jueves, 31 de diciembre de 2015

TAFAKARI: ALHAMISI, SIKU YA SABA YA OKTAVA YA NOELI

ALHAMISI, SIKU YA SABA YA OKTAVA YA NOELI
31/12/2015
Somo: 1Yoh 2:18-21
Zab: 95:1-2, 11-12, 13
Injili: Yoh 1:1-18
Nukuu:
Watoto, ni wakati wa mwisho; na kama vile mlivyosikia kwamba mpinga Kristo yuaja, hata sasa wapinga Kristo wengi wamekwisha kuwapo. Kwa sababu hiyo twajua ya kuwa ni wakati wa mwisho,” 1Yoh 2:18 

Nanyi mmepakwa mafuta na Yeye aliye Mtakatifu nanyi mnajua nyote,” 1Yoh 2:20
Hapo mwanzo kulikuwako Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu,” Yoh 1:1

Vyote vilifanyika kwa huyo; wala pasipo yeye hakikufanyika cho chote kilichofanyika,” Yoh 1:3

Ndani yake ndimo ulimokuwa uzima, nao ule uzima ulikuwa nuru ya watu,” Yoh 1:4

Nayo nuru yang'aa gizani, wala giza halikuiweza,” Yoh 1:5

Alikuwako ulimwenguni, hata kwa yeye ulimwengu ulipata kuwako, wala ulimwengu haukumtambua,” Yoh 1:10

Alikuja kwake, wala walio wake hawakumpokea,” Yoh 1:11

Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake; waliozaliwa, si kwa damu, wala si kwa mapenzi ya mwili, wala si kwa mapenzi ya mtu, bali kwa Mungu,” Yoh 1:12-13

Naye Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu; nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwa Baba; amejaa neema na kweli,” Yoh 1:14

Kwa kuwa katika utimilifu wake sisi sote tulipokea, na neema juu ya neema,” Yoh 1:16

Kwa kuwa torati ilitolewa kwa mkono wa Musa; neema na kweli zilikuja kwa mkono wa Yesu Kristo,” Yoh 1:17

Hakuna mtu aliyemwona Mungu wakati wo wote; Mungu Mwana pekee aliye katika kifua cha Baba, huyu ndiye aliyemfunua,” Yoh 1:18

TAFAKARI:Nanyi mmepakwa mafuta na Yeye aliye Mtakatifu.”

Wapendwa wana wa Mungu, tunaishi katika siku za mwisho. Watoto, ni wakati wa mwisho; na kama vile mlivyosikia kwamba mpinga Kristo yuaja, hata sasa wapinga Kristo wengi wamekwisha kuwapo. Kwa sababu hiyo twajua ya kuwa ni wakati wa mwisho,” 1Yoh 2:18. Hata hivyo si wakati wa kujawa hofu na wasiwasi. Wanafunzi wa Yesu pia walitaka kujua hasa siku hiyo itakuwa lini. Yesu Akawaambia, Si kazi yenu kujua nyakati wala majira, Baba aliyoyaweka katika mamlaka yake mwenyewe,” Mdo 1:7. Kwa muda tulibaki nao kila mmoja wetu atimize vyema utume wake kadiri ya wito na karama alizojaliwa na mwenyezi Mungu. Matokeo ya utume wake yatadumu milele kuliko matokeo ya kazi zako. Hivyo Yesu anawaambia wafuasi wake, Lakini mtapokea nguvu, akiisha kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu; nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, na katika Uyahudi wote, na Samaria, na hata mwisho wa nchi,” Mdo 1:8. Hili ndilo tunalopaswa kufanya sote tulio mpokea Roho huyu Mtakatifu kwa Sakramenti ya Ubatizo na Kipaimara.

Kwa maana nyingine siku ya mwisho ni mpaka pale dunia yote itakapofikiwa na habari njema ya wokovu. Hivyo kuharakisha siku hii ya mwisho ni sawa na kusema kila mmoja wetu atimize utume wake vyema na habari hiyo ifike kila kona ya dunia. La sivyo ni kupoteza muda buru kubashiri siku ya mwisho. Hakuna ajuaye siku hiyo. Naye Yesu anasema, Walakini habari ya siku ile na saa ile hakuna aijuaye, hata malaika walio mbinguni, wala Mwana, ila Baba peke yake,” Mt 24:36. Neno, yaani, Yesu kesha fanyika mwili na kesha ushinda ulimwengu, ila tunatembea katika siku zetu za mwisho. Hata hivyo udhihirisho ulio wazi na kamili wa ushindi wa Yesu upo unakuja. Katika safari hii kuelekea udhihirisho huo wazi na kamili kati yetu wapo mbwa mwitu waliovaa ngozi ya kondoo. Katika mtazamo huu, kuishi ni vita. Wapinga Kristo sio wale wazushi tu, bali ni mtindo pia wa kuishi.

Sote tu wapinga Kristo katika maana ya kwamba maisha yetu yasipo akisi ukweli na upendo wa Kristo. Haya ndiyo ayasemayo Mtume Paulo, Basi Roho anena waziwazi ya kwamba nyakati za mwisho wengine watajitenga na imani, wakisikiliza roho zidanganyazo, na mafundisho ya mashetani; kwa unafiki wa watu wasemao uongo, wakichomwa moto dhamiri zao wenyewe; wakiwazuia watu wasioe, na kuwaamuru wajiepushe na vyakula, ambavyo Mungu aliviumba vipokewe kwa shukrani na walio na imani wenye kuijua hiyo kweli,” 1Tim 4:1-3. Leo si jambo la ajabu kusikia dini za waabudu mashetani, wajenzi huru-free-masons.

Kristo kesha shinda ila vita inaendelea dhidi wa wema na uovu. Wale watakaokuwa katika kweli watakuwa katika hatua ya ukomavu na utakaso. Kuzaliwa kuliko kwa kweli kunatoka juu, ambako ndiko kupakwa mafuta kwetu kupitia Sakramenti ya Ubatizo na Kipaimara. Nanyi mmepakwa mafuta na Yeye aliye Mtakatifu nanyi mnajua nyote,” 1Yoh 2:20. Hivyo kuishi Ukristo ni vita dhidi ya mpinga Kristo. Utaielewa vizuri vita hii unapofanya tafiti moyo.

Injili ya leo mada kuu ni hii, Hakuna mtu aliyemwona Mungu wakati wo wote; Mungu Mwana pekee aliye katika kifua cha Baba, huyu ndiye aliyemfunua,” Yoh 1:18. Yesu, mwana, ni dhihirisho la Baba. Kwa hiyo kwa maneno haya, Hapo mwanzo kulikuwako Neno, naye Neno alikuwako kwa Mungu, naye Neno alikuwa Mungu,” Yoh 1:1, kati yetu uwazi wa utufuku wake unawezesha uelewa wetu wa maneno haya, Naye Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu; nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwa Baba; amejaa neema na kweli,” Yoh 1:14.

Ni kwa mantiki hilo kwamba katika mwili Mungu ni kama Baba, Yoh 1:1-3. Ye yote yule amtazamaye mwana, Yesu Kristo, amwona Baba. “Yesu akamwambia, Mimi nimekuwapo pamoja nanyi siku hizi zote, wewe usinijue, Filipo? Aliyeniona mimi amemwona Baba; basi wewe wasemaje, Utuonyeshe Baba?” Yoh 14:9. Ni katika tendo hili la “kuona,” upewa tu yule asikiaye neno, ni yule kwa imani kupitia mwili anaona utukufu wa Baba. Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake; waliozaliwa, si kwa damu, wala si kwa mapenzi ya mwili, wala si kwa mapenzi ya mtu, bali kwa Mungu,” Yoh 1:12-13.

Kwa hiyo ujio wa Kristo ni mgogoro katika maana ya mtengano wa wanaoishi katika mwanga na wale waishio katika giza, Kristo akiwa ndiye mwanga wa ulimwengu. Watakao upokea mwanga huu, watapokea kwa imani zawadi zilizo kubwa atakazo kuja nazo. Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake; waliozaliwa, si kwa damu, wala si kwa mapenzi ya mwili, wala si kwa mapenzi ya mtu, bali kwa Mungu,” Yoh 1:12-13

Wapendwa katika Kristo, pona yetu katika siku hizi za mwisho ni kuishi katika mwanga wa Kristo. Sote tuliobatizwa yatupasa kuziishi ahadi zetu za ubatizo kwa uaminifu. Pia tuwe makini kwa mafundisho ya uongo juu ya kweli na haki ya Kristo, kwani wengi watakuja kwa jina lake.

Tumsifu Yesu Kristo!


Wapenzi, msiiamini kila roho, bali zijaribuni hizo roho, kwamba zimetokana na Mungu; kwa sababu manabii wa uongo wengi wametokea duniani,” 1Yoh 4:1

No hay comentarios:

Publicar un comentario