JUMAMOSI WIKI YA 3 YA MAJILIO MWAKA-C
19/12/2015
Somo: Amu 13:2-7, 24-25a
Zab: 71:3-4a, 5-6ab, 16-19
Injili: Lk 1: 5-25
Nukuu:
“Palikuwa na mtu mmoja
wa Sora, wa jamaa ya Wadani; jina lake akiitwa Manoa; na mkewe alikuwa tasa,
hakuzaa watoto,” Amu 13:2
“Malaika wa Bwana
akamtokea yule mwanamke, akamwambia, Tazama, wewe sasa u tasa, huzai; lakini
utachukua mimba, nawe utamzaa mtoto mwanamume,” Amu 13:3
“Basi sasa, jihadhari,
nakuomba, usinywe divai wala kileo, wala usile kitu kilicho najisi; kwani tazama,
utachukua mimba, nawe utamzaa mtoto mwanamume; na wembe usipite juu ya kichwa
chake; maana mtoto huyo atakuwa mnadhiri wa Mungu tangu tumboni; naye ataanza
kuwaokoa Israeli na mikono ya Wafilisti,” Amu 13:4-5
“Basi yule mwanamke
akamzaa mtoto mwanamume akamwita jina lake Samsoni, mtoto huyu akakua, Bwana
akambarikia,” Amu 13:24
“Na wote wawili walikuwa wenye haki mbele za Mungu, wakiendelea
katika amri zote za Bwana na maagizo yake bila lawama,” Lk 1:6
“Nao walikuwa hawana mtoto, maana Elisabeti alikuwa tasa, na wote
wawili ni wazee sana,” Lk 1:7
“Akatokewa na malaika wa Bwana, amesimama upande wa kuume wa
madhabahu ya kufukizia,” Lk 1:11
“Lakini yule malaika akamwambia, Usiogope, Zakaria, maana dua
yako imesikiwa, na mkeo Elisabeti atakuzalia mtoto mwanamume, na jina lake
utamwita Yohana,” Lk 1:13
“Kwa sababu atakuwa mkuu mbele za Bwana; hatakunywa divai wala
kileo; naye atajazwa Roho Mtakatifu hata tangu tumboni mwa mamaye,” Lk 1:15
“Na wengi katika Waisraeli atawarejeza kwa Bwana Mungu wao. Naye atatangulia mbele
zake katika roho ya Eliya, na nguvu zake, ili kuigeuza mioyo ya baba iwaelekee
watoto, na kuwatilia waasi akili za wenye haki, na kumwekea Bwana tayari watu
waliotengenezwa,” Lk 1:16-17
“Zakaria akamwambia malaika, Nitajuaje neno hilo? Maana mimi ni
mzee, na mke wangu ni mkongwe wa siku nyingi,” Lk 1:18
“Malaika akamjibu akamwambia, Mimi ni Gabrieli, nisimamaye mbele
za Mungu; nami nimetumwa niseme nawe, na kukupasha habari hizi njema. Na tazama! Utakuwa bubu,
usiweze kusema, mpaka siku ile yatakapotukia hayo, kwa sababu hukuyasadiki
maneno yangu; nayo yatatimizwa kwa wakati wake,” Lk 1:19-20
“Hata baada ya siku zile mkewe Elisabeti alichukua mimba akatawa
miezi mitano, akisema, Hivi ndivyo alivyonitendea Bwana katika siku zile alizoniangalia
ili kuniondolea aibu yangu mbele ya watu,” Lk 1:24-25
TAFAKARI: “Hakuna lisilowezekana kwa Mungu. Mungu anahitaji kilicho
bora zaidi kutoka kwako.”
Wapendwa wana wa Mungu, tangu kufariki kwa Nabii Yoshua,
hali ya makabila ya Waisraeli haikuwa nzuri na yautulivu. Wafilistia
waliyanyanyasa sana makabila haya ya Waisraeli. Katika safari yake ya kumkomboa
mwananadamu, Mungu anakisikia kilio chao, na anamsimamisha mmoja kati ya wana
wa Israeli, na kuwarudishia furaha tena. Hakika kila afanyacho Mungu kina makusudi
yake makubwa ikiwa ni udhihirisho wa Utukufu wake, na furaha na amani kwa
waliosetwa. Mungu humuhusisha mwanadamu Mipango yake kwa sababu mwanadamu huyu
ndiye kwenye chapa yake, yaani, kamuumba kwa sura na mfano wake, Mwan 1:27.
Hivyo basi, kwa tendo hilo lenye matokea makubwa kwanza
kabisa linakuwa furaha na amani kwa mke wa Manoa ambaye alikuwa tasa. “Palikuwa na mtu mmoja wa Sora, wa jamaa ya Wadani; jina lake
akiitwa Manoa; na mkewe alikuwa tasa, hakuzaa watoto,” Amu 13:2. Malaika wa
Bwana akiwa ni mjumbe wa Mungu, na mambo muhimu ya Mungu na yamuhusuyo Mungu,
anamtokea Mke wa Manoa na kumwambia, “Tazama, wewe sasa u
tasa, huzai; lakini utachukua mimba, nawe utamzaa mtoto mwanamume,” Amu 13:3.
Hakika lisilowezekana kwa mwanadamu kwa Mungu linawezekana. Mungu anataka
kilicho bora kutoka kwetu. Bila shaka familia hii, yaani, Manoa na Mkewe
walikuwa na hofu yangu. Mungu kamwe hamtupi mja wake hasa pale anajiachia
kwake bila kujibakiza.
Kwa vile kitakachozaliwa lazima kijibu
mahangaiko ya watu wa Mungu, Malaika anatoa masharti yake kadiri ya matakwa ya
Mungu. Huku ndiko kule kuwa Mnadhiri wa Mungu kama tusomavyo kukoka kitabu cha
hesabu 6:2-8. Na haya ndiyo anayoyasema Malaika kwa Mke wa Manoa, kwamba, “Basi sasa, jihadhari, nakuomba, usinywe
divai wala kileo, wala usile kitu kilicho najisi; kwani tazama, utachukua mimba, nawe
utamzaa mtoto mwanamume; na wembe usipite juu ya kichwa chake; maana mtoto huyo
atakuwa mnadhiri wa Mungu tangu tumboni; naye ataanza kuwaokoa Israeli na
mikono ya Wafilisti,” Amu 13:4-5. Mtoto
huyu anatengwa rasmi kwa kazi ya Mungu na yanayomuhusu Mungu. “Basi yule mwanamke akamzaa mtoto mwanamume akamwita jina lake
Samsoni, mtoto huyu akakua, Bwana akambarikia,” Amu 13:24. Samsoni anachukua
jukumu kubwa kutoka kwa Mungu, na anashirikishwa kazi Takatifu ya Mungu, yaani,
mpako wa wokovu wa mwanadamu.
Jambo lingine kubwa lenye
mfanano kama huu linatokea pia kwenye Injili yetu ya leo. Mungu anavunja ukimya
kwa kuingia katika historia ya mwanadamu kwa kuleta furaha na Amani kwa wale
waliosetwa, na kuudhihirisha Utukufu wake. Zakaria na Mkewe Elizabeti hawakufanikiwa
kupata mtoto kwa muda mrefu sana. Kwa hali ya kibinadamu matumaini yao yalianza
kutoweka. Maandiko Matakatifu yanatuambia hivi,
“Nao walikuwa hawana mtoto, maana Elisabeti alikuwa tasa, na wote
wawili ni wazee sana,” Lk 1:7. Pamoja na hali hii isiyowezekana kutokana mipaka
yetu kibinadamu, bado Mungu anahitaji kilicho bora kutoka kwetu. Kilichobora
kutoka kwa Zakari na Elizabeti ilikuwa maisha yao ya uaminifu na Imani thabiti.
“Na wote wawili walikuwa
wenye haki mbele za Mungu, wakiendelea katika amri zote za Bwana na maagizo
yake bila lawama,” Lk 1:6. Hakika Mungu kamwe hamtupi mja wake anapojiachia
kwake bila kujibakiza!
Hivyo
Zakaria akiwa katika shughuli zake za kila siku hekaluni, “Akatokewa na malaika wa
Bwana, amesimama upande wa kuume wa madhabahu ya kufukizia,” Lk 1:11. Tukio
hili linamshtusha sana Zakari. Halikuwa jambo la kawada kwake. “Lakini yule malaika
akamwambia, Usiogope, Zakaria, maana dua yako imesikiwa, na mkeo Elisabeti
atakuzalia mtoto mwanamume, na jina lake utamwita Yohana,” Lk 1:13. Hii ni
habari njema kwa Zakaria na Mkewe Elizabati. Mungu ameamua kuwatoa aibu na
kuwapa hadhi yao kama wazazi. Hadhi hii ambayo kwa msingi na mtazamo katika
jamii ni heshima kubwa kwa wazazi wote wawili, na kwa namna ya pekee kwa upande
wa mama. Ujumbe huu ni habari njema na siyo adhabu. Ni habari njema kama
tusomavyo kutoka kitabu cha Nabii Sefania, “Imba, Ee binti Sayuni; piga kelele, Ee Israeli; Furahi na
kushangilia kwa moyo wako wote, Ee binti Yerusalemu. Bwana ameziondoa hukumu zako, Amemtupa
nje adui yako; Mfalme wa Israeli, naam, yeye Bwana, yu katikati yako; Hutaogopa
uovu tena. Katika siku ile
Yerusalemu utaambiwa, Usiogope, Ee Sayuni; mikono yako isilegee. Bwana, Mungu wako, yu katikati yako
shujaa awezaye kuokoa; Atakushangilia kwa furaha kuu, Atakutuliza katika upendo
wake, Atakufurahia kwa kuimba,” Sef 3:14-17
Malaika
anaendelea kuufunua ujumbe wa Mungu kwa kile kitakachozaliwa, ikiwa ni pamoja
na kazi atakayoifanya kwa sifa na utukufu wa Mungu. Atakayezaliwa atatengwa kwa
kazi ya Mungu, “Kwa sababu atakuwa mkuu mbele za Bwana; hatakunywa divai wala
kileo; naye atajazwa Roho Mtakatifu hata tangu tumboni mwa mamaye,” Lk 1:15.
Hakika ataongozwa na Roho Mtakatifu kabla hata ya kuzaliwa kwake. Jambo hili
litajidhihirisha kwenye maamkio kati ya Mariamu na Elizabeti baadaye.
Huyu
atakayezaliwa, yaani Yohane, na baadaye kama Yohone Mbatizaji atakuwa na kazi
hii ifuatayo, “Naye atatangulia mbele zake katika roho ya Eliya, na nguvu zake,
ili kuigeuza mioyo ya baba iwaelekee watoto, na kuwatilia waasi akili za wenye
haki, na kumwekea Bwana tayari watu waliotengenezwa,” Lk 1:16-17. Kwa ufupi
kazi yake itakuwa kuwaandaa watu na kuiandaa njia ya mwokozi, yaani, Yesu
Kristo. “Sikiliza, ni sauti ya mtu aliaye, Itengenezeni
nyikani njia ya Bwana; Nyosheni jangwani njia kuu kwa Mungu wetu,” Isa 40:3.
Huyu ndiye Yohane Mbatizaji na kazi ile atakayoifanya.
Lakini pamoja na Malaika kumwambia Zakaria asiogope juu ya
ujumbe huu, bado anakuwa na mashaka na kumwiya vigumu kuamini. Zakaria
anautazama zaidi uchakavu wake wa nje na kusahau utu wake wa ndani. “Zakaria akamwambia
malaika, Nitajuaje neno hilo? Maana mimi ni mzee, na mke wangu ni mkongwe wa
siku nyingi,” Lk 1:18. Mtume Paulo anatuambia, “Kwa hiyo hatulegei; bali ijapokuwa utu wetu wa nje unachakaa,
lakini utu wetu wa ndani unafanywa upya siku kwa siku,” 2Kor 4:16. Hivyo hakuna lisilowezekana kwa Mungu. Mungu anahitaji kilicho
bora zaidi kutoka kwako. Zakaria anashindwa kumpa Mungu kilicho bora zaidi
kutoka kwake, yaani Imani yake. Hivyo jambo hili linakuwa chukizo kwa Mungu, na
hivyo “Malaika akamjibu akamwambia, Mimi ni Gabrieli, nisimamaye mbele
za Mungu; nami nimetumwa niseme nawe, na kukupasha habari hizi njema. Na tazama! Utakuwa bubu,
usiweze kusema, mpaka siku ile yatakapotukia hayo, kwa sababu hukuyasadiki
maneno yangu; nayo yatatimizwa kwa wakati wake,” Lk 1:19-20.
Hata
pamoja na tukio hilo la kutokuamini kwake Zakaria, Mungu hakusitisha mpango
wake na nia yake njema katika safari hii ya ukombozi. “Hata baada ya siku zile
mkewe Elisabeti alichukua mimba akatawa miezi mitano, akisema, Hivi ndivyo alivyonitendea
Bwana katika siku zile alizoniangalia ili kuniondolea aibu yangu mbele ya
watu,” Lk 1:24-25. Huyu ndiye Mungu asiyeshindwa. Huyu ndiye Mungu anayetutoa
katika vifungo vya mateso na aibu zetu. Ndugu yangu tuliyesafiri wote katika
tafakari hii tunaalikwa wewe na mimi kutokukata tamaa hata pale tunapoona giza
tupu mbele ya maisha yetu. Mungu huyaona mahangaiko yetu yote. Bado anahitaji
kilicho bora zaidi kutoka kwetu, yaani, Imani thabiti.
Tumsifu
Yesu Kristo!
“Jaribu halikuwapata
ninyi, isipokuwa lililo kawaida ya wanadamu; ila Mungu ni mwaminifu; ambaye
hatawaacha mjaribiwe kupita mwezavyo; lakini pamoja na lile jaribu atafanya na
mlango wa kutokea, ili mweze kustahimili,” 1Kor 10:13
No hay comentarios:
Publicar un comentario