JUMAPILI
YA 2 YA MAJILIO YA MWAKA C
6/12/2015
Somo
I: Bar 5:1-9
Zab:
126:1-6
Somo
II: Flp 1:3-6, 8-11
Injili:
Lk 3:1-6
Nukuu:
“Ee Yerusalemu, vua
nguo za matanga na huzuni, uvae uzuri wa utukufu utokao kwa Mungu milele,” Bar
5:1
“Jifungie nguo ya haki itokayo
kwa Mungu, jipige kilemba kichwani cha utukufu wake Aliye wa Milele, maana
Mungu ataidhhirisha nuru yako duniani mwote,” Bar 5: 2-3
“Nami niliaminilo ndilo hili, ya kwamba yeye aliyeanza kazi njema
mioyoni mwenu ataimaliza hata siku ya Kristo Yesu,” Flp 1:6
“Na hii ndiyo dua yangu, kwamba pendo lenu lizidi kuwa jingi
sana, katika hekima na ufahamu wote; mpate kuyakubali yaliyo mema; ili mpate kuwa na mioyo safi, bila
kosa, mpaka siku ya Kristo,” Flp 1:9-10
“hali mmejazwa matunda ya haki, kwa njia ya Yesu Kristo, kwa
utukufu na sifa ya Mungu,” Flp 1:11
“neno la Mungu lilimfikia Yohana, mwana wa Zakaria,
jangwani. Akafika
nchi yote iliyo karibu na Yordani, akihubiri ubatizo wa toba liletalo ondoleo
la dhambi,” Lk 3:2b-3
“Sauti ya mtu aliaye nyikani, Itengenezeni njia ya Bwana,
Yanyosheni mapito yake,” Lk 3:4b
“Kila bonde litajazwa, Na kila mlima na kilima kitashushwa;
Palipopotoka patakuwa pamenyoka, Na palipoparuza patalainishwa,” Lk 3:5
“Na wote wenye mwili
watauona wokovu wa Mungu,” Lk 3:6
TAFAKARI: “Na wote wenye mwili
watauona wokovu wa Mungu.”
Wapendwa wana wa Mungu,
leo Mama Kanisa anaadhimisha Dominika ya pili ya Majilio ya Mwaka “C” wa
Kanisa. Leo tuikite tafakari yetu kwenye maneno haya ya Yohani Mbatizaji, “Na wote wenye
mwili watauona wokovu wa Mungu.”
Wapendwa katika Kristo, kwa vile kila mmoja wetu licha ya utofauti wake
kimwonekano kauumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, Mwa 1:27, ni kwa maana hiyo
kwamba wote tumealiwa katika ukamilifu wa Mungu ambao ndio Utakatifu wenyewe. “Basi ninyi mtakuwa wakamilifu, kama
Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu,” Mt 5:48. Wote wanaoitwa katika
ukamilifu huu ni viumbe dhaifu ukiwemo wewe na mimi. Ni katika kuushinda
udhaifu wetu kama wanadamu ndipo tutakapo ufikia ule ukamilifu. Ni kwa mantiki
hii kwamba “wote wenye mwili watauona wokovu wa Mungu,” Lk 3:6
Tunapotambua udhaifu wetu utokanao na ubinadamu wetu ndipo tunapozama ndani zaidi
katika tafakari huku tukijitakasa katika kipindi hiki cha Majilio. Tafakari ya
kina na kujitakasa huku kunaamsha matumaini mapya na yenye nguvu kumpokea
Masiha wetu, na hakimu wetu wa haki. Noeli itakuwa na maana tu pale
tunapotambua wajibu huu muhimu wa kujitakasa. Huu ndio ujumbe wa Yohani
Mbatizaji kutoka jangwa, kwamba, “Itengenezeni njia ya Bwana, Yanyosheni mapito
yake,” Lk 3:4b. Kuitengeneza njia kwa mtazamo wa kiroho ni kujitakasa, yaani
kuyatoa yale yote yasiyoendana na ukamilifu wa Mungu tulioitiwa. Ni kuyanyoosha
mahusiano yetu na Mungu, jirani, na mazingira yetu yaliyokunjamana kwa sababu
ya dhambi. Ni kufanya toba ya kweli, Lk 3:2b-3. Yohane anaiita hali hii sawa na
‘kujaza kila bonde, kushusha kila mlima wa
dhambi; kunyoosha kila mahali palipopotoka, na kulainisha pale palipo paruzika,
Lk 3:5. Kwa maneno mengine ni kuutengeneza uso wako ufanane na uso wa mfalme
ajaye yaani mwokozi wetu Yesu Kristo.
Ili tufanane na ule uso wa Masiha na Mfalme watu wa haki na
amani, yakupasa wewe na mimi kuvua nguo ya matanga na uzuni yetu, na kuvaa
uzuri wa utukufu utokao kwa Mungu wetu kama asemavyo Nabii Baruku: “Ee
Yerusalemu, vua nguo za matanga na huzuni, uvae uzuri wa utukufu utokao kwa
Mungu milele,” Bar 5:1. Utayari huu wa kulivua vazi hili la matanga na uzuni ni
tendo la toba ya kweli. Na baada ya toba ya kweli yanipasa kuishi na kudumu
katika kweli na haki. Ni kuishi “hali mmejazwa matunda ya haki, kwa njia ya Yesu Kristo,
kwa utukufu na sifa ya Mungu,” Flp 1:11. Kweli na haki hii idumu ndani
yangu, ionekane kwa jirani zangu, na iwe dira ya kuniongoza katika kweli na
haki ya milele ambayo nitahesabiwa haki na kweli hiyo na Mungu mwenyewe. Hivyo
basi, “Jifungie nguo ya haki itokayo kwa Mungu, jipige kilemba kichwani cha
utukufu wake Aliye wa Milele, maana Mungu ataidhhirisha nuru yako duniani
mwote,” Bar 5: 2-3. Je, waipenda nuru?
Wapendwa wana wa Mungu,
nuru hii tunayo ndani mwetu kwanza kabisa kwa kupitia Sakramenti ya ubatizo, na
kwa kuendelea kuyapokea Masakramenti katika hali ya usafi. Hii nuru kwa maana
nyingine ndiyo neema zile tuzipatazo kwa kupokea Sakramenti katika hali ya
usafi. Nuru hii au neema hizi ufifishwa ndani kwetu kwa kuchafuliwa na hali ya
dhambi. Tunatakaswa na kung’arishwa tena kwa kuweka makusudi ya kweli ya
kutokutenda dhambi kwa kupitia tanuri lile la utakaso, yaani Sakramenti ya
upatanisho. Sakramenti hizi katika Kanisa ni mbubujiko wa chemichemu za neema
isiyo na kikomo. Ili neema hizi kupitia Sakramenti hizi zifanye kazi kadiri ya
mastahili yake yatupasa kuwa katika hali ya usafi.
Huku ndiko kuishi katika hali ya usafi kama dua la Mtume Paulo kwa Mungu kwa ajili ya watu wake:
“Na
hii ndiyo dua yangu, kwamba pendo lenu lizidi kuwa jingi sana, katika hekima na
ufahamu wote; mpate kuyakubali yaliyo mema; ili mpate kuwa na mioyo
safi, bila kosa, mpaka siku ya Kristo,” Flp 1:9-10.
Basi
wapendwa katika Kristo tuelewe kwamba kipindi hiki cha Majilio tunajiandaa kwa
hali ya kuwa safi mwili na roho tukilenga kufanana na usafi wa yule
tunayamngoja kwa hamu, yaani, Bwana na Mwokozi wetu. Bila kusahau ukweli
kwamba, “wote wenye mwili watauona wokovu wa Mungu,”
Lk 3:6
Mtawa
Mark Mpole siku moja jioni akiwa kwenye tafakari katika pango la Mama Bikira
Maria alichukuliwa katika njozi na mara akajikuta akiwa anaongozana na Mama
Bikira Maria kuelekea sehemu moja iliyokuwa ikisikika kwa kelele za nyundo na
vyuma. Wakiwa njiani Bikira Maria alimwambia Mark Mpole kuwa huru kuuliza
chochote nami nitakujibu.
Baada ya
mwendo wa dakika kumi hivi, Mark Mpole na Mama Bikira Maria walifika eneo lile
lililokuwa likisikika kwa kelele za nyundo na vyuma. Mark Mpole aliwaona watu
wangi wakiwa wanaponda vyuma kwa nyundo na wengine wakikata vyuma vile kwa
misumeno ya chuma. Kwa upande wa pili Mark Mpole aliona rundo kubwa kama mlima
la vipande vya vyuma vyenye maumbo tofauti tofauti vikiwa na kutu.
Ndipo
Mark Mpole alipomuuliza Mama Bikira Maria, “kwa nini pamoja na kazi kubwa
wanayofanya wafua vyuma hivi kuna rundo kubwa la vyuma vilivyo na kutu na
vimekusanywa upande mmoja?” Mama Bikira Maria huku akitazama mlima ule alimjibu
Mark Mpole, “Mlima wa vyuma hivyo vilivyo na kutu ni ‘vyuma chakavu.’ Vyuma
hivyo havifai kwa matumizi yoyote yale na ndiyo maana vimekusanywa kwa ajili ya
kutupwa. Katika maisha yako jitahidi usiwe kama vyuma hivyo. Vyuma hivyo mapoja
na kufuliwa kwa muda mrefu vilikosa kuwa na umbo lile walilotaka wahunzi wale
viwe.”
Mbele
kidogo waliona mkusanyo mdogo wa vyuma, ndipo Bikira Maria akamuuliza Mark
Mpole, “Je, hapa unaona nini?” “Hapa naona sura yangu na yako kwenye vyuma
hivi,” Mark Mpole alimjibu Mama Bikira Maria kwa mshangao. Bikira Maria
akamwambia, “Hivi ndivyo vyuma vinavyofaa na vilivyo imara kwa matumizi yoyote
yale ya kudumu. Jitahidi kuwa kama vyuma hivi katika maisha yako. Tumeziona
sura zetu kwenye vyuma hivi kwa sababu hakuna uchafu wowote uliobaki ndani
yake. Hivyo haviwezi kupata kutu katika umilele wake. Visababishi vyote vya
uwezekano wa kupata kutu umeondolewa kwa moto mkali, na kufanya upondaji wake
kuwa mrahisi kwa kuliumba umbo hili kama tunavyoona.”
Wapendwa
wana wa Mungu, hapana shaka kabisa kwamba tunapovumilia mateso yetu na
kuvishinda vishawishi, ndiyo kwa namna hiyo tunatakaswa na kuifunua sura na
mfano halisi wa Mungu ndani yetu uliofifishwa kwa dhambi zetu.
Tumsifu
Yesu Kristo!
“Na kama
tulivyoichukua sura yake yule wa udongo, kadhalika tutaichukua sura yake yeye
aliye wa mbinguni,” 1Kor 15:49
No hay comentarios:
Publicar un comentario