lunes, 14 de diciembre de 2015

TAFAKARI: JUMANNE WIKI YA 3 YA MAJILIO-C

JUMANNE WIKI YA 3 YA MAJILIO-C
15/12/2015
Somo: Sef 3:1-2, 9-13
Zab: 34:2-3, 6-7, 17-18, 19, 23
Injili: Mt 21:28-32
Nukuu:
Siku ile hutatahayarikia matendo yako yote uliyoniasi; maana hapo nitawaondoa watu wako wanaotakabari na kujivuna, wasiwe kati yako, wala hutatakabari tena katika mlima wangu mtakatifu,” Sef 3:11 

Lakini nitasaza ndani yako watu walioonewa na maskini, nao watalitumainia jina la Bwana,” Sef 3:12 

Mabaki ya Israeli hawatatenda uovu, wala kusema uongo; wala ulimi wa hadaa hautaonekana kinywani mwao; kwa maana watakula na kulala, wala hapana mtu atakayewaogofya,” Sef 3:13

“Basi Yesu akawaambia, Amin nawaambia, watoza ushuru na makahaba wanatangulia mbele yenu kuingia katika ufalme wa Mungu,” Mt 21:31b 

Kwa sababu Yohana alikuja kwenu kwa njia ya haki, ninyi msimwamini; lakini watoza ushuru na makahaba walimwamini, nanyi hata mlipoona, hamkutubu baadaye, ili kumwamini,” Mt 21:32 

TAFAKARI:Watoza ushuru na makahaba wanatangulia mbele yenu kuingia katika ufalme wa Mungu.”

Wapendwa wana wa Mungu, kutangulia au kuchelewa kwa kuwa na ufahamu wa Mungu hakuna maana yoyote kama katika tendo hilo hatutimizi mapenzi ya Mungu. Mfano alioutoa Yesu kwenye Injili ya leo unathibitisha ukweli huo niliousema. Mtoto wa kwanza katika familia ile aliambiwa na Baba yake kwenda kufanya kazi shambani akakubali hata hivyo hakwenda. Mtoto wa pili alikataa kwenda kufanya kazi shambani, ila baada ya kujifikiria akafanya toba na kwenda kufanya kazi shambani. Mtoto huyu wa pili anawakilisha watoza ushuru na makahaba ambao kwa uhakika kwa kutubu kwao kadiri ya Injili ya leo wataingia katika ufalme wa Mungu.

Watoza ushuru na Makahaba hawakuwa na mwono mzuri nyakati zile za Yesu kutokana na matendo yao. Watoza ushuru walichukiwa sana kutoka na kodi waliyoitoza ambayo kwa kiasi kikubwa haikuhakisi maisha ya watu. Ilikuwa kodi ya dhuluma na iliyojaa unyanyasaji hasa kwa wanyonge. Makahaba hawakupendwa kutokana na mtindo wa maisha yao. Kwa ujumla makahaba walionekana kuwa najisi kabisa, na wachafu kupindukia. Kumbe kwa kutubu kwao bado wananafasi ya kuhesabiwa haki na Mungu. Na hii ndiyo sababu ya Yesu kuyasema maneno haya, Amin nawaambia, watoza ushuru na makahaba wanatangulia mbele yenu kuingia katika ufalme wa Mungu,” Mt 21:31b.

Yesu hayasemi maneno haya kwa Wakuu wa Makuhani, Waandishi, na Mafarisayo kwa kuwasingizia, bali hali halisi ilijionyesha pale walipojiinua kupita kiasi na hata kuchukua nafasi ya Mungu. Watu hawa walionekana kama miungu watu. Walikuwa wepesi kusema maneno mengi na mazuri bila wao wenyewe kutenda. Hakika walikuwa wanafiki sana. Yesu anasema, Waandishi na Mafarisayo wameketi katika kiti cha Musa; basi, yo yote watakayowaambia, myashike na kuyatenda; lakini kwa mfano wa matendo yao, msitende; maana wao hunena lakini hawatendi,” Mt 23:2-3. Mtazamo huu wa Dini ulipoteza msingi wake ambao ni maisha kuelelea uzima wa milele. Kila kitu kilionekana kubeba mitazamo ya kibinadamu na kusahau kwamba yote bila Mungu ni ubatili mtupu. Ni kwa maana hiyo basi siku ya mwisho mimi na wewe tutapigwa mshangao kama asemavyo Yesu, Yohana alikuja kwenu kwa njia ya haki, ninyi msimwamini; lakini watoza ushuru na makahaba walimwamini, nanyi hata mlipoona, hamkutubu baadaye, ili kumwamini,” Mt 21:32.  Ni vyema kila mmoja wetu akachunguza njia zake na mahusiano yake na Mungu.

Wapendwa wana wa Mungu, ufuasi wetu kwa Kristo siyo kitu cha majaribu. Jambo hili halina lele mama. Ni aheri kuwa baridi au joto kuliko kuwa vuguvugu katika imani ndani na katika Kristo. Yesu anaweka wazi kweli iliopo tunapotaka kumfuata na kuwa wanafunzi wake. Mambo yalikuwa kama ifuatavyo; “Mwingine katika wanafunzi wake akamwambia, Bwana, nipe ruhusa kwanza, niende nikamzike baba yangu. Lakini Yesu akamwambia, Nifuate; waache wafu wazike wafu wao,” Mt 8:21-22. Ufuasi wetu ndani na katika Kristo utasababisha wakati mwingine kuachana na mazoea yaliyojengeka kadiri ya mila na desturi zetu. Kumfuata Kristo ni kufuata utamaduni mwingine usio wa kawaida. Hakuna mfananano wa tamaduni nyingine za kibinadamu. Na hakuna tamaduni au mila fulani inayoweza kujigamba kwamba kwayo ni zoefu katika tamaduni hii mpya ya Kristo. Sote tu wanafunzi wa Yesu hadi kifo. Kila siku ni siku ya kujifunza yaliyo mapya anayotufunulia Kristo mwenyewe. Yesu analisema hili kama ifuatavyo: Mtu mwingine pia akamwambia, Bwana, nitakufuata; lakini, nipe ruhusa kwanza nikawaage watu wa nyumbani mwangu. Yesu akamwambia, Mtu aliyetia mkono wake kulima, kisha akaangalia nyuma, hafai kwa ufalme wa Mungu,” Lk 9:61-62. Hivyo ni kuanza upya na Kristo, na kuwa wapya kila siku tunapoongozana naye.

Ufuasi huu unatulazimu kwa hiari yetu kuyakabidhi yote mikononi mwa Kristo. Hatuendi kwake nusunusu na kubaki na yaliyo yetu. Kumfuata Yesu ni kujisalimisha bila kujibakiza. Yesu anasema, Wala mtu asiyechukua msalaba wake akanifuata, hanistahili. Mwenye kuiona nafsi yake ataipoteza; naye mwenye kuipoteza nafsi yake kwa ajili yangu ataiona. Mt 10:38-39. Kumbe sharti la kwanza tena la hiari ni kuchukua msalaba wako, yaani, kuyajua madhaifu yako na kuyachukua kama sehemu muhimu ya kuupata wokovu wako utakapo yashinda ndani na katika Kristo. Pili, kujiachia kwa Kristo bila kujibakiza ili kuiona nafsi yako.

Ufuasi huu pia unatutaka kuishi katika mfumo wa moja na ibaki kuwa moja, katika maana ya kujua ni nani hasa upasaye kumtumikia. Hapa Michanganyo hairuhusiwi hata kidogo. Kweli na uongo hapa haviivi chungu kimoja. Hivyo Yesu anasema, Hakuna mtu awezaye kutumikia mabwana wawili; kwa maana atamchukia huyu, na kumpenda huyu; ama atashikamana na huyu, na kumdharau huyu. Hamwezi kumtumikia Mungu na mali,” Mt 6:24. Kumbe kumfuata Yesu yakupasa kuamua kati ya haya yanayoonekana na kushikika ila ni ya muda tu, au kisichoonekana kwa urahisi na kisichoshikika ila kina uzima wa milele.

Ufuasi huu unatulazimu kutobandukana na Kristo hadi mwisho wa kiama. Kumbe ufuasi wangu usiwe ule wa jumapili tu na matukio mengine ya Kanisa. Siku zote na majira yote yanipasa kuishi ndani na katika Kristo. Naye Yesu anasema, Mtu ambaye si pamoja nami yu kinyume changu; na mtu asiyekusanya pamoja nami hutawanya,” Lk 11:23. Kumbe kuwa mkristu wa jina tu bila kuishi ahadi zako za ubatizo, ukristo wako hauna maana yoyote wala faida yoyote.Mtu asipokaa ndani yangu, hutupwa nje kama tawi na kunyauka; watu huyakusanya na kuyatupa motoni yakateketea,” Yoh 15:6. Hatuna uzima wa kiroho bila kuwa ndani na katika Kristo Yesu. Hatuwezi pia kukua kiroho na kimwili kama hatuna muunganiko ndani na katika Kristo Yesu.

Wapendwa wana wa Mungu, huyu ndiye Masiha tunayemsubiri. Ujio wake watupasa kuwa tayari, yaani katika hali isiyo ya dhambi. Leo yako isisubiri kesho ili ujiandae. Kesho hiyo hujaifikia, na jana yako ilishapita bila kufanya chochote. Hivyo, Siku ile hutatahayarikia matendo yako yote uliyoniasi; maana hapo nitawaondoa watu wako wanaotakabari na kujivuna, wasiwe kati yako, wala hutatakabari tena katika mlima wangu mtakatifu,” Sef 3:11. Aliyejiandaa ndiye atakaye kuwa mikono salama ya Mungu. Kundi hili ni lile la wenye hofu ya Mungu, Masikini na walioonewa. Lakini nitasaza ndani yako watu walioonewa na maskini, nao watalitumainia jina la Bwana,” Sef 3:12

Wenye hofu ya Mungu na wanyenyekevu wa moyo, hawana woga wala hofu kwa sababu maisha yao yapo mikononi mwa Mungu. Nabii Sefania anawataja watu hawa kwa kusema, Mabaki ya Israeli hawatatenda uovu, wala kusema uongo; wala ulimi wa hadaa hautaonekana kinywani mwao; kwa maana watakula na kulala, wala hapana mtu atakayewaogofya,” Sef 3:13. Hawa wanajua ni nani wanayemtumikia. Mungu huyu wa kweli na hai hatotuangusha kamwe tunapojitoa kwake bila kujibakiza.

Tumsifu Yesu Kristo!

Mwe na hofu wala msitende dhambi, Tafakarini vitandani mwenu na kutulia,” Zab 4:4


No hay comentarios:

Publicar un comentario