwingine wazazi ndiyo vielelezo vya
Mungu wakiwa kama washiriki wa Mungu katika uumbaji. Kazi hii hata Malaika
hakupewa. Ndugu yangu huna Baba zaidi ya Baba uliye naye. Hata kama ni
mwendawazimu huyu ndiye Baba yako na unapomweshimu na kutimiza wajibu wako hapo
ndipo penye chemchemu ya neema zote. “Amheshimuye baba yake atafanya upatanisho
wa dhambi, naye amtukuzaye mama yake huweka akiba iliyo azizi. Amheshimuye
babaye atawafurahia watoto wake mwenyewe, na siku ya kuomba dua atasikiwa,” YbS
3:3-5.
Hivyo ni wajibu wa kila
mtoto katika familia kuwaheshimu, kuwajali na kuwatunza wazazi katika uzee wao.
Tendo hili linakukumbusha kutoa shukrani kwa majitoleo yao katika maisha yako.
“Mwanangu, umsaidie baba yako katika
uzee wake, wala usipate kumhuzunisha siku zote za maisha yake. Akiwa
amepungukiwa na ufahamu umwie kwa upole, wala usimdharau iwapo wewe u mzima
sana,” YbS 3:12-13. Ndugu yangu, namna unavyomjali na kumweshimu mzazi wako ni
kwa namna hiyo hiyo utakavyo heshimiwa na kujaliwa na wanao ufikiapo uzee wako.
Ni vyema ukawekeza kuanzia sasa katika jambo hili la muhimu katika maisha.
3.
Changamoto za wazazi kwa watoto wao, na hasa malezi:
Pamoja na hayo
niliyokwisha kuyasema, wazazi yawapasa kuheshi matakwa ya watoto wao ikiwa ni
pamoja ya ndoa za watoto wao wakijua
wajibu wao wa kimalezi na kuwaacha watoto wao kuwa huru kuchagua mwenzi wake wa
maisha. Pia wapo wazazi wengi wanaowageuza watoto wao kama miradi yao. Kikomo
cha famili na kugawanyika ni pale watoto ndani ya familia wanapofikia kuwa na
familia. Hili mzazi lazima ulijue na ujiandae vizuri hasa kisaikolojia. Hata
kama unampenda vipi mtoto wako huwezi kuzuia asiumwe, asipate matatizo, na wala
asife. Cha kushangaza, unakuta binti kaolewa na mara kwa mara mama mzazi yupo
beneti naye kwenye shughuli zake, biashara zake, bila taarifa ya Mume wa binti
yake. Ndoa ni ya watu wawili. Muwaache. Wewe mama kila mnada unapenda kwenda na
binti yako kwa nini?
Jambo lingine la wazazi
ni manyanyaso kwa mwali wao. Manyanyaso yakimfumo yasiyokwisha. Mnamfanya mwali
wenu kama remote/kiongozea mbali. Anakuwa kama dekio lenu. Mwajiona ndoa yenu
ni bora kuliko ya mwali huyu. Mbona yenu hatuyasemi. Yawezekana wewe ulimpenda
huyo mume wako kwa kipande tu cha muwa. Usicheke! Kinachowaunganisha wawili na
kuwa familia ni fumbo kubwa sana. Hivyo, “Ninyi
akina baba, msiwachokoze watoto wenu, wasije wakakata tamaa,” Kol 3:21.
Waacheni waishi maisha yao. Ni kweli yawezekana kabla ya mtoto wenu kuoa au
kuolewa vimiminika (tumafuta, tusukari, tunyama, tunguo twa mtimba, na hata
tupesa) vilikuwa vingi nyumbani. Baada ya ndoa, hayo yamepungua au kutoweka
kabisa. Je hamjui ya kwamba, "kwa sababu hayo ndiyo mlioitiwa ili mrithi
baraka?" 1Pt 3:9c. Kuyakosa hayo isiwe kero na shiiida kwa ndoa yao.
Ndoa inakuwa na uhai
haya yakizingatiwa kadiri ya mtazamo wa Mtume Petro. "Neno la mwisho ni
hili; mwe na nia moja, wenye kuhurumiana, wenye kupendana kama ndugu, wasikivu,
wanyenyekevu; watu wasiolipa baya kwa baya, au laumu kwa laumu; bali wenye
kubariki; kwa sababu hayo ndiyo mliyoitiwa ili mrithi baraka," 1Pt 3:8-9.
4.
Changamoto za leo kwenye familia, na wajibu wake:
Ndugu yangu, maneno hayo
ni mazito sana kwa wanandoa. Kwa upande wa kina mama, wapo wanaoishi kwenye
ndoa bado hawana utambuzi au tofauti na usichana wao. Mama kwenye ndoa tambua
kwamba kila siku yakupasa "kupungua" kwa ajili ya familia yako
"iongezeke." Familia yaani Baba na watoto wenu waongezeke; upendo,
furaha, afya, akili na mambo mengine
mengi tu. Je, utapunguaje? Mtume Petro anatuambia, "kujipamba kwenu,
kusiwe kujipamba kwa nje, yaani, kusuka nywele; na kujitia dhahabu, na kuvalia
mavazi; bali kuwe utu wa moyoni usioonekana, katika mapambo yasiyo haribika;
yaani roho ya upole na utulivu, iliyo ya thamani kuu mbele za Mungu," 1Pt
3:3-4. Mtume Petro hapa hapingi mama usiende saloon au kutokuvaa vizuri; bali
muelewe kwamba hayo siyo vipauwa mbele katika familia.
Wengi tumetumia muda
mwigi nje badala ya ndani. Vikao kila siku visivyoisha. Sema za kiroho januari
hadi decemba, mikutano ya injili hadi manane ya usiku, nk. Je, saa ngapi
utaijenga nyumba yako? Huku ni kukosa busara kama tunavyoaswa, "Kama pete
ya dhahabu katika pua ya nguruwe, kadhalika mwanamke mzuri asiye na
akili," Mit 11:22. Kwa maana hiyo, "kila mwanamke aliye na hekima
hujenga nyumba yake; Bali aliye mpumbavu huibomoa kwa mikono yake
mwenyewe," Mit 14:1. Wakati mwingine tunamtafuta mchawi wakati mchawi
mwenyewe ndiwe wewe. “Ninyi wake, watiini waume
zenu, kama ipendezavyo katika Bwana. Ninyi
waume, wapendeni wake zenu msiwe na uchungu nao,” Kol 3:18-19. Huu ni wajibu
msingi katika maisha ya ndoa na ufahamu wake.
Wanawake wengi ni wawivu kupindukia. Jua
likichomoza tu utakuta mkeka upo nje. Nikujigalagaza kwenye mkeka kama dagaa wa
kigoma. Masikini wa Mungu labda mumewe alivutiwa na umbo lake la kushikika,
baada ya nusu mwaka afadhali ya mkuyu wa handeni. Licha ndoa ni zaidi ya haya
ya nje, ila nayo huleta matamanio ya kutazama kwingine kama tulipo kuna pazia
na kiza. Elewa mumeo kama ameajiriwa au kujiajiri mwenyewe, awapo huko naye
ameolewa na hiyo kazi yake. Awapo nyumbani anaitaji amani na utulivu. Wanawake
wengi hawana muda wa kuyasoma mapigo ya mioyo ya waume zao. Mmewe akifika
nyumbani tu anadakiwa mlangoni na risala ya mahitaji; utasikia, unajua hakuna
sukari, chumvi, unga, nk. Mpe kwanza nafasi ya kupumzika. Muulize habari za
huko alikotoka. Muulize angependa kupata nini kabla ya ulichoandaa. Wakati
mwingine kuandaa meza anafanya mfanyakazi wa ndani. Au akifanya yeye
utashangaa. Ugali kaupika saa sita mchana
wakati mumewe kafika nyumbani saa kumi jioni. Ugali unatoka jasho tu.
Kwa nin usiandae mboga tu na wakati mumeo anapata chai ukawa unasonga ukali?
Angalia! Huko alikotoka
kila mahali kuna ‘bar’ na nyama choma. Na nyumba nyingi pembezoni mwa barabara
kuna kibao kimeandikwa "vyumba bado vipo." Ni kwa namna hii sebule
ujeuka kuwa kwenye Bar. Pale anahudumiwa vizuri na kwa ujuzi. Huuliwa,
"uncle tukusaidie nini? Anajibu, "bia, kilimanjaro." "Ya
baridi "au ya moto? Mhudumu anasisitiza. Kwa vile nyumbani weshagombana na
mkewe, anajibu, "ya baridi." Tazama binti huyu hakai mbali na mteja
wake. Wewe ulipomwandalia chakula ulirudi kwenye mkeka wako. Binti huyu hukaa
nyuzi 45 hivi. Baba huyu akimeza fundo moja la bia ananyanyua macho anakutana
na tabasam. Kama Baba huyu alikuwa na mpango wa kunywa bia moja huongeza zadi
5. Hapa kwishakuwa sebuleni pake. Nani wa kulaumiwa?
Wanawake wengi huwasema
vibaya sana waume zao. Wengine ufikia hata kuwaita waume zao "vyuma
chakavu," kama nilivyokwisha kusema hapo mwanzo. Onyaneni kindugu tena
mkiwa chumbani.
Baadhi ya wanaume nao
ni balaa! Kumtukana hata kumpiga mkewe mbele za watu au marafiki zake na watoto
ni fursa. Ona matusi hayo anavyoyafyatua kama bomu la skadi. "Mwanamke
gani wewe nimekuokota bar? Bado sijaoa!" Unayasema maneno haya mbele ya
watoto wako. Hata kama ni kweli hubakia maumivu makubwa kwa watoto. Mtume Petro anasema, "ninyi waume, kaeni
na wake zenu kwa akili; na kumpa mke heshima, kama chombo kisicho na nguvu, na
kama warithi pamoja wa neema ya uzima, kusudi kuomba kwenu kusizuiliwe."
1Pt 3:7. Mke wako haitaji ununulie ndege ili awe na furaha. Ni wewe tu kusadifu
kila kitu kidogo anachokifanya nyumbani. Mmefikia hatua ya kuwaita wake zenu
"magoli kipa." Mkimaanisha wao ni kudaka tu! Jambo hili halipendezi
mbele ya Mungu. Nyote wawili yawapasa kusomana tabia na kupongezana kwa kila
kitu mfanyacho kizuri. Mmeo akikununulia kitu kabla ya kukikosoa mpongeze na
kumwambia siku nyingine ukitaka ninunulia kitu itapendeza tukienda sote wawili.
Kiukweli Wanaume hatuna uhalisi wa kuchambua uzuri kama uzuri, tupo zaidi
katika idadi ya kitu au vitu.
Wapendwa wana wa Mungu,
wazazi wetu wana nafasi yao muhimu sana katika maisha yetu kama viumbe
shirikishi katika uumbaji na Mungu, mahusiano yetu kimaagano yana nafasi yake
katika umilele wetu, na hivyo isiwe sababu ya kudharau au kukengeuka na
kuwakana wazazi wetu. Mwisho yatupasa kujua wajibu wetu kwa wazazi, maisha yetu
ya kimaagano kila mmoja kadiri ya wito wake, na kusudi la kuumbwa wetu na uwepo
wetu hapa duniani. Yote haya ni maandalizi ya maisha ya umilele, kama ilivyo
amri ya nne wa Mungu, “Waheshimu baba yako na mama yako; siku zako zipate kuwa
nyingi katika nchi upewayo na Bwana, Mungu wako,” Kut 20:12
Kijana
Felix aliyemaliza masomo yake ya udaktari alibahatika kumwoa mwanamke mwenye
elimu kama yake. Mwanamke huyu alijipenda sana kupita kiasi kutokana na
mazingira ya makuzi yake. Ni kweli alitoka familia yenye pesa na tajiri sana.
Felix
alitoka familia masikini sana, na soma yake ilikuwa ya shida sana. Felix
alifika hapa alipo kwa kutegemea biashara ndogo ndogo za mama yake mzazi. Baba
yake Felix alifariki muda mrefu, Felix angali darasa la pili.
Akiwa ameajiriwa
na kuwa na mji wake, mama yake mzazi alipenda kumtembelea mtoto wake. Kwa
bahati mbaya au nzuri Mama yake Felix alifika na kumkuta mke wa mtoto wake. Kwa
namna alivyokuwa mama yake Felix, mke wa Felix alikuwa na mashaka naye kwani
alionekana kama ombaomba fulani hivi. Hata kwa kujitambulisha kote kule mke wa
felix hakuweza kumpokea vizuri na kulazimika kumwifadhi moja ya vyumba vya
stoo.
Alipofika
Felix kutoka kazini mkewe alimwambia ujio wa mwanamke mmoja mchafu na waajabu
kutokea, na kusema, “eti mama huyo hapa stoo anasema kuwa wewe ni mwanaye.”
Felix kwa aibu naye hakumpokea vizuri mama yake, na ndipo ugomvi ulipoanzia.
“Kama unasema kuwa wewe ni mama yangu piga mahesabu ya gharama zote
ulizonitunza na kunilea nami nitakulipa,” Felix alimwambia mama yake kwa
hasiri.
“Naombeni
munionyeshe uhani nami nikirudi nitakupa hesabu yangu,” mama yake Felix mjibu
Felix. Baada ya muda kidogo mama yake Felix alirudi akiwa amejipaka kinyesi
chake mwili mzima na kumwambia Felix, “haya naomba uniogeshe na hii ndiyo
gharama yangu kwa siku moja tu katika utoto wako. Kutokana na harufu ile, Felix
hakuweza hata kumsogelea Mama yake. Je, Yesu angemlipa nini Mama yake kwa
mahangaiko aliyoyapata hadi chini ya msalaba alipokata roho? Yesu anamkabidhi
mama yake Kanisa na kusema, “Mama tazama mwanao.” Je, watambua nafasi yako
katika familia?
Tumsifu
Yesu Kristo!
“Mwanangu, wakati wa kufanikiwa
uendelee katika unyenyekevu; hivyo utapewa kuliko mwenye ukarimu,” YbS 3:17
Tusali:-Ee
Yesu Mwema, tujalie amani ya kweli, upendo na tulizo kwenye familia zetu ambazo
leo hazipo tayari kutaabikiana. Amina
Familia Takatifu ya Yesu, Maria, na
Yosefu, Mtuombee.