jueves, 3 de diciembre de 2015

TAFAKARI: IJUMAA WIKI YA 1 YA MAJILIO MWAKA-C

IJUMAA WIKI YA 1 YA MAJILIO
4/12/2015
Somo: Isa 29:17-24
Zab: 27:1, 4, 13-14
Injili: Mt 9:27-31
Nukuu:
Na katika siku hiyo viziwi watasikia maneno ya hicho chuo, na macho ya vipofu yataona katika upofu na katika giza,” Isa 29:18

Wanyenyekevu nao wataongeza furaha yao katika Bwana, na maskini katika wanadamu watafurahi katika Mtakatifu wa Israeli,” Isa 29:19

Kwa maana mwenye kutisha ameangamizwa, naye mwenye dharau amekoma, nao wote watazamiao uovu wamekatiliwa mbali; hao wamfanyao mtu kuwa amekosa katika neno, na kumtegea mtego yeye aonyaye langoni, na kumgeuza mwenye haki kwa kitu kisichofaa,” Isa 29:20-21

Basi, Bwana aliyemkomboa Ibrahimu asema hivi, katika habari za nyumba ya Yakobo; Yakobo hatatahayarika sasa, wala uso wake hautabadilika rangi yake,” Isa 29:22

vipofu wawili wakamfuata wakipaza sauti, wakisema, Uturehemu, Mwana wa Daudi,” Mt 9:27

Naye alipofika nyumbani, wale vipofu walimwendea; Yesu akawaambia, Mnaamini kwamba naweza kufanya hili? Wakamwambia, Naam, Bwana,” Mt 9:28

Ndipo alipowagusa macho, akasema, Kwa kadiri ya imani yenu mpate,” Mt 9:29

Macho yao yakafumbuka. Naye Yesu akawaagiza kwa nguvu, akisema, Angalieni hata mtu mmoja asijue,” Mt 9:30

TAFAKARI: “Mnaamini kwamba naweza kufanya hili? Kwa kadiri ya imani yenu mpate.”

Wapendwa wana wa Mungu, tukiachana na yote yale mazuri yaletwayo na Masiha wetu katika tuonavyo katika somo letu la kwanza kutoka kitabu cha Nabii Isaya, ni vyema tukajikita katika kuviondoa vilema vyetu na mapungufu yetu ili tuufaidi ujio wa Masiha. Huu ndio wito wa kipindi hiki cha Majilio. Hivyo leo tuangalie kwa undani juu ya mahangaiko yetu na mateso ambayo kwa kiasi kikubwa yanatutoa katika mwelekeo mzima wa Imani ya kweli. Ni kwa kadiri ya Imani yetu tutapata yale tuyaombayo.

Bila shaka wewe ni mmoja wa wale ambao kwa namna mmoja au nyingine umekuwa ukizunguka kila kona ukitafuta suluhu la tatizo lako bila mafanikio. Hakuna shaka pia kwa tatizo hilo au matatizo hayo umeshasali kila aina ya sala na novena bila mafanikio. Kwa mtiririko huu naona pia unavyoangaika kutafuta majibu ya matatizo yako kutoka kanisa moja kwenda lingine, toka mchungaji mmoja kwenda mwingine bila mafanikio yenye utulivu wa kutosha. Naona unavyoshawishika kufanya ibada za giza kwa maagizo ya waganga wa kienyeji kupitia marafiki zako unaowaamini.

Wapendwa katika Kristo, leo Yesu anakuambia wewe na mimi maneno haya ya uzima kama alivyowaambia wale vipofu waliotaka kuona tena; “Mnaamini kwamba naweza kufanya hili? Kwa kadiri ya imani yenu mpate.” Swali hili analotuuliza leo Yesu ni swali la msingi sana. Wengi wetu ni wakristo wa majina na zaidi sana ni wakrito wa jumapili. Dini na Imani ya wengi imekuwa kama kautaratibu fulani kitumikacho kama utambulisho wa kawaidi katika mtukio fulani ya maisha, na kisicho sema chochote kuhusu undani wa maisha wa mtu huyo. Licha ya kwamba mtu akiwa amebanwa na tatizo kubwa huweza kutekeleza ushauri wowote apewao, ni vyema kusimama katika Imani dhabiti bila kuterereka. Naye alipofika nyumbani, wale vipofu walimwendea; Yesu akawaambia, Mnaamini kwamba naweza kufanya hili? Wakamwambia, Naam, Bwana,” Mt 9:28. Yote hutendwa ndani yetu kwa uzito  ule ule tulionao kuhusu kile tuaminicho. Ndipo alipowagusa macho, akasema, Kwa kadiri ya imani yenu mpate,” Mt 9:29.

Mungu ana lengo kwa kila tatizo. Yeye hutumia mazingira kukuza tabia yetu kwa kweli. Yeye hutegemeza zaidi mazingira katika kutufanya tufanane na Kristo. Ukweli ni kwamba unakabiliwa na mazingira masaa ishirini na nne kila siku. Yesu alituonya kwamba tutakuwa na matatizo ulimwenguni. Hayo nimewaambieni mpate kuwa na amani ndani yangu. Ulimwenguni mnayo dhiki; lakini jipeni moyo; mimi nimeushinda ulimwengu,” Yoh 16:33. Hakuna aliye sugu kwa matatizo au amefunikwa asipatwe na mateso, wala hakuna aliye huru mbali na matatizo katika maisha. Maisha ni mfululizo wa matatizo. Kila unapotatua moja, jingine linasubiri kutokea. Si yote makubwa, lakini yote yana maana kwa Mungu katika kukuza tabia yako. Petro anatuhakikishia kwamba mtatizo ni ya kawadia, Wapenzi, msione kuwa ni ajabu ule msiba ulio kati yenu, unaowapata kama moto ili kuwajaribu, kana kwamba ni kitu kigeni kiwapatacho,” 1Pet 4:12.

Mungu anatumia matatizo kukusogeza karibu yake.Bwana yu karibu nao waliovunjika moyo, Na waliopondeka roho huwaokoa,” Zab 34:18. Ndugu yangu, wakati wako mzuri wa kuwa na ibada ya karibu na Mungu unaweza kuwa siku zile za giza sana-moyo wako unapokuwa umepondeka, unapohisi kuachwa, unapokuwa huna uchaguzi, maumivu yanapokuwa makubwa-na unamgeukia Mungu peke yake. Ni wakati wa taabu ndipo tunajifunza kusali sala za kweli na uaminifu kutoka moyoni. Tunapokuwa katika maumivu, hatuna nguvu za sala za juu juu. Maisha yakiwa ya raha, tunaweza kumfahamu Yesu juu juu tu, tukimwiga na kumnukuu na kusema juu yake. Lakini ni katika taabu ndipo tutamjua Yesu. Tunajifunza mambo katika mateso, mambo ambayo hatuwezi kujifunza kwa njia nyingine yeyote.

Mungu angeweza kuzuia Yusufu asitiwe gerezani, Mwa 39:20-22. Mungu angezuia Danieli asitupwe kwenye shimo la simba, Dan 6:16-23. Mungu angezuia Yeremia asitupwe katika shimo la matope, Yer 38:6. Mungu angezui Paulo asivunjikiwe na jahazi mara tatu, 2Kor 11:25. Na Mungu angewazuia vijana watatu Waebrania wasitupwe katika tanuru la moto, Dan 3:1-26. Pamoja ha hali hiyo Mungu hakufanya hivyo. Aliruhusu matatizo hayo kutokea, na matokeo yake kila mmoja wao alimsogelea Mungu karibu zaidi.

Matatizo hutulazimisha kumtazama Mungu na kumtegemea badala ya nafsi zetu wenyewe. Mtume Paulo anashuhudia faida hii. “Naam, sisi wenyewe tulikuwa na hukumu ya mauti katika nafsi zetu ili tusijitumainie nafsi zetu, bali tumtumaini Mungu, awafufuaye wafu,” 2Kor 1:9. Kamwe hutajua kwamba unachohitaji ni Mungu tu mpaka pale utakapojikuta umebaki na Mungu tu. Bila kujua chanzo, hakuna tatizo lolote linaloweza kukupata bila ruhusa ya Mungu. Kila kinachotokea kwa mtoto wa Mungu kinachujwa na Baba, na amekusudia kukitumia kuleta mema ingawa Shetani na watu wengine wanakusudia mabaya.

Kwa kuwa Mungu anatawala yote, ajali ni matukio tu katika mpango mzuri wa Mungu kwa ajili yako. Kwa sababu kila siku ya maisha yako iliandikwa kwenye kalenda ya Mungu kabla hujazaliwa. Macho yako yaliniona kabla sijakamilika; Chuoni mwako ziliandikwa zote pia, Siku zilizoamriwa kabla hazijawa bado,” Zab 139:16. Hivyo kila kinachotoka kwako kina umuhimu wa kiroho. Kila kitu! Nasi twajua ya kuwa katika mambo yote Mungu hufanya kazi pamoja na wale wampendao katika kuwapatia mema, yaani, wale walioitwa kwa kusudi lake. Maana wale aliowajua tangu asili, aliwachagua tangu asili wafananishwe na mfano wa Mwana wake, ili yeye awe mzaliwa wa kwanza miongoni mwa ndugu wengi,” Rum 8:28-29 

Wengi wetu hiki kifungu (Rum 8:28-29) hukinukuu na kukieleza vibaya. Hakisema, “Mungu husababisha kila kitu kufanya kazi kama ninavyopenda mimi.” Wala hakisemi, “Mungu husababisha kila kitu kufanya kazi ili kuleta maisha ya furaha duniani.” Hiii si kweli pia kuna miisho ya huzuni duniani. Tunaishi katika ulimwengu ulioanguka. Ni mbinguni tu ndiko mambo yanatendeka kikamilifu kama Mungu alivyokusudia. Ndiyo maana katika sala ya Baba Yetu tumeelezwa kusali, Mapenzi yako yatimizwe, hapa duniani kama huko mbinguni,” Mt 6:10. Ili kuelewa vyema kifungu hicho kutoka Barua ya Mtume Paulo kwa Warumi ni vyema tuangalie kwa makini kila fungu la maneno.

“Twajua:” Tumaini letu wakti wa magumu hutegemea kufikiri chanya, kufikiri kwa kutarajia, au kule kutegemea mazuri kwa kawaida. Huu ni uhakika uliojengwa kwenye kweli ya kwamba Mungu anatawala kikamilifu ulimwengu na kwamba anatupenda.

Katika mambo yote:” Mpango wa Mungu kwa maisha yako unahusisha ote yanaokutokea-pamoja na makosa yako, dhambi zako, na maumivu yako. Pia ni pamoja na magonjwa, madeni, majanga, talaka, kifo cha uwapendao. Mungu anaweza kuleta mema kutokana na jambo ovu sana. Alifanya hivyo pale Kalvari.

Mungu hufanya:” Kuna mbunifu nyuma ya kila kitu. Maisha yako siyo matokeo ya bahati mbaya, ajali, au bahati nzuri. Kuna msanifu nyuma. Historia ni hadithi yake. Mungu anavuta nyuzi. Tunafanya makosa, lakini Mungu hakosei kamwe. Mungu hawezi kufanya kosa-kwa sababu yeye ni Mungu.

“Hufanya kazi pamoja:” Siyo kwa kipekee au kwa kujitegemea. Matukio katika maisha yako hufanya kazi pamoja katika mpango wa Mungu. Siyo matukio yaliyojitenga, lakini matukio yanayotegemeana katika machakato mzima wa kukufanya ufanane na Kristo. Ili kutengeneza keki lazima utumie unga wa ngano, chumvi, yai bichi, sukari, na mafuta. Kama kila kimoja kikiliwa peke yake hakina ladha nzuri au hata ni kichungu. Lakini ukivioka pamoja vinakuwa chakula kitamu. Na hiyo ndiyo keki. Kama ukimpa Mungu maono yako yote mabaya, matukio yasiyopendeza, atayaunganisha pamoja kuwa kitu chema.

“Wale wampendao katika kuwapatia mema:” Hii si kwamba kila kitu maishani ni chema. Mengi yanayotokea katika ulimwengu ni maovu na mabaya, lakini Mungu ni mtaalam wa kutoa mema kutokana na hayo. Katika ukoo wa Yesu Kristo, Mt 1:1-6, wanawake wanne wameorodheshwa: Tamari, Ruthu, Rahabu, na Bethsheba. Tamari alimhadaa baba mkwe wake. Rahabu alikuwa kahaba. Ruthu hakuwa Myahudi na alivunja sheria kwa kuolewa na Myahudi. Bethsheba alitenda uzinzi na Daudi, jambo lililopelekea mauaji ya mume wake. Hizi hazikuwa ni sifa nzuri, lakini Mungu alileta mema kutokana na mabaya, na Yesu akaja kupitia ukoo wao. Kusudi la Mungu ni kubwa kuliko mataatizo yetu, maumivu yetu na  hata dhambi yetu.

“Wale walioitwa:” Ahadi ya Mungu ni kwa watoto wa Mungu tu. Si kwa kila mmoja. Kila kitu hufanya kazi pamoja kwa ubaya kwa wale wanaoishi wakimpinga Mungu na kukazia kufuata njia zao.

“Kwa kusudi lake:” Kusudi hilo ni lipi? Ni kwamba sisi “tufananishwe na mfano wa Mwana wake,” Kila kitu Mungu anachokiruhusu kutokea katika maisha yako kinaruhusiwa kwa kusudi hilo.

Wapendwa wana wa Mungu, sisi ni kama lulu, tumechongwa kwa nyundo n atezo ya taabu nyingi. Kama nyundo ya sonara haina nguvu sana kuweza kuondoa mikwaruzo, Mungu atatumia nyundo nzito zaidi. Kama sisi ni jeuri zaidi, anatumia nyundo nzito ya kunyanyuliwa na chombo maalum. Atatumia chochote kile.

Hivyo, kila tatizo ni nafasi ya kujenga tabia, na kadiri linavyokuwa gumu zaidi, ndivyo kunakuwa na matokeo makubwa katika kujenga msuli wa kiroho na uadilifu. Wala si hivyo tu, ila na mfurahi katika dhiki pia; mkijua ya kuwa dhiki, kazi yake ni kuleta saburi; na kazi ya saburi ni uthabiti wa moyo; na kazi ya uthabiti wa moyo ni tumaini,” Rum 5:3-4. Kila kinachotokea kwa maisha yako ya nje si cha muhimu sana katika kama kile kinachotokea ndani yako. Mazingira yako ni ya muda mfupi, lakini tabia yako itadumu milele.

Maandiko Matakatifu hufananisha majaribu na moto wa kusafisha madini ambao huchoma takataka zote. Mtume Petro anasema, “ili kwamba kujaribiwa kwa imani yenu, ambayo ina thamani kuu kuliko dhahabu ipoteayo, ijapokuwa hiyo hujaribiwa kwa moto, kuonekane kuwa kwenye sifa na utukufu na heshima,” 1Pet 1:7a-d. Mfua fedha aliulizwa, “Je, unafahamu vipi kwamba sana fedha ni safi? Alijibu, “ninapoona sura yangu ndani yake.” Unapokuwa umesafishwa kwa majaribu, watu wanaweza kuiona sura ya Kristo ndani yako. Yakobo anasema, mkifahamu ya kuwa kujaribiwa kwa imani yenu huleta saburi,” Yak 1:3.

Kwa kuwa Mungu anakusudia ufanane na Kristo, atakupitisha katika yale Yesu aliyopitia. Hii ni pamoja na upweke, majaribu, dhiki, kulaumiwa, kukataliwa, na matatizo mengine mengi. Biblia inasema Yesu “Alijifunza kutii kwa njia ya mateso” na alikamilishwa kwa njia ya mateso,” Ebr 5:8-9. Kwa nini Mungu atuepushe kutoka yale aliyomruhusu Mwana wake kuyapata? Mtume Paulo anasema, na kama tu watoto, basi, tu warithi; warithi wa Mungu, warithio pamoja na Kristo; naam, tukiteswa pamoja naye ili tupate na kutukuzwa pamoja naye,” Rum 8:17.

Tumsifu Yesu Kristo!


 “Mateso ya mwenye haki ni mengi, Lakini Bwana humponya nayo yote,” Zab 34:19

No hay comentarios:

Publicar un comentario