JUMATANO, SIKU 23 YA MAJILIO MWAKA-C
23/12/2015
Somo: Mal 3:1-4, 4:5-6
Zab: 24:4bc-5ab, 8-9, 10, 14
Injili: Lk 1: 57-66
Nukuu:
“Angalieni, namtuma mjumbe wangu, naye ataitengeneza njia
mbele yangu; naye Bwana mnayemtafuta atalijilia hekalu lake ghafula; naam, yule
mjumbe wa agano mnayemfurahia, angalieni, anakuja, asema Bwana wa majeshi,” Mal 3:1
“Lakini ni nani atakayestahimili siku ya kuja kwake? Au ni
nani atakayesimama atakapoonekana yeye? Kwa maana yeye ni mfano wa moto wa mtu
asafishaye fedha, ni mfano wa sabuni ya mtu afuaye nguo,” Mal 3:2
“Angalieni, nitawapelekea Eliya nabii, kabla haijaja siku ile
ya Bwana, iliyo kuu na kuogofya,” Mal 4:5
“Naye ataigeuza mioyo ya baba iwaelekee watoto wao, na mioyo
ya watoto iwaelekee baba zao, ili nisije nikaipiga dunia kwa laana,” Mal 4:6
“Mamaye akajibu akasema La, sivyo; bali, ataitwa Yohana,” Lk 1:60
“Akataka kibao, akaandika ya kwamba, Jina lake ni Yohana.
Wakastaajabu wote,” Lk 1:63
“Na wote walioyasikia wakayaweka mioyoni mwao, wakisema, Mtoto
huyu atakuwa wa namna gani? Kwa sababu mkono wa Bwana ulikuwa pamoja naye,” Lk
1:66
TAFAKARI: “Kwake vyote vitafanywa upya.”
Wapendwa wana wa Mungu, mazoea hujenga tabia. Na tabia ya
mtu kama ni mbaya huchukua muda sana kurudi katika njia iliyo sahihi. Kinyume
cha Kuhani aliyekuwa siyo mwaminifu, Nabii Malaki anatangaza siku ya Mungu
ambayo itakuwa ya kutisha sana. “Lakini ni nani atakayestahimili siku ya kuja kwake? Au ni
nani atakayesimama atakapoonekana yeye? Kwa maana yeye ni mfano wa moto wa mtu
asafishaye fedha, ni mfano wa sabuni ya mtu afuaye nguo,” Mal 3:2
Tunaweza kusoma
habari hii ya kutisha ya siku ya Bwana pia kutoka kwa Nabii Amosi, 5:18-20, na
Namii Joeli, 1:15-20. Katika hatua hii, Bwana atarudi katika hekalu lake na
kulitakatifuza kwa moto, Eze 22: 17.22, na kumweka Kuhani Mtakatifu na sadaka
ya haki itakayokubalika. “Angalieni, nitawapelekea Eliya nabii, kabla haijaja siku ile
ya Bwana, iliyo kuu na kuogofya,” Mal 4:5. Kama ilivyokuwa kwamba huwezi kumwona Mungu bila kufa, Kut
33:20, Mungu alionekana kwa watu mfano wa Malaika, Mwa 16:7, Kut 3:2. Malaika
wa agano ni Bwana ambaye anawatafuta watu wake, na siyo mjumbe.
Hii inamaanisha Mungu mwenyewe, anayeonekana, atakuwa
muhuri wa agano hili jipya, Yer 31:31ff, kwenye Hekalu lake. Maneno haya
yanamaanisha Yesu mwenyewe, Mt 11:10, Ebr 3:5-6. Ujio wa Bwana unamaanisha
kweli upya wa mambo na mtazamo wa maisha watu kuelekea umilele. “Naye ataigeuza mioyo ya baba iwaelekee watoto wao, na mioyo
ya watoto iwaelekee baba zao, ili nisije nikaipiga dunia kwa laana,” Mal 4:6.
Kinyume cha baraka ni laana. Hivyo pona ya watu wake ni kufuata maagizo yake
yenye uhai ndani yake.
Kuzaliwa kwa Yohane kunathibitishwa katika uhalisia wake
kwa tangazo la Malaika wa Mungu. Tunda la kwanza katika kuzaliwa kwake ni
furaha. Yohane tunda la muujiza, halina uhusiano na watu; hitimisho lake halipo
mikoni mwa familia yake, limefanywa hivyo na Mungu mwenyewe. Mungu amempa jina
ambalo linaelezea hatma yake, Mwa 17:3-8, Mt 16:17-19. Yohane anauvunja
mwendelezo uliokuwepo. Hivyo hataitwa Zakaria, jina lake litakuwa Yohane, Lk 1:60.
Elizabeti kama alivyokuwa Ana mama yake Samuel, anajua
mwanaye si mali yake. Mtoto Samweli alitwaliwa, na kuchaguliwa hata kabla ya
kuzaliwa kuwa ni mali yake Bwana, Yer 1:5. Zakaria Baba yake Yohane anakubali
hatma ya mtoto wake, na mdomo wake unafunguka na kumsifu Mungu. Haya ndiyo
maajabu ya Mungu kwa watu wake. “Na wote walioyasikia wakayaweka mioyoni mwao, wakisema, Mtoto
huyu atakuwa wa namna gani? Kwa sababu mkono wa Bwana ulikuwa pamoja naye,” Lk
1:66. Kwake Mungu vyote vitafanywa upya. Hakuna aliyekutana na Mungu katika
hali yoyote ile akabaki kama alivyo kuwa mwanzo.
Tumsifu
Yesu Kristo!
“Si kwa sababu ya
matendo ya haki tuliyoyatenda sisi; bali kwa rehema yake, kwa kuoshwa kwa
kuzaliwa kwa pili na kufanywa upya na Roho Mtakatifu,” Tit 3:5
No hay comentarios:
Publicar un comentario