lunes, 7 de diciembre de 2015

TAFAKARI: SIKUKU YA BIKIRA MARIA MKINGIWA DHAMBI YA ASILI

SIKUKUU YA BIKIRA MARIA MKINGIWA DHAMBI YA ASILI
8/12/2015
Somo I: Mwa 3:9-15, 20
Zab: 98:1, 2-3abcd-4
Somo II: Efe 1:3-6, 11-12
Injili: Lk 1:26-38
Nukuu:
Adamu akasema, Huyo mwanamke uliyenipa awe pamoja nami ndiye aliyenipa matunda ya mti huo, nikala,” Mwa 3:12

Bwana Mungu akamwambia nyoka, Kwa sababu umeyafanya hayo, umelaaniwa wewe kuliko wanyama wote, na kuliko hayawani wote walioko mwituni; kwa tumbo utakwenda, na mavumbi utakula siku zote za maisha yako,” Mwa 3:14

Adamu akamwita mkewe jina lake Hawa; kwa kuwa yeye ndiye aliye mama yao wote walio hai,” Mwa 3:20

kama vile alivyotuchagua katika yeye kabla ya kuwekwa misingi ya ulimwengu, ili tuwe watakatifu, watu wasio na hatia mbele zake katika pendo,” Efe 1:4

Kwa kuwa alitangulia kutuchagua, ili tufanywe wanawe kwa njia ya Yesu Kristo, sawasawa na uradhi wa mapenzi yake,” Efe 1:5

na ndani yake sisi nasi tulifanywa urithi, huku tukichaguliwa tangu awali sawasawa na kusudi lake yeye, ambaye hufanya mambo yote kwa shauri la mapenzi yake,” Efe 1:11

Malaika akamwambia, Usiogope, Mariamu, kwa maana umepata neema kwa Mungu,” Lk 1:30

Tazama, utachukua mimba na kuzaa mtoto mwanamume; na jina lake utamwita Yesu. Huyo atakuwa mkuu, ataitwa Mwana wa Aliye juu, na Bwana Mungu atampa kiti cha enzi cha Daudi, baba yake,” Lk 1:31-32

Malaika akajibu akamwambia, Roho Mtakatifu atakujilia juu yako, na nguvu zake Aliye juu zitakufunika kama kivuli; kwa sababu hiyo hicho kitakachozaliwa kitaitwa kitakatifu, Mwana wa Mungu,” Lk 1:35

Tena, tazama, jamaa yako Elisabeti naye amechukua mimba ya mtoto mwanamume katika uzee wake; na mwezi huu ni wa sita kwake yeye aliyeitwa tasa; kwa kuwa hakuna neno lisilowezekana kwa Mungu,” Lk 1:36-37

Mariamu akasema, Tazama, mimi ni mjakazi wa Bwana; na iwe kwangu kama ulivyosema,” Lk 1:38a

TAFAKARI: “Mimi ni mjakazi wa Bwana; na iwe kwangu kama ulivyosema.”

Wapendwa wana wa Taifa la Mungu, leo Mama Kanisa anaadhimisha Sikukuu ya Bikira Maria Mkingiwa dhambi ya Asili. Basi katika tafakari hii leo ili tuelewe fumbo hili ni vyema kujiuliza maswali yafuatayo. Ni kwa nini Bikira Maria akingiwe dhambi ya Asili? Kabla ya kujibu swali hili, ni vyema kujua dhambi ya Asili ni nini? Kadiri ya Maandiko Matakatifu hasa tuliyoyasoma kutoka somo la kwanza, na mafundisho ya Kanisa, dhambi hii ya asili ni mwelekeo wa kutenda dhambi ambao chanzo chake kilitokana na anguko la wazazi wetu wa kwanza, yaani Adamu na Hawa. Je, pamoja na anguko hili hatukuweza kurudi na kuuchuchumilia Utakatifu? Jibu ni kwamba tunaweza. Ukweli ni kwamba licha la anguko hili la wazazi wetu wa kwanza, Mungu hakutuondolea ili hali ya uhuru ndani mwetu. Hivyo basi, ni kwa kupitia uhuru huu twaweza kumrudia Mungu kwa njia ya toba na majuto, na vile vile kwa uhuru huu pia twaweza kuasi kabisa. Ni nini basi kilitokea kule Bustanini Edeni kati ya Adamu na Hawa?

Wapendwa wana wa Mungu, ni kweli kwamba mahali popote anapoishi zaidi ya mtu mmoja kuna kuwa na kautaratibu kake ili mawasiliano yaende vizuri. Utaratibu huu unaweza kuwa kimaandishi, au kimapokea katika hali ya kuaminiania na kujenga mazoea ya kuishi katika misingi hiyo. Hivyo Mungu alivyomuumba Adamu na kumpatia msaidizi wake, yaani Hawa. Bwana Mungu akasema, Si vema huyo mtu awe peke yake, nitamfanyia msaidizi wa kufanana naye. Bwana Mungu akamletea Adamu usingizi mzito, naye akalala; kisha akatwaa ubavu wake mmoja, akafunika nyama mahali pake, na ule ubavu alioutwaa katika Adamu Bwana Mungu akaufanya mwanamke, akamleta kwa Adamu,” Mwa 2:18,21-22.  Mungu aliwapa mahali pa kuishi na mahali hapo palijulikana kama bustani ya Edeni. Mungu aliwapa utaratibu wa kuishi mahali hapo kadiri ya mpango wake mwenyewe ili uzima uwepo ndani yao milele na kuepuka kifo. Bwana Mungu akamwagiza huyo mtu, akisema, Matunda ya kila mti wa bustani waweza kula, walakini matunda ya mti wa ujuzi wa mema na mabaya usile, kwa maana siku utakapokula matunda ya mti huo utakufa hakika,” Mwa 2:16-17

Makatazo haya yanajenga udadisi na ushawishi wa yule mwovu shetani. Hii ndiyo dhambi ile ya tamaa, ambayo hutujengea hali ya kutojipokea na kutoridhika kwa kile tulicho. Shetani kwa umbo la nyoka anatumia mwanya huu kumshawishi Eva. Dhambi hii inashirikishwa kwa wote wawili, yaani Hawa an Adamu. Matokeo yake ni anguko kubwa la wazazi wetu wa kwanza. Mungu anapotaka kujua kilichojiri kila mmoja anamtupia lawama mwenzake. Mwanamke anamlaumu nyoka, na Adamu anamlaumu mkewe. Adamu akasema, Huyo mwanamke uliyenipa awe pamoja nami ndiye aliyenipa matunda ya mti huo, nikala,” Mwa 3:12. Tukio hili linamfanya Mungu kutoa adhabu kwa yule mwovu-nyoka na kuvunja agano kati yake na Adamu na Hawa. Bwana Mungu akamwambia nyoka, Kwa sababu umeyafanya hayo, umelaaniwa wewe kuliko wanyama wote, na kuliko hayawani wote walioko mwituni; kwa tumbo utakwenda, na mavumbi utakula siku zote za maisha yako,” Mwa 3:14. Tangu hapa Hawa anakuwa Mama wa wote walio hai. Adamu akamwita mkewe jina lake Hawa; kwa kuwa yeye ndiye aliye mama yao wote walio hai,” Mwa 3:20. Na tangu nyakati hizo la anguko hili la wazee wetu wa kwanza, kifo hakikuepukika tena hadi leo.

Kwa vile Mungu ni Huruma na Upendo, alipenda kuurejesha uhusiano wake na wale aliowaumba kwa sura na mfano wake. Mpango huu ni tendo zima la kumwilishwa kwake, yaani Neno kufanyika mwili. Bikira Maria kwa upendeleo Mkubwa anachukua nafasi ya Hawa aliye dondoka. Bikira Maria katika mpango huu anakuwa sababu ya kuinuliwa mzazi wetu wa kwanza yaani Hawa. Hivyo kukingiwa kwa dhambi ya asili Bikira Maria kunaendana na kile kitarajiwacho kuzaliwa, “Neno kufanyika mwili.” Mama Bikira Maria anapatwa na mshtuko kwa jambo hili Mungu analotaka litokee kwake. Malaika Gabrieli anamwambia, “Usiogope, Mariamu, kwa maana umepata neema kwa Mungu,” Lk 1:30. Kukingiwa dhambi hii ya Asili Bikira Maria, yaani ule mwelekeo wa kutenda dhambi, kuliwezekana pia kwa sababu “alipata neema kwa Mungu.”  Akijua ubinadamu wake, Bikira Maria anauliza jambo hili litawezekanaje? Malaika akajibu akamwambia, Roho Mtakatifu atakujilia juu yako, na nguvu zake Aliye juu zitakufunika kama kivuli; kwa sababu hiyo hicho kitakachozaliwa kitaitwa kitakatifu, Mwana wa Mungu,” Lk 1:35. Kwa hiyo neema ile kutoka kwa Mungu inajidhihirisha kwa nguvu na uwepo wa Roho Mtakatifu na kufanya kile kitakachozaliwa kuitwa kitakatifu, Mwana wa Mungu.

Habari njema hii kwa Bikira Maria haikuishia hapo tu. Kuthibitisha jambo hilo linawezekana mbele ya Mungu kwake yeye Bikira Maria kukingiwa dhambi ya Asili na kumzaa Mwana wa Mungu kwa uwezo wa Roho Mtakatifu, Malaika anampa yaliyojiri kwa Elizabeti. Tena, tazama, jamaa yako Elisabeti naye amechukua mimba ya mtoto mwanamume katika uzee wake; na mwezi huu ni wa sita kwake yeye aliyeitwa tasa; kwa kuwa hakuna neno lisilowezekana kwa Mungu,” Lk 1:36-37. Mungu wetu aliye hai siyo Mungu wa kushindwa. Kwa unyenyekevu mkubwa Mama Bikira Maria anaupokea mpango mzima wa Mungu na kusema, “Tazama, mimi ni mjakazi wa Bwana; na iwe kwangu kama ulivyosema,” Lk 1:38a

Na kwa vile kile kitakachozaliwa kitakuwa kitakatifu, Mwana wa Mungu, ndani yake sisi nasi tulifanywa urithi, huku tukichaguliwa tangu awali sawasawa na kusudi lake yeye, ambaye hufanya mambo yote kwa shauri la mapenzi yake,” Efe 1:11. Mungu alichagua kutuumba kama tulivyo kwa sura na mfano wake kama vile alivyotuchagua katika yeye kabla ya kuwekwa misingi ya ulimwengu, ili tuwe watakatifu, watu wasio na hatia mbele zake katika pendo,” Efe 1:4. Tunaupata ukweli huu kutoka Mwinjili Yohane juu ya huyu atakaye mwilishwa, yaani Mwana wa Mungu. Vyote vilifanyika kwa huyo; wala pasipo yeye hakikufanyika cho chote kilichofanyika,” Yoh 1:3. Hivyo kila alifanyalo Mungu linamakusudi yake katika umilele. Hakuna yeyote katika yetu yupo katika ulimwengu huu kwa bahati mbaya. Hivyo vyote vinamuunganiko na Kristo Yesu. Kwa kuwa alitangulia kutuchagua, ili tufanywe wanawe kwa njia ya Yesu Kristo, sawasawa na uradhi wa mapenzi yake,” Efe 1:5.

Wapendwa katika Kristo, tumshangilie Mama Bikira Maria leo tunapo fanya sikukuu hii ya kukingiwa dhambi ya Asili. Tunamshangilia kwanza kabisa kwa utayari wake wa kuupokea mpango mzima wa Mungu kuelekea ukamilisho wa historia ya wokovu wetu. Pili, kwa utayari wake nasi tunahesabiwa haki na kufanywa wanawe Mungu kwa njia ya Yesu Kristo, sawasawa na uradhi wa mapenzi yake Mungu.

Tumsifu Yesu Kristo!


Kwa kuwa Mwenye nguvu amenitendea makuu, Na jina lake ni takatifu,” Lk 1:49

No hay comentarios:

Publicar un comentario