JUMAMOSI KIPINDI CHA NOELI
Sikukuu ya Mt.
Stefano Shahidi
26/12/2015
Somo: Mdo 6:8-10,
7:54-60
Zab: 30:3-8, 16-17
Injili: Mt 10: 17-22
Nukuu:
“Basi waliposikia maneno haya, wakachomwa mioyo, wakamsagia
meno,” Mdo 7:54
“Lakini yeye akijaa Roho Mtakatifu, akakaza
macho yake, akitazama mbinguni, akauona utukufu wa Mungu, na Yesu akisimama upande
wa mkono wa kuume wa Mungu,” Mdo 7:55
“Akasema, Tazama! Naona mbingu zimefunguka, na
Mwana wa Adamu amesimama mkono wa kuume wa Mungu,” Mdo 7:56
“Wakapiga kelele kwa sauti kuu, wakaziba
masikio yao, wakamrukia kwa nia moja, wakamtoa nje ya mji, wakampiga kwa mawe. Nao mashahidi wakaweka nguo zao
miguuni pa kijana mmoja aliyeitwa Sauli,” Mdo 7:57-58
“Wakampiga kwa mawe Stefano, naye akiomba, akisema, Bwana
Yesu, pokea roho yangu,” Mdo 7:59
“Akapiga magoti, akalia kwa sauti kuu, Bwana,
usiwahesabie dhambi hii. Akiisha kusema haya akalala. Na Sauli alikuwa akiona
vema kwa kuuawa kwake,” Mdo 7:60
“Jihadharini na wanadamu; kwa maana watawapeleka mabarazani,
na katika masinagogi yao watawapiga,” Mt 10:17
“Lakini hapo watakapowapeleka, msifikiri-fikiri jinsi
mtakavyosema; maana mtapewa saa ile mtakayosema,” Mt 10:19
“Kwa kuwa si ninyi msemao, bali ni Roho wa Baba yenu asemaye
ndani yenu,” Mt 10:20
“Na ndugu atamsaliti nduguye ili auawe, na
baba atamsaliti mwana, na wana watawainukia wazazi wao, na kuwafisha,” Mdo
10:21
“Nanyi mtakuwa mkichukiwa na watu wote kwa
ajili ya jina langu; lakini mwenye kuvumilia hata mwisho, ndiye atakayeokoka,”
Mt 10:22
TAFAKARI: “Waliposikia maneno haya, wakachomwa mioyo, wakamsagia
meno.”
Wapendwa wana Mungu, leo Mama Kanisa anafanya sikukuu ya
Mt. Stefano Shahidi kwa kwanza aliyemfia Kristo kadiri ya mapokea ya Kanisa.
Shahidi Stefano alikuwa kati ya wale
saba waliochanguliwa, Mdo 6:5, na
Mitume ili kusaidia utowaji wa huduma kutokana na ongezeko la wanafunzi/wafuasi
wa Kristo, na manung’uniko ya wayahudi wa Kiyunani juu ya Waebrania kwa sababu
wajane wao walisahaulika katika huduma, Mdo 6:1. Hivyo ili kuendelea na kazi ya
kulihubiri neno la Mungu, “Wale Thenashara wakawaita jamii ya wanafunzi, wakasema,
Haipendezi sisi kuliacha neno la Mungu na kuhudumu mezani,” Mdo 6:2
Shahidi
Stefano alikuwa mtu aliyejaa Imani na Roho Mtakatifu. Hata pamoja na huduma
aliyochaguliwa kuifanya, alilihubiri neno la Mungu kwa ufasaha. Stefano Shahidi
hakupindisha ukweli, na alisema lililo kweli mbele ya Mungu na mbele ya macho
ya watu. Stefano alionyesha wazi kupotoka kwao Wayahudi na kile walichomfanyia
Yesu na kuutoa uhai wake. Hakika maneno na mafundisho yake yalikuwa kama upanga
mkali uliopenyeza ndani ya mioyo ya watu.
Watesi
wake Shahidi Stefano hawakuweza kuvumilia hali ile na hasa maneno yake ya
kuchoma. Kwa hali hii ndipo walipomtungia uongo na kuwasimamisha mashahidi wa
uongo ili wamteketeze kama walivyo fanya kwa Bwana wetu Yesu Kristo. “Wakasimamisha mashahidi wa uongo waliosema, Mtu huyu haachi
kusema maneno ya kufuru juu ya mahali hapa patakatifu na juu ya torati; maana
tumemsikia akisema kwamba Yesu huyo Mnazareti atapaharibu mahali hapa, na
kuzibadili desturi tulizopewa na Musa,” Mdo 6:13. Kwa ushahidi huu wa uongo na
wakusuka, uliamsha hasira za watu katika sinagogi na kusababisha Stefano
kutolewa nje, kisha kushushiwa mvua ya mawe baada ya kuvuliwa nguo na
kukabidhiwa Sauli ambaye leo ndiye Mtume Paulo. Mambo yalikuwa hivi huko ndani
ya sinagogi baada ya ushahidi ule wa uongo, “Wakapiga kelele kwa sauti kuu,
wakaziba masikio yao, wakamrukia kwa nia moja, wakamtoa nje ya mji,
wakampiga kwa mawe. Nao mashahidi wakaweka nguo zao miguuni pa kijana mmoja
aliyeitwa Sauli,” Mdo 7:57-58. Hivyo kwa tendo hili, Stefano alikufa kama
shahidi mfiadini wa kwanza katika historia ya Kanisa. Kwa damu yake ilitoa
ushahidi wa upendo wake na Imani kwa Kristo Yesu.
Akiwa katika hali hii ya mateso makubwa mbingu zinafunga na
huko anamwona wana wa Adamu. “Akasema, Tazama! Naona mbingu zimefunguka, na Mwana wa
Adamu amesimama mkono wa kuume wa Mungu,” Mdo 7:56. Mahangaiko na mateso yake hayakuwa sababu ya
kumwasi Kristo. “Wakampiga kwa mawe Stefano, naye akiomba, akisema, Bwana
Yesu, pokea roho yangu,” Mdo 7:59 .Vile vile
Stefano hakuchukua nafasi hii ya mateso na mahangaiko yake kuwalaumu watesi
wake zaidi ya kuwaombea. “Akapiga magoti, akalia kwa sauti kuu, Bwana, usiwahesabie
dhambi hii. Akiisha kusema haya akalala. Na Sauli alikuwa akiona vema kwa
kuuawa kwake,” Mdo 7:60. Huku ndiko kufa kifo shahidi na dini, na damu yake
ilipelekea kukua kwa Imani na uthabiti wa Kanisa la Mwanzo.
Majaribu, Mateso, na Mahangaiko aliyoyapata Stefano
yawezekana kwa namna fulani na nyakati fulani umefikwa nayo ila kwa kiwango tofauti.
Swali ni hili: Je, katika nyakati hizo umefanya kufuru kwa kumwasi Kristo? Je,
umetumia nafasi hiyo kutoa lawama na hata kuwalaani watesi wako? Na mwisho,
katika hali hii ya majaribu, mateso, na mahangaiko umetumia nafasi hiyo
kujiombea, na kuwaombea watesi wako wapate wokovu? Bila shaka kabisa matokeo ya
sala njema na yenye dhamiri njema ya Stefano ilikuwa nguvu ya wokovu kwa Sauli
ambaye tunaambiwa alishuhudia kuuawa kwake, Mdo 7:60b. Tuishi mara zote tukiwa
na hofu ya Mungu, na tuepuke mara zote kutoa na kushuhudia uongo.
Injili ya leo inaweka bayana yatakayojiri pale tunapoamua
kwa dhati kuambatana na Kristo, na kuishi kwa ajili yake. “Jihadharini na wanadamu; kwa maana
watawapeleka mabarazani, na katika masinagogi yao watawapiga,” Mt 10:17. Vile vile Injili
inaweka bayana kabisa kwamba atakayeambatana na Kristo na kuishi kwa ajili
yake, Kristo hatomwacha kamwe. “Lakini hapo watakapowapeleka, msifikiri-fikiri jinsi
mtakavyosema; maana mtapewa saa ile mtakayosema. Kwa kuwa si ninyi msemao, bali
ni Roho wa Baba yenu asemaye ndani yenu,” Mt 10:19-20. Hivyo hatu sababu na
wala kuwa na hofu tunaposema na kusimama katika kweli. “Ninyi mkikaa katika neno langu, mmekuwa
wanafunzi wangu kweli kweli; tena mtaifahamu kweli, nayo hiyo kweli itawaweka huru,” Yoh 8:31b-32
Kuwa mfuasi wa Kristo ni kutangaza vita vya mwanga dhidi ya
giza. Hivyo kusalitiwa na kusalitiana ni mazingira halisi ya kufa kifo dini
kila siku. Tendo hili mbaya zaidi hufanyika na wale tunaowajua na wakati
mwingine ni ndugu zetu wa damu. “Na ndugu atamsaliti nduguye ili auawe, na baba atamsaliti
mwana, na wana watawainukia wazazi wao, na kuwafisha,” Mdo 10:21. Kumfuata
Kristo kwa uaminifu ni sababu pia ya kuchukiwa na wale wapendao giza, yaani,
watendao matendo maovu na kinyume na Kristo. Hata hivyo, shinda yetu, okoka
yetu, na salama yetu katika hali hii ni uvumilivu ndani na katika Kristo hadi
mwisho. “Nanyi mtakuwa mkichukiwa na watu wote kwa
ajili ya jina langu; lakini mwenye kuvumilia hata mwisho, ndiye atakayeokoka,”
Mt 10:22. Je, ndugu yangu tuliyesafiri wote
katika tafakari hii, unayo misuli ya Imani ya kuyashinda majaribu haya?
Usihofu! Mtazame kwa Imani yule waliyemtundika, Kristo Yesu Mshindi
Tumsifu
Yesu Kristo! Mt. Stefano Shahidi, Utuombee
“Jaribu halikuwapata ninyi, isipokuwa lililo kawaida ya
wanadamu; ila Mungu ni mwaminifu; ambaye hatawaacha mjaribiwe kupita mwezavyo;
lakini pamoja na lile jaribu atafanya na mlango wa kutokea, ili mweze
kustahimili,” 1Kor 10:13
No hay comentarios:
Publicar un comentario