JUMATATU, SIKU 21 YA MAJILIO MWAKA-C
21/12/2015
Somo: Wim 2:8-14
Zab: 32:2-3, 11-12, 20-21
Injili: Lk 1: 39-45
Nukuu:
“Mpendwa wangu alinena, akaniambia, Ondoka, mpenzi wangu,
mzuri wangu, uje zako,” Wim 2:10
“Maana tazama, kaskazi imepita, Masika imekwisha, imekwenda
zake,” Wim 2:11
“Maua yatokea katika nchi, Wakati wa kupelea umefika, Na sauti
ya mwigo husikiwa kwetu,” Wim 2:12
“Mtini wapevusha tini zake, Na mizabibu inachanua, Inatoa
harufu yake nzuri; Ondoka, mpenzi wangu, mzuri wangu, uje zako,” Wim 1:13
“Hua wangu, mafichoni mwa jabali, Katika sitara za magenge,
Nitazame uso wako, nisikie sauti yako, Maana sauti yako ni tamu na uso wako
mzuri,” Wim 2:13
“Ikawa Elisabeti aliposikia kule kuamkia kwake Mariamu, kitoto
kichanga kikaruka ndani ya tumbo lake; Elisabeti akajazwa Roho Mtakatifu,” Lk
1:41
“akapaza sauti kwa nguvu akasema, Umebarikiwa wewe katika
wanawake, naye mzao wa tumbo lako amebarikiwa,” Lk 1:42
“Limenitokeaje neno hili, hata mama wa Bwana wangu anijilie
mimi?” Lk 1:43
“Naye heri aliyesadiki; kwa maana yatatimizwa aliyoambiwa na
Bwana,” Lk 1:45
TAFAKARI: “Na heri aliyesadiki; kwa maana yatatimizwa aliyoambiwa na
Bwana.”
Wapendwa wana wa Mungu, somo letu la kwanza kutoka katika
kitabu cha “Wimbo ulio bora,” linaelezea mahusiano ya karibu kati ya Mungu na
viumbe vyake kwa lugha ya picha. “Mpendwa wangu alinena, akaniambia, Ondoka, mpenzi wangu,
mzuri wangu, uje zako,” Wim 2:10. Hata hivyo lugha hii ya picha inagusa agano
jipya la Kimasiha kati ya Mungu na watu wake. Wakati wa ukamilisho wa tendo
hili haupo mbali tena kama ilivyokuwa huko nyuma. “Maana tazama, kaskazi imepita, Masika imekwisha, imekwenda
zake,” Wim 2:11. Hivyo
ni halali kabisa kutumia maudhui haya ya uhusiano fumbo kati ya Mungu na viumbe
alivyopendezwa navyo.
Fumbo hili linaonyesha ukaribu uliopo kati ya wawili
wapendanao na walio wapenzi wa kweli kabisa. Ni upendo usioficha chochote na
ulio wazi kwa kila kitu. Ni upendo uliotayari kupokeana na kuchukuliana katika
hali zote licha ya mapungufu yaliyopo kwa upande mmoja, yaani, kwetu sisi
wanadamu. Upedo huu wafananishwa na wakati wa kupelea katika msimu wa kawaida
wa mwaka yaani, “Mtini wapevusha tini zake, Na mizabibu inachanua, Inatoa
harufu yake nzuri; Ondoka, mpenzi wangu, mzuri wangu, uje zako,” Wim 1:13. Mwisho
upendo huu unachukua fumbo la Hua, na kutoka kwa lengo la kukutana na yule
ampendaye. Hapa ndipo tunapoona hatua kuelekea kile kilichokuwa ndani
“kinadharia” na kufanywa katika uhalisia wake. Hili ndilo Mungu analolitaraji
kulifanya katika kipindi hiki cha kuja kwake, Majilio. “Hua wangu, mafichoni mwa jabali, Katika sitara
za magenge, Nitazame uso wako, nisikie sauti yako, Maana sauti yako ni tamu na
uso wako mzuri,” Wim 2:13. Fumbo
hili la njiwa/hua ndiyo fumbo zima la kumwilishwa kwa NENO na kukaa kwetu. Mama
Bikira Maria kwa “ndiyo” yake yote yanafanyika. Hii ndiyo habari tunayoisika
katika Injili yetu ya leo.
Wapendwa wana wa Mungu, Bikira Maria akiwa amejaa Neema na
kwa mtazamo wa hekalu la Mungu,
anaifunua neema hii na kuipeleka kwa wengine. Bikira Maria anabeba habari njema
ya wokovu wetu. “Basi, Mariamu akaondoka siku hizo, akaenda hata nchi ya milimani
kwa haraka mpaka mji mmoja wa Yuda,” Lk 1:39. Ni
furaha hiyo ya Kimasiha aliyojawa nayo inamsukuma kuondoka na kuelekea kwa
binamu yake Elizabeti. Hakika furaha ni kama kikohozi hakuna awezaye hawezi
kuzuiya!
Elizabeti, binamu yake Bikira Maria, anatafsiri tendo hili
la maamkio haya yaliyogusa mwitikio wa ndani katika nafsi yake kama tendo la
kinabii. “Ikawa
Elisabeti aliposikia kule kuamkia kwake Mariamu, kitoto kichanga kikaruka ndani
ya tumbo lake; Elisabeti akajazwa Roho Mtakatifu,” Lk 1:41. Elizabeti
anafunuliwa na kutambua fumbo lililojificha ndani ya Bikira Maria na Ukuu wa
Kichanga kilichokuwa tumboni mwake, na kujinyenyekeza. Naye “akapaza sauti kwa nguvu
akasema, Umebarikiwa wewe katika wanawake, naye mzao wa tumbo lako
amebarikiwa,” Lk 1:42. Hakika ndani ya tumbo la Maria ambayo ndiyo Terbenakulo
la kwanza, kumefichwa subira yote katika historia yote ya Israeli na wokovu wa
mwanadamu.
Kutokana
na ukubwa wa jambo hili, Elizabeti anajihoji na kusema, “Limenitokeaje neno hili,
hata mama wa Bwana wangu anijilie mimi?” Lk 1:43. Hakika Mungu hubaki kuwa
Mungu, njia na mipango yake ufunuliwa kwa wale tu wajinyenyekezao kumwelekea
Yeye. Ni katika hali hii, Bikira Maria naye anaamini matendo makuu ya Mungu
yaliyofichwa ndani mwake. Ni katika mazingira haya tunaona wimbo ule wa Bikira
Maria “Magnificant,” wa kumsifu Mungu kwa makuu yake kwake ambaye hana chochote
cha kujivunia zaidi kustaajabu Makuu ya Mungu.
“Ndiyo”
ya Bikira Maria inafanya kazi ya Mungu, Mpango wa Mungu, ambao unafanyika kwetu
pia. Hakika Bikira Maria katosheleza kabisa katika safari hii ya wokovu kwa
kuinurisha nuru ile iliyofifishwa na Hawa mzazi wetu wa kwanza. Bikira Maria ni
Mama yetu sote na vizazi vyote hadi mwisho wa nyakati. “Naye heri aliyesadiki; kwa
maana yatatimizwa aliyoambiwa na Bwana,” Lk 1:45. AMINA!
Tumsifu
Yesu Kristo!
“Wanyenyekevu nao wataongeza furaha yao katika Bwana, na
maskini katika wanadamu watafurahi katika Mtakatifu wa Israeli,” Isa 29:19
No hay comentarios:
Publicar un comentario