JUMAPILI
YA 4 YA MAJILIO YA MWAKA C
20/12/2015
Somo
I: Mik 5:2-5a
Zab:
80:2-3, 15-16, 18-19
Somo
II: Ebr 10:5-10
Injili:
Lk 1:39-45
Nukuu:
“Bali wewe, Bethlehemu Efrata, uliye mdogo kuwa miongoni mwa
elfu za Yuda; kutoka kwako wewe atanitokea mmoja atakayekuwa mtawala katika
Israeli; ambaye matokeo yake yamekuwa tangu zamani za kale, tangu milele,” Mik
5:2
“Kwa sababu hiyo atawatoa, hata wakati wa kuzaa kwake aliye na
utungu; ndipo hayo mabaki ya nduguze watawarudia wana wa Israeli,” Mik 5:3
“Naye atasimama, na kulisha kundi lake kwa nguvu za Bwana, kwa
enzi ya jina la Bwana, Mungu wake; nao watakaa; maana sasa atakuwa mkuu hata
miisho ya dunia” Mik 5:4
“Na mtu huyu atakuwa amani yetu,” Mik 5:5
“Kwa hiyo ajapo
ulimwenguni, asema, Dhabihu na toleo hukutaka, Lakini mwili uliniwekea tayari; Sadaka za kuteketezwa na sadaka za
dhambi hukupendezwa nazo,” Ebr 10:5-6
“Katika mapenzi hayo
mmepata utakaso, kwa kutolewa mwili wa Yesu Kristo mara moja tu,” Ebr 10:10
“Ikawa Elisabeti aliposikia kule kuamkia kwake Mariamu, kitoto
kichanga kikaruka ndani ya tumbo lake; Elisabeti akajazwa Roho Mtakatifu,” Lk
1:41
“akapaza sauti kwa nguvu akasema, Umebarikiwa wewe katika
wanawake, naye mzao wa tumbo lako amebarikiwa,” Lk 1:42
“Limenitokeaje neno hili, hata mama wa Bwana wangu anijilie
mimi?” Lk 1:43
“Naye heri aliyesadiki; kwa maana yatatimizwa aliyoambiwa na
Bwana,” Lk 1:45
TAFAKARI:
“Limenitokeaje neno hili, hata mama wa Bwana wangu
anijilie mimi?”
Wapendwa wana wa Mungu,
Leo Mama Kanisa anaadhimisha Dominika ya 4 ya Majilio ya Mwaka “C” wa Kanisa.
Ujumbe wa leo umebeba ustaajabivu na upekee wa maamkio ya Mama Bikira Maria kwa
familia hii ya Yohane. Maamkio haya ni ya pekee kwa sababu yamebeba fumbo zima
la kumwilishwa kwa Neno na kukaa kwetu. Maamkio mengine ya Mungu katika
historia ya wokovu yalikuwa na mtazama wa “kutembelea” tu na siyo “kukaa nasi.”
Maandiko Matakatifu yanaonyesha ukweli huu na hasa maneno haye, “Maana Bwana asema hivi, Babeli
utakapotimiziwa miaka sabini, nitawajilia ninyi, na kulitimiza neno langu jema
kwenu, kwa kuwarudisha mahali hapa,” Yer 29:10. Hapa tunaona “kujiliwa” tu na
si “kukaa.”
Maamkio ya mwisho ya Mungu kwa tendo hili la kumwilishwa ni
kwa wale walio wake. “Atukuzwe Bwana, Mungu wa Israeli, Kwa kuwa amewajia watu wake,
na kuwakomboa,” Lk 1:68. Masiha huyu
lazima atoke kwa watu wake, na awe kwa ajili yao. Tendo hili linawapa watu hofu
ya Mungu na hivyo kwa vinywa vyao hukiri makuu ya Mungu. “Hofu ikawashika wote, wakamtukuza Mungu, wakisema, Nabii mkuu
ametokea kwetu; na, Mungu amewaangalia watu wake,” Lk 7:16. Hiki ndicho
kilichompata Elizabeti baada ya Maamkio ya Bikira Maria. Naye Elizabeti “akapaza sauti kwa nguvu
akasema, Umebarikiwa wewe katika wanawake, naye mzao wa tumbo lako
amebarikiwa,” Lk 1:42. Familia hii ya Zakaria na Elizabeti ndiyo ya kwanza
kushiriki ugeni huu na kutembelewa huku na Mungu.
Tendo
hili la kuamkiana huku hakuonyeshi tu ukawaida wa kuwasiliana, bali kuna beba
mawasiliano ya kiroho ndani yake. “Ikawa Elisabeti aliposikia kule kuamkia kwake Mariamu, kitoto
kichanga kikaruka ndani ya tumbo lake; Elisabeti akajazwa Roho Mtakatifu,” Lk
1:41. Haya ni makutano ya mara ya kwanza ya kiroho kati ya Neno aliyemwishwa,
yaani mtarajiwa Yesu Kristo, na Mtarajiwa Yohane. Kwa namna nyingine tunaweza
kusema utendaji wa Roho Mtakatifu unajionyesha hapa, na kwa njia hiyo wote
wawili yaani Yesu na Yohane wataongozwa na Roho huyo katika safari nzima ya
wokovu, ambayo Kristo ndiye ukamilifu wake.
Hakuna
shaka yoyote kwamba ziara hii ya Bwana katika familia hii ya Yohane Mbatizaji imewezeshwa kwa upande mmoja
na Bikira Maria, Mama wa Yesu. Kwa tendo hili Bikira Maria anaunganishwa pamoja
katika ziara ya wokovu wa Bwana kwa watu wake. Ni unganiko la umoja uliobeba
“Umama” ndani yake. Unganiko hili linaendelea kwa watu wote na hasa maisha ya
Kanisa. Kanisa kama ‘Mama’ linabeba ujumbe huu kama Bikira Maria alivyoubeba,
Neno kumwilishwa na kukaa kwetu. Kanisa linakuwa Sakramenti ya wokovu wetu. Ni
kwa maana hiyo Kanisa kama Sakramenti ya wokovu, ambayo ni mwili wa Kristo,
fadhila hizi za Kristo; {upendo, ukarimu, utii, unyenyekevu, msamaha, huruma,
upole, amani} hulidhihirisha Kanisa pale lilipo.
Hivyo
Kristo mwana wa Mungu ni wokovu na hatenganishwi na ujumbe huu wa wokovu hapa
duniani. Na Kanisa ikiwa ni mwili wake Kristo, wokovu ndiyo msingi wa uwepo
wake leo na sasa na hata mwisho wa nyakati. Hivyo ujumbe huu ni furaha na amani
kwetu kwa sababu kwa njia ya Kanisa wokovu unapatikana. Hivyo Kanisa lina
wajibu mmoja tu wa kufanya, yaani mapenzi ya Mungu ikiwa ndiyo msingi na kielelezo
cha wokovu wetu, na mwisho kufikia
maisha ya umilele. Na kwa namna hiyo, “Katika mapenzi hayo
mmepata utakaso, kwa kutolewa mwili wa Yesu Kristo mara moja tu,” Ebr 10:10.
Sadaka yake na majitoleo yake yanatosha. Kristo ndiye utimilifu wa yote katika
yote.
Wapendwa wana wa Mungu, Masiha wetu “kwa hiyo ajapo ulimwenguni, asema, Dhabihu na toleo hukutaka,
Lakini mwili uliniwekea tayari; Sadaka
za kuteketezwa na sadaka za dhambi hukupendezwa nazo,” Ebr 10:5-6. Kwa maana
nyingine uwepo wa Kristo ambao ni uwepo wa Mungu katika maisha yetu unatosha.
Maisha ya Kristo na sadaka yake pale Msalabu ulifuta sadaka zote na kwa sadaka
yake ilikuwa kielelezo cha sadaka hai zote, na wokovu na uzima wetu. Kwa hiyo
uwepo wake Kristo ambao ni uwepo wa
Kanisa ni kufanya mapenzi ya Mungu. Huu ndio wito wa Kanisa.
Kwa hiyo wapendwa wana wa Mungu, tunapokaribia
fumbo hili la kumwilishwa kwa Neno na kukaa kwetu, tutambue kwamba licha ya
udogo wetu, udhaifu wetu, mapungufu yetu,
na unyonge wetu, sasa ni wakati wa kuinuliwa kwetu kutoka katika utumwa
wa dhambi na kuwa watu wapya. Mungu anapenda kuanza upya na kila mmoja wetu na
kuusimika ufalme wake milele. Nabii Mika nawaambia wana wa Israeli, “Bali wewe, Bethlehemu Efrata, uliye mdogo kuwa
miongoni mwa elfu za Yuda; kutoka kwako wewe atanitokea mmoja atakayekuwa mtawala
katika Israeli; ambaye matokeo yake yamekuwa tangu zamani za kale, tangu
milele,” Mik 5:2. Huyo atakayechomolewa kutoka katika Taifa hili la Israeli,
atasimama na kulilisha kundi lake kwa nguvu za Bwana. “Naye atasimama, na kulisha kundi lake kwa nguvu za Bwana, kwa
enzi ya jina la Bwana, Mungu wake; nao watakaa; maana sasa atakuwa mkuu hata
miisho ya dunia” Mik 5:4. Utawala wake siyo kwamba utaleta amani tu, bali Yeye
mwenyewe ni Amani. “Na mtu huyu atakuwa amani yetu,” Mik 5:5.
Wapendwa katika Kristo,
utendaji wa Mungu ni wa ajabu sana! Uteuzi wake hauna upendeleo hata kidogo.
Ila jambo ambalo lililo wazi ni hili; Mungu hupenda kuwainua wanyonge na hasa
wale waliodharauliwa, na wakati huo huo kuwanyenyekesha wale wote wanaojiinua
na kujikweza. Historia nzima ya wokovu wetu inaufunua ujumbe huu wa Mungu. Embu
watazama watu hawa; Zakaria, Elizabeti, Manoa na Mke wake, Samsoni, Mariamu, na
wengine wengi tu, walikuwa watu wa kawaida kabisa na wakati mwingine
walidharauliwa kutoka na mtindo wa maisha yao na mitazamo ya nyakati. Ila Mungu
hupenda kuvitumia vile vilivyodhaifu na kuvinyeyekeza vile vijikwazavyo.
Mawazo haya ya Mungu na
utendaji wake unanikumbusha tukio moja kutoka kijiji cha jirani. Familia ya
Mzee Kichaka ilijulikana sana kwa kazi za vibarua vya kulima kwenye mashamba ya
majirani zake ambo kwa kiasi kikuwa walikuwa matajiri sana. Hivi ndivyo
ilivyokuwa namna yao ya kuishi kwa familia. Thadei ni mmoja ya watoto wa mzee
kichaka ambaye alifaulu kwenda seminari baada ya elimu ya msingi kati ya watoto
wake saba. Kwenda kwa Thadei seminarini halikuwa jambo la ajabu sana kwani
ilionekana wazi hatoweza kufika popote kwa mwono wa familia yake ukilingaisha
na familia zilizobahatika kuwa na Mapadre katika kijiji kile. Hivyo hakuna
yeyote aliyekuwa na wazo kama inawezekana hilo kutokea kwenye familia ya Mzee
Kichaka.
Thadei alisomeshwa kwa
kazi hiyo ya vibarua na hata alipokuwa likizo aliendelea kufanya kazi hiyo na
wazazi na ndugu zake. Kwa vile Mungu kamwe siyo Edgar, na hubaki kuwa Mungu,
muda ulipita na bila watu kufahamu walipata taarifa za ushemasi wa Thadei.
Hakuna aliyeamini! Basi ushemasi ulifanyika kwa shidashida tu. Maandalizi ya
Upadrisho yalianza kwa ndugu na jamaa kujipiga hapa na pale. Kwa kweli ilikuwa
shida sana. Hata hivyo alipata daraja lake la Upadre.
Basi siku ile ya Misa
yake ya Shukrani, kila kitu kiliazimishwa kutoka kwa majirani. Mama yake mzazi
alienda kwa jirani yake kuomba sufuria kubwa kwa ajili ya maandalizi ya
chakula. Jirani yake ambaye naye alikuwa na mtoto aliyekwenda seminari ila
hakufanikiwa kufika mwisho wa safari yake, alimjibu ‘Mama Padre Thadei’ hivi,
“siwezi kukupa sufuria langu. Kama uliweza kumsomesha mwanao hadi kufikia kuwa
Padre, umeshindwa nini kununua sufuria?” Mama yake Padre Thadei aliondoka kama kamwagiwa maji.
Wapendwa wana wa Mungu,
Mungu wetu ni waajabu sana. Hufanya njia pasipo njia. Tunapoyaona haya basi
tusema tu kama alivyosema Elizabeti. “Limenitokeaje neno hili, hata mama wa Bwana wangu
anijilie mimi?” Lk 1:43. Mawazo ya Mungu na utendaji wake si kama mawazo yetu
na utendaji wetu. Mwisho wa siku, sifa na shukrani zimrudie Mungu mwenyewe kwa
sababu yote huyafanya kwa lengo lake na lenye uzima ndani yake. Mama Bikira
Maria anatufundisha namna ya kusema tunapoyaona mambo makuu katika maisha yetu:
“Kwa kuwa ameutazama Unyonge wa mjakazi wake. Kwa kuwa Mwenye nguvu amenitendea
makuu, Na jina lake ni takatifu,” Lk 1:48a, 49
Tusifu
Yesu Kristo!
“Ee Bwana, jinsi yalivyo makuu matendo yako! Mawazo yako ni
mafumbo makubwa,” Zab 92:5
No hay comentarios:
Publicar un comentario